DINI YA SHETANI (6)
Zephiline F Ezekiel
---
Jina: DINI YA SHETANI
Mtunzi: Aziz Hashim
SEHEMU YA SITA
TULIPOISHIA...
TULIPOISHIA...
Kwa bahati nzuri kumbe baba mkubwa alikuwa tayari amewasili pale stendi akiwa na mkewe na mwanaye mmoja wa kike, nilipoanza kushuka tu, nikamsikia akiniita jina langu.
Nilifurahi sana kwani tayari nilishaanza kuchanganyikiwa, nikiwa sijui nielekee wapi.
KAMA UNASOMA SIMULIZI HII NJE YA APPLICATION YA CnZ Media INSTALL ILI USIPITWE NA MIENDELEZO
SASA TUENDELEE...
Walinipokea kwa furaha, tukakumbatiana na kusalimiana. Wakanipokea mzigo na kuniongoza mpaka nje ya stendi ambapo tulipanda teksi na safari ya kuelekea Kimara Kona alikokuwa anaishi baba mkubwa ikaanza.
“Tulizungumza mambo mengi kwenye gari, wakawa wananiuliza hali za wazazi na ndugu zangu wengine niliowaacha Tukuyu. Niliwajibu kuwa wote wapo salama na wanawasalimia sana. Baada ya muda, tulikuwa tayari tumefika Kimara, dereva akasimamisha taksi kisha tukateremka. Wenyeji wangu wakaniongoza mpaka nyumbani.
“Karibu sana, hapa ndiyo tunapoishi,” alisema baba mkubwa wakati akifungua geti, tukaingia ndani huku nikiwa na furaha tele ndani ya moyo wangu. Nilifurahi sana kufika Dar es Salaam. Kesho yake, baba mkubwa alienda kunitembeza mjini, akanipeleka Posta, tukaenda mpaka Feri na kuvuka ng’ambo ya pili, Kigamboni kwa kutumia kivuko.
Tulirudi na tukaelekea Kariakoo.
Kila kitu kilikuwa kigeni kwangu, kuanzia wingi wa watu, magari, maghorofa marefu na kila aina ya mambo ya kuvutia.
“Kumbe ndiyo maana wanasemaga mjini kuzuri, cheki maghorofa?” nilijisemea kimoyomoyo tukiwa tunakaribia Kariakoo. Tulipofika baba mkubwa alininunulia zawadi ndogondogo kisha tukaondoka. Akanipeleka mpaka Manzese, tukapanda mpaka kwenye daraja maarufu ambalo nilikuwa nalisikia sana nikiwa nyumbani Tukuyu.
“Na mimi nataka kupiga picha juu ya daraja,” nilimwambia baba mkubwa ambaye bila hiyana alimuita mpigapicha, tukapiga kadhaa. Nilipanga kwenda kuwaringishia wenzangu nikirudi Tukuyu kwani hakuna aliyewahi kufika Dar es Salaam zaidi yangu. Baadaye tulirudi mpaka nyumbani.
Tukiwa tumekaribia, nililiona jengo moja lililokuwa na maandishi ukutani yaliyosomeka FAJI. Kumbukumbu zangu zikarudi kwenye kile kitabu changu, nikakumbuka kuwa kilielekeza kuwa Kimara Kona kuna sehemu panaitwa Familia ya Jitambue au kwa kifupi FAJI ambapo elimu ya utambuzi inatolewa.
Nikashusha pumzi ndefu huku kimoyomoyo nikichekelea kwani kile nilichokuwa nakitaka sasa kilikuwa kimekaribia kutimia. Nilipaangalia vizuri kwa lengo la kukariri uelekeo ili nisipotee hata nikirudi peke yangu. Kwa kuwa haikuwa mbali sana na nyumbani kwa baba mkubwa, niliishika ramani vizuri.
Siku kadhaa baadaye, jioni niliaga nyumbani kuwa naenda kunyoosha miguu. Kwa kuwa tayari nilikuwa nimeanza kufahamu sehemu mbalimbali, niliruhusiwa, nikaelekea moja kwa moja pale kwenye jengo la FAJI, nikaenda mapokezi na kupokelewa na mwanamke mmoja wa makamo, akawa ananiuliza anisaidie nini.
“Nataka kuonana na mwalimu wa Utambuzi aitwaye Munga,” nilisema huku nikiwa sina uhakika na nilichokuwa nakiulizia. Sikumfahamu Munga ila kupitia kile kitabu nilichokuwa nimenunua, nilisoma kuwa mwalimu wa masomo ya utambuzi katika kituo hicho alikuwa akitambulika kwa jina hilo.
Mwanamke yule wa makamo aliyekuwa amekaa juu ya meza kubwa pale mapokezi, alinitazama kwa muda halafu ukimya ukatanda kwa sekunde kadhaa. Nilipomtazama machoni, niligundua kuwa alikuwa akitokwa na machozi. Sikuelewa sababu za kumfanya atokwe na machozi wakati nilimuuliza kistaarabu.
“Ma’mdogo mbona unalia? Kwani kuna nini?” nilimuuliza huku nikianza kuingiwa na wasiwasi mkubwa ndani ya moyo wangu. Alinitazama tena, badala ya kunijibu akaniuliza natokea wapi?
“Natokea Tukuyu, nimekuja kuishi kwa baba mkubwa, anakaa hapo mtaa wa pili,” nilimjibu, akaniambia kuwa Munga alishafariki dunia miezi kadhaa iliyopita. Nilishusha pumzi ndefu nikiwa siamini kile nilichokisikia.
“Amefariki?” niliuliza tena huku machozi yakianza kunilengalenga, nilisogea pembeni mpaka kwenye benchi, nikakaa huku mwili ukiwa umeniishia nguvu kabisa. Niliona kama safari yangu ya kutaka kufahamu mambo mengi kuhusu elimu ya utambuzi ilikuwa imefikia mwisho.
Nikiwa katika hali ile, mwanaume mmoja wa makamo aliyekuwa na mvi kichwa kizima, begani akiwa amebeba begi dogo, aliwasili. Akavua viatu nje na kuingia mpaka pale ndani, akanisabahi kwa uchangamfu kama tuliyekuwa tunajuana naye kwa siku nyingi, akaenda kumsabahi na yule mama wa makamo kisha akarudi na kukaa karibu yangu.
“Bila shaka wewe ni mgeni hapa,” aliniuliza, nikatingisha kichwa kama ishara ya kumkubalia. Akaniuliza kuwa uso wangu ulionesha kuwa nina majonzi, ni jambo gani lilikuwa linanisumbua? Kabla sijamjibu, yule mama wa mapokezi alidakia na kumweleza kuwa nilienda pale kumuulizia Munga, nilipopewa taarifa juu ya kifo chake ndiyo nikawa kwenye hali ile.
“Usijali, kama Munga hayupo wapo wengine wanaoweza kukusaidia ulichokuwa unakitaka, pengine kwa kiwango cha juu kuliko hata huyo Munga. Pia inawezekana unasikitika kwa sababu huelewi tafsiri ya kifo,” alisema yule mzee ambaye baadaye nilikuja kumtambua kuwa anaitwa Mhagama.
Angalau moyo wangu ulitulia, nikainua kichwa changu na kuanza kumtazama, akanipigapiga mgongoni kama ishara ya kunifariji, kisha akaanza kuniuliza juu ya historia yangu na asili yangu. Nilimjibu kuwa nimetokea Tukuyu, nikamweleza kuhusu familia yetu, kwamba baba yangu ni mchungaji na kumweleza jambo lililonipeleka pale.
“Unataka kujua kuhusu nini hasa?”
“Nataka kujitambua, nataka kujua kuhusu mimi na dunia ninayoishi. Nataka kujua uhusiano kati ya maumbile na ulimwengu,” nilimjibu, akanitazama kwa makini usoni kama anayejiuliza ‘utaweza kweli?’.
“Basi hakuna shaka, hapa ndiyo umefika, naamini kila unachohitaji kukijua utakipata, cha msingi ni uvumilivu wako na juhudi kwenye masomo,” aliniambia, nikamuomba anifafanulie kuwa kuna masomo ya aina gani yaliyokuwa yanafundishwa pale.
“Kuna madarasa mengi ya utambuzi, wanaoanza kuna darasa lao, wale wanaofahamu kidogo kuna darasa lao lingine na wale waliofuzu kuna darasa lao pia. Kuna madarasa ya meditation kulingana na ngazi kama ilivyo kwenye masomo ya utambuzi, naamini utafurahia,” alisema Mhagama huku akinitazama kwa furaha.
Baada ya maelezo yale, aliniambia kuwa nilikuwa nimefika siku muafaka kwani kulikuwa na mafunzo siku hiyo, akaniambia baada ya muda wanafunzi wengine wataanza kuwasili eneo lile.
Kweli baada ya muda, niliona watu mbalimbali wakiwasili eneo lile, vijana kwa wazee, wanaume kwa wanawake, wakawa wananisabahi kwa uchangamfu. Kitu nilichojifunza mapema ni kwamba wanafamilia wa Jitambue walikuwa na upendo mkubwa sana ndani ya mioyo yao. Kila aliyekuwa akinipita alikuwa akinisabahi kwa uchangamfu licha ya umri wangu mdogo, nikajihisi kama nipo nyumbani.
“Hata wewe ukianza kusoma masomo ya utambuzi, utajikuta taratibu ukianza kuwapenda binadamu wenzako na kuondoa roho za chuki, visasi, wivu na kuwawazia wengine mabaya. Hapa tunafundishana namna ya kuishi kama ambavyo Mungu alikusudia binadamu tuishi,” alisema Mhagama, nikashangaa kumsikia akimtaja Mungu.
“Mbona watu wanasema wanaojifunza utambuzi wanajifunza kumwabudu shetani?” nilimuuliza kwa shauku, akanitazama usoni na kuniambia kwa mafumbo: “Huwezi kuujua mti mpaka wewe mwenyewe utakapoamua kuwa mti.”
Nilitafakari maana ya fumbo lile lakini sikupata majibu, akaendelea kuniambia kuwa kuna falsafa na propaganda nyingi sana zinazoenezwa juu ya watu wanaoutafuta ukweli, akaniambia niwe makini na nielekeze nguvu zangu zote kwenye kuusaka ukweli badala ya kusikiliza maneno ya watu.
Baada ya kuniambia hivyo, tayari watu wengi walikuwa wameshaingia ndani ya jengo hilo, akanishika mkono na kuniambia nimfuate. Nilifanya kama alivyonielekeza, tukaongozana mpaka kwenye chumba maalum kilichokuwa upande wa kulia wa jengo lile.
Tukaingia na kukaa kwenye jamvi kama wenzetu tuliowakuta, majadiliano yakawa yanaendelea. Kuna hoja ilitolewa juu ya vyakula ambavyo binadamu anapaswa kula ili awe na afya njema ya akili na roho, watu mbalimbali wakawa wanachangia.
“Binadamu tuliumbwa kula mbogamboga, nafaka na matunda ndiyo maana hata mpangilio wetu wa meno (dental formula) ni tofauti na wanyama wanaokula nyama,” alisema mjumbe mmoja, mwingine akaunga mkono hoja ile.
“Ni makosa sana kuendekeza kula vyakula kama nyama nyekundu, vyakula vya kwenye makopo na vinywaji vyenye kemikali, maisha ya binadamu siku hizi yamekuwa mafupi, yaliyotawaliwa na magonjwa mengi kwa sababu tunaishi kinyume na Mungu alivyokusudia alipotuleta duniani.”
Nilivutiwa sana na mada ile, nikawa nasikiliza kwa makini. Baada ya kumaliza majadiliano, lilifuata zoezi la kufanya meditation kwa pamoja.
Hakuna kitu nilichokuwa nakisubiri kwa hamu kama muda huo wa kufanya meditation ya pamoja. Lengo langu lilikuwa ni kujifunza kama ninavyofanya meditation mwenyewe huwa napatia au nakosea, nikawa nasubiri kwa hamu kuwaona watu walionizidi umri na uzoefu wakifanya.
Tulielekezwa kukaa kwenye jamvi kwa mfumo wa duara, katikati pakawekwa mshumaa mkubwa uliokuwa unawaka. Tukaelekezwa kuwa siku hiyo tutafanya meditation ya mshumaa, kila mmoja akakaa vizuri tayari kwa kuanza.
Niliposikia kuna meditation ya mshumaa, shauku ndani ya moyo wangu iliongezeka maradufu, nikawa nasubiri nione inavyofanywa.
Baada ya dakika chache, tulielekezwa wote kuutazama ule mshumaa uliokuwa unawaka katikati yetu, tukaambiwa tusipepese macho na kuelekeza akili zote kuutazama mshumaa ule. Aliyekuwa anatoa maelekezo alisisitiza kuwa tutazame ile sehemu ya juu iliyokuwa inawaka, akasema tukishautazama kwa dakika kadhaa, atatoa ishara maalum ambapo wote tutatakiwa kufumba macho.
Tulianza kuutazama mshumaa ule huku kila mmoja akipumua kwa uhuru, ukimya wa ajabu ukatanda mle ndani. Nilikuwa makini kuhakikisha sikosei hata kidogo, nikawa nautazama ule mshumaa huku nikiwa na hamu kubwa ya kuona kitakachotokea.
Baada ya kuuangalia kwa dakika kadhaa, nilianza kuona hali ambayo nilishindwa kuitafsiri. Watu wote waliokuwa mle ndani sikuwaona tena, nikawa nahisi kama nilikuwa peke yangu chumba kizima, jambo ambalo halikuwa kweli. Baada ya muda, yule aliyekuwa anatoa maelekezo alitoa ishara kama alivyokuwa ameeleza awali, watu wote tukafumba macho.
Kingine kilichonishangaza ni kwamba hata baada ya kufumba macho, niliendelea kuuona ule mshumaa ukiwaka kupitia kile ambacho baadaye nilielezwa kuwa ni jicho la tatu.
Nilitulia katika hali ile kwa muda mrefu, nikaanza kujihisi kama nahama kifikra kutoka pale nilipokuwa nimekaa na kwenda sehemu ambayo siijui.
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni