Mtunzi: Aziz Hashim
SEHEMU YA ISHIRINI NA SABA
TULIPOISHIA...
TULIPOISHIA...
Hatimaye meneja mkuu aliwasili ambapo alimkuta Edmund akiendelea kufurahi na wafanyakazi wenzake,
IKIWA UNASOMA SIMULIZI NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI USIPITWE NA SIMULIZI
TUENDELEE...
akamchukua mpaka ofisini kwake ambapo alianza kuzungumza naye. Alimuonya kuhusu tabia yake ya kukaa nyumbani bila kutoa taarifa yoyote ofisini na kumtaka asirudie tena tabia hiyo.
Edmund alikiri makosa yake na kuomba asamehewe, meneja huyo akamwambia akaendelee na kazi wakati wakimsubiri mkurugenzi mkuu ambaye kimsingi ndiye aliyeagiza aitwe haraka iwezekanavyo.
Saa tatu asubuhi juu ya alama, Edmund aliitwa kwenye ofisi ya mkurugenzi wa kampuni hiyo, alipoingia akashtuka kugundua kuwa karibu viongozi wote wakubwa wa kampuni walikuwepo, kuanzia mkurugenzi, meneja mkuu, mhasibu mkuu na maafisa wengine kadhaa.
Meneja ndiye aliyevunja ukimya na kumueleza Edmund kwamba mkurugenzi alikuwa akihitaji kuzungumza naye, akakaribishwa ambapo alianza kumpa pole kwa matatizo yaliyomtokea lakini akamsisitiza tena kuacha tabia ya kukaa tu nyumbani bila kutoa taarifa.
“Kikubwa nilichokuitia, kwa kipindikirefu tangu ulipoajiriwa, nimekuwa nikifuatilia kwa ukaribu mwenendo wako wa kazi na kimsingi nimeridhishwa na juhudi na maarifa ambayo unayaonesha ili kuhakikisha kampuni inasonga mbele.
“Tumefikiria kufungua tawi letu jingine jijini Arusha na mambo yote ya kimsingi yameshakamilika. Kampuni imekuteua wewe kwenda kuwa meneja mkuu wa tawi la Arusha ambapo utakuwa ukiripoti moja kwa moja kwangu.
“Maslahi yako yameboreshwa sana ikiwemo kuongezwa mshahara, kutafutiwa nyumba ya kuishi na gari la kukuwezesha kufanya kazi zako vizuri. Meneja mkuu atakupa maelekezo zaidi ya namna ya kupata vitu vyote nilivyovitaja na jinsi utakavyoenda kuanza kazi.
“Kabla sijahitimisha, unachochote cha kuzungumza?” alihoji mkurugenzi na kumfanya Edmund ashindwe kuzizuia hisia zake, machozi ya furaha yakawa yanamtoka ambapo aliushukuru uongozi kwa kumuamini na kuahidi kwamba atafanya kazi kwa bidii kuhakikisha tawi jipya la Arusha linachanua kwa kasi.
Baada ya hapo, mkurugenzi alifunga kikao hicho na kumpa mkono wa pongezi Edmund, akifuatiwa na viongozi wengine ambapo walipotoka, walielekea kwenye ofisi ya meneja mkuu ambaye alianza kumpa maelezo ya nini anachotakiwa kufanya akifika Arusha.
Akamkabidhi barua mpya ya kupandishwa cheo na kuongezwa mshahara, akaambiwa akajiandae mpaka asubuhi ya siku inayofuata ambapo angesafiri na meneja huyo mpaka jijini Arusha kwa ajili ya kwenda kumkabidhi ofisi rasmi. Hakuna siku ambayo Edmund alikuwa na furaha kama siku hiyo, akawa anamshukuru Mungu wake kwa miujiza aliyomtendea.
Kesho yake asubuhi, Edmund na meneja mkuu walisafiri mpaka jijini Arusha ambapo Edmund alienda kukabidhiwa rasmi ofisi mpya za Hashcom Mobile, akatambulishwa kwa wafanyakazi kuwa ndiyo meneja mkuu wa ofisi hizo. Kiumri, Edmund alikuwa bado mdogo ukilinganisha na madaraka aliyokabidhiwa lakini mwenyewe hakuogopa chochote kwa sababu alikuwa akiuamini utendaji kazi wake. Ofisi zilikuwa mkabala na Stendi Kuu ya Mabasi ya Arusha wakati nyumba ya kuishi, ikiwa na kila kitu ndani ilikuwa maeneo ya Njiro, jirani na pale alipokuwa anaishi kwa siri na Samantha. Alikabidhiwa pia gari la kutembelea, Toyota Harrier pamoja na dereva ambaye angekuwa akilipwa na kampuni.
Baada ya meneja mkuu kumkabidhi kila kitu, alipanda ndege kurejea jijiniDar es Salaam ambapo Edmund naye alielekea kwenye makazi yake ya awali, alikomuacha mpenzi wake, Samantha. Alipofika alipokelewa kwa shangwe kubwa na Samantha ambaye alimtaka amueleze kilichotokea katika safari yake hiyo.
Samantha alipoelezwa, naye alishindwa kuficha hisia zake, akamwaga machozi mengi ya furaha na kumshukuru Mungu kwa kilichotokea.Siku tatu baadaye, tayari walishahamia kwenye nyumba ya kampuni na Edmund akaanza kazi rasmi huku Samantha akiwa ndiyo mshauri wake mkubwa.
***
Maisha mapya ya wazazi wa Samantha, yalimbadilisha kabisa baba yake. Muda mwingi akawa ni mtu wa kukaa na kujutia mambo yote mabaya aliyowahi kuyafanya. Hakukuwa na chochote tena baada ya serikali kutaifisha mali zake karibu zote huku nyingine zikiteketea kwa moto au kuharibika katika mazingira ya kutatanisha.
Hata hivyo, kama alivyokuwa ameshauriwa na mganga Kiswigo, aliendelea kufuata maelekezo yote aliyopewa. Taratibu akaanza kubadilika na kurudi kuwa mtu mwema, kama alivyokuwa mwanzokabla ya kukumbwa na tamaa ya utajiri haramu.
“Mke wangu!”
“Naam mume wangu.”
“Nimekaa na kufikiria sana kuhusu suala la Samantha na Edmund, nafikiri hakuna sababu ya kuendelea kuwazuia kuishi pamoja lakini cha msingi lazima wafuate sheria zote muhimu ili wafunge ndoa na kuishi kihalali, au wewe unasemaje mke wangu?” alisema baba yake Samantha, kauli ambayo ilimfanya mkewe apigwe na butwaa, akiwa haamini alichokisikia, akawa anamshukuru Mungu kwa miujiza yake.
Bila kupoteza muda, mama yake Samantha aliwasiliana na Samantha na Edmund na mipango ya kuchumbiana ikaanza kufanywa. Wiki mbili baadaye, wawili hao waliwasili jijini Dar es Salaam ambapo taratibu za kuvalishana pete ya uchumba zilifanyika. Baadaye wakaoana kwa ndoa ya kawaida, wakala kiapo cha kuwa mume na mke na huo ukawa mwanzo wa kufungua ukurasa mpya wa maisha yao.
Kwa kuwa Edmund alikuwa akilipwa mshahara mkubwa, alimsaidia baba mkwe wake mtajiwa kuanzisha upya biashara, jambo ambalo mzee huyo hakuwahi kuhisi linaweza kutokea hata mara moja!
Yaani Edmund yule aliyekuwa anamdharau na kumkosakosa kumuua mara kadhaa, leo ndiyo anampa mtaji wa kuanza upya biashara baada ya kufilisika! Ilikuwa ni zaidi ya maajabu kwa mzee huyo. Maisha yalizidi kusonga mbele, taratibu biashara za baba yake Samantha zikaanza kuchangamka, ukiongeza na uzoefu aliokuwa nao, kazi haikuwa ngumu.
Akaikarabati vizuri nyumba yake mpya na kurudisha vitu vingi alivyovizoea kablahajafilisika. Safari hii alikuwa amebadilika mno, hakuwa kama mwanzo, alikuwa na heshima kwa kila mtu, aliwajali maskini na wenye shida na kila siku ilikuwa ni lazima amuombe Mungu wake na kutubu dhambi zake zote alizowahi kuzifanya.
Vijana wengi ambao waliwahi kuchukuliwa misukule enzi za utajiri wake, nao waliendelea kuombewa na kupatiwa tiba za uhakika na wakaanza kurudi kwenye hali zao za kawaida kama walivyokuwa mwanzo.
Miezi michache baadaye, Samantha alipata ujauzito, akiwa mke halali wa Edmund ambapo miezi tisa baadaye, alijifungua watoto mapacha, wa kike na wa kiume aliowapa majina ya Emanuel na Emanuela, yakimaanisha Mungu yupo pamoja nasi. Maisha yakaendelea kwa raha mustarehe, huku ufanisi wa Edmund kazini nao ukizidi kuongezeka kila kukicha.
Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi
MWISHO
JIUNGE KWA UPDATE NA BURUDANI ZAIDI
WhatsApp Channel=> CnZ Media(Follow)
Telegram Channel=> CnZ Media(Join)