Simulizi Mpya
Tidak ada notifikasi baru.

DINI YA SHETANI (1)

Mtunzi: Aziz Hashim

SEHEMU YA KWANZA
Jina langu naitwa Mkanwa Sebastian au Saba kama wengi walivyozoea kuniita, mkazi wa Itete, Tukuyu wilayani Rungwe, Mbeya. Baba yangu mzazi, Sebastian Mwambenja alikuwa ni mchungaji wa Kanisa la Wokovu lililokuwa kwenye kijiji nilichozaliwa huku mama yangu akiwa ni muuguzi katika Zahanati ya Lufingo iliyokuwa kijiji cha pili kutoka pale tulipokuwa tunaishi.

Mimi nilikuwa ni mtoto wa mwisho kuzaliwa katika familia yetu iliyokuwa na watoto saba. Baba yangu alikuwa akitokea kwenye ukoo wa kichifu wa Mzee Mwambenja ingawa baada ya babu yetu kufariki, aliamua kuokoka na ndipo alipoupata uchungaji wa kanisa hilo.

Tangu nikiwa mdogo, wazazi wangu walinilea katika misingi ya kumuabudu na kumtukuza Mungu huku mara kwa mara wakinieleza kuwa Yesu alikufa msalabani kwa ajili ya dhambi zangu. Kila Jumapili nilikuwa nikiongozana na wazazi wangu kuelekea kanisani na baba alikuwa akitaka nikae mbele kabisa, jirani na madhabahu ambayo alikuwa akiyatumia kutangazia Injili na kuhubiri Neno la Mungu.

Mara kwa mara alikuwa akiniambia kuwa imani ndiyokitu pekee kinachoweza kumkomboa mwanadamu kutoka kwenye kifungo cha mateso ya dunia.

Watu wengi walikuwa wakimheshimu sana baba, kila alipokuwa anapita alikuwa akiitwa baba mchungaji, mama yeye akawa anaitwa mama mchungaji huku mimi nikiitwa mtoto wa mchungaji.

KAMA UNASOMA SIMULIZI HII NJE YA APPLICATION YA CnZ Media INSTALL ILI USIPITWE NA MIENDELEZO

SASA TUENDELEE...
Nakumbuka wakati baba anaanza kushika cheo cha mchungaji, nilikuwa na umri wa kati ya miaka sita au saba. Katika siku za mwanzo, hakuwa na uwezo wowote wa kufanya miujiza na kanisa lake halikuwa na waumini wengi zaidi ya ndugu zetu wa karibu na majirani ambao walikuwa wakijumuika nasi kila muda wa ibada ulipofika.

Mimi kazi yangu ilikuwa ni kumbebea baba Biblia, sadaka na vifaa vingine vilivyokuwa vinatumika kwenye sala na wakati mwingine nilikuwa nikibeba zawadi ndogondogo alizokuwa anapewa na waumini wake.

Kwa kadiri siku zilivyokuwa zinazidi kusonga mbele na mimi kuwa mkubwa, baba alianza kubadilika kwa vitu vingi, nilianza kumshuhudia akiwa na uwezo wa kufanya miujiza na mambo ambayo katika hali ya kawaida ni vigumu kuyaelezea. Kila Jumapili, alikuwa akifanya miujiza ya kuwaponya watu wenye matatizo mbalimbali yakiwemo magonjwa sugu, kuwaombea watu wenye shida mbalimbali na kutoa huduma ya kiroho.

Kila nilipokuwa nikimuuliza anapata wapi nguvu za kufanya miujiza kama ile ambayo awali nilizoea kuiangalia kwenye mkanda wa video wa Yesu, aliniambia kuwa alikuwa amefikia hatua ya ukomavu wa kiimani na ndiyo maana alikuwa na uwezo wa kufanya chochote na kikatokea kweli kama alivyotaka.

“Sasa baba, kama una uwezo wa kufanya chochote, kwa nini usiombee familia yetu tukawa matajiri na kumiliki mashamba makubwa ya migomba na magari ya kusafirishia mizigo kama baba yake Angenile?” nilimuuliza siku moja, akanitazama usoni kisha akanijibu kuwa umri wangu ulikuwa mdogo kuuliza maswali kama yale, akaniambia nikikua nitayaona mwenyewe.

Sikuridhika na majibu yake, nikaona njia pekee inayoweza kuniridhisha nafsi yangu ni kuutafuta ukweli mimi mwenyewe. Siku ziliendelea kusonga mbele, kanisa la baba likawa linazidi kuwa maarufu pale kijijini, vijiji vya jirani na wilaya nzima ya Rungwe.

Ilifika mahali watukutoka Tukuyu Mjini, Ushirika, Katumba, Kiwira na sehemu nyingine wakawa wanakuja kijijini kwetu na kujaa kwenyekanisa la baba. Kwa kuwa awali kanisa lilikuwa dogo na lisilo na ubora wowote, baada ya waumini kuanza kuongezeka, nilimsikia baba akijadiliana na watu fulani kwenye simu, akawaomba wamjengee kanisa kubwa na la kisasa.

Baadaye baba aliniambia kuwa wale ni Wamisionari waliokuwa wanaishi Ulaya ambao alifahamiana nao katikakazi yake ya kutangaza injili.

Siku iliyofuatia, tukamtafuta mpiga picha ambaye alilipiga picha lile kanisa la zamani na maeneo ya kuzunguka eneo hilo, tukasafairi na baba hadi Tukuyu mjini ambapo nilimsaidia kuzituma zile picha kwa njia ya mtandao kwenda kwa Wamisionari hao wa nchini Denmark.

Wiki kadhaa baadaye, wale wamisionari walimpigia simu baba na kumweleza kuwa fedha zilikuwa tayari, tukaenda tena mjini kufungua akaunti benki kisha tukasubiri baada ya siku tatu, fedha nyingi zikaingia kwenyeakaunti hiyo.

Baada ya hapo, baba alisaidiana na wazee wa kanisa pamoja na wauminji wengine kupanga namna kanisa jipya litakavyokuwa.

Baada ya mipango kukamilika, kanisa zuri la kisasa lilijengwa pembeni kidogo ya lile la zamani. Watu wengi wakavutiwa nalo, hali iliyosababisha waumini wazidi kuongezeka.

Kila baada ya misa kumalizika, kama kawaida yangu ya siku zote, nilikuwa nikibeba boksi lenye sadaka na kulipeleka nyumbani. Safari hii sadaka ziliongezeka kuliko kawaida, kila Jumapili watu wakawa wanamtolea Mungu wao kwa sana, noti za shilingi elfu kumikumi zikawa zinatolewa kwa wingi, tofauti na zamani ambapo waumini wa kiwango cha juu walikuwa wakitoa shilingi mia tano au elfu moja.

Maisha yetu nayo yalizidi kubadilika kila siku, tukaachana na kula mbalaga (ndizi zinazopikwa na kupondwa), sasa tukawa tunakula vyakula vizuri huku tukibadilisha milo kila siku.

Mama naye alianza kuvaa vitenge vya wax na kupaka mafuta yanayonukia vizuri.

Miezi sita baada ya ujenzi wa kanisa jipya, niliwasikia baba na mama wakijadiliana kwenda kununua nyumba Tukuyu mjini nakuhama kule kijijini. Nikawasikia wakisema kuwa kule tutakuwa tunaenda kila Jumapili kwa ajili ya ibada tu kisha baada ya hapo tutarudi mjini.

Nilifurahi sana kwani hata mimi sikuwa nikiyapenda maisha ya kijijini, baba akatuita wanaye wote na kutueleza juu ya mpango ule wa kuhama Itete na kwenda kuishi Tukuyu.

“Baba kwani tayari umeshajenga nyumba nyingine?”

“Hapana hatujengi bali tutanunua nyumba ambayo tayari imeshajengwa. Kuna madalali wanaendelea na kazi hiyo.”

“Itakuwa nzuri kama kanisa lako?”

“Ndiyo, tena nataka iwe nzuri zaidi,” tulikuwa tukizungumza na baba. Kila mmoja alikuwa na furaha.

Siku kadhaa baadaye, kweli nyumba ilipatikana katika Mtaa wa Msasani, Tukuyu, jirani na chuo cha ualimu. Ilikuwa ni nyumba nzuri yenye kila kitu, taratibu za kuhamia makazi mapya zikaanza mara moja. Wakati zoezi la kuhamisha vitu likiendelea, niliona kitu kilichonishtua mno.

Wakati nikikusanya vitu chumbani kwa baba na kuvipeleka kwenye gari lililokuwa nje, niliona vitu kama ndumba, hirizi, shanga, mapembe, fuvu la mtu, mifupa na vifaa vingine vya kishirikina vikiwa chini ya kitanda ya baba. Nilishtuka sana kwani sikuwahi kudhani kama baba anashiriki katika imani za kichawi.

Nikiwa bado nimeduwaa, nilimsikia baba akifungua mlango, akanibamba nikiwa nimeinama mahali palipokuwa na vitu vile.

“Unafanya nini?” aliniuliza kwa ukali. Nilishindwa cha kumjibu, nikabaki nimeduwaa.

“Nakuuliza unafanya nini? Wewe si nimekwambia kasaidiane na wenzako kuhamisha vitu kwenye chumba chenu?”

“Samahani baba,” nilisema huku nikiwa natetemeka, akanipokonya vile vitu nilivyovishika na kunitishia kuwa nikimwambia mtu yeyote kuhusu kile nilichokiona, atanifunza adabu. Harakaharaka nikatoka na kwenda kuungana na wenzangu na kuendelea kuhamisha vitu na kuvipakiza kwenye gari, tayari kwa safari ya kuhamia Tukuyu mjini.

Nikiwa naendelea nakazi ya kuhamisha vitu na wenzangu, bado tukio la kile nilichokiona chini ya kitanda cha baba kilikuwa kikiendelea kunisumbua.

Nilijiuliza maswali mengi ambayo yote yalikosa majibu.

Kwa kifupi nilikosa raha kabisa, nikawa najiuliza kama baba anafanya miujiza kanisani kwa kutumia nguvu za Mungu au giza kama nilivyokuwa nikisikia kwa watu kuwa kuna watumishi wa Mungu wana kamchezo hako.

“Mbona unaonekana una mawazo mwanangu, hujafurahia kuhama huku kijijini na kwenda mjini?” aliniuliza mama wakati tukiendelea na kazi ile, sikumjibu kitu zaidi ya kujichekelesha na kumuonesha kuwa sikuwa na chochote kichwani mwangu.

Kazi iliendelea mpaka jioni, hatimaye tukamaliza na kuanza kuondoka. Baba na mama walipanda mbele ya lile gari, mimi na ndugu zangu wengine tukapanda nyuma na kushikilia vyombo, safari kutoka Itete kwenda Tukuyu Mjini ikaanza.

Tukasafiri kwenye barabara ya vumbi kwa karibu kilometa kumi,tukafika njia panda ambapo dereva alikata kona na kuingia kwenye barabara ya lami ya Mbeya- Tukuyu. Bado niliendelea kufikiria mambo mengi ndani ya kichwa changu kuhusu kile nilichokiona.

Kule mbele baba na mama walipokuwa wamekaa, kulikuwa na kifurushi kidogo kilichokuwa kimefungwa kwa ustadi mkubwa, nikatambua kuwa lazima vile vitu vya baba vilikuwa ndani ya kifurushi kile, nikajiapiza kuwa tukifika na kuanza kushusha vyombo, nitamfuatilia baba kwa makini ili nijue ataenda kuviweka wapi.

Safari iliendelea, cha ajabu tulipofika sehemu inayoitwa Katumba, njia panda ya kuelekea Mwakaleli, baba aliteremka kwenye gari akiwa na kile kifurushi, akatuambia sisi tutangulie nay eye atafuata baada ya muda si mrefu. Kwa kuwamama alikuwa akipafahamu tunapohamia, tulikuwa na uhakika wa kufika salama.

Nikamtazama baba ambaye tayari alikuwa ameteremsha kile kifurushi chini, macho yake na yangu yakagongana, nikamuona akinipa ishara kama ya kunitisha kuwa endapo nitasema nilichokiona, atanifanya kitu kibaya.

Dereva akawasha gari na safari ikaendelea. Niliendelea kumsindikiza baba kwa macho, nikamuona akizamia kwenye migomba mingi iliyokuwa kando ya barabara, hakuna aliyeelewa anakwenda wapi. Baada ya dakika kadhaa, tuliwasili Tukuyu, mama akamuelekeza dereva njia ya makazi mapya.

Tulienda mpaka kwenye jumba kubwa la kifahari lililokuwa limeezekwa kwa vigae vyekundu. Mama akatuambia kua pale ndiyo tutakapokuwa tukiishi, sote tukapigwa na butwaa kutokana na uzuri wa nyumba ile.

Tulianza kuteremsha vyombo kwenye gari kwa kusaidiana na vijana tuliowakuta pale nje ya nyumba ile ya kifahari. Wakati tukiendelea na kazi ile, nilikuwa makini kumuangalia baba kama atatokea lakini haikuwa hivyo. Kikubwa nilichokuwa nataka kukiona, ni mahali anapoenda kuhifadhi ule mzigo wake aliokuwa ameushika mkononi.

Tuliendelea na kazi mpaka tukamaliza kushusha vyombo vyote, mama akamlipa dereva na utingo wake gharama walizokubaliana, wakawasha gari na kuondoka. Wale vijana waliotusaidia kushusha vyombo pia walipewa kifuta jasho, wakaondoka na kutuacha mimi, ndugu zangu na mama tukiendelea kupanga vitu.

USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi
64 Dini ya Shetani featured Simulizi
Jiunge kwenye mazungumzo
Chapisha Maoni