Mwandishi: Andrew Mhina
SEHEMU YA SITA
ILIPOISHIA...
ILIPOISHIA...
Najua Mungu amenipangia maisha mazuri sana mbali na kijiji hiki cha Tabu yanini. Maisha ni popote babu. Kuna msemo usemao kuwa ‘’Mwanamme hana kwao’’. Sijajua kuwa ni msemo wa busara sana, lakini haya ya leo yanaufanya usemi huo kuwa na maana kwangu.
KUNA MATANGAZO YANATOKEA YAGUSE KILA UNAPOFUNGUA SIMULIZI ILI KUNIPA NGUVU YA KUENDELEA
INSTALL CnZ Media ILI USIPITWE NA MIENDELEZO KILA INAPOKUWA TAYARI
SASA ENDELEA...
“Hapana Ramson ninawaza baadaye niende ofisini kwa mwenyekiti ili niongee naye aitishe kikao cha kamati ya kijiji tuyazungumzie mambo haya. Sipendi uondoke na kukaa mbali na mimi tumekuwa wazee sasa mimi na bibi yako wewe ndio Mwangalizi wetu na mrithi wa mali hizi.” Alisema Mzee Kihedu kwa hamaki!Sawa kabisa unavyosema, mpiganie mjukuu wako. Uhalifu wafanye watoto wao wamsingizie mjukuu wangu? Kwanini lakini mambo haya mabaya hayachunguzwi ninani wanaohusika badala yake watu wanafuata majungu tu?” Alisema bibi Namkunda kwa kufoka.
“Bibi achana nao! Babu naomba sana usiende kulizungumzia jambo hili ofisini kwa mwenyekiti. Utaonekana kama unanitengenezea mazingira ya kuwepo kijijini hapa kama mjukuu wako na si kama mtu mwema. Acha nikajaribu maisha sehemu nyingine.” Ramson Aliingia ndani na kuchukuwa baadhi ya nguo zake na kuziingiza ndani ya begi lake. Baadaye alichukuwa akiba yake ndogo ya hela kama laki moja na ishirini aliyoipata kwa kuuza magunia mawili ya karanga.
Pesa hii alikusudia aifanyie bustani za mbogamboga kando ya kisima kilichopo shambani kwao. Lakini baada ya kutokea matatizo hayo akazifutika mifukoni zikamsaidie mbele ya safari. Kisha baada ya kufungasha vitu vya muhimu na kuweka kwenye begi lake dogo alimuaga babu yake na bibi yake kuwa anaondoka. Bibi yake alimpatia kiasi cha Shilingi elfu ishirini na babu yake alimpa kama Shilingi laki mbili na kumtaka aende lakini atakapopata nafasi awe anarudi kuchukuwa fedha ya matumizi au mtaji pale mambo yatakapokaa vizuri.
Walimwombea heri na kumtakia baraka nyingi. Machozi yaliwatoka kwa huzuni pale walipokuwa wakiagana kwa kukumbatiana. “Msijali sitakuwa mbali na hapa. nitakuwa hapo mjini Tanga na sitaacha kuwatembelea na kuwajulia hali zenu.” Alisema Ramson kisha akabeba begi lake na kuanza safari kwa mwendo wa haraka!
Ilikuwa ni maisha ya Geto ambayo hakuyaweza, wala hakupata kwa haraka jambo la kufanya hapo mjini. Alipotoka kijijini kwao hakusumbuka kumpata rafiki. Tayari alikuwa na rafiki yake aitwaye Richard Rafiki huyu walisoma naye Kidato cha tano na cha sita katika shule ya Tanga Technical Secondary School. Richard alikuwa akiishi Makorora.
Baada tu ya kufika mjini mtu wa kwanza kumtafuta alikuwa ni Richard. Urafiki wao walipokuwa Shuleni ulifanyika kama undugu, kwani walisaidiana kwa mengi. Walisoma pamoja na pia waliazimana vitabu na kusaidiana katika matatizo madogo madogo. Waliishi vizuri sana katika chumba cha Richard, wakashirikishana mawazo kuhusu maswala ya maendeleo. Kwa bahati mbaya wote hawakuwa wamepata nafasi ya kuchaguliwa kwenda Chuo kikuu. Hatua waliyoifikiria ambayo ingewawezesha kupata kazi ilikuwa ni kuandika barua katika mashirika mbalimbali na makampuni.
Njia hii ilikuwa ni ndefu sana japo kila mahali walipewa matumaini aidha kwa kuitwa kwenye majaribio, pengine waliahidiwa kuwa nafasi zikipatikana za kazi watajulishwa. Miezi mitatu ilipopita bila mafanikio yoyote Ramson alipata maamuzi mapya. “Ndugu yangu mimi nimechoka kabisa kusubiri hapa kwa muda wote huo. Unajua tukiwa tunasubiri kitu fulani huku tukiwa tunakitu kingine tulichoshika kuna unafuu, kuliko kuangalia hicho kimoja?” Alisema Ramson siku moja wakiwa wanatoka katika ofisi moja ambapo majibu ya kuomba kazi hayakuwa mazuri. “Mawazo yako ni ya kweli kabisa japo sasa tukiangalia kwa haraka tushike kipi kwa wakati huu? Pesa ndiyo hiyo imeisha kwa upande wako na wangu. Na mimi nimechoka kwenda kumwomba baba mkubwa ambaye kabla hajakusaidia anatanguliza masimango kwanza.” Alisema Richard kwa namna ya kukata tamaa.
“Mimi naona twende mwahako kuna bonge ya ufukwe! Nilikwenda pale wakati tulipokuwa shuleni, nikatamani sana siku moja kama nikifanikiwa nipatengeneze Beach ambayo watu wangelipia huduma ya kuogelea. Nilizingatia yale wanayofanya watu wa Mombasa. Siku moja nilikwenda huko na babu yangu Alipomtembelea rafiki yake. Nilitembezwa na marafiki niliowakuta pale mpaka kwenye fukwe mbalimbali.
Kila ufukwe kulikuwa na biashara zilizokuwa zinaendeshwa na vijana. Wanachofanya vijana wale ni kutengeneza vibanda vidogo vidogo na kujinunulia mipira ya ndani ya matairi ya gari; kisha baada ya hapo huweka maji safi na sabuni kwenye vibanda vile. Wakishafanya hivyo labda huongeza na viti kadhaa vya Plastiki na kuvipanga vizuri. Tuko pamoja mpaka hapo?” Aliuliza Ramson kwa utani.
“Tuko pamoja ninaisikiliza vizuri hadithi yako ya Mombasa endelea mtu wangu, ehee wakishaweka viti ndio wanapataje hela baada ya hapo?” Aliuliza Richard. Yaani nakwambia wale watu wanatengeneza hela sijapata kuona.” Watu wanapokuja kuogelea ufukweni hapo wanawakaribisha kwenye viti wakae, kisha huwashawishi kama wanataka kuogelea wawape mipira ya kujifunzia kuogelea. Na wengi kipindi cha joto hupendelea kuogelea kama tu watahakikishiwa usalama wa vitu vyao yakiwepo mavazi.” Kisha baada ya kuogelea huelekezwa yalipo maji safi na sabuni. Mtu mmoja anaweza kulipishwa pesa ya kukaa kwenye kiti, kuogelea na baadaye kujisafisha na maji safi. Jumla ya bei ya huduma hizo zote ni hela nzuri, ambapo wakitokea kama watu kumi na tano ni kiasi kinachokuwezesha kutumia kwa wiki moja.
Mimi naona tukibuni mradi huo Mwahako utakuwa ni mzuri zaidi ya kuajiriwa.” Alihitimisha Ramsoni kutoa somo kwa Rafiki yake. “Ni ndoto nzuri sana rafiki yangu! Ndoto ya matumaini mema ya mafanikio kwa njia hiyo. Lakini kwangu ni ndoto tu kama ndoto nyingine tena za mchana kweupe! Ndoto za namna hii huitwa ndoto za mchana! Alisema hayo Richard Kwa dhihaka kisha akasafisha koo lake na kuendelea.. “Huwezi wewe kufananisha Tanga na Mombasa kwenye maswala ya Beach! Fukwe za wenzetu zina viwango na watalii wengi hupenda kuzitembelea kwa jinsi zinavyovutia.
Uwekezaji wa wakenya kwenye Beach zao ni wa faida kubwa kwa sababu unaingiza fedha nyingi za kigeni kwa kupitia watalii. Usione watu weusi wengi wanakuja katika fukwe hizo kwa kufurika. Ni kwa sababu kuna watalii. Wengine hujipatia ajira humo na marafiki, ambao baadaye huwapa nafasi za kuwatembelea katika nchi za kwao. Wengine pia hupata bahati ya wachumba wa kizungu wakike au wakiume. Yote haya hufanyika katika fukwe hizo.
Hii ndiyo sababu wengi huvutwa kwenda kule ufukweni. Labda wale wanaoenda bila makusudio hayo huenda tu kustarehe kwa sababu fukwe zenyewe ziko viwango umenipata rafiki yangu? Hayo ni machache ya mengi niliyoyataja kuhusu fukwe za wenzetu. Ndio maana nikakuambia kuwa mawazo yako ya kuweka biashara kwenye ufukwe wa Mwahako hapa Tanga ni ndoto nzuri sana lakini ni ndoto ya mchana!”
Alisema Richard na kupuuza wazo la rafiki yake.“Nimekusikia rafiki yangu ila nia yangu ni kwenda kufanya kazi hiyo kwa sababu nijuavyo mimi ni kwamba hata Mbuyu ulianza kama mchicha. ukubwa na umaarufu wa Fukwe za wenzetu haukutokea tu bila kutengenezwa.
Na si ajabu lilikuwa wazo la mtu mmoja ambalo baadaye limekuwa kama cheche ya kuambukiza moto kwa maeneo mengi ya Fukwe zilizozunguuka ukanda wote wa Pwani ya Mombasa na popote pengine duniani. Wazo langu ni cheche ndogo sana labda kama tu njiti ya kiberiti mbele ya msitu uliofunga giza.
Lakini mara baada ya muda fulani kila kitu kinaweza kikatazamika kivingine. Hayo ndiyo maoni yangu kuhusu maendeleo. Maendeleo hayatokei kwa miujiza ya Mwenyezi Mungu bali maendeleo hutengenezwa na watuwenyewe.TukiangaliaHistoria ya mambo makubwa yanayoonekana yakimaendeleo duniani leo yanatokana na wazo. Ndege zinazoruka angani leo zinatokana na wazo la mtu mmoja tu. Maendeleo mengi sana yaliyopo leo kwa wingi na uajabu wake, havikuteremshwa kwa miujiza kutoka juu bali yalianzia katika wazo, kisha watu wakahusika kuvitengeneza. Hata leo mipango hii ninayoipanga ya kuweka Beach maeneo haya ya Mwahako hapa Tanga, hii ni cheche ndogo itakayosababisha moto mkubwa sana wa kimaendeleo katika fukwe zetu hizi.
Nina Imani siku moja kutatapakaa Mahoteli makubwa sana kandokando ya Fukwe hizi. Watalii watakuja kwa wingi na kusababisha fedha nyingi za kigeni kuingia katika nchi yetu. Hayo ndiyo maoni yangu rafiki yangu na sasa ninajiandaa kwenda kuweka Beach maeneo ya Mwahako, kama wazo langu linavyonituma.” Alisema Ramson kwa uhakika juu ya azimio lake hilo. Sawa rafiki?”
“Mimi ninafikiri wazo lako ni sahihi sana ila mtaji unahitajika tena mkubwa sana. Huwezi kuwashawishi watalii waje kwenye Beach yako isiyo na vitu vya kukidhi haja yao. Ninaamini hata watu tu wa hapa hapa Tanga hawawezi kushawishika kuacha fukwe nyingine na kukufuata Mwahako kama hawataona kitu cha tofauti na cha kuvutia.
Labda nikutakie mafanikio katika zoezi lako lakini angalia kwa makini na kuzingatia maneno yangu, mtaji ni lazima uwepo katika mkakati wako.” Alisema Richard kisha akakohoa halafu akaendelea..”Ninajaribu tena kukushauri kuwa unaweza kuvuta uvumilivu tukahangaikia maswala ya kazi fedha itakayopatikana ikusaidie katika njozi yako hiyo. Kufanya jambo hili kwa sasa ni kama kupoteza muda wako tu ambao baadaye utakuja kuujutia,na na pengine kuchukia wazo lako hilo ambalo ni la thamani kama ukisubiri lifanyike kwa wakati wake.”
Richard alisema hayo huku akisimama na kusogelea Televisheni. Aliiwasha na kutafuta chanel kwa Rimote huku akirudi taratibu kwenye kiti alichokuwa amekalia. “Nafikiri umenielewa kama mimi nilivyokuelewa na wazo lako.” Alisema huku akijiweka sawa kwenye kiti chake. “Nimekuelewa rafiki yangu ila kazi kupata hapa ni ngumu sana.
Angalia mwenyewe tangu tulivyoanza kutafuta miezi mitatu imeshapita hakuna jibu lolote. Nina wazo la kuwepo maeneo yale ya Mwahako kusudi nijishughulishe na kazi mbalimbali, hata ikibidi za uvuvi huku nikiwekeza katika kutengeneza ufukwe wangu taratibu. Waswahili wanasema, “pole pole ndio mwendo.”..“Kama nitavuta muda ili nipate kazi na baadae ndio nifanyie kazi wazo hili hakuna kitakachofanyika. Heri wazo hili lifanyiwe kazi likiwa bado la moto likipoa hapa halifanyiki tena. Unajuaje huenda kuna mtu anawaza pia kufanya hivyo katika eneo lile lile? Vichwa vina mengi hivi ndugu yangu.
Mimi kesho ninataka kuhamia mahali pale ili nitengeneze sehemu ya kukaa, huku nikiangalia uwezekano wa nini cha kufanya.” Alisema hivyo kuonyesha msimamo kwa maamuzi yake. “Unataka kuniambia umeamua kujitengenezea mahali pa kukaa pale Ufukweni sivyo?”Aliuliza kwa hamaki Richard!
USIKOSE SEHEMU IYOFUATA
Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi