Mtunzi: Aziz Hashim
SEHEMU YA NNE
TULIPOISHIA...
TULIPOISHIA...
Edmund akatii alichoambiwa ambapo katika hali ambayo hakuitegemea, msichana huyo mrembo kupindukia alimkumbatia kwa nguvu kifuani huku akipumua kwa fujo mithili ya mtu aliyetoka kukimbia mbio za marathon, ngozi yake laini iliyokuwa na joto la huba vikazidi kumchanganya Edmund.
IKIWA UNASOMA SIMULIZI NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI USIPITWE NA SIMULIZI
TUENDELEE...
“Nakupenda sana Edmund, hata sijielewi mwenzio, nimejikuta nakupenda tu ghafla wakati siyo kawaida yangu,” alisema Samantha kwa sauti ya kudeka, akaanza kumwagia mvua ya mabusu sehemu mbalimbali za mwili wake.
Ni kama Edmund alikuwa akiusubiri kwa hamu muda huo kwani hakutaka kulaza damu, naye akawa anamuonesha ushirikiano mkubwa msichana huyo, wakagandana kama ruba huku mapigo ya moyo ya kila mmoja yakizidi kuongezeka kadiri muda ulivyokuwa unazidi kusonga mbele, miguno ya raha ikawa inasikika kutoka kwa kila mmoja.
Waliendelea kupasha miili yao tayari kwa mechi ya kirafiki isiyo na refa wala jezi, huku mara kwa mara msichana huyo akirudia kumuomba radhi Edmund kwa kilichotokea asubuhi ya siku hiyo kwa sauti yenye uwezo wa kumtoa nyoka pangoni, kufumba na kufumbua wakajikuta wote wakiwa kama walivyoletwa duniani.
“Unazijua love bites?” Samantha alimuuliza Edmund kwa sauti ya chini mno huku akiendelea kumfanyia vituko vya hapa na pale, akawa anatingisha kichwa kuonesha kukubali kwani japokuwa hakuwa mzoefu sana kwenye ulimwengu wa mapenzi, Edmund alikuwa akijua baadhi ya vitu.
“Naomba unitoe hapa,” alisema Samantha huku akimuoneshea Edmund shingo yake, kijana wa watu akatii, naye akamng’ang’ania Edmund shingoni, kazi hiyo ikaanza.
Hata hivyo, tofauti na Edmund alivyokuwa anafahamu, Samantha alikuwa akilifanya zoezi hilo kwa nguvu kiasi cha kumfanya Edmund aanze kuhisi maumivu makali kwenye shingo yake lakini akawa anajikaza kwani alikuwa na uhakika kuwa muda mfupi baadaye wataingia ‘msambweni’ , jambo alilokuwa analisubiri kwa hamu kwani mpaka muda huo hakuwa akijielewa tena.
Kufumbana kufumbua, Samantha alikurupuka kama mtu aliyezinduka usingizini, akajitoa kwenye kifua cha Edmund, kwa kasi ya ajabu akasimama huku mapigo ya moyo wake yakimuenda mbio kuliko kawaida. Akaanza kutafuta nguo zake ambazo kila moja ilikuwa imeangukia upande wake.
“Vipi tena?” Edmund aliuliza kwa mshangao lakini Samantha hakumjibu kitu, akaendelea kuvaa nguo zake na muda mfupi baadaye, tayari alikuwa amemaliza, akawa anataka kuondoka.
Kwa kuwa tayari Edmund alikuwa kwenye hali mbaya, hakutaka kukubali kirahisi Samantha aondoke na kumuacha kwenye hali ile kwani kile alichokuwa anakisubiri kwa hamu hakikuwa kimekamilika.
Akajaribu kumzuia huku akitaka kujua ni jambo gani limetokea mpaka Samantha abadilike ghafla kiasi kile lakini tayari alikuwa amechelewa, Samantha alitoka mbiombio mpaka nje alikopaki gari lake la kifahari. Wakati Edmund akihangaika kutafuta nguo zake ili amuwahi kabla hajaondoka, alisikia muungurumo wa gari la kifahari la msichana huyo likiondoka kwa kasi eneo hilo, akabaki amepigwa na butwaa, akiwa haelewi kabisa kilichotokea.
Ni hapo ndipo alipoanza kuhisi maumivu makali kwenye shingo yake, alipopeleka mkono wake pale alipotolewa ‘love bite’ na Samantha, hakuyaamini macho yake baada ya kugundua kuwa palikuwa na kidonda huku damu zikianza kumchuruzika kwa wingi.
“Mungu wangu, hiki nini tena?” alisema Edmund huku akisogea kwenye kioo kikubwa kujiangalia.
Alipojiangalia shingoni, mahali alipotolewa ‘love bite’ na Samantha, alishtuka kugundua kuwa kumbe msichana huyo alikuwa amemng’ata na kumtoa kidonda kikubwa kilichokuwa kikiendelea kutoka damu kwa wingi.
Harakaharaka alikimbilia kwenye kabati na kutoa kiboksi kidogo cha huduma ya kwanza, akatoa pamba na ‘spirit’ na kurudi kwenye kioo, akawa anajisafisha huku akiwa ameuma meno kutokana na maumivu makali aliyokuwa anayasikia.
Kidogo ‘spirit’ ilimsaidia kupunguza kuvuja kwa damu ingawa maumivu yaliendelea kuwa makali kadiri muda ulivyokuwa unasonga mbele. Akakata kipande kikubwa cha pamba na kukiweka juu ya kidonda hicho huku akiendelea kuugulia maumivu, akameza vidonge vya kupunguza maumivu huku akiendelea kujiuliza maswali yaliyokosa majibu.
Aliporudi kitandani, aligundua kuwa shuka safi alilolitoa muda mfupi uliopita, lilikuwa limeingia madoa makubwa kutokana na damu iliyokuwa inamvuja, akapata kazi nyingine ya kuanza kubadilisha mashuka. Kila kilichokuwa kinaendelea, alikifananisha na ndoto ya kutisha, akawa anatamani ndoto hiyo ifike mwisho haraka lakini haikuwa hivyo.
Muda mfupi baadaye, pamba aliyokuwa amejiweka juu ya jeraha lake, ilikuwa imelowa damu chapachapa, ikabidi aitoe na kukata nyingine, akaiweka huku bado akiwa haamini kilichokuwa kinatokea.
“Kwani Samantha ni nani hasa? Kwa nini ameniumiza hivi na kukimbia? Kosa langu kwake ni lipi? Ina maana haya ndiyo malipo ya wema wangu kwake?” Edmund aliendelea kujiuliza huku akifuta damu iliyochafua vitu mbalimbali ndani ya chumba chake.
Alitoka mpaka nje na kupatazama pale msichana huyo alipokuwa amepaki gari lake. Hakuwepo wala hapakuwa na dalili zozote za uwepo wake, akarudi ndani na kufunga mlango mkubwa wa nje, akachukua simu yake na kujaribu kumpigia Samantha, mara simu ikaanza kuita.
“Haloo!” Haloo! Samantha! Samantha!” Edmund aliita baada ya simu kupokelewa lakini hakuitikiwa, akaendelea kuita lakini hakusikia majibu yoyote, akakata simu na kujaribu kupiga tena.
“Namba ya simu unayopiga haipatikani kwa sasa, tafadhali jaribu tena baadaye,” sauti ilisikika kwenye simu yake ikimaanisha kwamba simu ya Samantha imezimwa. Akazidi kujikuta kwenye wakati mgumu.
Alipotazama saa ya ukutani, aligundua kuwa tayari ilishatimia saa sita za usiku. Kwa kuwa muda ulikuwa umeenda sana, hakuwa na cha kufanya zaidi ya kwenda kulala, huku akiendelea kuugulia maumivu makali.
***
“Mbona umechelewa kurudi? Ulikuwa wapi?”
“Kuna sehemu nilikuwa nimepitia.”
“Ndiyo uchelewe mpaka muda huu?”
“Nilikuwa nafanya kazi ya muhimu baba.”
“Kazi gani ya muhimu? Hivi siku hizi umekumbwa na nini wewe mtoto? Majukumu ninayokupa hutimizi kila siku visingizo.”
“Baba! Hivi unafikiri hizo kazi zako unazonipa ni rahisi sana, si ndiyo? Kwanza kwa taarifa yako mimi nimechoka, sitaki kuendelea kuwa mtumwa?” Samantha alisema kwa sauti ya juu wakati akijibizana na baba yake.
“Unasemaje? Hebu rudia tena?”
“Jamani kwani kuna nini tena?” mama yake Samantha aliingilia ugomvi huo kati ya baba na mwanaye, Samantha alipomuona mama yake akamkimbilia na kumkumbatia huku akiendelea kulia.
“Kwani kuna nini mwanangu?”
“Eti baba ananifokea kisa nimechelewa kurudi wakati nilikuwa kufanya kazi aliyonipa mwenyewe, kwanza mama mimi nimechoka kuendelea kuwa mtumwa, sitaki,” alisema Samantha huku akijitoa kwenye mikono ya mama yake, akakimbilia ndani na kuwaacha wazazi wake wakitazamana.
“Na wewe mume wangu, kwa nini unamfokea Samantha? Unafikiri huyo bado ni mtoto mdogo?”
“Amekuwa jeuri sana siku hizi, kazi hafanyi kama ninavyomuelekeza kila siku visingizio kibao, na leo umemsikia mwenyewe anasema amechoka. Sasa unafikiri itakuwaje?”
“Huenda ameongea kwa hasira tu mume wangu, tumuache atulie kwanza,” alisema mama yake Samantha, akamuita dereva wao na kumuamuru alipaki vizuri gari alilokuja nalo Samantha, harakaharaka dereva huyo akatii alichoambiwa, akaliingiza gari hilo kwenye maegesho kulikokuwa na magari mengine ya kifahari.
“Nisamehe Edmund! Nisamehe jamani, halikuwa kusudi langu kukufanyia hivyo, naomba sana unisamehe kwani hukustahili kulipwa ubaya,“ alisema Samantha huku akilia kwa uchungu, akiwa amejifungia chumbani kwake.
Hakukumbuka hata kubadilisha nguo, akawa anajigalagaza kitandani huku akiwa amekumbatia mto wake, machozi mengi yakiendelea kumtoka. Alikuwa anajua ni jambo gani litakalomtokea Edmund, akawa anajisikia vibaya mno ndani ya moyo wake. Hiyo haikuwa mara yake ya kwanza kufanya kazi hiyo lakini hata yeye alijishangaa kumuona huruma Edmund kiasi hicho, akawa anaendelea kulia kwa kwikwi.
***
Muda ulizidi kuyoyoma, Edmund akiendelea kuugulia maumivu makali mno. Usingizi ulimpaa kabisa, kwa mbali akaanza kuhisi mwili wake ukimchemka kuashiria kwamba tayari alishapata homa.
Kadiri muda ulivyokuwa unazidi kusonga mbele ndivyo homa hiyo ilivyokuwa inazidi kuwa kali, akawa anatetemeka kama mtu aliyemwagiwa maji ya baridi. Mpaka inafika alfajiri, Edmund alikuwa hoi mithili ya mtu aliyeugua kwa muda wa wiki nzima mfululizo.
Kwa kuwa alikuwa anaishi peke yake, alijua endapo akiendelea kujilegeza, anaweza kufia chumbani humo bila msaada, akajikongoja na kuamka mpaka mlangoni, akafanikiwa kufungua mlango lakini kabla hajatoka nje, alianza kutapika mfululizo mpaka akaishiwa nguvu. Kilichozidi kumtia hofu, ni pale alipogundua kuwa kumbe alikuwa anatapika damu.
Akajikongoja mpaka kwenye mlango wa chumba cha jirani, akamgongea mpangaji mwenzake aliyeamka haraka kutaka kujua kulikoni agongewe mlango alfajiri hiyo.
“Edmund?!!” aliita jirani huyo huku akionesha kushtushwa mno na hali aliyokuwa nayo kijana huyo.
“Ni...sa..idie na...ku...” Edmund alishindwa kumalizia kauli yake, akaanza tena kutapika damu mfululizo na muda mfupi baadaye, akadondoka chini kama mzigo, puuh!
Akapoteza fahamu, jambo lililosababisha jirani yake arudi ndani haraka kubadilisha nguo kwani alikuwa amejifunga taulo tu, akatoka na kuanza kuwaamsha majirani wengine kwa lengo la kumsaidia Edmund ambaye mpaka muda huo hakuwa na fahamu.
“Kwani kumetokea nini?” baba mwenye nyumba aliuliza lakini hakuna aliyekuwa na majibu.
“Amekuja kunigongea mlango, nilipotoka nimemkuta kwenye hali mbaya mno akitapika damu na muda mfupi baadaye ndiyo akadondoka na kupoteza fahamu,” alisema yule jirani aliyekuwa wa kwanza kumuona Edmund.
“Kwa hiyo tufanye nini jamani?”
“Tumkimbize hospitali, hali yake inaonesha siyo nzuri kabisa, anaweza kupoteza maisha huku tukishuhudia,” baba mwenye nyumba na wapangaji wake walikubaliana, alfajiri hiyohiyo pilikapilika zikaanza.
Kwa kuwa kulikuwa na mpangaji aliyekuwa akifanya kazi ya udereva wa teksi na alikuwa akilala na gari la bosi wake hapohapo nyumbani, ilibidi teksi hiyo ndiyo itumike.
Wakasaidiana kumbeba Edmund na kumpakiza kwenye teksi hiyo, muda mfupi baadaye, tayari walishaondoka, dereva akawa anajitahidi kukanyaga mafuta kwa kasi ili kumuwahisha hospitalini.
Kwa bahati nzuri, alfajiri hiyo hakukuwa na foleni, dakika kadhaa baadaye wakawa tayari wameshawasili kwenye Hospitali ya Mwananyamala, akapokelewa na wahudumu waliokuwa zamu na kumlaza juu ya kitanda chenye magurudumu,
Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
JIUNGE KWA UPDATE NA BURUDANI ZAIDI
WhatsApp Channel=> CnZ Media(Follow)
Telegram Channel=> CnZ Media(Join)