Mwandishi: Andrew Mhina
SEHEMU YA NANE
ILIPOISHIA...
ILIPOISHIA...
Hawakubanduka mahali hapo kwa muda mrefu sana kwani pia hawakupewa nafasi ya kuingia katika chumba hicho cha wagonjwa mahututi. Mchana wa siku hiyo iliwabidi waende kutafuta chakula kwenye Hoteli iliyopo karibu na Hospitali hiyo.
KUNA MATANGAZO YANATOKEA YAGUSE KILA UNAPOFUNGUA SIMULIZI ILI KUNIPA NGUVU YA KUENDELEA
INSTALL CnZ Media ILI USIPITWE NA MIENDELEZO KILA INAPOKUWA TAYARI
SASA ENDELEA...
Njaa iliwafanya wasivumilie japo kuwa walikuwa na huzuni juu ya ugonjwa wa Mpendwa wao. Waliporudi walikutana na Muuguzi wa kike akiwa amesimama nje ya Word ile. Muuguzi huyu inaelekea alikuwa akiwasubiri wao, ndipo alipowapa ujumbe kuwa wanahitajiwa kwa Daktari Mkuu wa Hospitali hiyo. Haraka sana walichapusha mwendo kuelekea ofisini kwa Mganga mkuu huyo.
Waliingia na kukaribishwa viti, taarifa waliyopewa ilikuwa ya huzuni sana kwao. “Ninasikitika kuwaambia kuwa mgonjwa wetu ametutoka!” Alisema Daktari huyo kwa sauti ya Upole na ya busara kubwa. “Heee!! mke wangu namkunda! kafanyaje?!” Alisema kwa hamaki sana Mzee Kihedu na kulegea mwili. Haraka sana Ramson pamoja na kwamba alichanganyikiwa alisaidiana na Daktari kumweka babu yake sawa pale alipoangukia.
Daktari alipiga simu na kuita wasaidizi wake, nao walikuja na kumbeba Mzee Kihedu na kumpeleka chumba cha matibabu. Drip la Glucose lilimsaidia baada ya muda wa masaa mawili aliamka, baadaye aliungana na Ramson kwa mipango ya kuihifadhi maiti na kutoa taarifa kwa jamaa na marafiki juu ya msiba ule.
Huu kwao ulikuwa ni msiba mkubwa sana, kwani aliyeondoka alikuwa ni kiungo muhimu sana wa familia yao. Familia yao ilikuwa ya watu watatu tu! Bibi kuondoka lilikuwa ni pigo kubwa sana katika familia hiyo. Ramson alilia na kubeba uchungu mkubwa sana moyoni mwake. Babu yake naye alikuwa hajiwezi aligumia tu kila saa bila kutoa maneno ya kueleweka.
Mpaka mazishi yanafanyika baada ya kusafirishwa kwa mwili wa Marehemu kwenda kijijini, Mzee Kihedu hakuwa na nguvu kabisa. Ramson ndiye aliyekuwa msimamizi wa kila kitu akisaidiana na wanakijiji na jamaa zake waupande wa bibi wakiwemo wajomba na ndugu zao. Ushirikiano wa wanakijiji ulikuwa ni mkubwa sana baada ya kukaa matanga kwa siku tatu walitawanyika. Lakini ndugu na marafiki waliendelea kuja kutoa pole kwa babu Kihedu.
“Babu inabidi nikuache mara moja niende kuangalia mradi wangu. Unajua jamaa niliyemwacha mpaka sasa haelewi kuwa nimepotelea wapi. Wiki mbili hizi tangu Tumefiwa kwake pia zitakuwa ni kitendawili, maana nilimwaga kuwa nitakaa kwa muda wa siku mbili tu.”Ramson alimwaga babu yake. “Mjukuu wangu Ramson mimi sina neno na wewe. Ila kumbuka kuwa mimi sasa niko peke yangu, wewe ndiye mwenzangu. Usikae sana huko ukikaa kidogo njoo uangalie mashamba yako na mifugo na mimi Babu yako unasikia?” Alisema Mzee Kihedu huku akitokwa na machozi mengi.
“Babu usilie tuko pamoja! Nitakuwa karibu na wewe mara kwa mara. Isitoshe wafanyakazi wetu wa shamba na wa mifugo wataendelea kuwa msaada kwako wakati nikisimamia kazi yangu kule mjini.Usijali babu kwaheri Rafiki yangu.” Ramsoni alimwaga babu yake kwa kumpigapiga begani kisha akabeba begi lake na kuondoka. Nje ya nyumba alikutana na Mfanya kazi wao anayesimamia mifugo yao.
“Mimi ninaondoka tafadhali mwangalieni mzee na kumchukulia kwa upole sawa?” Alisema Ramson akitoa maagizo kwa jamaa huyo. “Sawa bwana kaka tutafanya hivyo Mzee wetu hana neno na sisi tunampenda. tutaendelea kufanya vizuri katika nyanja zote.” Alisema jamaa huyo aitwaye Habibu.
“Sawa naenda lakini nitarudi muda sio mrefu kuangalia maendeleo yake.” Alisema Ramson na kuondoka kuelekea katika kituo cha magari kijijini hapo. Alipanda gari baada ya kufika hapo na gari hilo halikuchukuwa muda mrefu liliondoka kuelekea mjini Tanga. mawazo aliyokuwa nayo yalimfanya apitiwe na usingizi hadi aliposhtuliwa na kondakta kuwa Tayari wamefika mjini.
Mandhari ya ufukwe yalianza kuchukuwa kasi katika kuwa bora kila siku. Watu waliokuwa wanakuja kila mwisho wa juma walizidi kuwa wengi. Ramson alipata marafiki walioahidi kumletea viboti vya kutembezea watalii, katika maeneo mbalimbali baharini. Kuna visiwa vyenye historia nyingi ambavyo vinaweza kuwa na kumbukumbu nyingi. Ramson ametamani kupata boti za kuwatembezea baadhi ya watalii watakaopenda kutembelea maeneo hayo.
Hizo ni ndoto ambazo anaendelea kuzifanyia kazi kila siku ili kuinua kipato na kuridhisha moyo wake, kwa kufikia malengo yake ya kimaendeleo.Ringo alikuwa akijishughulisha kwa bidii sana katika kufungasha bidhaa mjini na kuwauzia wateja pia alisimamia mazingira. Kwa namna hii walipiga hatua kubwa ya kimaendeleo.
Kila hatua walipongezana na kukaa mahali ili kutathimini faida na hasara lakini ilikuwa ni aghalabu sana kupata hasara katika kazi yao hiyo. Kwa Ramson Ringo alifanyika kuwa ndugu yake kabisa. Alifarijika kuona kuwa hata Ringo alimchukulia vilevile. kilichoweka muhuri juu ya undugu wao ni uaminifu na bidii yao. Walishirikiana kwa mambo yote na hata mawazo yao hayakutofautiana.
Kitu kingine hawakutaka pombe, wala tabia za kujihusisha na mambo ya uhuni hayakuwepo vichwani mwao Walizingatia miiko waliyojiwekea kuwa ndio msingi wa maendeleo yao kama wakiishika. “Unajua kama tusingejiwekea miiko hii hapa tulipofikia pangebakia katika ndoto?” Alisema Ramson siku moja walipokuwa katika kikao chao cha kujadili maendeleo ya ufukwe wao.
“Ni kweli Rafiki yangu. Daah unajua nimeheshimu sana mipango yako mtu wangu. Katika maisha yangu sijawahi kuwaza kuwa tunaweza kuwa wamiliki wa sehemu nzuri hivi. Ungeniuliza mapema juu ya suala hili ningepiga mahesabu ya mamilioni ya mtaji kumbe ni bidii na maarifa tu!” Alisema Ringo huku akishangaa aina ya maendeleo yalivyokuja kwao.
“Mtu wangu naweza kusema kuwa hii ni hatua ndogo sana. Hatujafika popote ila tayari tumepata fununu tu ya kule tunakotaka kwenda. Unajua mara zote ukijiona uko juu bila kuangalia walioko juu zaidi yako, unaweza kujibweteka. Lakini mara kwa mara unapopiga hatua fulani usiridhike kuwa uko juu. Jambo la kufanya Kila unapopiga hatua angalia juu, Utakapowaona wengine walivyo juu kimaendeleo kuliko wewe, jipange na utamani kufika pale walipo na kuzidi, hii ndio chachu ya kimaendeleo siku zote.
Unajua Rafiki yangu maendeleo ni nia na juhudi kwa kile unachotamani ukipate. Hapa tulipo tunamshukuru Mungu tunapata riziki yetu ya kila siku. Tunaweza kubadilisha mavazi kila siku tukitaka. Pia tunaweza kufanya vitu vingi kiasi kwa uwezo wa Mungu. Lakini bado hatujapiga hatua ya kimaendeleo. Tunatamani usafiri wa kufungashia bidhaa zetu mjini. Tunatamani boti za kuwatembezea wateja wetu baharini, tunatamani pia kujenga nyumba za maana hapa ufukweni na kuzifanya hoteli kwa ajili ya wageni wetu.
Tunaangalia mbele zaidi kuwa siku moja tuwe na Hoteli za kitalii mahali hapa. Ukiangalia mipango hiyo na ukirudi kuangalia hapa tulipo lazima ujione kuwa bado uko chini sana.” Alisema Ramson kwa utulivu kuonyesha kuwa kichwani kwake bado mipango iko mingi inayohitaji kufikiwa. “Kweli Rafiki yangu unaangalia mbali sana.” Alisema Ringo kwa msisimko. Maelezo yako yanahamasisha na kutia ujasiri wa kufanya kazi kwa bidii.
Najua kama Mungu ametuwezesha kufika hapa tulipo tutashindwaje kufikia malengo hayo uliyoyasema? Hii ni hatua ya kwanza mbele yetu tunazo hatua nyingi sana zinazohitajika kutufikisha katika kila kimoja cha hayo malengo uliyonayo.” Alisema kwa hamasa Ringo. “Naamini kila jambo litafikiwa katika yote tuliyopanga.” Alisema Ramson kwa uhakika kisha akaamka kwenda kupokea wageni waliokuwa wanapaki gari lao.
“Yule jamaa ameleta Mabarafu?” Aliuliza wakati akiendelea kutembea kuwaendea wageni wake. “Ataleta saa sita maana yalikuwa bado kuganda sawa sawa.” Alijibu Ringo kwa sauti.
Ilikuwa ni ajali mbaya sana. Ajali iliyotokea mjini Tanga kwenye barabara iitwayo Taifa Road. Gari ndogo ilikuwa ikitokea maeneo ya Mabanda ya papa kwenda maeneo ya Mjini kati. Gari hili lilikuwa likienda kasi sana inaelekea Dreva wake alikuwa na haraka sana. Gari hili mara tu lilipokuwa kwenye raundi about ya barabara ya kumi na tano lilikutana na pikipiki iliyotoka soko mjinga.
Mwendesha pikipiki hakuwa akiangalia na badala yake alikuwa akitaka kupitiliza ili kwenda ng’ambo akiambaa ambaa na barabara hiyo ya kumi na tano kwenye maduka ya vyakula.Alipokuwa katikati ya barabara ya Taifa road kabla hajaifikia barabara nyingine pacha na ile, ndipo gari lile lilipogonga pikipiki ile vibaya. Gari liliserereka kwa kukosa mwelekeo kisha liliingia kwenye mfereji wa barabara hiyo. Dreva wa pikipiki alikufa hapohapo. Ndani ya gari walikuwepo abiria wawili pamoja na Dreva, abiria wote walifariki dunia lakini dreva alivunjika mguu wa kushoto na kupata majeraha mengi usoni.
Miongoni mwa abiria walikufa kwenye ajali hiyo alikuwepo Ringo! Ringo alitoka asubuhi hiyo ufukweni ili awahi kununua bidhaa mjini. Ilikuwa ni Jumamosi kwa hiyo wateja ni wengi sana ufukweni. Hivyo waliagana na Ramsoni kufungasha bidhaa za kutosha, ili wateja wasikose mahitaji muhimu. Kabla hajafika kwenye vidaladala vya kumpeleka mjini, alikutana na rafiki yake Kejo aliyekuwa na gari.Alijipakia ndani ya gari hilo ndani yake akiwepo mtu mwingine, mbali na Kejo aliyekuwa akiendesha.
Kwa ufupi ulikuwa ni msiba mwingine wa kutisha na kusikitisha sana kwa Ramson, baada ya kupewa habari. Moyo wake ulimuuma sana, kwa kumkosa tena mtu muhimu kwake na kwa shuguli zake. Ramson alisimamia msiba huo kama wa ndugu yake kabisa.
Kila kitu alihakikisha kinafanyika kwa viwango vikubwa. Alisafirisha yeye mwili wa aliyekuwa rafiki yake na kusimamia mambo yaliyopungua kwa ajili ya matayarisho ya mazishi. Mwisho wa yote aliwapa wazazi wa Ringo kiasi cha fedha, kilichokuwa mgao wa fedha kwa ushirikiano na mtoto wao. Kisha aliahidi kuendelea kuwahudumia kama kukumbuka ushirikiano wake na Mtoto wao katika kazi zake.
Baada ya miezi miwili Ramson akiwa katika maeneo yake ya kazi alipata wageni. Ni kawaida yake kupata wageni kila siku lakini wageni wa leo walikuwa hawajawahi kufika ufukweni hapo, walikuwa ni mwanamme na mwanamke. Walionekana watu hawa ni matajiri kutokana na uonekano wao, pia Usafiri wao ulikuwa wa thamani sana. Baada ya kupaki gari waliteremka na kuja mbele ya Ramson kwa hatua za taratibu, wakiwa wameshikana mikono. Ukweli walikuwa wamependezana sana.
“Karibuni sana Wageni wangu.” Alikaribisha Ramson. “Asante sana habari za hapa?” Aliitikia yule wa kiume. “Nzuri sana karibuni sana. Mimi naitwa Ramson lakini Rafiki zangu hupenda kuniita The Beach Man! Karibuni mjisikie vizuri kuwepo hapa.” Alisema Ramson. “Asante Mimi naitwa Jackson Kigoi kwa fani ni Dokta hivyo watu wamezoea kuniita Dr.Jackson, huyu niliyenaye ni Mke wangu mpenzi anaitwa Mrs Mary Jackson.” Alisema Jamaa huyo aliyejitambulisha kama Jackson.. kisha akaendelea..“Kuja kwetu hapa ni ili tujipumzishe na kuogelea.
USIKOSE SEHEMU IYOFUATA
Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi