PETE YA MVUVI (4)

0

SEHEMU YA NNE
ILIPOISHIA...
Mimi sikufahamu chochote hivyo niliendelea na kazi yangu ya kutafuta maji ya kunywa nimpelekee Neema niliyemuacha kwenye kiota na yatakayobaki ninywe mimi.

IKIWA UNASOMA SIMULIZI NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI USIPITWE NA SIMULIZI

ENDELEA...
Wanakijiji wale walipofika kwenye kiota kile na kuona kitu kikijigusa gusa bila kutoa sauti walihisi moja kwa moja atakua ni yule nyoka, hivyo walimwaga mafuta ya petroli kwenye kiota kile na kisha waliwasha moto, Sikufanikiwa kupata maji hata tone moja hivyo nilianza safari ya kurudi kwenye kile kiota, kwa mbali niliona moshi na moto mkali ukitokea eneo lile lile nililomuacha mdogo wangu, Nilikimbia kama mwehu na nilipofika eneo lile palipokuepo na kile kiota nilichukua nimemuacha Neema sikuamini macho yangu kwani kiota kile kiliteketea chote kwa moto ule mkali wa mafuta ya Petroli……

Sikuweza kuendelea kuangalia tukio lile kwani roho iliniuma sana kuona kiota kile alichokuewpo mdogo wangu kikiteketea na moto ule mkali, Hivyo niliondoka eneo lile na kuelekea nyumbani. Maisha bila ya Babu na Neema yalikuwa magumu sana kwangu kwani nilikua mpweke sana, Na kila nilipokua nawakumbuka niliishia kulia bila kupata wa kunifuta machozi yangu………

Nilipiga moyo konde na nilianza maisha yale mapya nikiwa peke yangu, Muda wa miaka 10 ulipita, Kipindi hicho nikiwa mtu mzima na Mvuvi mwenye uzoefu na umakini wa kiwango cha juu kiasi ambacho wavuvi wenzangu walipenda kufanya kazi na mimi kwani niliipenda sana kazi yangu. Wanakijiji wengi walinipa jina la “JOSHUA NYOTA YA LUVILE” Kwa jinsi nilivyokua nikijitolea kwenye shughuli za kuisaidia na kuendeleza jamii yangu, Nilipewa wadhifa wa kuongoza wavuvi wenzangu huku pia nikiwa kiongozi wa vijana wa kijiji changu.

Nilipendwa na wengi kwa jinsi nilivyokua nikiwaongoza wenzangu wa ziwani huku nikiwa mshauri mzuri wa vijana ambapo nilifanikiwa kuwawezesha vijana wengi wa kila jinsia wa kijiji kile kwa kuwapa elimu ya uvuvi ambayo hapo awali ilikua ikitolewa na marehemu babu yangu. Maisha ya Luvile yalibadilika sana kwani nguvu kazi za vijana wenzangu zilishamiri kwa kasi na kufanya kijiji chetu kuwa na chakula cha kutosha huku mazao mengi tulianza kuyalima kwenye ardhi yetu na kuepekua gharama za kununua na kusafirisha chakula kutoka mikoani kuleta kijijini kwetu na badala yake mazao yetu ndio tuliyokua tukiwauzia watu wa mijini.

Mali za marehemu babu zilichukuliwa na Shangazi tangu nikiwa mdogo na hivyo sikubahatika kufaidi jasho la babu yangu, ila nilikua nikijisemea moyoni mwangu kwamba, “Ipo siku waliodhurumu mali za marehemu babu yangu, Mungu atawaadhibu kwa mabaya yao”. Siku moja nilipokua njiani kuelekea ziwani ikiwa ni mida ya jioni nilibahatika kuonana na binti mrembo aliyejulikana kwa jina la Bahati, Bahati alikua ni binti mrembo sana aliyekua akiishi nje kidogo ya kijiji chetu na nilikua nikilisikia jina lake mara kwa mara kwa rafiki zangu ila sikuwahi kupata nafasi ya kuonana nae ila leo hii nilibahatika kuonana nae. Kwa sura bado mdogo ila umbile lake alionekana mkubwa kwani alikua ni mrefu mwenye shepu ya kumfanya kila mwanaume amtamani,

Nilimsimamisha na tulianza kufahamiana kwa majina na aliposikia mimi ndio Joshua alifurahi sana kwani sifa zangu zilienea kila kona. Mazungumzo yetu hayakua marefu kwani mrembo yule aliniambia ana haraka mno kwani bibi yake ni mgonjwa sana na hakua na pesa ya kununua dawa kwani kwa bahati mbaya alidondosha fedha zile alizopewa na bibi yake, Kwa roho ya huruma niliyojaliwa na Mungu nilizama mfukoni na kumpa kiasi chote cha pesa nilichopanga nikawalipe vibarua wangu. Kawaida ya mapenzi huwa ni hisia za mtu kwa mtu na huwa hakuna sababu nyengine ya msingi Zaidi ya hisia.

Hisia zangu zilitokea kumpenda sana bahati japokua ilikua ni siku yangu ya kwanza kuonana nae, Hivyo sikumuacha aende peke yake na badala yake niliongozana nae mpaka duka la madawa na kisha nilibahatika kwenda nae mpaka alipokua akiishi na bibi yake, Nilifurahi sana kwani bibi yule aliponiona tu na kujua jina langu alianza kucheka na hakika sifa zangu nzuri zilimfanya bibi yule kupata nguvu ya kushuka kitandani na kisha tuliongea vizuri mno.

Nilipokua naaga kuondoka bibi yule hakuniruhusu mpaka pale alipomuomba Bahati apike haraka mno japo nile chochote kile kama ishara ya kuacha baraka zangu nyumbani pale, Chakula aina ya Roshoroo kipikwacho kwa mchanganyiko wa maziwa na mahindi kililetwa na Bahati jamvini nilipokua nimeketi na bibi yule, Nilifurahi sana kupata muda wa kukaa na bibi yule kwani nilikumbuka nilivyokua na marehemu babu yangu, licha ya yote nilifarijika sana nilipomuona bibi yule akipata nguvu hadi ya kuniimbia nyimbo zao za zamani enzi za ujana wao, Bahati alikua mwenye furaha mno kwani alinishukuru sana kutokana na bibi yake kugoma kula chakula ila kwa uwepo wangu pale alikula vizuri na kunywa dawa zake bila shida yeyote.

Niliaga na kuanza safari ya kurudi nyumbani, Nilipokaribia na nyumbani ghafla nilivamiwa na kundi la vijana walionimulika na mwanga mkali wa tochi sikuweza kuwatambua kwa haraka na hivyo walinifunga mikono na miguu yangu kwa kutumia Kamba na kisha walinigonga kichwani kwa kitu kilichokua kama chuma na hivyo nilipoteza fahamu zangu. Nilipokuja kushtuka na kurejesha fahamu zangu nilihisi upepo mkali sana huku mawimbi yakipiga mahala pale nilipokua, kwakua ilikua ni usiku mno sikuweza kujua nilipo ila baada ya kuhisi maji yakinilowesha miguuni nilishtuka sana na nilijikuta nikiwa ziwani peke yangu kwenye mtumbwi ambao ulishaanza kujaa maji. Mikono na miguu yangu ikiwa imefungwa na kamba ngumu, nilihangaika sana lakini sikuweza kujifungua kamba zile. Mtumbwi ulijaa maji na bila hata kupoteza muda mtumbwi ule ulianza kuzama………

Juhudi za kujifungua zile kamba nilizokua nimefungwa mkononi hazikufanikiwa na mtumbwi ule ulizima nikiwa chini ya maji pumzi iliniishia baada ya kunywa maji mengi, nilihisi nina sekunde chache mno kufika mwisho wa maisha yangu, Nilihema kwa tabu sana na baada ya sekunde chache nilipoteza nguvu zangu zote huku pumzi ikielekea ukingoni.

Kwa chini kabisa niliona kipande cha chuma nilijitahidi kwa nguvu zangu zote huku moyoni nikisema, “Eeeh Mungu wangu naomba unijalie nguvu na pumzi japo kwa dakika chache niweze kujiokoa, nikishindwa basi nitaomba unichukue” Sikujua nguvu na pumzi zilitoka wapi papo hapo nilijikuta nikipata nguvu ya kukifata kile kipande cha chuma kilichokua chini kabisa ya ziwa lile, Nilifanikiwa kukifikia na niliweza kujifungua kamba za miguuni kwanza na kisha kamba za mikono.

Mungu ni Mungu tu! kwani sikutegemea kama ningeweza kujiokoa ila kwa mapenzi yake niliweza. Niliogelea mpaka kufika ngambo ya ziwa lile, Watu wengi walinishangaa sana kwani nilikua uchi wa mnyama huku nikiwa nimeishiwa nguvu kabisa. Kwa msaada wa wavuvi wenzangu walionitoa ziwani pale mpaka hospitali kupata matibabu kwani nilikohoa damu huku nikitapika maji kila baada ya dakika, Daktari alinipa dawa na maelekezo ya vyakula vya moto huku niliambiwa nisiende ziwani kwa muda wa wiki tatu kwani hali yangu haikuniruhusu kufanya hivyo.

Wiki ya kwanza ilipita salama na ilipofika wiki ya pili hali yangu ilianza kubadilika kwani nilianza kukohoa damu kila dakika, Wanakijiji wenzangu walianza kunitenga kwani habari zilizozagaa zilikua mimi ni muathirika wa virusi vya ukimwi kwa jinsi nilivyoanza kukonda huku nikitoka mabaka baka ya rangi ya kijani mwilini wangu. Kilichonisikitisha zaidi ni pale niliposikia Bahati karibuni angechumbiwa na kuwa mke wa mtu, Maisha yangu yalibadilika sana kwani nilikua ni mgonjwa nisiyekua na mtu wa kuniangalia na kuniuguza, Heshima yangu yote ilipotea huku uongozi niliyokua nao kwenye nyanza mbali mbali za kijiji kile zikichukuliwa na watu wengine kwani kila mwana kijiji alijua mimi sitopona tena na huku wakiniambia, “Joshua wewe sidhani kama utafika mwakani, Wewe ni wa kufa tu” maneno hayo yalikua yakiambatana na vicheko vya kejeli…

Hakuna kitu kibaya kwenye maisha ya binadamu kama kutengwa na jamii yako, Afya yangu ilizidi kuwa mbaya mno kandri siku zilivyozidi kwenda mbele kwani sikua na mtu wa kunisaidia kupika wala kunisimamia ninywe dawa kwa muda sahihi. Siku moja nikiwa kitandani mida ya usiku nilikumbuka sana maneno ya marehemu babu kwani alikua akinisisitizia kuwa, “Joshua mjukuu wangu wewe ni jasiri kwani ulizaliwa kwenye mazingira magumu sana ambayo isingekua ujasiri wako usingefanikiwa kufika hapo ulipo, hivyo naomba ulitambue hilo” Palipokucha nilijitahidi kuamka na kisha kuanza safari ya kuelekea ziwani kutafuta chakula kwani sikua na chakula kabisa, Nilipokua njiani nilikutana na Bahati ambaye sikutegemea angenikimbia bila hata kuitikia salamu yangu.

Niliumia sana kwani kitendo kile kilinifanya niishiwe nguvu ya kuendelea na safari yangu ya ziwani, nilipiga magoti na kisha kuziangalia mbingu huku nikitamka kwa sauti ya nguvu, “Baba Mungu mwanao napitia yote haya sina wakunipenda tena hapa duniani, Ewe Mwenyezi naomba unijalie afya njema” Nilipomaliza kuongea maneno yale machozi yalianza kunitoka na ghafla niliona mkono wa mwanamke ukinishika begani huku sauti ikiniambia, “Joshua usilie mwanangu nimekuja kukusaidia” Nilipomtazama mtu huyo sikuamini macho yangu kwani alikua Shangazi yangu.

Shangazi aliniinua pale nilipokua nimeketi kwa huruma na kisha alinikumbatia huku akiniambia, “Joshua pole sana mwanangu, Niliota ndoto mbaya sana kuhusu wewe na kwa kuwa nilifata ushauri wako nimrudie Mungu wangu niache ushirikina naamini Mungu aliniotesha ndoto ile ili nije nikusaidie, Punguza kulia nimekuja kukusaidia, Nyanyuka twende nyumbani”.

Tulipofika nyumbani Shangazi aliingia jikoni na kunipikia ndizi na samaki, Nilikula na kisha nilimeza dawa na kisha tulianza kuzungumza, Nilimwambia Shangazi, “Shangazi nashukuru sana kwa upendo wako pia nashukuru kwa kufata ushauri wangu, Naamini Mungu ameshakusamehe makosa yako yote” Shangazi alinijibu, “Joshua, Marehemu baba yako alikua mtu mwema sana na alipenda sana kumsaidia kila mtu bila kujali ni tajiri au maskini, Naona umerithi tabia zake, Joshua nitakuangalia mpaka upone kabisaa na kama utahitaji twende wote mjini basi sina shida na hilo, Sawa mwanangu kipenzi?” Nilimjibu kwa furaha, “Ndio Shangazi yangu kipenzi”…

Shangazi aliniangalia vizuri sana kiasi ambacho madonda yote ya mwilini yalianza kupotea huku hali yangu ya kukohoa damu ikitoweka kabisaaa!!

Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)