Mtunzi: ___
SEHEMU YA KUMI NA MBILI
TULIPOISHIA...
TULIPOISHIA...
Proper alisikitika kukosa fursa na kuzungumza na Unono ili kujua yote anayofahamu juu yake na wapi alikopata picha ambayo Neema aliizungumzia wakati alipomhoji baada ya kumlewesha kwa dawa zake.
IKIWA UNASOMA SIMULIZI NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI USIPITWE NA SIMULIZI
TUENDELEE...
Aliamua kummalizia Neema, baada ya kuona kuwa hakujua lolote lingine la haja. Ndiyo akamnywesha sumu ile maalumu ambayo ilikusudiwa kumuua Neema kwa utulivu, baada ya muda fulani. Kisha alimfuata kwa hila hadi hapa ambapo alijificha katika uchochoro akimsubiri Unono. Alifanikiwa kumwona wakati anaingia ndani na alivyotoka mbio. Kabla hajaanza kumfuata, ilitokea gari na kumgonga kwa bahati mbaya.
Proper alifanikiwa kujisokomeza katikati ya umati wa watu waliojaa hapo barabarani. Akiwa kajibadili kimavazi na kitabia, hakuwa yule profesa Kimara tena, bali mmoja wa watu kadhaa wa mkitaani na hakuna yeyote ambaye angeweza kumshuku. Hivyo hakuna aliyemwona akiinama na kuokota mkoba wa marehemu na kwenda kando ambako aliufungua na kupekuwa ndani. Ndani ya mkoba huo hakukuwa na chochote alichohitaji. Aliutupa mkoba huo chini na kupishana na watu waliokuwa wakielekea kwenye tukio hilo la ajali, akaelekea nyumbani kwa Neema.
Hakuna aliyemwona akiingia. Alisimama kando ya kitanda akitabasamu kwa ‘uzuri’ wa kazi yake. Neema alikuwa amekufa kwa namna aliyotaka. Yeyote ambaye angeingia na kumtazama haraka haraka angedhani yuko usingizini. Hata hivyo Proper hakuridhika kikamilifu. Akambeba na kumlaza juu ya kitanda na kumfunika kwa shuka hadi usoni. Kisha akafanya msako wa haraka haraka. Alikuwa akiitafuta ile picha aliyosema Neema. Hakuiona. Akalazimika kuondoka
Mlangoni alikutana na jirani mmoja wa Neema ambaye alimtazama kwa macho ya kuuliza japo hakuuliza chochote.
“Nilikuwa mgeni wa huyu dada lakini naona amelala”, Proper alieleza.
“Amelala?” jirani huyo alihoji akijaribu kuchungulia ndani. alipoona mwili wa Neema umetulia kitandani aliamini. “Naona tumwache alale. Shoga yetu lapatwa na msiba mkubwa”.
Akiufahamu umbeya wa wanawake wa Dar es Salaam, Proper hakusubiri kumsikiliza. Alifanya haraka kurejea nyumbani kwake ambako aliendelea kuandaa mpango wake. Kisha akaipitia tena taarifa yake ambayo alikwisha iandaa kwa ajili ya kuipeperusha nje. Aliirekebisha taarifa hiyo hapa na pale, kisha akavuta mtambo wake wa kupeperusha habari na kuufungua. Kisha aliufunga na kusubiri muda wa majibu. Aliyahofia majibu hayo lakini hakujali. Maadamu alikuwa kadhamiria. Lolote lisingemfanya ashindwe kuutekeleza.
Kidogo hofu ilikuwa ikimwingia kwa kufikiri wapi yule marehemu aliyegongwa na gari aliipata picha yake na vipi picha hiyo isipatikane ingawa alikuwa ameitafuta kwa umakini. Kuna jambo la kutisha linamnyemelea? Wapi? alijiuliza.
Hakuna vipi angeweza kuacha mwanya wa kupatikana kwa urahisi. Mambo mengi ama yote aliyotaka yafanyike kikamilifu alikuwa akiyafanya mwenyewe, japo alikuwa na watu wengi chini yake ambao wanalipwa vyema na wamekamilika kimauaji. Wote hao yeye anawafahamu lakini hakuna yeyote anayemfahamu. Yeyote anayedhani kuwa anamfahamu basi alikuwa akijidanganya kwani Proper unayeongea naye leo si Proper wa kesho. Kadhalika vifo vyote vilivyotokea alivitekeleza mwenyewe kiufundi zaidi ya alivyofundishwa. Alimuua Waridi kikatili, ili polisi waamini kuwa ni mwendawazimu mwingine ambaye anaipenda sana kazi ya kuua watu wasiokuwa na hatia. Joram amekufa kwa bomu, Neema alikuwa msiri wa Joram! Yeyote aliyemuua Joram asingesita kumuua Neema. Zaidi, Neema kafa kwa sumu ile ile iliyokusudiwa kumuua Joram. Katika hali kama hiyo, nani angefanya nini kumtia hatiani kwa urahisi? Polisi? Wao wasingeenda mbali na ukweli. Joram aliyekuwa na uwezo wa kunusa chochote sasa yuko kuzimu.
Hata hivyo Proper alihisi kama uovu fulani uliojificha kando ukimnyemelea. Kama angeipata ile picha… Kama yule mwanamke asingepatwa na ajali… angeweza kujisikia salama zaidi. Aliifukuza hofu kwa kujiliza kwa moja ya sigara zake kali, ambazo huzivuta kwa nadra sana. Kisha akaitazama saa yake. Alipoona imepungua dakika moja ili kupata majibu yataarifa yake, aliubonyeza mtambo wake. Karatasi yenye maandishi ikajitokeza. Akaichukua na kuanza kuisoma.
…Utapewa majibu rasmi kesho muda kama huu… taarifa hiyo ilieleza, akaisoma tena kisha akaichana, mabaki akayatia katika mtambo mwingine wa kusaga karatasi hata ikawa kama majivu.
Hakujua jibu rasmi litakuwa lipi na lilimhusu vipi. Alichotuma yeye halikuwa swali wala ombi. Ilikuwa taarifa ambayo watake wasitake ingefanyika. “Wapuuzi”, aliwaza. Akawatoa akilini na kuanza kuandaa mkutano mwingine baina yake na washirika wake. Washirika ambao kiasi fulani hawakuwa zaidi ya mateka wake.
Mkutano huo wa siri ulifanyika chini ya Uenyekiti wa Proper. Bado alifanya mpango wake kuwa siri, alijificha nyuma ya taa kali za umeme kwa namna ambayo iliwafanya washirika wake wasimuone vizuri japokuwa walikuwa na matarajio ya kazi.
Mkutano huu kama ulivyokuwa wa awali, ulikuwa umeitishwa kwa namna ya hadhari na siri, jambo ambalo liliwaongezea mashaka baadhi ya wajumbe. Kila mmoja alijikuta akiwa mkutanoni bila kutarajia wala hiari.
Huyo alikuwa akipita zake mitaani, kaiacha pale gari na dereva wake. Mara kashikwa mkono na mtu aliyekuwa akipita ghafla. Alipoutazama mkono wake aliona kadi ndogo yenye maandishi yasemayo ‘BAADA YA NUSU SAA… NJOO PALE KWA SIRI… ONYESHA KADI HII MLANGONI’. Akijua maana ya kadi hiyo, mtu huyo alimruhusu dereva wake kuondoka. Kisha akatembea kuelekea nyumba hiyo ambayo nje ilionekana kuwa nyumba ya kawaida lakini kwa ndani ilikuwa nyumba ya aina yake. Mlangoni kila aliyetoa kadi aliruhusiwa kuingia katika chumba ambacho kilikuwa na lifti iliyowasafirisha kwenda chini ambako walipitishwa vyumba kadhaa hadi kwenye chumba cha mkutano.
Mwingine alikuwa kastarehe na mkewe nyumbani kwake. Alipoinuka kwenda maliwatoni aliuona mkono wa mtu ukiingia kupitia dirishani ukiwa umeshika kadi iliyosomeka. ‘BAADA YA NUSU SAA… Aliipokea na kumuaga mkewe haraka kuwa anarudi kazini. Lakini nje aligeuza safari na kuelekea kwenye kikao cha Proper. Mwingine alikuwa kazini. Simu ilipigwa ghafla ikimwarifu kuwa ana mgeni alimsubiri kwenye mghahawa mtaa wa pili. ‘Mgeni’ huyo alimkabidhi kadi yake iliyomtaka kufika haraka kwenye kikao, ambapo sasa wajumbe wote walikuwa wamefika wakimsubiri Mwenyekiti afungue mkutano.
“Tungeanza kwa kukumbushana kuwa Joram ambaye tulimuona kama tishio kwetu sasa ni marehemu. Yuko kuzimu. Hiyo ni habari njema. Au?”, alihoji.
“Nadhani ni habari njema”, mmoja wa wajumbe alijibu, “Igawa kifo chake hakikuwa kizuri sana . Watu wanashuku kuwa pengine alipewa sumu. Nadhani bado wanaendelea na uchunguzi wa kifo chake”.
“Wanajisumbua, hakuna watakalogundua kuhusu kifo cha Joram”, Mwenyekiti aliwajibu. Kisha alicheka kidogo na kusema, “Pia napenda kutumia fursa hii kuwafahamisha kuwa Joram hakufa kwa sumu. Walipanga hila ili watulaghai tu baada ya kunusurika kwake. Nililazimika kumteketeza kwa bomu”.
Hii ilikuwa taarifa ngeni kwa wajumbe. “Si lazima watazidisha mashaka? Nazungumzia polisi. Walipoona amepona kufa kwa sumu na hatimaye kuuawa kwa bomu nadhani watakuwa macho sana, wakipeleleza kwa makini zaidi hadi…” akasita kidogo baada ya kuona ameongea muda mrefu zaidi ya anavyotakiwa kuongea.
“Hadi nini?”, Mwenyekiti alihoji. “Hakuna lolote watakalogundua. Watakuwa wakibabaika tu kama mfamaji asiye na msaada wowote. Hawatafahamu iwapo ubaya utatoka mashariki au magharibi. Hawatajua ni kitu gani kinatokea. Watakapofahamu, mambo yatakuwa yamekamilika. Watakachofanya ni kuteremsha bendera zote nusu mlingoti na kuanza maomboleza ambayo hayajawahi kutokea katika historia ya dunia.
Wajumbe waliduwaa. Mioyo yao ikadunda kwa hofu. Ingawaje walikuwepo mkutanoni kama washiriki kamili katika njama hii, lakini hawakuelewa barabara kilichokusudiwa. Tamaa ya pesa nyingi zaidi, madaraka makubwa zaidi, ndio sababu zilizowafanya wakubali kushiriki katika mkutano huo wa siri. Lakini hayo hayakuwafanya watokwe na mashaka. Hawakujua kama mambo yalikuwa heri kama alivyodai Mwenyekiti wao au shari kama miayo yao ilivyokuwa ikinong’ona. Hasa mashaka hayo yalitokana na kuteuliwa kwao. Hakuna mjumbe aliyefahamu wajibu wake. Hakuna aliyekuwa na fununu sababu ya kuteuliwa kuhusika katika mkutano huo. Ni kweli kwamba wajumbe hao walikuwa watu wenye nafasi nyeti katika chama na serikali. Ni kweli pia wote walikuwa pamoja kwa nafsi zao: wote wangependa cheo zaidi na pesa. Lakini umoja huo haukuwafanya washindwe kujiuliza vipi mtu huyu anayejificha nyuma ya mwanga, mbele yao aliwezaje kuisoma mioyo yao, hata akawateua katika jumuia hii. Vipi aliweza, japo katika nchi na ulimwengu mzima? Watu wenye njaa kama zao ni wengi mno, endapo si wengi. Sheria na katiba zisingekuwepo, kulinda haki na usawa, ingethihirika ni jinsi gani wengi walivyo na tamaa ya madaraka na kiu ya kupata pesa.
Ingawa kuna sheria zinazotisha, pamoja na katiba zinazoadili, wengi huzikiuka kwa siri na kulinda nafasi ya kufanya mengi kinyume cha mwelekeo. Wako wachache walio ‘jaaliwa’ wakafaulu kufanya mengi kwa siri wakati wao ndio wanaongoza kulinda katiba na sheria za nchi. Baadhi ya watu hao ni hawa ambao sasa hivi walikuwa mbele ya Proper wakimsikiliza kwa hofu. Walikuwa na mengi ambayo waliamini ni siri zao binafsi, ambayo hawakupenda jamii ifahamu. Hata hivyo tamaa yao haikuwa kubwa kiasi cha kuwafanya wafurahie jambo la kutisha wasilolifahamu eti kwa ahadi ya pesa na vyeo zaidi.
“Unakusudia kufanya nini?”, mmoja wa wajumbe alifoka ghafla.
“Ndiyo… Tufahamishe ni jambo gani unataka kufanya?”, mwingine alidakia na kuuliza.
Proper kama mtu aliyekuwa akiyasoma mawazo yao kitambo, alicheka kidogo, kisha akawaambia. “Sikilizeni. Kazi iliyo mbele yenu ni ndogo kuliko kazi zote mlizowahi kufanya… Hamna haja ya kuwa na hofu yoyote”.
Alipoona wametulia kumsikiliza aliendelea, “Nimepata fununu kuwa hivi karibuni utafanyika mkutano wa viongozi kutoka nchi mbalimbali za Afrika wanaojiita wenye msimamo wa kimapinduzi wamealikwa pia. Nitakachohitaji kwenu ni ratiba kamili ya mkutano huo, wapi kiongozi fulani analala, wapi anakula, jumba lipi wanakutana na kadhalika. Nataka taarifa kamili, ya siri, si ile ambayo hutangazwa katika magazeti yanayouzwa mitaani. Kulingana na nafasi zenu najua kazi hiyo ni ndogo mno. Kitakachofauata niachieni mimi.
“Nini kitafuata?”, mjumbe mmoja aliropoka kwa shauku.
Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
JIUNGE KWA UPDATE NA BURUDANI ZAIDI
WhatsApp Channel=> CnZ Media(Follow)
Telegram Channel=> CnZ Media(Join)