KITABU CHA SHETANI (26)

0
Mtunzi: Aziz Hashim

SEHEMU YA ISHIRINI NA SITA
TULIPOISHIA...
“Ishi hapa duniani ukiwa unaelewa kwamba sote ni wapita njia tu na kunamaisha baada ya kifo, jiandae leo kwa kutenda mema na kuishi kulingana na asili ya binadamu ili kesho hata zamu yako ya kufa ikifika, usiwe na hofu tena.

IKIWA UNASOMA SIMULIZI NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI USIPITWE NA SIMULIZI

TUENDELEE...
“Ukiyatimiza hayo, utakuwa umefikia hatua ya utakaso,” alisema mganga Kiswigo, baba yake Samantha akawa anatingisha kichwa tu huku akiwa ni kama haamini kwa sababu alitegemea labda mganga huyo atakuwa anazungumzia habari za mashetani, majini, misukule na viumbe wa kutisha lakini haikuwa hivyo.

Kwa kuwa hiyo ndiyo ilikuwa siku ya mwisho kukaa nyumbani kwa mganga huyo, baba yake Samantha alimshukuru sana mganga huyo na kumwambia kwamba mpaka muda huo, alikuwa anajihisi ni kama amezaliwa upya, akaahidi kwenda kufanyia kazi mambo yote aliyoelekezwa.

Mganga Kiswigo na wasaidizi wake walimsindikiza baba yake Samantha mpaka nje ya msituhuo, wakampeleka mpaka sehemu aliyokodishiwa baiskeli kwa ajili ya kumsogeza mpaka sehemu anayoweza kupata usafiri wa magari madogo au ya mizigo yatakayomfikisha mjini ili aendelee na safari yake. Walimfungashia zawadi mbalimbali za kuwapelekea watu wa mjini. Hatimaye safari ye kurejea jijini Dar es Salaam ikapamba moto.

***

Maisha ya Edmund na Samantha jijini Arusha yaliendelea vizuri huku mara kwa mara wakiwasiliana na mama yake Samantha ambaye naye nafsi yake ilitulia na taratibu akaanza kuamini kwamba mwanaye yupo kwenye mikono salama kwani kila alipokuwa akizungumza naye, alikuwa anaonesha kuwa na furaha kubwa.

Edmund naye aliendelea kuhakikisha Samantha anapata huduma zote za kiafya kama alivyomuahidi mama yake na baada ya wiki mojakuisha, Samantha alikuwa na ahueni kubwa kwani tayari jerahalake la kupigwa risasi mguuni lilikuwa likikaribia kupona kabisa.

Ili kuharakisha kuponakwake, Edmund akawa anamfanyisha mazoezi ya kutembea ambapo safari hii alianza kumudu kutembea mwenyewe ingawa bado alikuwa akichechemea. Jioni moja akiwa anamfanyisha Samantha mazoezi ya kutembea, nje ya nyumba waliyokuwa wanaishi, simu ya Edmund ilianza kuita mfululizo, alipotazama namba ya mpigaji, alishtuka na kumtazama Samantha usoni.

“Vipi?”

“Bosi wetu kazini ananipigia simu, sijui anataka kusema nini? Naogopa hata kupokea.”

“Pokea tu umsikilize, kwani tatizo liko wapi?”

“Si unajua tangu nilipopatwa nayale matatizo kipindikile sijarudi tena kazini na wala hawana taarifa kama niko wapi kwa siku zote hizo?”

“Pokea, nakuomba upokee na uzungumze naye,” Samantha alisemakwa sauti ya upole na kumkumbatia Edmund, ikabidi atii alichowambiwa, akapokea.

“Edmund!”

“Naam mkuu.”

“Uko wapi wewe mbona unatupa wasiwasi? Tumekuja nyumbani kwako ulikokuwa unaishi karibu mara kumi, haupo wala hakuna taarifa za mahali ulipo, una tatizo gani?”

“Nina matatizo ya kifamilia.”

“Lakini ulipewa ruhusa kwa sababu ulikuwa unaumwa, kama una matatizo ya kifamilia kwa nini usitoe taarifa? Karibu mwezi mzima unaisha hujaripoti kazini. Au kwa sababu unajua unategemewa na kampuni ndiyo maana unaleta dharau?

“Sasa sikia, nilichokupigia simu ni kwamba inatakiwa Jumatatu uje kazini, vyovyote itakavyokuwa lazima uje, kuna kazi maalum umechaguliwa kuifanya, no excuse! (Hakuna visingizio!)” alisema meneja mkuu wa Kampuni ya Hashcom Mobile, Erick Salawi kisha akakata simu.

“Edmund alishusha pumzi ndefu na kumgeukia Samantha ambaye muda wote alikuwa ametulia akimsikiliza Edmund alivyokuwa anazungumza na simu.

“Vipi anasemaje?” alihoji Samantha huku akionesha kuwa na shauku kubwa ya kutaka kusikia atakachoambiwa, ikabidi Edmund amueleze kila kitu.

“Umeamuaje?”

“Siwezi kuondoka na kukuacha Samantha, nipo tayari kupoteza kila kitu lakini siyo wewe,” alisema Edmund, Samantha akamvutia kifuani kwake na kumkumbatia, mazungumzo mazito yakaanza. Huku akizungumza kwa sauti ya upole, iliyojaa ujumbe mzito, Samantha alimtaka Edmund asafiri mpaka Dar es Salaam kwenda kusikiliza alichoitiwa na kwamba asiwe na wasiwasi kuhusu yeye.

“Napenda kukuona ukifanya kazi mume wangu mtarajiwa, nataka tuishi kwa kujitegemea, naamini tunaweza. Wewe ukifanya kazi na mimi nikifanya kazi, tukiunganisha mshahara wetu tunaweza kufanya mambo makubwa sana, tafadhali nakuomba usiniangushe,” alisema Samantha, Edmund akawa anatingisha kichwa kama ishara ya kukubaliana na kilichokuwa kinasemwa na Samantha.

Siku hiyo ilipita, kesho yake Edmund akaanza kujiandaa kwa ajili ya safari ya kuelekea Dar es Salaam. Alihakikisha anamuacha Samantha katika mazingira mazuri, akamuandalia kila kitu ili asihangaike atakapoondoka.

Hatimaye muda wa kuondoka uliwadia, akakumbatiana na Samantha kwa muda mrefu huku wakimwagiana mvua ya mabusu, wakaagana huku msichana huyo mrembo akimtakia kila la heri.

***

Baada ya safari ndefu na yakuchosha ya basi, kutoka Sumbawanga, hatimaye baba yake Samantha aliwasili jijini Dar es Salaam majira ya saa tano za usiku. Alimshukuru Mungu kuwasili usiku kwani kwa hali aliyokuwa nayo, kila mtu anayefahamiana naye ambaye angemuona, asingeacha kumshangaa.

Aliposhuka Stendi ya Mabasi ya Ubungo, alikodi teksi iliyompeleka moja kwa moja mpaka nyumbani kwake. Kwa muda wote huo hakuwa amewasiliana na mkewe wala hakumpa taarifa zozote juu ya ujio wake.

Mlinzi wa nyumba ya kifahari waliyokuwa wanaishi, alishtuka baada ya kusikia kengele ya geti ikigongwa, jambo ambalo halikuwa kawaida. Harakaharaka akasogea getini na kutazama kupitia kioo maalum kilichokuwepo eneo hilo, akashtuka kumuona bosi wake huku akionesha kubadilika sana.

Harakaharaka alifungua mlango na kumkaribisha kwa heshima, akaingia na kupitiliza moja kwa moja mpaka ndani ambako aligonga mlango na kufunguliwa na mkewe muda mfupi baadaye.

“Mume wangu, ni wewe? Ooh! Ahsante Mungu, siamini macho yangu,” alisema mama Samantha na kumkumbatia mumewe kwa nguvu huku machozi yakimtoka kwa wingi.

“Mbona umekonda hivi? Unaumwa?” alimuuliza wakati akimkaribisha ndani, baba yake Samantha akawa anatingisha kichwa kuonesha kwamba hakuwa akiumwa, akamwambia mkewe atamuelezea kila kitu. Walipoingia ndani, jambo la kwanza lilikuwa ni kwenda kuoga kwani udongo mwekundu ulikuwa umemchafua na kumfanya abadilike kabisa.

Baada ya kuoga kwa zaidi ya dakika ishirini, akitumia sabuni nyingi, alitoka bafuni na kuelekea chumbani. Muda mfupi baadaye akatoka na nguo alizotoka nazo safarini na kwenda kuzichoma moto, akarudi ndani ambako alikuta tayari mkewe ameshamuandalia chakula.

Wakakaa mezani ambapo alianza kukifakamia chakula kwa fujo kutokana na njaa kali iliyokuwa inamsumbua. Alipomaliza kula walielekea chumbani ambapo mama yake Samantha alianza kumuelezea kila kitu kilichotokea katika kipindi chote ambacho hakuwepo.

Alimueleza kuanzia jinsi Samantha alivyotoroka hospitalini akiwa na Edmund, jinsi mali zao nyingi zilivyoshikiliwa na serikali kwa madai ya kutolipiwa kodi stahiki kwa muda mrefu na jinsi nyumba hiyo waliyokuwa wanaishi ilivyokuja kupigwa ‘X’ kwa madai kwamba ilikuwa imejengwa katika eneo la hifadhi ya barabara.

“Na nyumba nayo imewekwa ‘X’?”

“Ndiyo na nasikia tayari watu wengine wameshaanza kubomolewa mtaa wa pili, inabidi tufanye mpango wa kuhamia kwenye nyumba yetu ya Bunju haraka iwezekanavyo.”

“Lakini ile bado haijaisha!”

“Sasa unafikiri tutafanya nini mume wangu? Au unasubiri nyumba ije ivunjwe tukiwa humuhumu ndani?” alisema mama yake Samantha kwa sauti ya upole, akaendelea kumuelewesha mumewe mambo mbalimbali.

“Utakachokutana nacho nyumbani kwako kisikushangaze, unatakiwa kwenda kuanza upya kabisa, utajiri wa kishirikina hauna nafasi tena na mali zote ulizozipata kwa njia ya kishirikina zitayeyuka na kukuacha ukiwa huna kitu,” kauli ya mganga Kiswigo ilijirudia kichwani mwake mithili ya mkanda wa video.

Hakuwa na cha kufanya zaidi ya kukubaliana na kila kitu, wakalala mpaka asubuhi ya siku iliyofuata ambapo maandalizi ya kuhamia Bunju yalianza. Hata suala la kuhamisha vitu lilikuwa gumu kwa sababu akaunti zote za benki zilizokuwa na mamilioni ya fedha zilikuwa zinashikiliwa na serikali.

Ilibidi abangaize kwenye miradi yake mingine ambayo nayo ilikuwa ikisuasua, fedha zikapatikana na kazi ya kuhamisha vitu ikaanza huku pia mafundi wakilipwa kwa ajili ya kukamilisha vitu vidogovidogo ambavyo bado havikuwa vimekamilika kwenye nyumba mpya, ikiwemo madirisha na milango.

Mpaka jioni ya siku hiyo, vitu vyote muhimu vilikuwa vimeshahamishwa. Wazo alilolitoa mama Samantha lilisaidia sana kwa sababu usiku wa siku hiyo, tingatinga la serikali liliwasili kwenye mtaa huo na kuanza kubomoa nyumba zote zilizokuwa zimewekewa alama ya ‘X’.

Mpaka kunapambazuka, eneo kulipokuwa na nyumba ya kisasa ya akina Samantha, lilikuwa jeupe kabisa. Hakukuwa na nyumba wala bustani nzuri za maua tena. Kila kitu kilikuwa kikibadilika kwa kasi kubwa kwenye maisha ya familia hiyo, wakayaanza maisha mapya ya hadhi ya chini, Bunju, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

***

Basi la Dar Express lililokuwa likitokea Arusha, liliendelea kuchanja mbuga kwa kasi kubwa na baada ya kusafiri kwa saa nyingi, hatimaye liliwasili Ubungo ambapo abiria walianza kuteremka, Edmund akiwa miongoni mwao.

Akashuka akiwa na kibegi chake kidogo mgongoni na kutoka mpaka nje ya stendi ambapo alikodi Bajaj iliyompeleka mpaka Sinza. Hakutaka kwenda kulala kwenye nyumba waliyokuwa wanaishi na Samantha kabla ya kutokewa na matatizo, akaenda kupanga chumba kwenye nyumba ya kulala wageni iliyokuwa karibu na kazini kwao ili asubuhi iwe rahisi kuwahi kazini.

Moyoni alikuwa na shauku kubwa ya kutaka kujua aliitiwa nini kazini kwani ilionekana kuna jambo la muhimu sana.

Kesho yake asubuhi, Edmund aliwahi kuamka na kujiandaa, akatoka na kuelekea kazini ambapo siku hiyo alikuwa miongoni mwa watu wa kwanzakwanza kusaini na kuingia ofisini.

Kila mfanyakazi mwenzake aliyekuwa akikutana naye alikuwa akimshangaa kwani kilipita kipindikirefu bila kuonekana kazini. Kingine kilichofanya watu wazidi kumshangaa, ni kwamba licha ya kuelewa kwamba ametoka kwenye matatizo, Edmund alikuwa amebadilika sana kimwonekano.

Alikuwa amenawiri, rangi ya ngozi yake ambayo awali ilikuwa imefifia ikawa inapendeza kuonesha kwamba sasa alikuwa akiishi maisha mazuri. Hata mavazi yake nayo yalibadilika kwani alipendeza sana kiasi cha kuwafanya mpaka marafiki zake waanze kumuonea wivu.

Hatimaye meneja mkuu aliwasili ambapo alimkuta Edmund akiendelea kufurahi na wafanyakazi wenzake,

Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

JIUNGE KWA UPDATE NA BURUDANI ZAIDI
WhatsApp Channel=> CnZ Media(Follow)
Telegram Channel=> CnZ Media(Join)

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)