DINI YA SHETANI (13)
Zephiline F Ezekiel
---
Jina: DINI YA SHETANI
Mtunzi: Aziz Hashim
SEHEMU YA KUMI NA TATU
TULIPOISHIA...
TULIPOISHIA...
Tulimtuliza na kwa pamoja tukakubaliana kuwa siku inayofuata tumsafirishe baba mpaka Chipata, Malawi kwa mganga wake. Tuliweka nadhiri ya kufanya kila kitu kwa siri ili waumini wake wasijue chochote.
KAMA UNASOMA SIMULIZI HII NJE YA APPLICATION YA CnZ Media INSTALL ILI USIPITWE NA MIENDELEZO
SASA TUENDELEE...
Alfajiri na mapema tuliamka kabla watu wengine hawajaamka, tukaanza kujiandaa kwa safari. Tulikubaliana kuwa mimi, mama, baba mkubwa na mzee Mwalyego ndiyo tusafiri na baba hadi Chipata nchini Malawi. Kwa kuwa baba alikuwa na hali mbaya, akiwa hawezi kufanya chochote zaidi ya kulala kama mfu, ilibidi tumsafirishe kwa gari maalum la kukodi.
Mama alimudu kulipia gharama za kukodi gari kwani hali ya kiuchumi ya familia yetu ilikuwa imeimarika sana kutokana na fedha alizokuwa anazipata baba ikiwa ni sadaka pamoja na michango mingine kutoka kwa waumini, ikiwemo fungu la kumi. Tulipomaliza kujiandaa, mama alimpigia simu dereva wa gari alilokodi ambaye alifika mpaka nyumbani kwetu, Makandana na kusimamisha gari nje.
Mimi, baba mkubwa na mzee Mwalyego tukasaidiana kumbeba baba mpaka kwenye gari, siti moja ikateguliwa na kuwa kama kitanda, tukamlaza na kumfunika, na sisi tukapanda na kila mmoja akakaa kwenye siti yake. Mzee Mwalyego alikaa mbele na dereva kwa sababu yeye ndiyo alikuwa anaifahamu njia vizuri.
Baada ya muda, safari ilianza, tukaenda mpaka tulipoikuta barabara kuu ya kuelekea Kyela, dereva akakata kona upande wa kulia na kuingia barabarani, safari ikapamba moto. Ilituchukua zaidi ya saa mbili kufika mjini Kyela, dereva akanyoosha na barabara iliyokuwa inaelekea Kasumulu, kwenye mpaka kati ya Tanzania na Malawi.
Kabla ya kufika mpakani, mzee Mwalyego alimwambia dereva asimamishe gari, akatueleza kuwa tukishavuka mpaka, fedha za Kitanzania hazitumiki tena.
“Inabidi tubadilishe fedha ili kupata Kwacha za Malawi,” alisema mzee Mwalyego, mama akafungua pochi yake na kutoa bunda la noti nyekundunyekundu. Mimi nikadakia na kumuuliza kiwango cha kubadilishia fedha kwani nakumbuka nikiwa Dar niliwahi kumsikia Firyaal akisema kuwa fedha ya Malawi ina thamani kubwa kuliko ya Tanzania.
Mzee Mwalyego akanijibu kuwa shilingi elfu moja ya Tanzania ilikuwa ni sawa na wastani wa Kwacha mia moja za Malawi. Nilipigwa na butwaa kugundua kuwa ni kweli wenzetu fedha yao ilikuwa na thamani kubwa kuliko ya Kitanzania.
Kwa kuwa hakuna aliyekuwa na passport, ilibidi mzee Mwalyego ambaye alikuwa mzoefu na mpaka wa Kasumulu, apewe fedha na mama ambazo alizishika mkononi kwa ajili ya kuwahonga maafisa uhamiaji waliokuwa pale mpakani.
“Mabwanji soja,” (Habari mwanajeshi) Mzee Mwalyego alimsalimia askari mmoja kwa lugha ya Kichewa iliyokuwa inatumika sana nchini Malawi, naye akamjibu:
“Bwino, kulichi kung’anda?” (Nzuri, vipi za nyumbani?)
“Kulichete,” (Salama) alijibu mzee Mwalyego huku akifungua mlango na kutoka kwenye gari.
Niliwasikia wakiendelea kuzungumza kwa Kichewa, lugha ambayo mzee Mwalyego alionesha kuifahamu vizuri. Baada ya muda, niliona Mzee Mwalyego akimshikisha fedha yule askari, akarudi na kutufungulia geti, akatuelekeza sehemu ya kupita mpaka
tulipovuka eneo lile la mpakani.
“Penye uzia penyeza rupia,” alisema mzee Mwalyego kwa masihara, wote ndani ya gari tukacheka isipokuwa baba ambaye hakuwa akielewa kinachoendelea. Safari iliendelea, tukawa tunachanja mbuga kuelekea Chipata. Safari haikuwa nyepesi kwani kuna maeneo dereva alilazimika kusimamisha gari pembeni ya barabara kutokana na mvua kubwa iliyokuwa inanyesha na kusababisha maji kujaa barabarani.
Ilituchukua siku nzima kusafiri kuelekea Chipata, mji uliokuwa jirani na mpaka kati ya Malawi na Zambia, ndanindani kabisa. Baada ya safari ngumu hatimaye tuliwasili Chipata, sote tukiwa tumechoka sana, njaa na kiu vikitutesa.
Baada ya kufika mjini Chipata, mzee Mwalyego alituelekeza kuwa mganga wao alikuwa akiishi ndani ya pori kubwa la Chintengo, nje kabisa ya mji huo wa Chipata.
Tulisimama kwa muda kwenye Mji wa Chipata kwa ajili ya kununua mahitaji muhimu kwani mzee Mwalyego alitueleza kuwa huko tunakokwenda hakuna duka wala genge, ikabidi tununue mahitaji yetu yote ikiwemo chakula na kuyapakiza kwenye gari, tukaendelea na safari.
Ilibidi dereva awe anaendesha gari kwa mwendo wa taratibu kwani ulikuwa ni msimu wa mvua na udongo wa eneo hilo ulikuwa ukituamisha maji na kunata sana. Baada ya muda, tulifika mahali palipokuwa na geti la miti, ndani kabisa ya msitu, mzee Mwalyego akatuambia kuwa tayari tumefika kwenye himaya ya mganga, tukalazimika kuliacha gari pale na kuteremka kwani hakukuwa na barabara ya kuwezesha gari kupita.
Tukasaidiana kumteremsha baba kisha tukambeba juujuu na kuanza kuelekea kwa mganga. Ilibidi tuwe tunapokezana kwani baba alikuwa mzito sana, mzee Mwalyego akawa anatuongoza kupita kwenye njia nyembamba iliyosongwa na miti mikubwa iliyofungamana. Msitu wa Chintengo ulikuwa unatisha sana, huku milio ya ndege wa ajabu ikisikika.
Tayari kigiza cha jioni kilishaanza kuingia. Baada ya kufika kwenye mti mkubwa
wa mbuyu, mzee Mwalyego alituelekeza kumshusha baba, tukafanya hivyo ambapo
alituambia sote tuvue viatu kwani tulifika eneo ambalo kwa mujibu wa mganga, ni sehemu takatifu ya mizimu.
Mzee Mwalyego akapiga magoti na kuanza kusali kwa lugha ambayo hakuna aliyeielewa, akatuelekeza na sisi tupige magoti kama yeye. Wakati tukiwa tumepiga magoti, Mwalyego akiendelea kutamka maneno ya ajabuajabu, tulisikia sauti kubwa ikitoka kwenye ule mti.
Ilikuwa kubwa kiasi cha kufanya ndege waliokuwa kwenye miti ya jirani wakimbilie mbali, baada ya sauti ile kusikika, tukamsikia mzee Mwalyego akishukuru kwa kilugha kisha akatuelekeza tusimame, tukambeba baba na kuendelea kusonga mbele.
“Kabla ya kumfikia mganga ni lazima uombe kwanza ruhusa kwa mizimu, hicho ndiyo kitu tulichokuwa tunakifanya pale kwenye mti mkubwa,” alisema mzee Mwalyego huku akituongoza njia kuelekea kwa mganga. Kwa mbali tukaanza kuona moshi angani kuashiria kuwa tulikuwa tumekaribia kufika nyumbani kwa mganga.
Cha ajabu, baba ambaye safari nzima alikuwa amelala kama mfu, alianza kupiga chafya mfululizo tukiwa tumembeba. Kama hiyo haitoshi, alianza kupepesa macho yake kama
anayetaka kuyafumbua, sote tukapigwa na butwaa. Hatua chache mbele, tuliwakuta wanaume wawili waliokuwa wamejifunga mashuka mekundu na kujifunga vitambaa vyeusi kichwani wakiwa na machela ya miti na ngozi, inavyoonesha walishapata taarifa za ujio wetu.
Wakasalimiana na mzee Mwalyego kwa lugha ya Kichewa kisha wakaiweka ile machela chini, wakamlaza baba kisha wakaibeba mabegani mwao, angalau na sisi tukapumua. Wakatangulia mbele na sisi tukawa tunawafuata kwa nyuma. Mzee Mwalyego aliendelea kuzungumza nao huku wakionekana kumfahamu vyema.
Baada ya kutembea umbali wa mita kadhaa, tulitokezea kwenye eneo lenye uwazi, katikati kukiwa na nyumba ya miti iliyoezekwa kwa makuti. Wale wanaume walipitiliza mpaka ndani na baba, wakatuelekeza sisi tukae nje kwenye viti maalum vilivyotengenezwa.
Tayari giza lilishaingia, tukakaa huku tukiwa na shauku kubwa ya kumuona huyo mganga na kujua nini hatima ya baba. Baada ya dakika kadhaa, wale wanaume walitoka wakiwa na machela tupu, mmoja akamfuata mzee Mwalyego na kumwambia aingie ndani.
Alipoingia, tukaanza kusikia watu wakipiga manyanga na kuimba nyimbo za asili. Ilivyoonesha, ndani kulikuwa na watu wengi sana, wanaume kwa wanawake kwani
sauti zao zilisikika vyema. Shauku ya kutaka kujua kilichokuwa kinaendelea ikazidi kupanda. Baada ya muda, alitoka mwanamke mmoja aliyekuwa amejifunga kaniki, akauliza mke wa mgonjwa alipo.
Mama akasimama na kumfuata, wakaingia naye ndani. Walikaa ndani kwa muda, baadaye nikamuona yule mwanamke ametoka tena nje na kuuliza mahali nilipokuwa
nimekaa. Nilishtuka kwa sababu aliniita kwa jina, nikasimama harakaharaka na kumfuata pale mlangoni. Akanitazama kwa macho ya udadisi kisha akaniuliza tena kama mimi ndiyo Mkanwa, nilimuitikia kisha akaniambia nimfuate.
Tuliingia ndani na kupita kwenye kiambaza chembamba kilichokuwa na giza, tukakata kona upande wa kushoto kisha tukatokezea kwenye ukumbi mkubwa uliokuwa na watu wengi ndani yake. Nilishtushwa na ukubwa wa ukumbi wenyewe kwani kwa nje, nyumba ile haikuwa inaonekana kama ni kubwa kiasi kile.
Pia nilishtushwa na idadi kubwa ya watu waliokuwa ndani ya nyumba ile, wakiwa wamekaa kwenye busati kubwa na kujipanga kwa mpangilio mzuri. Mbele kabisa kulikuwa na kiti kikubwa cha ngozi kilichokuwa na nakshi za mapambo ya wanyama.
Upande wa kulia kulikuwa na sanamu kubwa mfano wa mbuzi mwenye pembe ndefu, upande wa kushoto kukawa na sanamu ya mfano wa mtu aliyekaa kwa uzingativu kama anasali na michoro mingi ukutani.
Juu ya kiti kile, alikaa mwanaume mzee ambaye kichwa chake kilikuwa kimejaa mvi, akionesha kuwa mzee sana. Alikuwa amejifunga shuka jeupe mwilini na kujifunga mikanda ya rangi nyekundu kiunoni, kwenye mkono wa kulia na kichwani. Alikuwa amefumba macho huku akionekana kutabana maneno fulani ambayo sikuwa nayasikia.
Pembeni ya kiti chake, kulikuwa na kitanda cha ngozi ya mnyama, nilipotazama vizuri nikagundua kuwa baba alikuwa amelazwa juu ya kitanda kile huku akifukizwa moshi wa dawa na mwanaume mmoja. Nilijikuta nikitetemeka sana kwani sikuwahi kufika sehemu inayotisha kama ile. Niligeuza shingo huku na kule, nikawa nawatazama watu wengi waliokuwa wamekaa kwa mpangilio, ambao nao walikuwa wakinitazama kwa makini.
Nilijaribu kuangaza macho nikitarajia nitamuona mama au mzee Mwalyego lakini haikuwa hivyo, miguu ikawa inatetemeka.
“Mkanwaaaa!” sauti nzito ilisikika ikiniita kutoka pale kwenye kile kiti. Nilipogeuka, yule mzee ambaye bila shaka ndiyo alikuwa mganga, alikuwa amenikodolea macho yake makubwa, mekundu na ya kutisha. Niliitikia kwa heshima huku nikizidi kutetemeka, msaidizi wake mmoja akaja na kunishika mkono, kisha akanielekeza kuelekea kwenye mlango mdogo uliokuwa umefunikwa kwa kipande cha gunia.
Nikawa natembea huku nikianza kuhisi kizunguzungu kutokana na hofu kubwa niliyokuwa nayo. Wakati nikitembea kuelekea kwenye ule mlango, huku nyuma niliwasikia wale watu wengine waliokuwa wamekaa chini wakianza kuimba mapambio kwa lugha ambayo sikuielewa.
Cha ajabu, nilipofika kwenye mlango nilioelekezwa niende, nilipofunua kile kipande cha gunia, nilikutana na mzee Mwalyego na mama waliokuwa wamekaa kwa huzuni, nikaingia na kuungana nao huku nikiwahoji nini kilichokuwa kinaendelea.
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni