DOKTA SIUMWI HUKO (8)

0
Mtunzi: ___

SEHEMU YA NANE
ILIPOISHIA...
“Najua sana lakini siwezi kukusaliti mume wangu, amini.”
“Lakini si mlikuwa mnapelekana wote?”
“Ndiyo, lakini sijatembea na Dokta Kisarawe.”
“Je, nikigundua umetembea naye?”

IKIWA UNASOMA SIMULIZI NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI USIPITWE NA SIMULIZI

ENDELEA...
“Nifanye lolote lile.”
“Sawa.”
***

Mume wa Monica alifika nyumbani akiwa amechoka sana. Mkewe alipomwona alitoka mbio kumlaki…
“Pole na kazi mume wangu.”
“Asante sana.”
“Sasa ikawaje, mbona hujajibu meseji yangu wala hujapokea simu?”
“Niache Monica.”
Monica alishtuka sana kwani si kawaida mume wake kumwita kwa jina la Monica, alizoea darling au mke wangu, wakati mwingine alimwita mama. Akajua pana jambo zito limetokea…
“Kwani kuna nini?”
“Umenitumia meseji kwamba una limimba?”
“Ha! Baby, nina limimba au nina mimba?”
“Una limimba, mimba kwani kitu cha kufurahia wakati unajua kila kitu?”
“Kwani mume wangu kuna nini?”
“We! Mimi siyo mume wako.”
“He! Yamekuwa hayo jamani, kwa nini kwani?”
“Hilo limimba ni la nani?”
“Si yako.”
“Wewee, mimi sijakupa mimba wewe.”
“Kanipa nani sasa?”
“Unamjua, tena nitakupiga sasa hivi.”

Monica alimkwepa mumewe na kwenda kukaa sehemu nyingine lakini akiwa amejaa mawazo…
“Au kajua kuhusu mimi na Dokta Kisarawe?”
“Lakini kama kajua, kajuaje? Mbona hakuna mawasiliano kati yake na dokta?”
“Mh! Labda Sulee kamwambia hisia zake maana Sulee sijawahi kumwambia kwamba nimetembea na dokta, sasa?”
“Ha! Liwalo na liwe bwana, sasa nitafanyaje?”
“Monica,” aliitwa na mumewe Monica tena sauti iliyotumika ilikuwa kali sana.
“Abee.”

Monica aliinuka, akatembea kwa kasi mpaka kwa mumewe…
“Nataka tukapime DNA…”
“DNA ndiyo nini mume wangu?”
“DNA ni kipimo kitakachoweza kusema ukweli kama hilo litumbo lako ni la kwangu kweli au la!”
“He! Mume wangu jamani, umefikia huko?”
“Ndiyo.”
“Mh! sawa.”
“Kesho tutakwenda.”
“Sawa.”

Alipoondoka, Monica alimtumia meseji Dokta Kisarawe na kumuuliza kama amewasiliana na mwanaume yeyote anayeitwa David…
“Hapana.”
“Kwani vipi?”
“Nahisi mume wangu amejua natembea na wewe na ana wasiwasi na ujauzito wangu.”
“Unasema kweli?”
“Dokta kwa nini unauliza kama nasema kweli, ina maana hata wewe unajua huu ujauzito unaujua si wake?”
“Sijasema hivyo.”
“Sasa?”
“Nimeshtuka kusikia mtu ana wasiwasi na mimba yake.”
“Kasema kesho tunakwenda kwenye DNA sijui.”
“Mh! amefikia na huko?”
“We acha tu. Sina amani hapa nilipo.”
***

Usiku akiwa sebuleni, mume wa Monica alimpigia simu mume wa Sulee ambaye naye alikuwa amekaa sebuleni na mke wake…
“Haloo, kesho bwana nakwenda kwenye ile DNA, nakwenda na shemeji yako, nadhani imefika mahali ukweli ujulikane.”
“Sawasawa, naunga mkono.”
“Je, utakuwa tayari unisindikize?”
“Unataka niwepo kaka?”
“Muhimu sana.”
“Basi hakuna shida, nitakuwa na wewe.”

Baada ya kukata simu…
“Unaongea na nani umsindikize?” Sulee alimuuliza mume wake.
“David, kesho anampeleka mkewe wake kupima DNA ili ajue kama kweli ile mimba ni yake au la!”
“Mh!” aliguna Sulee.
“Unaguna nini, au unajua si yake kweli?”
“Hapana, nimeguna kuona amefikia huko.”

Palepale, Sulee alishika simu na kumtumia meseji Monica…
“Mwenzangu unalo, mpaka kwenye DNA?”
Monica aliposoma meseji ya shoga yake huyo alishtuka sana, lakini pia aliumia moyoni…
“Ina maana mume wangu amemwambia Sulee kuhusu hili?”
“Mbona siamini! Mume wangu na Sulee wapi kwa wapi mpaka amwambie mambo mazito kama haya?” aliwaza moyoni Monica huku akiseti namba za Sulee ili amtwangie…
“Ee…”
“Sulee, nani amekwambia?”
“Ni kweli si kweli?”
“Ni kweli ndiyo, lakini nani amekwambia?”
“Mume wangu.”
“Kaambiwa na nani?”
“Si kaambiwa na shemeji.”
“Kamwambia tu au?”
“Kamwambia amsindikize hospitali.”
“Mh!” aliguna Monica, mapigo ya moyo yalimwenda kwa kasi ya ajabu.
***

Usiku wa kuamkia siku ya kwenda hospitali, Monica alimwamsha mumewe…
“Baby…baby.”
“Mh!”
“Nataka kuzungumza kidogo.”
“Kuhusu nini?”
“Hivi ni kweli kabisa umedhamiria kesho kwenda kupima DNA?”
“Hilo lilishapita na kama umeniamsha kwa ajili hiyo naomba aniache nilale vinginevyo niambie ukweli una mwanaume mwingine nje?”
Monica hakujibu swali hilo. Moyoni alijua anaye mwanaume hata kama si rasmi ambaye ni Dokta Kisarawe, lakini atawezaje kumwambia mumewe kuhusu hilo?
“Sina,” alijibu kwa mkato.
“Basi majibu tutayapata kesho kwenye DNA.”
“Mh!” Monica aliguna, akabaki kimya. Usingizi haukumpata, muda mwingi akili yake ilikuwa ikifikiria namna ya kufanya ili kuepukana na zoezi la kwenda kupima hiyo DNA…
“Au niamke mgonjwa?” aliwaza…
“Tena nataka kukwambia hivi Monica, kesho asubuhi hata ukiamka unaendesha tumboni, daktari na vipimo vyake atakuja hapahapa nyumbani,” alisema mume wake na kuuza mawazo kwamba aamke anaumwa japokuwa naye alitoa kauli ya kumchimba mkwara tu.
***

Asubuhi Monica ndiyo alikuwa wa kwanza kutoka kitandani, hakupata usingizi kwa usiku kucha huku akiendelea kuwaza kitanzi kilicho mbele yake…
“Za asubuhi?” alimsalimia mumewe.
“Nzuri, jiandae tuwahi.”
***

Saa mbili na nusu walifika hospitali yenye kutoa huduma ya DNA ambapo pia walimkuta mume wa Sulee…
“Za leo mkubwa?” mume wa Sulee alimsalimia mume wa Monica…
“Salama kaka, mzima?”
“Mzima sana. Naona tumewasili.”
“Sana tu.”
Sura ya Monicha ilionesha wazi kwamba haikutaka kusalimiwa na wala haikuwa tayari kupokea salamu kutoka kwa mtu mwingine.
“Shemeji vipi?” mume wa Sulee alijipa kichwa ngumu na kumsalimia hivyohivyo tu, aitikie, agome angejijua mwenyewe.

“Salama,” Monica aliitikia kwa mkato, mumewe aligundua lakini hakuhusika naye kumuuliza kuna nini mpaka ameitikia salamu kwa staili hiyo.
Walipata huduma kwa kuchukuliwa vipimo muhimu ambapo Monica alichomwa sindano ya tumbo na kuchukuliwa sampo ya maji huku mumewe akichukuliwa vipimo vya kawaida.
“Majibu mje baada ya wiki mbili,” alisema dokta.
“Sawa dokta, hakuna neno.”
***

Mchana wa siku hiyo, Monica alikuwa kwenye chumba cha Dokta Kisarawe kwa mazungumzo muhimu…
“Kwa hiyo dokta kama nilivyokwambia, hapa sijalala. Mawazo yote ni kuhusu hicho kipimo je, kitasema mtoto wa nani wakati yeye kaenda kupima akaambiwa hana uwezo wa kuzaa?”
“Mimi ninavyojua, mtoto huyo tumboni ni kweli si wa mume wako.”
“Nini dokta? Unamaanisha ni wa nani sasa? Maana mwanaume pekee niliyekutana naye kwa mwaka huu nje ya mume wangu ni wewe.”
“Inaweza kuwa ya kwangu.”
“Aaah! Dokta, lengo lako ni nini?”
“Ilitokea tuu!”
“Ili?”

“Unajua mazingira yalikuwa si ya kutafuta kinga Monica, sasa tungejikingaje? Halafu we shida yako si ilikuwa kupata mtoto kwa sababu mumeo hakuwahi kukupa ujauzito…”
“Sasa ndiyo we unipe kwa njia ya ukweli dokta?” alihoji Monica huku akianza kulia machozi.
“Ndiyo njia ninayoitumia Monica, hata rafiki yako Sulee pia ana ujauzito wangu.”
“Ha! Kweli dokta?”
“Sana tu.”
Kidogo Monica alijiona kama amepoa kusikia Sulee naye ni mjamzito…
“Sasa utanisaidiaje mimi kuhusu maji ya DNA?”
“Rahisi sana, ila kama uko tayari kusaidiwa twende gesti sasa hivi.”

Mh! halafu?”
“Aah! Kwani Monica hujui tukienda gesti halafu ni kitu gani?”
“Ina maana dokta bado unataka?”
“Si sana, ila kwa ajili ya kuburudika mwili wangu.”
“Hivi dokta huoni kama sitajisikia vizuri kutokana na matatizo?”
“Ni akili tu Monica, unaweka pembeni mawazo yote. Kwani si nimekwambia nitakwenda kuongea na daktari wa DNA kwenye ile hospitali?”
“Utamwambiaje?”
“Najua mimi.”
“Nihakikishie kwanza ili kama nikiona kweli inawezekana tunaweza kwenda huko gesti.”
“Nitamwambia ayapindishe majibu. Yawe ni kweli mimba ni ya mumeo.”
“Lakini si amepimwa imeonekana hawezi kuzaa?”
“Bwana wewe Monica, kila kitu kinawezekana, ujue hilo kwanza ili mengine yaendelee.”
“Mh! Dokta huo ni mtihani mkubwa kwangu. Lakini poa twende.”
“Sasa sikia, wewe tangulia kufika kwenye ileile gesti ya siku ile.”
“Usichelewe.”
“Ndani ya dakika sifuri nitakuwa nimefika na mimi.”

Monica alikwenda gesti bila kupenda, lakini angefanyaje wakati aliitaka ndoa yake. Dada yake wa kwanza aliachika, wa pili pia, watatu hajaolewa, wa nne kaachika na uzee juu, sasa ilikuwa lazima yeye ajichunge.
Wakati anaingia gesti hiyo, mume wa Sulee akamwona akiwa ndani ya teksi…
“Haa! Yule si shemeji Monica?”
Alichofanya mwanaume huyo alimpigia simu mkewe, Sulee ili amsimulie lakini namba ikawa haipatikani hewani…
“Khaa! Huyu naye vipi? Mbona hayupo hewani!”
Alijaribu mara mbili tatu, mwishowe akaamua kumpigia simu mume wa Monica…
“Mshikaji wapi saa hizi?”
“Job, niambie…”
“Mh! Kuna ishu moja hivi lakini naona kama haijakaa sawasawa.”
“Ipi hiyo tena?”
“Nimepita kwenye gesti moja hivi, nimemuona shemeji akiingia. Mna mgeni yeyote ambaye amefikia gesti?”
“Hapana! Ni wapi?”
“Hapa Kinondoni Mkwajuni.”
“Nakuja, nisubiri hapohapo ulipo.”
“Poa.”

Mume wa Monica alikodi teksi akamuomba dereva aendeshe kwa kasi hadi Kinondoni Mkwajuni. Hakutaka kumpigia simu mke wake asije akapoteza ushahidi. Alikutana na mume wa Sulee ambaye alihama kwenye teksi akaiacha iende na kuingia kwenye teksi aliyofika nayo mume wa Monica.
“Vipi mshikaji, gesti gani?”
“Ile pale yenye maua. Lakini ni vyema umpigie umuulize aliko si ajabu si yeye, nilifananisha tu.”
“Hapana, nikimpigia nitapoteza ushahidi.”
“Huwezi, kwani akiwa yeye kweli na sisi tumesimama hapa nje atajiteteaje?”
“Lakini kweli.”
Mume wa Monica aliiseti simu yake akampigia mke wake, simu iliita kwa muda mrefu mpaka ikakatika…
“Hapokei,” alisema mume wa Monica kwa sauti iliyoambatana na mtetemesho wa ghadhabu kama siyo hasira za kupitiliza.

Mara Dokta Kisarawe akatokea, mume wa Sulee anamjua alishakutana naye siku moja…
“Ha! Mshikaji, huyo anayeshuka kwenye gari ndiye Dokta Kisarawe ambaye anawatibu wake zetu.”
“Mh! Au ndiyo jamaa mwenyewe?”
“Huenda.”
“Sasa?”
“Tusubiri hapahapa nje.”
Mara, simu ya Monica iliingia kwa mume wake…
“Huyo anapiga.”
“Pokea.”
“Haloo.”
“Ee my husband, nimeona missed call yako hapa.”
“Uko wapi kwani mpaka hukupokea simu?”
“Kwani we uko wapi?”
“Khaa! Mimi nakuuliza na wewe unaniuliza, una akili kweli wewe?”
“Mimi nipo jirani na nyumbani kwa mama Mariam.”
“Oke, sawa.”
Upande wa pili, yaani kwa Monica ikakata simu haraka.
“Sasa sikia, tukisema tukavamie vipi?” aliuliza mume wa Monica.
“Mawili. Kwanza niambie, kama kweli ni yeye utachukua hatua gani mzee?”
“Talaka tu.”
“Una uhakika?”
“Mungu vile ni talaka tu.”
“Okey, kama ni talaka basi tusivamie, tukae mpaka watoke sisi tushuke kwenye gari tukiwa wawili hivihivi.”
“Sawa, niko tayari.”

Mara, mume wa Sulee alimpigia
mke wake…
“Enheee, Sulee hebu njoo hapa Kinondoni Mkwajuni haraka sana, chukua Bajaj,” alisema mwanaume huyo.

Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)