Simulizi Mpya
Tidak ada notifikasi baru.

DINI YA SHETANI (12)

Mtunzi: Aziz Hashim

SEHEMU YA KUMI NA MBILI
TULIPOISHIA...
Baada ya muda nilienda kujumuika na ndugu zangu wengine kupata chakula cha usiku kisha nikarudi na kulala. Akili zangu hazikuwa kwenye mapenzi bali kwenye dini ya shetani ambayo sasa nilikuwa natamani kuijua kuliko kitu kingine chochote.

KAMA UNASOMA SIMULIZI HII NJE YA APPLICATION YA CnZ Media INSTALL ILI USIPITWE NA MIENDELEZO

SASA TUENDELEE...
Kesho yake kulipopambazuka, niliwahi kuamka na kujiandaa kumsubiri Firyaal kwani aliniambia atakuja asubuhi sana ili tupate muda mrefu wa kuwa pamoja. Pale nyumbani niliaga na kuruhusiwa kwa urahisi kwani baba mkubwa alikuwa bado

hajarudi kutoka safari yake.

Baada ya muda, ujumbe mfupi uliingia kwenye simu yangu kutoka kwa Firyaal, akaniambia anikute barabarani. Harakaharaka nilitoka hadi pale barabarani tunapokutania siku zote na kusimama kumsubiri. Baada ya muda mfupi alifika akiwa na gari lake lilelile la siku zote.

Nilipomuona tu, nilijikuta moyo wangu ukilipuka kwa furaha, sikujua ni kwa sababu gani lakini nahisi na mimi nilishaanza kumpenda. Nikaingia kwenye gari na salamu yetu kwa siku hiyo ilibadilika kwani tulikumbatiana kwa nguvu, akawa ananibusu sehemu mbalimbali za mwili wangu, hasa shingoni.

Baada ya kuridhika, aliwasha gari na kuligeuza, tukaelekea nyumbani kwake. Tulipofika mbele ya nyumba moja ya ghorofa moja, alisimamisha gari na kupiga honi, mlinzi aliyekuwa amevalia sare maalum alifungua mlango na gari likaingia mpaka ndani.

Nilibaki nimepigwa na butwaa kwa jinsi nyumba ile ilivyokuwa nzuri. Kila kitu kilikuwa kizuri, kuanzia mandhari mpaka nyumba yenyewe. Kwa nje kulikuwa na bwawa la kuogelea, bustani nzuri za maua na miti ya vivuli. Sikutaka kuamini kama kweli alikuwa akiishi peke yake kama alivyoniambia.

Aligundua kuwa nilikuwa nashangaa sana, akanishika mkono huku akinivuta kimahaba kuelekea kwenye ngazi za kupandia vyumba vya juu.Tulitokezea kwenye sebule nzuri ya kisasa iliyokuwa na samani za mbei mbaya. Nilijua tutakaa pale lakini alizidi kunivuta mpaka kwenye chumba chake cha kulala ambacho nacho kilikuwa si

mchezo.

“Karibu sana mpenzi,” alisema huku akinikumbatia, akanimwagia mvua ya mabusu kisha nikamuona akianza kuvua nguo moja baada ya nyingine. Ama kwa hakika Firyaal alikuwa ameumbika haswaa. Kwa jinsi alivyokuwa mzuri, ungeweza kumfananisha na msichana wa miaka kumi na nane wakati tayari alishakuwa mtu mzima.

Bila hata kunionea aibu alivua zote na kubakia na nguo ya ndani tu, akatembea kimadaha hadi pale nilipokuwa nimesimama, akanivamia mwilini na kugusanisha midomo yetu, akaanza kunifungua vifungo vya shati huku akinifanyia mambo mengine ambayo kwangu yalikuwa mageni.

Siwezi kuelezea jinsi mwili wangu ulivyosisimka, akanivutia kwenye kitanda kikubwa cha kisasa na kunidondosha kimahaba, na yeye akaja juu yangu mzimamzima. Akawa anaupasha joto mwili wangu kwa ufundi mkubwa huku akinifanyia mambo mengine ambayo hayaelezeki.

Kwa kadiri alivyokuwa anaongeza ufundi ndivyo na mimi nilivyozidi kuchanganyikiwa, ikafika hatua nikawa sijielewi.

Kutokana na vituko alivyonifanyia Firyaal siku hiyo, nilijikuta nikishindwa kuvumilia hasa kutokana na ukweli kwamba

licha ya udogo wangu, nilikuwa mwanaume niliyekamilika. Kwa mara ya kwanza nikajivinjari kwenye ulimwengu wa kikubwa na huo ukawa mwanzo wa mahaba yangu na Firyaal. Mara kwa mara akawa ananipa fedha nyingi sana.

Siku kadhaa baadaye, tulipokea simu kutoka nyumbani, Tukuyu ikitutaarifu kwamba baba yangu alikuwa akiumwa sana na kwamba mimi na baba mkubwa tulitakiwa kwenda haraka. Kwa bahati mbaya, nilisahau simu yangu nyumbani kwa Firyaal kutokana na haraka niliyokuwa nayo baada ya kupokea taarifa hizo.

Hatukupoteza muda, harakaharaka nilichukua nguo zangu kadhaa na kuziweka kwenye begi dogo, nikachukua na zile fedha alizonipa Firyaal kisha tukaianza safari ya kuelekea kituo cha mabasi yaendayo mikoani cha Ubungo nikiwa na baba mkubwa.

Tulipofika Ubungo, tulianza kutafuta basi la New Force ambalo ndiyo baba mkubwa alikuwa amekata tiketi. Baada ya kuzunguka huku na kule, tukipishana na abiria wengi ambao nao walikuwa wakitafuta mabasi yao, hatimaye tulifanikiwa kulipata. Tukapanda na kwenda kukaa kwenye siti ambazo tiketi zilituelekeza. Baba mkubwa alinunua mikate na zawadi nyingine kwa ajili ya kuwapelekea ndugu zangu. Japokuwa nilikuwa na fedha, sikutaka kununua chochote kama zawadi kwa sababu safari yenyewe sikuipenda.

Niliona imeniharibia kabisa mipango yangu. Ilipofika saa kumi na mbili kamili za asubuhi, basi tulilopanda lilianza kutoka stendi, likawa linakwenda mwendo wa taratibu mpaka lilipofika nje. Likakata kona kulia na kuingia kwenye Barabara ya Morogoro, safari ikapamba moto.

Njia nzima nilikuwa kimya kabisa, nikimuwaza Firyaal na jinsi nilivyofanya uzembe wa kusahau simu yangu nyumbani kwake. Sikujua nitawasiliana naye vipi, kiukweli alikuwa ameniingiza kwenye ulimwengu wa tofauti ambao sikuwahi kuujua kabla.

“Mbona unaonekana una mawazo sana,” baba mkubwa aliniuliza baada ya kuhisi sipo sawa.

“Namfikiria baba yangu, sijui nitamkuta na hali gani?” nilidanganya. Safari ikaendelea mpaka tulipofika Kitonga, basi likasimama na abiria wote tukateremka kwenda kula kwenye Hoteli ya Montfort. Japokuwa nilikuwa na njaa, sikuwa na hamu ya kula kabisa kutokana na mawazo, hata hivyo nilijilazimisha kwani bado tulikuwa na safari ndefu.

Baada ya muda wa kula kuisha, tulirejea kwenye basi na safari ikaendelea. Nakumbuka tulifika Uyole, Mbeya saa 12 jioni, basi likakata kona upande wa kushoto na kuingia Barabara ya Kyela. Safari ikaendelea mpaka Tukuyu ambapo tuliwasili saa moja za jioni.

Tuliteremka kwenye basi na kubeba mizigo yetu, tukapanda bajaj iliyotupeleka mpaka nyumbani kwetu, Makandana. Mimi ndiyo nilikuwa namuongoza baba mkubwa kwani tangu tuhamie makazi mapya, hakuwahi kuja nyumbani.

“Mh! Mnaishi kwenye nyumba nzuri sana siku hizi, siyo kama zamani. Baba yako aliinunua hii nyumba au alijenga?” baba mkubwa aliniuliza huku na yeye akionesha kushtuka kwani nyumba yetu ilikuwa ya kifahari mno. Nilimjibu kuwa aliinunua, akanipachika swali lingine:

“Kwani siku hizi anafanya biashara gani mpaka awe na fedha nyingi kiasi hiki?”

“Hana biashara yoyote zaidi ya kazi yake ya siku zote ya uchungaji,” nilimjibu baba

mkubwa huku tukisaidiana kuteremsha mizigo kwenye Bajaj. Nilielewa mshtuko

alioupata baba mkubwa ulitokana na nini lakini kamwe sikutaka kufungua mdomo

wangu kuzungumza chochote.

Wakati tukiendelea kuteremsha mizigo, ndugu zangu wengine walitoka, waliponiona walinikimbilia na kunikumbatia kwa nguvu, tukasalimiana kisha wakamsalimu baba mkubwa na kutupokea mizigo. Tuliingia mpaka ndani, nikashangazwa na mazingira niliyokutana nayo. Nyumba ilikuwa imepooza sana tofauti na nilivyoizoea.

Muda mfupi baadaye, mama alitoka chumbani na kuja kutusalimia. Alianza kwa kumsabahi baba mkubwa kisha akaja kunikumbatia na kuanza kulia.

Nami nilishindwa kujizuia, nikaanza kulia. Alinisimamisha pale nilipokuwa nimekaa

na kunipeleka chumbani ambapo nilimkuta baba akiwa amelala kama maiti. Hakutingishika wala kufumbua macho, alikuwa ametulia kimya akiwa haelewi chochote kinachoendelea.

Nilimtazama baba kwa dakika kadhaa, nikamgeukia mama na kumuuliza kilichomtokea, akaniambia kuwa alianguka ghafla kanisani wakati akiongoza misa ya Jumapili. Nilimuuliza maswali mengine kadhaa nikitaka kujua kama kuanguka kwake kulikuwa na uhusiano na nguvu za giza alizokuwa anazitumia kanisani kama ilivyokuwa kawaida yake.

Kwa mujibu wa mama, tukio zima la kuanguka kwake lilikuwa limejawa na utata mkubwa, akanisimulia kuwa katika siku za karibuni, aligombana na msaidizi wake wa kanisani, hali iliyosababisha msaidizi huyo ajitenge na kwenda kuanzisha kanisa lake, wakaanza kugombea waumini ambapo kuna wengine walibaki kwa baba na wengine

wakahamia kwa yule msaidizi wake.

Akazidi kuniambia kuwa siku chache kabla ya kuanguka kanisani, alisafiri na kwenda Malawi ambako alilala siku mbili, aliporejea alikuwa na furushi la dawa mbalimbali za mitishamba ambazo nyingine alienda kuzifukia kwenye pembe nne za kanisa wakati nyingine alizihifadhi mle ndani.

Nilimhoji mama kuhusu safari hiyo kwani nilihisi tatizo lilianzia hapo. Kwa bahati nzuri, alinielekeza mtu aliyeongozana na baba kwenye safari hiyo ya Malawi. Bila kupoteza muda nikatoka na kumfuata mzee Mwalyego ambaye kwa mujibu wa mama, ndiye aliyesafiri na baba mpaka Malawi.

Huku nyuma, baba mkubwa naye aliingia chumbani kwa baba kumjulia hali mgonjwa. Nilienda moja kwa moja mpaka nyumbani kwa mzee Mwalyego na kwa sababu naye alikuwa akiishi hapohapo Makandana, nilifika baada ya muda mfupi. Aliponiona alishtuka lakini akawa ni kama anayeficha mshtuko wake.

Nilikaa naye na kuanza kumhoji kuhusu safari yao ya Malawi. Mara kwa mara alikuwa akijikanyaga huku akijitahidi kunificha nisijue kuwa baba alikuwa akitumia ushirikina katika huduma zake za kanisa. Nilimtoa wasiwasi na kumweleza kuwa najua kila kitu na kubwa zaidi nataka kushirikiana naye kuokoa maisha ya baba. Nilipomwambia hivyo akakubali kuniambia ukweli. Akanieleza kuwa kuna masharti baba alikuwa

ameyakosea ndiyo maana akaanguka madhabahuni. Akasema mganga waliyemfuata Malawi alitoa tahadhari mapema juu ya kutokiukwa kwa masharti yake na akashangaa kwa nini baba alifanya hivyo.

“Huu siyo muda wa kulaumiana, nataka baba apone, mengine yatafuata baadaye.”

“Nimekuelewa, mtu pekee anayeweza kumponya baba’ako ni mganga yuleyule aliyetupa dawa kwa mara ya kwanza,” alisema mzee Mwalyego, nikamuuliza jinsi tunavyoweza kufika nyumbani kwake ambapo alinielekeza kila kitu.

Akaniambia anaishi sehemu iitwayo Chipata, Malawi ndanindani kabisa. Nilimshukuru na kuagana naye, nikamwambia aanze kujiandaa kwani tutaondoka muda wowote kwenda huko Chipata. Nilirudi nyumbani na kumuita mama pembeni, nikamueleza kila kitu nilichoambiwa na mzee Mwalyego.

“Kila siku nilikuwa namkataza baba yako kuacha kuitumikia dini ya shetani akawa mbishi, matokeo yake ndiyo haya,” alisema mama na kuanza upya kuangua kilio. Nilimbembeleza na tukakubaliana kuwa tumweleze na baba mkubwa ili awe anafahamu ukweli wa kilichokuwa kinamsumbua baba.

“Inawezekanaje mtu akawa anaendesha kanisa kwa kutegemea nguvu za giza? Kumbe ndiyo maana amepata mafanikio ya ghafla na kununua jumba la kifahari kama hili?” alihoji baba mkubwa huku akionesha kuwa na jazba.

Tulimtuliza na kwa pamoja tukakubaliana kuwa siku inayofuata tumsafirishe baba mpaka Chipata, Malawi kwa mganga wake. Tuliweka nadhiri ya kufanya kila kitu kwa siri ili waumini wake wasijue chochote.

USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi
64 Dini ya Shetani Simulizi
Jiunge kwenye mazungumzo
Chapisha Maoni