DINI YA SHETANI (2)
Zephiline F Ezekiel
---
Jina: DINI YA SHETANI
Mtunzi: Aziz Hashim
SEHEMU YA PILI
TULIPOISHIA...
TULIPOISHIA...
Tuliendelea na kazi mpaka tukamaliza kushusha vyombo vyote, mama akamlipa dereva na utingo wake gharama walizokubaliana, wakawasha gari na kuondoka. Wale vijana waliotusaidia kushusha vyombo pia walipewa kifuta jasho, wakaondoka na kutuacha mimi, ndugu zangu na mama tukiendelea kupanga vitu.
KAMA UNASOMA SIMULIZI HII NJE YA APPLICATION YA CnZ Media INSTALL ILI USIPITWE NA MIENDELEZO
SASA TUENDELEE...
Kikubwa nilichokibaini ni kuwa vyombo vyetu tulivyotoka navyo kule kijijini havikuwa na hadhi ya kuwekwa kwenye nyumba ile ya kisasa. Viti vichakavu, vitanda na samani nyingine kuukuu tulizokuwa nazo, zilionekana kuwa za hadhi ya chini sana
ukilinganisha na thamani ya ile nyumba ambayo sakafu yote ilikuwa imewekwa marumaru za kisasa.
Tuliendelea kuishangaa ile nyumba na mazingira yake ya nje, kila mmoja alikuwa na furaha kubwa ya kuhamia mjini, tena kwenye jumba la kifahari kama lile. Wakati ndugu zangu wakiendelea kufurahia, mimi bado nilikuwa najiuliza maswali ambayo sikupata majibu kirahisi.
Niliendelea kushangaa iweje baba awe anajihusisha na mambo yakishirikina wakati yeye ni mchungaji anayeaminiwa na waumini wengi, tena akiwa na uwezo wa kufanya miujiza kama kuponya wagonjwa, kukemea mapepo na mambo mengine mengi ambayo katika hali ya kawaida ni ngumu kufanywanamtu asiye na upako.
“Ina maana baba anamuabudu shetani? Lakini mbona anakemea mapepo kwa kutumia jina la Mungu? Mbona sielewi kinachoendelea?” nilijiuliza lakini hakukuwa na wa kujibu maswali yangu.
“Mbona mwenzetu unaonekana kuwa mbali kimawazo? Au hujafurahia kuhamia kwenye jumba la kifahari kama hili?” mama aliniuliza, safari hii akiwa amenikazia macho. Nilijaribu kumdanganya kwa kujichekesha lakini alinibana na kuniambia kuwa
amegundua tofauti tangu wakati tukihamisha vyombo, akanitaka nimweleze ukweli.
“Mimi ndiyo mama’ako, kama utashindwa kuniambia ukweli unafikiri utamwambia nani? Niambie mwanangu.”
“Mama kuna kitu nimekiona wakati tunahamisha vitu kule nyumbani kimenikosesha raha kabisa.”
“Kitu gani mwanangu? Naona kweli umekosa raha.”
“Nimeona vitu kama vifaa vya kichawi vikiwa chini ya kitanda chenu na baba, nikiwa naviangalia baba akanikuta na kunitishia, akaniambia kuwa nisimwambie mtu yeyote.”
“Hicho ndicho kilichokuchanganya?”
“Ndiyo mama, kwani baba si mtumishi wa Mungu, kwa nini anakaa na vitu vya kichawi ndani? Waumini wake wakijua itakuwaje?”
“Mwanangu haya mambo we yaache kama yalivyo, mimi mwenyewe nimekorofishana sana na baba yako kuhusu hilo suala lakini baadaye nikaamua kunyamaza, kama
alivyokwambia, na mimi nakuomba uitunze siri hii kwani watu wengine wakijua itakuwa hatari sana.”
Mama aliendelea kuniambia mambo mengi ambayo sikuwa nayajua hapo awali, akanisisitiza kuitunza siri ile huku akiahidi kuendelea kuzungumza na baba ili atambue makosa anayoyafanya. Tukiwa tunaendelea kuzungumza, tulisikia mtu akigonga mlango, mama akatoka kwenda kumfungulia. Alikuwa ni baba.
Baada ya kuingia, baba alitupa pole kwa kazi ya kushusha mizigo na kupanga vitu vizuri mle ndani, akatuahidi kuwa kesho yake atatupa zawadi nzuri, pia akaahidi kuwa
tutaenda kununua samani mpya kama masofa ya kisasa, makabati na vitu vingine vinavyoendana na hadhi ya ile nyumba tuliyokuwa tunaishi.
Wakati akizungumza hayo, akili yangu nilikuwa nimeielekeza kwenye mkoba wa ngozi aliokuwa ameubeba baba. Mama alipotaka kumpokea, alikataa na kuendelea kuubeba vilevile, nikajua kuwa lazima vile vitu vya kichawi atakuwa ameviweka mle na ndiyo maana aliteremka kwenye gari tukiwa njiani kuhamia makazi mapya.
Baada ya muda, aliondoka na kuelekea chumbani huku ule mkoba akiwa ameubeba vilevile. Kwa kuwa nilikuwa na shauku kubwa ya kutaka kuona mahali anapoenda kuuhifadhi mkoba ule, alipoinuka kuelekea chumbani, na mimi nilisimama na
kujifanya nataka kwenda chooni.
Harakaharaka nilitoka nje na kuzunguka upande kulipokuwa na dirisha la chumba chao. Kwa kuwa bado tulikuwa hatujaweka mapazia, niliweza kuona ndani bila shida, nikatulia na kuanza kuangalia kilichokuwa kinaendelea ndani.
Nilimuona baba akiwa amepiga magoti na kuweka mikono kama mtu anayesali, huku ule mkoba wake akiwa ameuweka mbele yake, akakaa katika hali ile kwa zaidi ya dakika kumi, kisha nikamuona akiinuka na kufungua begi kubwa la nguo, akatoa joho lake la kichungaji na kulivaa juu ya nguo alizokuwa amezivaa.
Kwa uangalifu mkubwa akaanza kufungua ule mkoba, akatoa vitu vyote vilimokuwemo, kibuyu kikubwa kilichokuwa kimefungwa shanga nyeupe, nyeusi na nyekundu upande wa juu, fuvu la kichwa, pembe kubwa la mnyama ambaye sikumtambua, dawa kibao za mitishamba na vikorokoro vingine vya kutisha.
Akavipanga sakafuni, akakaa akiwa amevaa lile joho lake na kuanza kuzungumza na kile kibuyu kwa lugha ambayo sikuielewa. Mara kile kibuyu kikaanza kutoa moshi mweupe, nikajikuta nikipiga kelele huku nikitetemeka mwili mzima.
Baba alishtuka sana kusikia sauti ya mtu pale dirishani, akaacha kila alichokuwa
anakifanya na kusimama kwa jazba, akageukia pale dirishani nilipokuwa nimejificha.
Kwa kasi ya ajabu niliinama chini na kutimua mbio kukwepa baba asije akaniona, nikafanikiwa kuingia ndani bila mtu yeyote kugundua kuwa nilikuwa nimetoka nje, nikapitiliza moja kwa moja chooni na kujifungia.
Nikawa nahema kama mwanariadha wa Marathoni. Kwa mbali nikamsikia baba akifungua mlango wa chumbani kwake na kutoka kwa hasira hadi sebuleni.
“Saba yuko wapi?” aliuliza kwa jazba, nikamsikia mama akimjibu kuwa nimeenda chooni. Hakutaka kuamini, akaja mpaka chooni ambapo alijaribu kuusukuma mlango kwa nguvu ili ahakikishe kama kweli nilikuwa chooni.
“Kuna mtu,” nilijibu huku nikijifanya sihafamu chochote kinachoendelea.
“Ni wewe Saba!”
“Ndiyo baba, tumbo la kuendesha linanisumbua,” nilimjibu bila kufungua
mlango, nikamsikia akitembea harakaharaka kuelekea nje. Alifungua mlango na kuubamiza, akazunguka nyuma ya nyumba yetu huku akionekana kuwa na hasira kupita kiasi.
Nilimshukuru Mungu kwa akili niliyoitumia kwani kama angenikuta kule nje, sijui hata angenifanya nini.
“Kwani kuna nini mume wangu,” mama aliuliza mama huku naye akionekana kushtushwa na hali aliyokuwa nayo baba.”
“Kuna vibaka wanachungulia madirishani, hawa vijana wa hapa Tukuyu
wahuni sana,” alisema huku akimulika huku na kule kwa kutumia tochi kubwa. Licha ya kuzunguka karibu nyumba nzima, baba hakumuona mtu yeyote, akarudi ndani huku akiwa amefura kwa hasira.
Kwa muda huo na mimi nilikuwa tayari nimeshatoka chooni, nikaenda kukaa
sebuleni na ndugu zangu. Baba alirudi ndani huku mama akiwa anamfuata nyuma, akapitiliza hadi chumbani kwake na kujifungia tena mlango, sisi tukabaki na mama ambaye aliendelea kutusimulia hadithi na mambo mbalimbali ya kufurahisha.
Ilipofika saa tano za usiku, mama alituaga na kutuambia kila mmoja aende kulala, na yeye akainuka na kuelekea kwenye kile chumba alichokuwemo baba. Tulienda kulala lakini kichwa changu bado kiliendelea kutawaliwa na mawazo mengi, nikawa najiuliza maswali ambayo sikuyapatia majibu. Baadaye usingizi ulinipitia.
Kulipopambazuka, nilikuwa wa kwanza kuamka. Muda mfupi baadaye mama naye aliamka, tukawa tunasaidiana kufanya usafi wa nyumba na mazingira ya nje. Wakati tukiendelea kufanya usafi, mama aliniita na kuniuliza jambo.
“Wewe ndiyo ulikuwa unamchungulia baba yako jana?”
“Hapana mama, siyo mimi!”
“Acha uongo we mtoto, hizi nyayo za miguu mbona zinafanana na za kwako? Unataka nikamwambie baba yako?”
“Basi mama usimwambie baba, ni kweli mimi ndiyo nilikuwa namchungulia,” nilimwambia mama kwa sauti ya chini huku nikimsihi asimwambie baba. Kutokana na jinsi mama alivyokuwa ananipenda, alikubali kunifichia siri ile, tukasaidiana kufuta
nyayo za miguu yangu ambazo zilikuwa zimejichora ardhini kwenye matope, ikabaki kuwa siri yetu.
“Mama kusema ukweli nimeanza kumuogopa sana baba, mambo niliyoyaona jana yalinitisha sana, sitaki kuamini kama kweli baba anashiriki kwenye ushirikina wakati ni mchungaji.”
“Kwani uliona nini mwanangu?” mama aliniuliza huku akiacha kila alichokuwa anakifanya, akanisogelea na kuanza kunipapasa mgongoni kwa upendo. Nilimwambia kila nilichokiona, akaniambia nisiwe na wasiwasi kwani ushirikina wa baba haukuwa kwa ajili ya kutudhuru sisi bali kwa ajili ya kazi yake.
Aliendelea kunibembeleza na kunisihi nisimwambie mtu yeyote juu ya kile nilichokiona, akaniuliza kama sikuwa nayafurahia mabadiliko ya kimaisha tuliyokuwa tunapitia, kutoka ufukara uliopindukia hadi utajiri tulioanza kuupata. Nilimjibu kuwa nafurahia lakini naogopa hatua watakayochukua waumini wake siku wakiujua ukweli
kuwa baba huwa anatumia nguvu za giza.
Mama alinihakikishia kuwa kamwe hawataweza kugundua chochote, tukaendelea kufanya usafi. Tulipomaliza, mama aliandaa chai kisha tukawaamsha baba na ndugu zangu wengine, tukajumuika pamoja kupata kifungua kinywa. Wakati tukiendelea
kupata kifungua kinywa, baba alikuwa akinitazama kwa jicho kali kama anayesema ‘ole wako umwambie mtu juu ya ulichokiona’.
Kila macho yetu yalipokuwa yakikutana, nilikuwa nikiyakwepesha ya kwangu na kutazama chini, tukaendelea kupata kifungua kinywa mpaka tulipotosheka. Baada ya muda, nilimuaga mama kuwa nakwenda stendi kutafuta magazeti kwani nilikuwa napenda sana kusoma Gazeti la The Bongo Sun.
Aliniruhusu na kunipa shilingi elfu moja, akaniambia niwe makini barabarani. Nilitoka na kuanza kuelekea kwenye stendi ya mabasi ya Tukuyu. Nilipandisha kilima kidogo kutoka kule tulikokuwa tunaishi kwani Mji wa Tukuyu umejawa na milima na mabonde, muda mfupi baadaye nikafika stendi na kwenda kwenye meza ya kuuzia magazeti .
Nikanunua Gazeti la The Bongo Sun lakini pale juu ya meza ya magazeti, niliona kitu kingine ambacho kilinivutia sana. Kilikuwa ni kitabu kilichokuwa na picha ya fuvu na maandishi makubwa yaliyoandikwa Uchawi; Unavyofanya kazi na jinsi ya kujikinga kilichoandikwa na mwandishi mahiri na mtaaalamu wa elimu ya utambuzi, Munga Tehenan.
Nikajikuta navutiwa nacho sana, nikauliza bei. Aliponitajia, niliondoka haraka na
kurudi nyumbani kwa lengo la kwenda kumuomba mama fedha ili nikakinunue.
Niliporudi nyumbani, sikumkuta mama, ikabidi nikae kumsubiri. Baada ya takribani saa mbili kupita, mama alirudi ambapo kitu cha kwanza nilichokifanya ilikuwa ni kumueleza shida yangu.
“Ukanunue kitabu? Kitabu gani?”
“Ni kitabu cha masomo shuleni, naamini nikikipata kitanisaidia sana.”
“Yaani nitoe shilingi elfu saba kwa ajili ya kitabu? Mimi sina fedha, kamuombe baba yako,” alijibu mama huku akionekana kutokuwa na imani na mimi.
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni