PETE YA MVUVI (2)

0

SEHEMU YA PILI
ILIPOISHIA...
“Mungu weeeeee!!! Mungu!!!! Niokoe mimiiii!!!” nilitamka maneno yale huku nikiendelea kukimbia mara ghafla sikusikia sauti wala vishindo vya fisi wale hivyo nilisimama na nilipojaribu kukohoa nilikohoa damu nzito huku pua zangu nazo zilianza kutokwa na damu

IKIWA UNASOMA SIMULIZI NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI USIPITWE NA SIMULIZI

ENDELEA...
Maskini!!! Hali yangu ilikua mbayaaa mnoo…Nilikumbuka msemo wa babu uliosema, “Mwanaume ni shujaa na kila apatapo majaribu basi hana budi kupambana kuyashinda” Hivyo msemo ule ulinipa nguvu ya kuendelea kutembea na baada ya muda wa dakika 10 nilifanikiwa kufika ziwani.

Nilitazama huku na kule nikitafuta mtumbwi wa babu ila sikufanikiwa kuuona japo kwa mbali, Machozi yalianza kunitoka taratibu taratibu na kadri nilipokua nikiangalia ziwa lile bila kuona dalili yoyote ya babu yangu kurudi nilianza kulia kwa nguvu kwani nilihisi kuna kitu kibaya kimemtokea babu. Ghafla kuna kitu kiliugusa moyo wangu na nilinyamaza, nilikumbuka nimeacha mlango wa nyumba yetu wazi na huku ndani nilimuacha mdogo wangu Neema, Nilishtuka sana na kusema, “Mungu wangu kumbe nimeacha mlango wazi?”

Niliogopa sana kwani kawaida ya kijijini kwetu pindi mvua kubwa inyeshapo huwa kuna wanyama na wadudu kama nyoka na nge huwa na tabia ya kuingia ndani ya nyumba za watu kutafuta joto. Nilizidi kuogopa kwani ni lazima nipite tena kati kati ya lile pori lakini kutokana na upendo wa dhati niliokua nao kwa mdogo wangu (Neema) nilijikaza kiume na nilifanikiwa kupita bila kufukuzwa na mnyama yeyote. Nilipofika karibu na nyumba yetu nilimuona nyoka mkubwaaa!!! Akiwa anatoka ndani ya nyumba yetu huku tumbo lake likiwa limejaa.

Daaaah!!!! Niliishiwa nguvu kabisaaa!! Kwani nyoka yule alikua mkubwa sana na alitoka huku akionekana amekula kitu na nilihisi atakua amemmeza Neema, Nilimsubiri nyoka yule apotee kabisa na ndipo kwa haraka sana nilikimbilia ndani na moja kwa moja nilielekea chumbani nilipokua nimemuacha Neema. Kwa bahati nzuri nilimkuta neema akiwa ameamka huku akicheza cheza na shuka, Nilihema kwa nguvu na kusema, “Ooooooh!! Asante Mungu”.

Nyoka yule alimeza kiroba kilichokua na mabaki ya samaki na nyama ya mbuzi. Nilirudishia mlango wa nyumba yetu na kisha nilipanda kitandani kulala, Nikiwa ndotoni niliota ndoto mbaya sana kwani niliota nipo msituni nikizungukwa na watu waliokua na sura za wafu huku shangazi yangu aishio mjini akiwa na kisu kikali kilichotapakaa damu ya babu. Sikuweza kuendelea na ndoto ile kwani Neema alishtuka na kuanza kulia……

na kwa uwelewa nilijua ana kiu cha maji, Hivyo nilitoka kitandani kumfatia maji na kumnywesha baada ya muda kidogo alilala. Baada ya kuota ile ndoto sikupata usingizi kabisa kwani nilianza kuitafakari ile ndoto huku nikitokwa jasho na mikono yangu kutetemeka, Nilizidi kuogopa na nilikua nikitamani asubuhi ifike mapema. Asubuhi ilifika na mlango wa nyumba yetu uligongwa kwa nguvu, Mimi nilikua bado usingizini ila kwa mbali sana nilisikia sauti za watu zikisema, "Joshuaaaa!!! Weweee!!! Amkaaaa!! Babu yako ana hali mbaya sanaaa!! Fungua mlango"

Mhhhh!!! Niliposikia jina la babu yangu limetajwa nilishtuka mara moja na nilitoka nje kuona ni nini kiliendelea. Maskiniiii!!!! Nilimuona babu yangu akiwa amelazwa chini huku anatokwa na damu za pajani na kifuani huku sura yake ikijawa na uchungu kwa kuvumilia majeraha yale, Babu aliniambia, "Joshua baba naomba uniletee maji kwenye kikombe changu cha kahawa" Nilinyanyuka haraka na nilimletea maji, Babu alikunywa yale maji na yalipofika nusu kikombe aliniangalia kwa huruma na kisha alisema,"Mjukuu wangu kikombe hiki na maji haya nakukabidhi yawe baraka zangu kwako na mdogo wako, Pia nakuomba uzisimamie mali zangu vizuri ukiwemo mtumbwi wa kuvulia samaki na hili shamba lililopo hapa nyumbani, Babu yako sidaiwi chochote na mtu yeyote yule hivyo asije mtu akakudanganya, Joshua Mungu akusimamie, Kwaheri mjukuu wangu"

Kabla hata sijaanza kumuuliza kwanini ananiambia maneno yote yale, Babu yangu alifumba macho huku pumzi yake ikikata, Maskini babu alifariki akiwa mikononi mwangu….Kifo cha babu yangu kilisababishwa na majeraha makubwa aliyoyapata baada ya kungatwa na fisi alipokua akirejea nyumbani usiku ule ambao masaa machache kabla ya tukio lile nilienda kumtafuta eneo zima la pale ziwani lakini sikumuona. Kuchelewa kwa babu yangu kurudi nyumbani kulisababishwa na upepo mkali uliokua ziwani huku zile mvua zilizopiga kwa nguvu mno zilimfanya babu pamoja na rafiki zake kusubiri mpaka upepo na mvua ile kubwa ipungue,

Na usiku huo walirudi wakiwa na furaha mno kwani walivua samaki wakubwa na wengi sana hivyo kwa furaha ile babu pamoja na rafiki zake walielekea moja kwa moja kilabuni japo kujipongeza na chupa kadhaa za pombe aina ya BALIMI, Babu yangu hakutaka kunywa pombe hivyo aliwaacha rafiki zake yeye alianza safari ya kurudi nyumbani, Kumbe alipokua kati kati ya lile pori alikua amebeba mfuko mkubwa uliojaa samaki huku alikua akiimba nyimbo zake kwa kupiga miruzi. Harufu ya samaki wale na mlio ule wa mruzi uliwakurupusha fisi na hivyo walitafuta harufu hiyo ipo wapi na walipomuona babu akiwa na mfuko mkubwa wa samaki,

Kwa nguvu walimshambulia babu na kumjeruhi sehemu kubwa sana mwilini mwake. Maagizo yake yote aliyoniachia marehemu babu nilianza kuyatimiza pale tu! tulipomaliza kumzika,lakini kwa kuwa nilikua mdogo kujua nini hatma zile mali zake niliona ni vizuri nimshirikishe Shangazi yangu kwani yeye ndiye aliyekua mtoto wa pekee aliyebaki kwa babu yangu. Nilimueleza Shangazi kila kitu nilichoambiwa na babu huku nilimpa zile karatasi ambazo sikujua maana yake ni nini?, Shangazi alishtuka sana kwani aliona jina langu kwenye kila karatasi zile ambazo ni hati za mali za marehemu babu yangu.

Shangazi yangu kwa hasira alisema, “Niniiiiiii!!!!? Eboooo!!? Joshua? Yani wewe ndio mrithi wa mali za baba yangu? Thubutuuu!!! Labda mimi sio binti wa marehemu” Niliogopa sanaaa!! Kwani aliongea kwa hasira huku macho yake yalianza kubadilika na kuwa myekundu, Kwa uwoga ule niliondoka eneo lile na kukimbilia ndani kumuangalia mdogo wangu (Neema) asiyejua lolote lilokua linaendelea. Enzi za uhai wa babu yangu alipenda sana kunisihi nisije nikamuamini Shangazi yangu hata chembe lakini nilikua sina wa kumuomba msaada kwa mzigo ule mzito wa kusiamamia mali niliokua nimekabidhiwa na marehemu baba kwani umri wangu ulikua ni mdogo kuweza kuhimiri jukumu lile peke yangu……

Baada ya muda wa siku tatu kupita Shangazi aliniomba nikaishi nae mjini huku akinilazimisha nimuache mdogo wangu Neema kwa jirani kwani aliniahidi atanipeleka shule ya ufundi nikasomee Umeme, Nilikataa katu katu!! Kumuacha mdogo wangu kwa jirani kwani Neema alikua mdogo sana kuachwa mikononi mwa watu asiowajua. Niliendelea kusimamia msimamo wangu ule ule na ndipo Shangazi alikubali niondoke na mdogo wangu kuelekea mjini alipokua anaishi na familia yake.

Nilimfunga Neema mgogoni na kipande cha msuli wa marehemu babu na tulipofika stendi ya magari Shangazi aliniambia, “Sasa wewe mtoto naomba unisikie tena unisikilize haswaaaa!!! Huyo mtoto wa kuokota uliyengangania uende nae kwangu!! Mimi sina hela ya kumlisha hivyo basi sitaki nisikie unaniomba ela ya uji sijui maziwa!! Hilo kwangu hapana, Umenielewaaa!!??” Shangazi aliongea kwa hasira sana huku akimfinya Neema mashavuni na mimi akinibamiza kofi la shavuni.

Maskiniii!!! niliumia sana kuona maisha yetu yanabadilika na kuwa maisha ya kuteseka kwani enzi za uhai wa babu tulikua tukiishi kwa upendo na Amani licha ya kuwa na kipato cha chini lakini sasa nilienda kuanza maisha ya mateso na manyanyaso huku nikiwa na mtoto mdogo asiyejua kinachoendelea. Safari ya kuelekea mjini ilianza na tulipokua njiani Neema alianza kulia na kwa kuwa nilishamzoea mdogo wangu nilihisi itakua ni njaa, niliogopa sana kumwambia Shangazi kwani alishanionya nisimwambie habari zozote kuhusu Neema.

Kila dakika iliyosogea mbele Neema alizidi kulia kiasi cha kuwafanya abiria wote kuamka kwani alilia sana na niliposhika kichwa chake kilikua ni cha moto, Nilinyanyuka na kuomba abiria wanisikilize japo nipate msaada, nilisema, “Shikamooni wote, Mimi naitwa Joshua na huyu ni mdogo wangu anaitwa Neema tunasafiri kuelekea mjini na hatuna msaada wowote ule, Mdogo wangu analia kwasababu ya njaa kwani hajala tangu asubuhi na sasa ni saa 12 jioni, Baba na mama zangu naomba msaada japo mdogo wangu ale tu! Mimi nitavumilia”. Macho ya Shangazi yaliniangalia vibaya mno huku yakianza kubadilika na kuwa myekundu,

Kwakua sikusema tulikua tunasafiri na Shangazi yangu hivyo Shangazi alijifanya kama mtu mwema alinyanyuka na kunifata kisha alininongoneza akisema, “Wewe mtoto hunuji eeeh?? Yani unataka kunihaibisha mbele za watu sasa subiri uone, mlete huyo paka wako” Shangazi alionyesha tabasamu la kinafki na kunipokonya Neema huku akiwaambia abiria wale waliokua wakinisikiliza huku wakionyesha sura za huruma, “Msijali ndugu zangu nitamsaidia huyu mtoto, nimeguswa Sanaa na alichotuambia” Abiria wale hawakujua kilichokua kinaendelea hivyo walimpigia makofi shangazi na kumsifu kwa moyo wake wa huruma.

Neema alikunywa uji baada ya kupata msaada kwa mama mmoja aliyekua na mtoto mdogo umri sawa kidogo na Neema, Ilipofika usiku wa saa 4 nikiwa ndotoni niliota ndoto mbaya sana kwani niliota sauti ya shangazi ikiniambia “Joshua nisikilize vizuri huyu mtoto hana faida yoyote kwako ni mzigo tu! Giza litakapoingia nitakusaidia kumtupa nje ya basi hili bila mtu yoyote kujua, Sawaaa Joshuaaaaa!!!” Nilishtuka!! Na nilipojaribu kupapasa mapajani mwangu nilipokua nimemlaza Neema sikubahatika kumgusa huku nikiangalia alipokua amekaa shangazi yangu sikumuona,

Mapigo yangu ya moyo yalienda mbio sanaa……Nilisema moyoni mwangu, “Neema yupo wapi Mungu wangu, au shangazi kashamtupa dirishani? Maana hii ndoto si bureee!!” Niliendelea kumtafuta mdogo wangu na kwa bahati nzuri kumbe yule mama aliyenisidia uji wa mwanae nikamnywesha mdogo wangu (Neema) alimchukua ili acheze na mtoto wake. Niliporudi kuketi nilijikutta nikikalia kifuu kilichokua na maji ya moto, Ghafla nilinyanyuka na nilipojaribu kukitoa maji yale yalikauka mara moja huku kifuu kikipotea bila kuelewa nini kinaendelea.

Shangazi yangu alikua amelala huku akikoroma kama shetani na ghafla niliona vitu vya ajabu kama funza wa chooni wakimtoka shangazi puani, mdomoni na masikioni, Mungu wangu!!! Nilijisemea moyoni, “Shangazi mbona anatoa funza mwilini mwake? Ameoza au macho yangu hayaoni vizuri? Eeeh Mungu ni balaa gani tena hili?”

Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)