SITOISAHAU FACEBOOK (25)
Zephiline F Ezekiel
6 min read
Mwandishi: Emmy John Pearson
SEHEMU YA ISHIRINI NA TANO
ILIPOISHIA...
ILIPOISHIA...
“Naitwa Isabela.” “Mh!! Isabela!! Ulibadilisha jina ama..maana nakumbuka walikuwa wanakuita nani vilee.” Alijaribu kuvuta kumbukumbu. Mimi nikawa namtazama tu! Nilibadilishaje jina sasa mimi.“Hata sijabadili mbona.” Nilimwelewesha. Akazidi kupinga.
KUNA MATANGAZO YANATOKEA YAGUSE KILA UNAPOFUNGUA SIMULIZI ILI KUNIPA NGUVU YA KUENDELEA
INSTALL CnZ Media ILI USIPITWE NA MIENDELEZO KILA INAPOKUWA TAYARI
SASA ENDELEA...
Hatukufikia makubaliano, akapigiwa simu akaniaga huku akisisitiza kuwa nimemdanganya jina. Mimi sio Isabela.Nilimsindikiza kwa macho hadi akatokomea. Nilijitazama iwapo nilifanana na mmoja kati ya ndugu zangu lakini hakuna niliyefanana naye ambaye ningeweza kumtupia lawama kuwa watu wananifananisha naye.
Kile kitendo cha yule dada kuonekana kana kwamba amenifananisha kisha akakataa kuwa jina la Isabela si la kwangu nilikipuuzia na kumchukulia yule dada kuwa amepoteza kumbukumbu zake kwa kuwa miaka imepita mingi sana.Nilivyotoka pale moja kwa moja nikaenda nyumbani kwa dada Suzi kwani tangu nirejee Makambako sikuwa nimeenda kumsalimia mume wake na familia kwa ujumla zaidi ya kukutana msibani.Nilimkuta yupo nyumbani akiwa na familia yake jikoni wakiandaa chakula.Alinipokea vyema tukasalimiana kisha nikataka kumsaidia kupika.
“Kuliko kunisaidia kupika ni heri unisaidie kumbeba huyu mwanao.” Alizungumza huku akijitoa mtoto aliyekuwa amembeba mgongoni. Nikampokea na kumbeba.Ghafla mtoto akaanza kulia taratibu kisha anaongeza kilio.“He! Haka nako lini tena kameanza kuchagua watu.” Nilimuuliza dada. Hakunijibu zaidi ya kuguna akimaanisha kuwa huenda ni jambo la kawaida.“We dogo wewe..mama yako mdogo huyo.” Alisema akimaanisha kumweleza yule mtoto mdogo wa mwaka mmoja. Japo hakumuelewa.Mtoto akazidi kutoa kilio.“Hebu mchukue mwanao nadhani ana kisilani cha usingizi.”
Nilimkabidhi dada Suzi mtoto wake, cha ajabu hakunyamaza zaidi ya kuongeza kulia. Sasa Suzi akashtuka na kulichukulia uzito hili suala ambalo mwanzo ulikuwa kama mzaha fulani hivi. Alimkagua mwanae kama amechubuka mahali. Hakuna kitu!Huenda basi ameumwa na mdudu, hata hilo pia halikuwepo!!!Mapishi yakakoma kwa muda. Mtoto analia kwa sauti ya juu sana. Machozi yanamtoka kwa wingi mno. Hatari!!Ilianza dakika moja na sasa zilikuwa zinatimia sitini, yaani saa zima bila kilio kukoma. Mtoto alikuwa analia sana.
Majirani wakakisikia kilio hicho kikuu wakajongea pale nyumbani kwa Suzi. Na wao pia wakashangaa.Suzi akajaribu kumpa titi mtoto aweze kunyonya, akalikataa. Kila mmoja alijaribu kumbeba bila mafanikio.Kimbilio lililofuata likawa hospitali.Huko napo hapakuwa na nafuu yoyote. Madaktari walimfanyia uchunguzi na kurejea na majibu yasiyoridhisha hata kidogo. Walisema kuwa mtoto hakuwa na ugonjwa wowote ule. Hivyo hawakuwa na msaada wowote ule.Tulirejea nyumbani. Tulipofika huku kila aliyetazama tukio hili akiwa katika mfadhaiko wa hali ya juu na kuegemeza imani zao katika mambo ya kishirikina. Ni hapa na mimi nilijishtukia na kuanza kuamini kuna jambo. Lakini jambo lenyewe ni mimi!!
Niliamini kuwa ni mimi baada ya kuyakumbuka maneno ya yule mzee kule Iringa. Aliyeniambia nisipofuatilia jina langu basi nitasababisha majanga mengi sana popote nitakapokuwa.Usiku mzima mtoto alikuwa analia. Na kama hiyo haitoshi mara mkono wake wa kushoto ukaanza kujikunja. Suzi naye akawa analia sasa maana hakuwa na njia nyingine.Baba wa mtoto alipigiwa simu akiwa safarini kuelekea Songea akalazimika kuhairisha safari, mama yetu alikuwa hapo nyumbani pia.
Suzi alikuwa Amelia sana na alikuwa amewaacha walokole wenzake wakimwombea kwa namna zote mtoto yule. Lakini hali iliendelea kuwa tete.Mtoto huyu akifa itakuwa juu yangu!! Niliwaza na kufikia maamuzi.Dada Suzi alikuwa mtu pekee ambaye angeweza kunisaidia katika hili. Maana tayari tulikuwa tunamtambua kuwa alikuwa mwanamke wa kipekee aliyeweza kuhifadhi siri nzito nzito.Huenda hata siri aliyokufa nayo baba nayo angeweza kuwa nayo!! Nikarusha karata yangu.Nikamfuata dada Suzi nje alipokuwa amekaa chini ya mti akilia kwa juhudi zote.
“Da Suzi.” Nilimuita, akageuka akanitazama na macho yake mekundu yaliyovimba kutokana na kulia kwa muda mrefu.“Nahitaji kuzungumza nawe dada.”Alinitazama tena bila kusema lolote.“Kuna jambo nahisi….”“Nini?”“Naweza kuwa najua chanzo cha tatizo hili.”Suzi akageuka mzima mzima akanitazama kwa umakini kabisa akisubiri niseme neno.Sikuwa na haja ya kumueleza kuwa ile ninayotaka kumwambia ni siri, nilikuwa namuamini sana.
“Suzi…” nilianza kumuelezea kwa kirefu na mapana juu ya maisha niliyopitia, nikamueleza juu ya ile mimba ya maajabu ambayo mwisho wake ulikuja baada ya kukatwa ilea lama ya 666 katika makalio yangu, nilimueleza pia juu ya Dokta Davis na pesa zake haramu, ndoto za maajabu zote pia nilimuelezea.Dada Suzi alinisikiliza vyema sana nilipokuwa namueleza juu ya makaburi ya Kiyeyeu huko Iringa na jinsi nilivyokutana na babu nisiyemfahamu aliyenieleza kuwa jina la Isabela sio jina langu. Natakiwa kulitafuta jina langu.
Alishangazwa na kukwama kwa basi letu hadi pale niliposhuka mimi, kifo cha mwanaume aliyekuwa anasoma risala ya marehemu baba pia alishangaa nilivyomweleza kuwa yawezekana ni moja ya majanga niliyoyasababisha.“Hata baba alikuwa ameniahidi kunieleza jambo fulani lakini ajabu kabla hajaweza kunieleza ametutoka. Nahisi ni yaleyale. Najua dada yangu hauamini mambo haya lakini niamini mdogo wako.”Nilimsisitiza na ili kumfanya aamini tuliingia ndani nikamfunulia kovu langu. Hapo sasa aliweza kuniamini.
“Kwa hiyo mwanangu anaweza kufa pia.” Aliniuliza kwa wasiwasi.“Sijui nisemeje lakini kiukweli naogopa sana…” nilimjibu.“Sasa Bela mimi nafanyaje hapa katika hili.”“Dada kama unaweza kujua lolote lile kuhusiana na mimi tafadhali nieleze tumuokoe mtoto. Hana makosa hata kidogo.” Nilimsihi Suzi. Kilio cha mtoto kilikuwa juu kama kilivyoanza na alikuwa anazidi kujikunja mkono.Suzi alinitazama usoni kama anayesoma kitu fulani kwangu.“Bela…yapo baadhi ninayoyajua….nitakueleza, sio kwa imani za kishirikina hapana!! Nakueleza kwa kuwa ni lazima uyajue. Kama mwenyezi Mungu amenipa pigo hili ili nikueleze siri hii basi nakueleza. Lakini jitahidi kuwa na moyo mgumu.”
Nilianza kutetemeka kwa maneno hayo ya dada, hakika nilikuwa namuheshimu kwa kuwa na siri nzito nzito.Kabla ya kunieleza aliniongoza katika sala. Nikamfuatisha hadi alipomaliza.Sasa uwanja ukawa wake nami nikawa katika zamu ya kusikiliza.“Siri hii hata aliyenieleza hajui kama alinieleza.”“Kivipi?”“Mzee alikuwa amelewa siku hii. Na pesa ya kulewa nilimpa mimi. Baada ya kulewa akawa anasemezana nami kwa njia kama ya kupitiwa ama hajui anazungumza na nani.”Nikakubali kwa njia ya kichwa.Suzi alinielezea juu ya upendo wa baba kwa mama yangu ulivyomlazimisha kufanya jambo hili la ajabu. Tendo la kuiba mtoto na kumpatia mama bila yeye kujua.
“Aliiba mtoto…kivipi?”“Baada ya mimi kuzaliwa mama alizaa mtoto mwingine, akafariki dunia akiwa tumboni. Siku chache kabla ya kuzaliwa. Baada ya hapo akashika mimba nyingine tena. Alipojifungua tu mtoto akafariki tena.” Alinieleza dada Suzi, taarifa ile ya pili ikanisisimua kuliko ile ya kwanza, maana nilikuwa naifahamu hiyo kuwa iliwahi kutokea. Hii ya pili sikuwa naifahamu.“Baba akazungumza na manesi, akawapatia pesa nyingi ambazo ziliwafanya wasahau wajibu wao. Wakakiuka maadili wakaiba mtoto na kumpelekea mama halafu yule mtoto aliyekufa akapelekwa wanapojua wao.”“Kwa hiyo mama alipozinduka?”“Akajikuta ana mtoto wa kike….akaamini ni mtoto wake wa kumzaa.”“Kwa hiyo mama anajua kuwa hayo yalitokea?” niliuliza kwa hamaki.
“Si yeye wala ndugu mwingine anayefahamu jambo hili. Kama nilivyokwambia hata mimi baba alinieleza akiwa amelewa.”“Sasa huyo mtoto mwingine yupo wapi sasa hivi? Na anaitwa nani jamani”Ndiye huyu mbele yangu, anaitwa Isabela.”Nilipiga yowe la mshtuko!! Suzi akawahi kuniziba mdogo na kunikanya kuwa niwe mtulivu kama kweli nimeamua kuichukua siri hiyo. Nikajilazimisha kutulia.“Isabela…wewe sio mtoto wa familia hii ya mwalimu Nchimbi, mimi sio dada yako wa damu, mwalimu sio mama yako na hata marehemu pia hakuwa baba yako.” Alisema Suzi huku akiwa amenitazama usoni moja kwa moja.
Nikashtushwa na kauli hiyo. Nilitegemea kuwa Suzi atabadili kauli hiyo huenda amesema kimakosa, lakini hakubadili.Mapigo ya moyo yakaenda kasi sana!! Nikatamani ile iwe filamu na itamalizika baada ya muda fulani. Lakini hali ikaendelea kuwa kama ilivyo.“Dada Suzi, kwahiyo mimi…eeh!” nilikuwa nimepegawa. “Hiyo ndiyo siri Isabela. Haya je inahusika kwa namna yoyote na tatizo la mwanangu???” “Dada yawezekana kweli yahusika sana. Kwa maana hiyo mimi sio Isabela. Hili jina alinipa nani.”
“Baba na mama….namaanisha mwalimu Nchimbi na marehemu mume wake.”“Basi mimi sio Isabela. Mama yangu na baba yangu watakuwa wapi Mungu wangu!!” nilijiuliza huku nikijikuna kichwa changu pasipo kuwashwa.Wakati najikuna kichwani zikarejea zile kumbukumbu za kudekezwa sana na mwanamke huyu ambaye sasa naambiwa kuwa sio mama yangu. Upendo wa dhati alionionyesha tangu nikiwa mdogo ulizidi kunifanya kimya kimya nipingane na kauliza dada yangu. Lakini ule uwezo wa dada kutunza siri ulinirejesha kuamini kuwa ule ni ukweli.“Kwa hiyo inakuwaje.” Alinishtua Suzi na kunifanya nikumbuke kuwa tulikuwa na tatizo.Natakiwa kulipata jina langu na ukoo wangu!! Nilimwambia Suzi.
Kama ilivyokuwa kwangu ndivyo ilivyomuwia mwalimu Nchimbi ugumu sana kuweza kuamini alichokuwa anaelezwa na dada Suzi. Alimanusuru azimie kama zisingekuwa jitihada za dada Suzi kulegeza maneno makali na kuyafanya laini.Hatimaye mama aliyekuwa mbishi kipindi chote cha maziungumzo alikubali kwa shingo upande kuwa mimi sio mwanaye.Kwa kuokoa maisha ya mtoto wa dada Suzi ambaye alikuwa analia mfululizo tuliamua kwa pamoja kushirikiana kulitatua tatizo hili.
Hospitali!! Hapa ndio tulianzia kumtafuta mama yangu. Ilikuwa hospitali ya serikali na ni miaka mingi sana ilikuwa imepita. Kila kitu kilikuwa kimebadilika, hakuwepo wa kuweza kutusikiliza na kutusaidia.Mtoto akiwa amebaki nyumbani, sisi tukiwa katika hekaheka hizi ndipo mama alipokuja na wazo la kumwendea mkunga ambaye alimzalisha. Mama alikiri kumkumba mama huyo ambaye ni mstaafu tayari. Hakuna aliyelalamika kuhusu kuchoka. Tulitembea kwa miguu. Tulipofika maeneo ambayo mama alihisi kuwa ndipo anaishji yule mkunga tulianza kuulizia. Ilituchukua muda mfupi tu kuweza kuyapata makazi yake.
“Ameenda sokoni lakini atarudi muda si mrefu.” Msichana tuliyemkuta pale nyumbani alitujibu.Tukajiweka katika mkeka tulioukuta pale nje na kumsubiri.Kama tulivyoelezwa mama huyo mkongwe kiasi alifika, kwa kumtazama alionyesha kuwa ujanani alikuwa mrembo sana lakini mwenye maringo.Licha ya uzee huo bado alikuwa na maringo kiasi katika sauti yake.Alitukaribisha huku akiwa amesimama kwa namna ya kutusikiliza shida yetu ni ipi.
Kila mmoja akamwachia mama jukumu la kuzungumza.“Naitwa mama Isabela au …” kabla hajamaliza kujitambulisha ilisikika sauti kutokea dirishani, “Shakamoo mwalimu!!”“He! We ni nani tena unanisalimia umejificha…” alisema mama kwa kitetemeshi cha ualimu.Yule mkunga akasaidiana nasi kutazama mlangoni. Akatoka msichana kwa makisio ni umri wa miaka kumi na moja.Akamsalimia mama kwa kupiga magoti.Kabla ya kujibu mama akaanza kuvuta kumbukumbu.“Eliza….nimekosea!!!” alimkumbuka jina lake kwa usahihi.“Mjukuu wangu huyu, kumbe ni mwanafunzi wako.” Yule mkunga aliyekuwa amesimama akasema huku sasa akikaa.
USIKOSE SEHEMU IYOFUATA
Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni