Simulizi Mpya
Tidak ada notifikasi baru.

DINI YA SHETANI (3)

Mtunzi: Aziz Hashim

SEHEMU YA TATU
TULIPOISHIA...
“Ni kitabu cha masomo shuleni, naamini nikikipata kitanisaidia sana.”

“Yaani nitoe shilingi elfu saba kwa ajili ya kitabu? Mimi sina fedha, kamuombe baba yako,” alijibu mama huku akionekana kutokuwa na imani na mimi.

KAMA UNASOMA SIMULIZI HII NJE YA APPLICATION YA CnZ Media INSTALL ILI USIPITWE NA MIENDELEZO

SASA TUENDELEE...
Alihisi huenda nataka kumtapeli fedha zake. Aliponiambia nikamuombe baba, nilikataa katakata, nikaendelea kumbembeleza mpaka akakubali. Akatoa noti ya shilingi elfu kumi na kuniambia nimrudishie chenji yake.

Harakaharaka nilitoka na kurudi stendi, mahali nilipokiona kile kitabu, nikampa yule muuza magazeti fedha yake, akanipa chenji na kile kitabu. Nikakificha kwenye shati nililokuwa nimevaa na kurudi nyumbani haraka, sikutaka mtu yeyote akione. Nilienda kumpa mama chenji yake kisha nikaingia chumbani na kujifungia.

“Hicho kitabu chenyewe kipo wapi?” nilimsikia mama akiniuliza lakini nilijifanya kama simsikii. Sikutaka ajue ni kitabu gani nilichokuwa nimekinunua. Nilianza kukitazama vizuri kile kitabu kuanzia ukurasa wa kwanza hadi wa mwisho. Ama kwa hakika kilikuwa na mada zilizonivutia sana.

Bila kupoteza muda nikaanza kusoma mada motomoto zilizokuwa ndani ya kitabu kile, kuanzia ile ya kwanza iliyokuwa inauliza wewe ni nini? Nilisoma kwa makini lakini cha ajabu, kila nilichokuwa nakisoma kilikuwa ni kama kinanichanganya kwani sikuwahi kukisikia sehemu yoyote wala kukiwaza.

Naikumbuka vizuri mada ya kwanza kuhusu utu na thamani ya binadamu ambapo mwandishi alifafanua kwa kina tafsiri ya mtu, akili na roho. Nikajikuta narudiarudia mada moja zaidi ya mara tatu ili niweze kuelewa.

“Wewe ni nini? Ni mwili wako, akili zako, uzuri wako, mali au elimu yako? Kwa nini mtu akifa tunasema tunaenda kuuzika mwili wa fulani, huyo anayeumiliki mwili ni nani?” hayo yalikuwa baadhi ya maswali magumu ambayo ama kwa hakika yalinifanya nijikune kichwa. Uelewa wangu ukaanza kufunguka.

Niliendelea kusoma juu ya umuhimu wa kila mtu kujitambua na kufahamu thamani yake na malengo yaliyomleta duniani. Nikasoma kuhusu nguvu zinazozalishwa na watu bila ya wao wenyewe kujua kuanzia kwenye kauli, mawazo na matendo.

Mwandishi akafafanua kwa kina namna watu wanavyoshindwa kuzitumia nguvu walizojaaliwa ndani ya akili zao na kujikuta wakiishia kuishi maisha ya kifukara mpaka wanakufa. Akaeleza kwa nini watu wengine wanaishi maisha ya kifukara, mlo wa siku moja ukiwa ni tatizo kubwa kwao ilhali kuna wanaoishi kifahari, wakila, kunywa na kusaza.

“Wewe ndiyo uliyechagua aina ya maisha unayotaka kuishi, ukiamua kuwa tajiri, bila shaka utakuwa tajiri kwa sababu akili na mawazo yako vinazalisha nguvu kubwa ambayo inaweza kuyafanya yale uliyokuwa unayafikiria yatokee katika maisha halisi,” ilisomeka sehemu ya kitabu kile.

Niliendelea kushangaa kwani kila neno nililokuwa nalisoma kwenye kitabu kile, lilikuwa likiniamsha ari ndani ya nafsi yangu kutaka kufahamu kwa undani kilichokuwa kinazungumziwa. Mwandishi aliendelea kutoa mifano jinsi binadamu alivyojaliwa uwezo mkubwa wa kufikiri na kufanya kila analofikiri litokee.

Alitolea mfano watu wenye uwezo wa kupindisha vitu kama kijiko au chuma chochote kwa kukitazama tu, akazungumzia pia watu wenye uwezo wa kupasua glasi kwa kuitazama au kuhamisha kitu kimoja kwenda sehemu nyingine. Nilijiuliza kile kilichokuwa kinazungumziwa ni uchawi au nguvu za mawazo? Mwandishi alinijibu katika ufafanuzi kuwa hakuna uchawi katika suala lile na kila mmoja anaweza kufanya akifundishwa.

Nilipoendelea kusoma, kuna sehemu mwandishi alitoa mfano kwa kila msomaji kujaribu kujipima kama ana nguvu za mawazo kiasi gani. Na mimi nikajaribu.

Nilikaa sakafuni na kutulia, nikawa navuta pumzi ndefu na kuzitoa taratibu kupitia mdomo huku nikiwa nimeweka uzingativu wa kutosha akilini mwangu. Nikiwa katika hali ile, nilishangaa nikijihisi kitu tofauti kabisa kwenye mwili wangu. Nikawa ni kama nimehama kwenye ulimwengu wa kawaida na kwenda mahali nisipopajua.

Nilishtuka kwa nguvu hadi nikaanguka sakafuni, nikawa nafikicha macho ili kuhakikisha kama sikuwa kwenye ndoto. Nilikaa vizuri kisha nikaendelea kukisoma kile kitabu, safari hii nikiwa naelewa na kuamini kila nilichokuwa nakisoma kwani nilihakikisha mwenyewe kuwa kile kilichokuwa kinaelezewa hakikuwa porojo bali ukweli mtupu.

Nikiwa naendelea kukisoma kile kitabu, kumbe baba alikuwa amezunguka nyuma ya nyumba na kuja mpaka kwenye dirisha la chumba changu, akawa ananiangalia nafanya nini kwani nilikuwa nimetulia kwa muda mrefu.

“Unafanya nini? Aliniuliza kwa sauti ya ukali.”

“Najisomea baba, mitihani imekaribia,” nilimjibu huku nikijitahidi kukificha kile kitabu ili asikione.

“Hebu lete hicho kitabu,” aliniambia, nikawa nasita kama nimpe au la lakini kwa jinsi alivyokuwa ananitazama kwa ukali, ikabidi nifanye kama alivyoniambia. Nikampa kile kitabu huku nikitetemeka kuliko kawaida.

“Haaa! Unasoma kitabu cha kichawi? Unataka kujiunga na jamii za siri na dini ya shetani siyo? Hujui kama mimi baba yako ni mtumishi wa Mungu? Kwa nini unataka kunitia aibu?” alisema baba huku akiendelea kufunua kurasa za kile kitabu. Sikumjibu kitu, nikawa naendelea kutetemeka kwa hofu.

Akiwa na hasira za hali ya juu, nilimshuhudia akikichanachana kile kitabu, akatupatupa karatasi huku na kule huku akinitolea macho ya ukali. Kwa kuwa alikuwa upande wa nje, aliniambia nisitoke mle chumbani nimsubiri, nikajua anataka kuja kuniadhibu vikali, nikawa nafikiria namna ya kumkimbia.

Nilipata akili ya kukimbia haraka kabla baba hajaingia ndani na kuja kuniadhibu, nikatoka na kuingia chumba kingine, nikajifungia mlango kwa ndani. Nilimsikia baba akiingia ndani na kusukuma mlango kwa nguvu, nikawa natetetema kwa hofu.

“Yuko wapi?” nilimsikia baba akiuliza kwa jazba. Nilijibanza kwenye kabati la nguo la ukutani na kujifungia, nikawa namuomba Mungu asinione kwani kwa jinsi nilivyokuwa namfahamu, angeniadhibu vikali.

“Kwani kuna nini tena?”

“Huyu mwanao mshenzi sana, yaani anajifunza mambo ya dini ya shetani ndani ya nyumba yangu, leo atanikoma.”

“Mambo ya dini ya shetani? Ndiyo mambo gani hayo,” mama aliuliza huku akiwa haelewi kinachoendelea. Nilimsikia baba akimfafanulia kuwa amenikuta nikiwa nasoma na kujifunza mambo ya kichawi kwenye kitabu.

Mama alimuuliza yeye amejuaje kama nilichokuwa nakisoma kinahusu dini ya shetani? Nikawasikia wakianza kufokeana wenyewe kwa wenyewe. Nilishukuru sana mama kuingilia ugomvi ule kwani hiyo ndiyo ilikuwa ahueni yangu. Wakaendelea kujibizana, baba akatoka na kwenda kukusanya karatasi za kile kitabu changu alichokichanachana.

Akarudi ndani na kumuonesha mama, akawa anaziangalia huku na yeye akishangaa. Baadaye nilisikia wakianza kuzungumza vizuri, nikajua wameshapatana, hasira za baba zikawa zimepungua, nikatoka mafichoni na kufungua mlango.

“Njoo hapa,” nilimsikia baba akisema. Kumbe wakati nafungua mlango alikuwa ameshaniona, nikawa sina ujanja zaidi ya kujipeleka mwenyewe kwake. Mkononi alikuwa ameshika fimbo mbili ngumu, nikasogea huku nikiendelea kuomba kimoyomoyo.

Tofauti na nilivyotegemea, baba hakunipiga bali aliutumia muda ule kuzungumza na mimi kwa busara. Akaniambia nimshukuru mama kwani bila yeye kuingilia kati na kuniombea msamaha, ningekiona cha mtema kuni. Aliendelea kuzungumza na mimi kwa kirefu, akaniambia sitakiwi kujifunza au kushiriki kwa namna yoyote mambo yanayohusu imani ya dini ya shetani.

Kiukweli sikumuelewa anamaanisha nini kwani kile nilichokuwa nikikisoma kwenye kile kitabu alichokichana, hakikuwa na matatizo yoyote ukilinganisha na matendo yake aliyokuwa anayafanya gizani.

Hata hivyo, sikutaka kubishana naye kwa chochote, nikawa namsikiliza mpaka alipomaliza kuongea. Alipomaliza aliniambia niondoke ili waendelee kuzungumza na mama.

Kiukweli nilichukizwa sana na kitendo chake cha kunichania kitabu changu, nikajiwekea nadhiri kuwa lazima nitaenda kununua kingine.

Siku iliyokuwa inafuatia ilikuwa ni Jumapili, baba akatuambia tuvae vizuri kwa sababu ataenda kututambulisha rasmi kwenye kanisa jipya mbele ya waumini wengi zaidi tofauti na kule kijijini Itete.

Wenzangu walifurahia sana lakini kwangu mimi ilikuwa tofauti. Baada ya kugundua mambo aliyokuwa anayafanya baba, nilikosa imani naye kabisa, nikawa nachukizwa na tabia yake ya kuwadanganya watu, tena wengine wakiwa wamemzidi umri.

Jumapili ilipofika, kama baba alivyokuwa ametuambia, wote tulivaa suti mpya tulizokuwa tumenunuliwa, mama akavaa gauni lake jipya na kujifunga kilemba kama wafanyavyo wanawake wa Kinigeria, tukaondoka mpaka kanisani.

Baba alinipa Biblia yake nimshikie, akaniambia nisiende kukaa upande waliokuwa wamekaa waumini wengine pamoja na ndugu zangu, akaniambia nitakaa nyuma ya madhabahu. Sikuelewa kwa nini aliniambia vile lakini nilitii, nikawekewa kiti nyuma ya madhabahu na baba akaanza kuongoza ibada akitumia Biblia nyingine tofauti na ile.

Ulipofika muda wa kuwaombea wagonjwa na watu wenye shida mbalimbali, baba alishuka madhabahuni na kuja pale nilipokuwa nimekaa, akachukua ile Biblia niliyokuwa nimeishika, akarudi kwenye madhabahu na kuanza kufanya maombezi.

Wagonjwa na wenye shida mbalimbali walijitokeza kwa wingi lakini miongoni mwao, kuna mmoja alinishangaza sana. Jina lake alikuwa anaitwa Sinai na wakati tukiishi kijijini Itete, alikuwa akija nyumbani mara mojamoja na kuzungumza na baba. Kilichonishangaza ni kwamba alikuwa akitembelea magongo huku miguu yake ikiwa kama mtu mwenye ulemavu.

Nilishangaa sana Sinai amepata ulemavu lini na ilikuwaje kwani mara mwisho kumuona, hata miezi sita haikuwa imeisha. Nikanyamaza ili nijionee kitakachotokea. Baba aliteremka kwenye madhabahu na kusogea pale mbele wagonjwa walipokuwa wamesimama.

Nikamuona akiwapita wale wengine na kwenda moja kwa moja kwa Sinai, akaanza kumhoji maswali huku akimuwekea kipaza sauti mdomoni, watu wote waliokuwa kanisani wakawa wanasikia alichokuwa anakisema.

“Nilizaliwa nikiwa mlemavu, mama yangu alirogwa akiwa na mimba yangu, naomba uniombee nipone,” alisema Sinai, nikazidi kupigwa na butwaa kwani nilikuwa nikimfahamu vizuri na hakuwahi kuwa mlemavu.

Baba alimuwekea mikono kichwani, akaanza kumuombea huku akinena kwa lugha, nikaona Sinai ameanza kuongea hovyo kama mtu aliyepandwa na mapepo, kisha akaanguka chini. Baba akamshika miguu aliyodai ina ulemavu, akaendelea kuomba kwa nguvu.

Muda mfupi baadaye Sinai alijifanya amezinduka, akamshikilia baba mwilini na kujaribu kusimama, eti akaanza kusema miguu yake iliyokuwa na ulemavu wa kuzaliwa nao imepata nguvu baada ya kuombewa, akatupa magongo na kuanza kurukaruka kwa furaha.

USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi
64 Dini ya Shetani Simulizi
Jiunge kwenye mazungumzo
Chapisha Maoni