PETE YA MVUVI (3)

0

SEHEMU YA TATU
ILIPOISHIA...
Shangazi yangu alikua amelala huku akikoroma kama shetani na ghafla niliona vitu vya ajabu kama funza wa chooni wakimtoka shangazi puani, mdomoni na masikioni, Mungu wangu!!! Nilijisemea moyoni, “Shangazi mbona anatoa funza mwilini mwake? Ameoza au macho yangu hayaoni vizuri? Eeeh Mungu ni balaa gani tena hili?”

IKIWA UNASOMA SIMULIZI NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI USIPITWE NA SIMULIZI

ENDELEA...
Kwakua abiria wengi walikua wamelala pemebeni yangu nilikaa na mzee mmoja wa kitanga (Msambaa) nilishindwa kuvumilia kwani niliogopa sana na ndipo nilimuamsha mzee yule na alipoamka nilimuonyeshea maajabu yale, Mzee hakusema chochote aliangalia funza wale na kisha alicheka kidogo na kurudi usingizini. Nilizidi kupatwa na maswali juu ya hatma yangu na mdogo wangu pindi tufikapo mjini kwa shangazi,

Nikiwa nawaza ghafla nilipojaribu kumuangalia tena shangazi tulikutana macho kwa macho huku funza zile zikiwa zinarudi mwilini mwake, Nilipiga kelele kwa nguvu nikisema, “Jamaniii!! Eeeeeh!!! Nakufa mimi!!!” Abiria wa basi lile hawakuamka hata mmoja, kilichonishangaza zaidi hadi wale waliokua macho walipata usingizi wa ghafla na kulifanya basi lile kuwa kimya huku dereva wa basi lile akiwa anapiga miyayo ya usingizi na baada ya sekunde chache basi lile lilisimamishwa na dereva alilala.

Shangazi yangu alikua na nguvu kali sana za kichawi na niliamini hilo baada ya kuamua kuchukua watoto wote wa kwenye gari lile na kuondoka nao bila mtu yeyote kujua zaidi ya mimi na yeye tu!. Shangazi aliwachukua watoto wale akiwemo Neema na kuwakabidhi wachawi wenza waliokua wamalizunguka basi lile kama sadaka yake kwao, Niliishia nguvu ya kujaribu kumpokonya mdogo wangu na kila nilichokua naongea kilikua hakisikiki wala hakitoi sauti. Maskinii!! Shangazi alinichukulia mdogo wangu kipenzi pamoja na watoto wengine wa abiria wa basi lile bila kujua anaenda kuwafanyia nini yeye pamoja na wachawi wenzake…

Nilimkumbuka sana marehemu babu kwani alipenda kunisihi kila jaribu huja kwa maana yake na linaweza likaja kwa nia ya kukujenga au kukubomoa, hivyo niliichukilia hali ile kama sehemu ya maisha yangu ambayo niliamini Mungu ana makusudi yake ya mimi kupitia wakati ule mgumu. Asubuhi ilifika huku sauti za abiria wengi zikilalamika kuwa wamechoka sana huku wengi wao wakiumwa na viungo vya miili yao na uchovu ule ni kama walifanya kazi ya kulima usiku kucha,

Kumbe uchawi wa Shangazi uliowafanya walale ndio uliwachosha na kuwaumiza viungo vya miili yao. Mama mmoja aliyekua ameketi mwisho kabisa wa basi lile alianza kupiga kelele akisema, “Jamani dereva hebu simamisha gari tafadhali” Dereva alisimamisha gari na mama yule aliendelea kuongea, “Jamani abiria wenzangu nimepotelewa na watoto wangu mapacha wawili wa kike siwaoni, naomba mnirudishie watoto wangu” mama yule alianza kulia na baada kumaliza kuongea mama wengine waliokua na watoto pia walishtuka kwani hakukua na mtoto hata mmoja.

Mzozo wa kelele na vilio vya kina mama vilianza kwani watoto wote walipotea katika mazingira ya kutatanisha, Lakini mimi nilikua najua kila kitu ila sasa Shangazi alinitupia ububu wa muda hivyo sikuweza kuongea chochote ila nilitamani niseme ukweli kwani tukio lile nililiona na lilikua la kinyama sana kwani watoto wale akiwemo mdogo wangu (Neema) walifungashwa kwenye kiroba cha mkaa bila kujali kuwa wengine ni vichanga na wengine kidogo viungo vyao vimekomaa na kusafirishwa hadi makao makuu ya uchawi wao.

Yule mzee wa kitanga aliyekua ameketi pembeni yangu alihisi kuna kitu nafahamu juu ya kupotea kwa watoto wale kwani nilipomuamsha aone wale funza waliokua wakimtoka shangazi yangu puani, mdomoni na masikioni mzee yule aliona kama ni ndoto ivyo hakuitilia maanani lakini mzee yule alinisikia nikiongea na nikitaja jina la shangazi yangu hivyo alishangaa sana kuona nimekua bubu ghafla. Mzozo ukiwa unaendelea huku basi likiendelea na safari, Mzee yule alinipa kalamu na karatasi japo nimuandikie tukio zima lilivyokua kwa bahati mbaya nilishindwa kwani sikuwahi kwenda shule hivyo sikujua kuandika wala kusoma.

Wakati safari ikiendelea huku vilio na kelele zikishamiri, Ghafla!!! mbele ya kioo cha basi tulilokuwemo nyama za mikono, miguu, kichwa cha mtoto zikiwa zimekatwakatwa zilitupwa mbele ya basi letu huku damu zikiwa na maandishi yaliyosema, “BADO DAMU YA MTOTO MMOJA”. Dereva alisimamisha basi kwa haraka mno na abiria wote tulishuka kushuhudia tukio lile ndipo mama mmoja aligundua mtoto yule aliyekatwakatwa alikua ni mwanae kwani alikua na alama ya kuungua kwenye eneo kubwa la paja lake,

Vilio vilianza huku maombi ya kumkemea shetani yakishamiri kwa kasi ya hatari na nilipomuangalia Shangazi sikumuona eneo lile wakati abiria wote tulikua eneo lile. Yule mzee wa kitanga alitoa msaafu wake na kuomba apewe muda wa nusu saa afanye swala zake kisha tuendelee na safari, Abiria wote tulikubaliana nae na aliomba kisha tukaanza safari, Ilipofika mida ya saa 2 usiku nilianza kuogopa sana kwani mtoto niliyebaki kwenye basi lile ni mimi tu! Na ujumbe ule wa kishirikina ulitaka damu ya mtoto mmoja. Nikiwa nashangaa nje ghafla niliona shangazi akishushwa kwenye mbawa ya mnyama wa ajabu ambaye alifanania na mwewe mkubwaaa!! Na sekunde chache nilimuona Shangazi karejea kwenye siti yake huku akiniangalia kwa hasiraaa……

Nilishindwa kuendelea kumuangalia shangazi kwani sura yake ilitisha sana na alipojaribu kuinuka na kunifata alijikuta akiishia nguvu kwani Mzee wa kitanga alinipa kitabu kitakatifu (MSAAFU) nilioukumbatia kifuani mwangu. Nguvu zake za giza hazikuweza kunifikia kwani nilikua nikilindwa na nguvu za Mungu hivyo kutokana na kuishia nguvu, Shangazi alirudi kuketi kwenye siti yake akiwa na uchovu kwani nguvu za Mungu kupitia MSAAFU ulimfanya aishiwe nguvu zote.

Wakati tukio lile likitokea Mzee wa kitanga alikua amelala fofofo na abiria wengi pia walikua wameshalala hivyo tukio lile nililishuhudia peke yangu, Nilikumbuka kuna dawa babu alinipa inilinde na nguvu zozote za giza niliichukua dawa ile na kujipaka mikononi na kisha nilimfata shangazi na kumuuliza, “Shangazi naomba uniambie wale watoto umewapeleka wapi? Niambie haraka kabla sijatangaza ukweli wako mbele ya hawa abiria, Semaaa!! Neema na wenzake wapo wapi?”

Niliongea kwa hasira na ujasiri wa hali ya juu kwani dawa ile ilinibadilisha na kunifanya niwe na ujasiri wa kuzungumza chochote kile, Shangazi kwa kuwa aliishiwa nguvu hakuwa na msaada wowote na hivyo kuepuka aibu ile alinijibu, “Nenda msitu wa mashetani uliopo CHANIKA utamkuta Neema tena inabidi uwahi maana damu ya Neema imependwa na mizimu yetu na kabla jua kutoka watamfanya sadaka yao” Nilikosa cha kumjibu shangazi Zaidi ya kumwambia, “ Unasema nini!!! Neema anatolewa sadaka? Kwenye msitu wa mashetani uliopo CHANIKA? Sasa nisikilize wewe mwanga mguu wako mguu wangu mpaka huko msitu wa washenzi wenzako,nyanyuka twendeee!!”

Dawa ile niliopewa na babu ilinipa nguvu nyingi sana za kupambana na uchawi wowote ule hivyo nilimchukua shangazi na kupotea nae hadi tulipofika msituni pale. Niliona vitu vya ajabu sanaaa, kwani kulikua na vichwa vya watoto vikipikwa kama supu na huku miguu yao ikichomwa kama nyama choma. Mungu wangu!!! Kwa mbali nilimuona mdogo wangu Neema akiwa anapakwa unga mweupe akiwa uchi wa mnyama wakimwandaa kwajili ya kumtoa sadaka,

kwa nguvu ya ile dawa niliyojipaka nilikimbia kwa haraka sana mpaka pale alipokua Neema na nilimnyanyua bila wachawi wale kuona ni nani au nini kimemnyakua mtoto yule. Tukiwa njiani kurudi kwenye basi lile tulihisi harufu ya damu za binadamu zilizomwagika muda si mrefu, Kumbe tulipofika msituni pale nikiwa na shangazi, Shangazi aliweza kunitoroka bila mimi kujua na kumfata mkuu wa kikosi kile cha wachawi na kumuelezea ukweli wote na ndipo mkuu yule aliondoka haraka kuelekea kwenye basi lile ambapo alilisababishia ajali na abiria wote akiwemo Mzee wa kitanga walifariki.

Tulifika eneo lile la ajali mimi nikiwa sijui lolote lile nilibahatika kumuona mzee wa kitanga akikaribia kukata roho na ndipo aliniambia maneno machache, “Kijana Mungu akulinde, chukua MSAAFU huu uwe kiongozi wako” Mzee yule alikata roho papo hapo. Niliamini ni ajali ya kawaida, hivyo nilimchukua mdogo wangu (Neema) na kuanza nae safari ya kutafuta usafiri wa kurudi kijijini kwetu “Luvile”.

Kabla ya kuondoka nilimwambia shangazi, “Naomba sana ukae mbali na maisha yetu tena usijaribu kutufata na nguvu zako za kichawi kwani umeona jinsi gani nguvu za Mungu zinaweza kuzishinda nguvu za giza, na kwa kuwa nakupenda Shangazi yangu naomba uache tabia ya uchawi na umrudie Mungu wako, Kwaheri Shangazi sisi tunarudi kijijini kuendeleza biashara (UVUVI WA SAMAKI) ya marehemu babu yetu”…

Safari ya kurudi kijijini haikuwa ngumu kwani tulipata bahati ya kupanda gari la mizigo lililokua lilikisafirisha mahindi na maharage hadi kijijini kwetu. Safari ile ilichukua muda wa siku tatu mpaka kufika Luvile kwani gari lile lilipatwa na itilafu za kiufundi hivyo tulifika kijijini pale ikiwa ni mishale ya saa 4 usiku nikiwa na Neema aliyekua begani amelala fofofo!!. Niliangalia huku na kule japo nipate sehemu ya kujilaza mimi na mdogo wangu mpaka itakapokuwa ikikaribia asubuhi ndio tuanze safari ya kuelekea nyumbani kwani kwa muda ule na umbali wake nilishindwa kuvumilia kwani nilikua na mdogo wangu begani ambaye uzito wake pia ulichangia mimi kukosa nguvu za kutembea mpaka nyumbani.

Kwa bahati nzuri nilibahatika kuona nyasi zilizokua zimetengenezwa kama kiota cha ndege na bila kujiuliza mara mbili nilijitupa kwenye nyasi zile huku mdogo wangu nikimlaza pembeni kidogo na mimi, Usingizi ulinoga sana kwani nyasi zile hazikua zikiwasha wala kuchoma na hivyo sikuweza kuwaza chochote zaidi ya kulala tu, Nilishtuka usingizini kwani kiu cha maji kilikua kimenibana huku Neema nae akishtuka kwajili ya maji,

Hivyo nilitoka kwenye kile kiota na kuanza kutembea huku na kule nikitafuta maji ya kunywa ila kabla ya kuondoka nilimfunika mdogo wangu na zile nyasi ili nimlinde na wadudu wakali wasije kumshambulia, Kumbe kiota kile kilikua ni cha nyoka aina ya kobra na hivyo baadhi ya wanakijiji walikua wameshamchoka nyoka yule mwenye sumu kali kwani alishaua watoto zaidi ya watatu ndani ya wiki moja hivyo nilipokua kuwa nikitembea kutafuta maji nilipishana na kundi lile wa wanakijiji wenye hasira za kumuua nyoka yule akiwa kwenye kiota chake, Mimi sikufahamu chochote hivyo niliendelea na kazi yangu ya kutafuta maji ya kunywa nimpelekee Neema niliyemuacha kwenye kiota na yatakayobaki ninywe mimi.

Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)