SALAMU KUTOKA KUZIMU (15)

0
Mtunzi: ___

SEHEMU YA KUMI NA TANO
TULIPOISHIA...
Wajumbe wote walikuwa wamehudhuria mkutano huu, ingawa baadhi hawakuuona kama ulikuwa mkutano wa kawaida. Kwanza, hawakutegemea kama ungeweza kufanyika mapema kiasi hicho na kisha njia zilizotumika kuitisha mkutano huu hazikuzingatia usalama wa hali ya juu kama walivyozoea.

IKIWA UNASOMA SIMULIZI NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI USIPITWE NA SIMULIZI

TUENDELEE...
Safari hii kila mmoja alikuwa amepata kadi kwa njia ya posta ‘Express’ ikiwa wa ujumbe mfupi sana ambao kila mmoja aliuelewa ukisema “LEO SAA MBILI PALE PALE.”

Kila mmoja alikuja kwa shingo upande. Hofu ikiwa tele moyoni pamoja na hasira dhidi ya “Mwenyekiti”. ‘Mwenyekiti alikwisha wafanya kuwa kama mateka au watumwa wake. Ahadi zake za utajiri na vyeo vilikuwa na ladha ya uchachu mdomoni. Hawakuwa na hila ya kumwepuka. Haikuwepo njia nyepesi, hasa walipokumbuka mauaji ya kinyama ambayo mtu huyu alikuwa akiyaendesha bila ya serikali kumshuku. Zaidi, wasingeweza kusahau maneno yake aliyowaambia katika mkutano wa mwisho akisema “Kifo kitakuwa kando kikikusubiri…” na “Hautajua kitu gani kimekupiga.” Hivyo walimtii na kufika mkutanoni. Na waliketi kwa utulivu kumsubiri afungue mkutano baada ya kumkuta katulia nyuma ya meza yake, juu ya kiti na, kama ilivyo kawaida, nuru ya taa ikiwamulika macho hata wasiweze kumuona kikamilifu, na kumfanya yeye awaone vyema zaidi.

“Nadhani hatukutegemea mkutano huu ndugu Mwenyekiti,” Mjumbe mmoja aliinuka na kuropoka ghafla. “Umeuitisha kinyume cha kanuni iliyowekwa na haukuwa na usalama. Bila shaka lipo jipya lililokulazimisha kuuitisha. Pengine ingefaa uanze kutueleza mapema ili tuweze kuondoka mahala hapa.”

“Ni kweli” Sauti mbili tatu zilimuunga mkono.

“Kweli kabisa,”Mwenyekiti alisikika akiunga mkono pia. “Lakini ningeomba tufanye subira kidogo. Yuko mgeni mmoja ambaye amealikwa kama msikilizaji tu wa kikao hiki.”

Sauti yake ilikuwa ngeni masikioni mwao. Haikuwa ile ambayo waliizoea. Ikawafanya washangae. Mmoja wao hakuwa amevutiwa na sauti hiyo. Yeye kilichomshangaza zaidi ni madai ya Mwenyekiti.

“Mgeni?” aliuliza kwa sauti ya juu kidogo. “Nadhani tulikubaliana kitambo kuwa suala hili ni siri kubwa baina yetu tuliopo hapa tu. Vipi tena mambo ya kuleta wageni wengine?”

Mwenyekiti alikohoa kidogo kabla hajamjibu mjumbe huyo kwa kusema, “Nchi hii ni kubwa sana ndugu zangu. Tulioko hapa hatuwezi kuifaidi peke yetu. Lazima tuwakaribishe baadhi yao vilevile. Mmoja wao ni huyo ambaye atafika hapa karibuni,” alimaliza kwa kuitazama saa yake.

Sasa ilikuwa dhahiri kuwa sauti hii ilikuwa ngeni kabisa masikioni mwao. Baada ya juhudi zao za kumtazama kutozaa matunda kwa sababu ya nuru iliyotengwa, waligeuka na kutazama kwa mshangao. Mwenyekiti akiusoma mshangao wao, alisikika akiangua kicheko, kicheko ambacho kilitofautiana kabisa na kile cha kikatili walichokizoea.

Kabla hawajajua la kufanya, mlango ulisikika ukugongwa na kisha ukafunguka. Mgeni aliyeingia alikuwa wa mwisho kati ya watu wote ambao wajumbe wangependa kumuona wakati huo. Inspekta Kombora, Mkuu wa Kikosi Maalumu cha Polisi Nchini ambacho hujishughulisha na masuala ya hujuma za kiuchumi na kisiasa! Mtu ambaye sifa zake za ushindi dhidi ya watu wa aina hiyo si haba. Alikuwa kavaa mavazi yake kamili ya kikazi. Nyota zikipepea mabegani.

Kombora pia aliduwaa mbele ya umati huu. Haikuwepo sura yoyote ngeni machoni mwake. Wote walikuwa watu ambao madaraka yao yalifanya picha zao kutokea magazetini mara kwa mara, majina yao kutajwa redioni, na katika mikutano ya hadhara walikalia vile viti vya mbele vinavyowaelekea watu. Sasa wanafanya nini katika chumba hiki ambacho kilikuwa siri mno hata akawa amekifikia baada ya mzunguko mrefu kutoka chumba hadi chumba? Alipoyatupa macho kumtazama yule huyo aliyejiweka kitini mbele yao kwa maana ya uenyekiti, aliyarejesha chini mara moja baada ya kulakiwa na ile nuru kali ya taa za umeme.

“Sijaelewa…” alianza kusema. Kisha alinyamaza ghafla ili kufikiri kabla ya kutia neno lolote katika kikao hiki. Simu iliyopigwa ilimwambia aje hapa, ili apewe salamu zake kutoka kwa Joram, kuzumu. Alikubali kuja hapa hasa simu ilipomwelekeza katika jumba hili. Jumba ambalo machoni mwa wapita njia lilikuwa la kawaida lakini kwake halikuwa la kawaida. Kwa muda mrefu, alikuwa akilitupia macho yenye maswala ambayo yalitaka kujua kipi hasa kinachofanywa kwenye nyumba hii. Alikuwa hajapata nafasi hadi leo hii.

“Karibu sana Inspekta,” sauti ya mwenyekiti ilimhimiza. Nimefurahia sana kufika kwako. Haja yangu ni kutaka ufahamu kuwa tulioko mbele yako ni raia na wazalendo wa nchi hii wenye njaa kubwa ya utajiri na kiu kali ya vyeo kiasi cha kushiriki kikamilifu katika njama za hatari ambazo hazijawahi kutokea katika historia ya ulimwengu.” Wote walimsikiliza kwa mshangao. Kombora aliduwaa. Wajumbe walitetemeka.
“Labda nirudi nyuma kidogo kimaelezo. Mpango huu umeandaliwa kwa muda mrefu. Majaribio ya aina aina yamekwishafanyika. Sumu maalumu zimeandaliwa. Moja ya sumu hizo ni ile ambayo ilikusudia kumuua Joram Kiango. Iliposhindwa, msichana aliyeteuliwa kuutekeleza mpango huo, aliuawa kikatili kuliko kifo chochote cha kikatili kilichowahi kutokea. Utakumbuka Inspekta kuwa, Viungo vya msichana huyo viliokotwa chumbani kwake mfano wa nyama inayouzwa. Baada yake ndipo Joram aliuawa kwa bomu. Viungo vyake vilitapanywa ovyo hata asijulikane kabisa. Sivyo Inspekta? Na baada ya Joram, akauawa Neema Iddi yule msaidizi wake. Ni sisi hawa ambao tuko mbele yako…”

Wajumbe ambao walikuwa wakitetemeka walianza kuinuka. mmoja alipiga hatua mbili tatu kuelekea mlangoni. Lakini alirejeshwa na bastola ya Kombora ambayo ilikuwa ikimwelekea. “Yeyote atakatyeinuka atakuwa maiti. Kuanzia sasa, wote mko chini ya ulinzi.”

“Usiwe na haraka Inspekta,” Mwenyekiti aliendelea kwa utulivu kama awali. “Bado kuna mengi yatakayokusisimua. Kumbuka umealikwa kama msikilizaji tu. Tulioko mbele yako si tishio kubwa kwako. Yuko kiongozi wetu ambaye si mroho sana wa vyeo na utajiri, lakini anayo maradhi ya hatari zaidi. Yeye ni mtu anayependa sana mauaji. Mengi kati ya mauaji yaliyokwisha fanyika ameyafanya kwa mkono wake. Na anafurahia sana kuua. Twaweza kusema kuwa ana wazimu. Yeye ndiye kiongozi wa mpango huu na ameapa kuwa ataufanikisha. Kwa bahati mbaya hayupo hapa tena. Ametoweka…”

“Wewe ni nani?” Kombora alifoka.

“Mjumbe tu mwenye jukumu la kukupa salamu kutoka kuzimu aliko…”

“Sikia,” Kombora alikatiza tena. “Huu sio wakati wa mzaha ata chembe. Kuna mtu mmoja tu mwenye sauti na tabia kama yako. Mtu ambaye alifariki kitambo na nilimzika mwenyewe. Joram Kiango. Sasa wawa ni nani? Huonekani kama mmoja wa kikundi hiki cha hatari sana. Pengine hii ni ndoto tu kesho mambo yatakuwa shwari?”

“Sio ndoto Inspekta” Mwenyekiti huyo alijibu. Labda nindoe nuru hii inayowanyimeni nafasi ya kuniona vyema.” Aliupeleka mkono wake chini ya meza na kubonyeza mahala. Nuru ikatoweka. Aliyekuwa nyuma ya nuru hiyo alikuwa Joram Kiango!

Na alikuwa akitabasamu.

“Joram Kila mmoja aliropoka kwa mshangao. Akuna aliyeyaamini macho yake.

“It can’ be true,” Kombora alifoka kwa lugha ya kigeni. Akijisahihisha mara moja akisema, “haiwezekani. Lazima iwe ndoto ulifariki kitambo Joram. Dunia nzima inafahamu hivyo.”

“Ndiyo,” Joram alijibu baada ya kucheka kidogo. “Nilifariki. Na ni rafiki zangu hawa ambao walinihukumu kifo na kuhakikisha nimekufa. Lakini kuna mengi yalitokea. Nadhani Muumba alikuwa alikuwa hajaweka saini katika mkataba wa kifo changu, au ameikubali rufaa yangu. Hivyo nimerudi ili nitoe salamu zangu kwa kikao hiki. Salamu nilizozipata uko akhera,” alimaliza akiachia tena tabasamu.

Lakini tabasamu la dhihaka.

Tabasamu ambalo liliwatesa sana wajumbe zaidi ya kufichulika kwa ukweli. Wote walikuwa wameamini kuwa Joram alifariki kama walivyoafikiana. Na walikuwa wamesikia hivyo katika vyombo vya habari. Na walikuwa wamehakikishiwa na “Mwenyekiti” wao ambaye hawakuwa na shaka kuwa angetimiza jukumu hilo. Vipi tena Joram awe hai! Tena mbele yao! Akiwadhihaki na kuwakebehi! Kitu gani kinatokea! La kutisha zaidi ni kufahamu kuwa Joram bado yu hai. Waliona matumaini yao yakifa mbele yao. Tazama anacheka! Tazama macho yake yanavyotoa nuru ambayo inadhihirisha kuwa siri kamili alikwisha fahamu. Siri ya kutisha ambayo inatosha kuwafanya wahukumiwe kitanzi! Yu wapi? “Mwenyekuti” huyu aliyewatumbukiza katika mkasa huu? Au tayari ametiwa mikononi?

Kombora hangeweza kustahimili, akasema “Sikia Joram. Pengine nimeanza kuzeeka mno. Lakini nadhani mtu yeyote aweza kutiwa kicha na suala huli kama nilivyochanganyikiwa sasa. Kabla sijaanza jukumu lolote la muhimu nadhani unao wajibu wa kufafanua vipi uko hai baada ya lile bomu ambalo lilitapanya maungo yako. Sipendi kuamini kuwa umekufa ukafufuka…”

“Sikufa Inspekta,” Joram alifafanua. “Lile bomu halikunidhuru,” akaendelea kueleza

Bomu lilipuka muda mfupi baada ya Joram kumwona mtu yule aliyekuwa akinyatia mlangoni. Joram hakujuwa mtu yule katokea wapi. Anachojua ni kwamba, aliona kila kitu ndani ya nyumba kikipaa angani na kutua sakafuni. Alijikuta chini ya vitu vingi ambavyo vilimkandamiza sakafuni. Kichwa kilisikia maumivu makali. Maumivu ambayo yalimfanya asikie kelele za watu bila ya uwezo wa kuomba msaada. Mwishowe, kukawa kimya. Joram akafahamu kuwa watu wameondoka katika eneo hilo bila ya kumwona. Tumaini la kunusurika likamtoka. Akatulia asubiri kifo. muda si mrefu, alizirai.
Fahamu zilipo mrudia, alijikuta yumo katika chumba cha nyumba mbovu mbovu kalazwa kitandani akihudumiwa, ndio macho yake yalipopambana na kitu chenye sura ya kutisha na kuchekesha. Kitu ambacho kilikuwa mithili ya binaadamu. Dalili pekee iliyomfanya ajuwe kuwa mtu huyo ni mwanamke, ni furushi la matiti lililokuwa kifuani bila mpangilio wowote uwezao kuvutia macho ya mwanaumwe.

Mtu huyu alitabasamu alipomwona Joram akirudiwa na fahamu.Tabasamu ambalo lilikuwa ni vigumu kutofautisha na kilio.

“Naitwa Unono. nimekuokoa kutoka katika kifusu cha nyumba iliyopatwa na ajali. Unajisikiaje bwana wangu?”

“Bwana wake hili lingemchekesha Joram Kiango. Lakini maumivu yaliyokuwa yakimsumbua hayakuwa madogo. Yakamfanya amshukuru na kuuthamini msaada wa Unono. Alijuwa kuwa bila ya unono angekuwa marehemu. “AHsante sana,” akijikongoja kutamka.

“Usijali mpenzi.”

Mpenzi! Joram aliwaza kwa hasira kidogo. Kisha alitabasamu alipojikumbusha kuwa huenda mama huyu hana akili timamu. Kwani Joram hakumbuki lini aliwahi kuitwa “Mpenzi” na mtu wa aina yake.

Tabasamu la Joram lilimtia Unono moyo. Akacheka na kueleza kwa mnong’ono.

Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

JIUNGE KWA UPDATE NA BURUDANI ZAIDI
WhatsApp Channel=> CnZ Media(Follow)
Telegram Channel=> CnZ Media(Join)

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)