Mtunzi: ___
SEHEMU YA KUMI NA SITA
TULIPOISHIA...
TULIPOISHIA...
Mpenzi! Joram aliwaza kwa hasira kidogo. Kisha alitabasamu alipojikumbusha kuwa huenda mama huyu hana akili timamu. Kwani Joram hakumbuki lini aliwahi kuitwa “Mpenzi” na mtu wa aina yake.
Tabasamu la Joram lilimtia Unono moyo. Akacheka na kueleza kwa mnong’ono.
IKIWA UNASOMA SIMULIZI NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI USIPITWE NA SIMULIZI
TUENDELEE...
“Nimekuleta kwa siri. Majirani wote wamelala. Hakuna anayejua kama uko humu. Kama wangejua wangekupokonya kutoka mikononi mwangu. Hakuna mtu anayependa kuniona nikipata kitu kizuri. Nawe u mzuri bwana wangu. Mzuri na mwenye afya. Nimekubeba kwa taabu kubwa sana. Baada ya muda si mrefu utapona. Utakuwa wangu. Nitakupa chochote na kila kitu utakachokitaka kutoka kwangu.”
Joram hakuwa amemsikiliza. Alikuwa ameirejesha akili yake katika tukio zima na kulitafakari. Akajikumbusha kuwa kuna mtu aliyekuwa amedhamiria kumuua. Mtu ambaye ametumia njama namna kumuua. Kwanza, akamtumia yule msichana kumpa sumu. Pili, ametumia bomu. Na ameponea chupuchupu kuuawa na bomu hilo. Pengine mtu huyu anaamini kuwa amekwishafariki. Ama asingeshindwa kuja hapa na kummaliza kwa urahisi. Kwanini mtu huyu akataka kumuua kwa vyovyote vile? Amefanya kosa gani ili aweze kuchukuwa na binaadamu mwenzake kiasi hiki? Joram hakupenda kuwindwa kama mnyama mwituni. Hasira zilimjaa. hasira zilizompa nguvu. AQkashindana na udhaifu aliousikia mwilini. Akainika kwa kujikongoja. Akajitahidi kusimama wima.
“Una nguvu za ajabu mpenzi,” Unono alisema kwa mshangaoJoram alimtazama bila kumsikia. Akilini mwake aliwaza: Ni vipi angekuwa mwinda badala ya mwindwa? Vipi angemtia mkononi mtu huyu wa hatari? Alikuwa na fursa nzuri sana kwani huyu alikwisha mtoa akilini kwa kudhania kuwa tayari amemwangamiza. Aliona kuwa isingekuwa kazi ngumu kumtia mikononi.
Hata hivyo, aliuona ugumu wa Jukumu hili. Alikuwa amepoteza silaha zake zote. Alipoteza ndevu zake za bandia pamoja na kilemba chake. Begi lake lililobeba vifaa vyake muhimu lilikuwa limepotea pia. Basi, alifurahi mno kupata pochi yake kwenye kwenye mfuko wa suruali. Pochi ambayo ilisetiri mambo yake mawili muhimu, noti zake chache na picha ya adui yake. Picha ambayo alikuwa ameipiga kwa siri sana kule hotelini ambako adui yake huyu alikuwa akimwandalia kifo chake. Joram aliitazama picha kwa makini, kisha akaihifadhi, na kujilazaq kitandani akisubiri mapumziko.
Unono, ambaye wakati huu wote alikuwa ametulia akimtazama Joram, alimfuata kitandani. Buibui amelivua tayari kusheherekea vuno lake. Weusi wa umbo lake haukupendeza hata kidogo. Lakini Unono alikuwa amedhamiria.
“Naona umepona mpenzi,” alisema
“Tunaweza kufurahi kidogo…”
Hili Joram hakulitegemea. Alitamani kumwachia kofi kali ambalo lingetuwa katika sura hiyo mbaya na kuirejeshea akili. Lakini kwa kuwa bado alimhitaji, hili hakulifanya. Badala yake, alizungumza kwa sauti ya udhaifu zaidi. “Baada ya kunitoa hatarini unataka kuniua hapa? Huoni kama niko hoi?”
“Pole!”
Usiku huo ulikuwa mgumu kwa Joram. Kwa kweli Joram alikuwa amezoea kukutana na wanawake wazuri. Lakini alikuwa hajazoea kupambana na wanawake aina ya Unono. Mwanamke mzuri anaponuna, Joram huwa anaelewa na sura yake haichukizi, na anapocheka inapendeza. Huyu akicheka inachukiza, na akinuna tazama anavyotisha! Ulikuwa usiku mgumu. Usingizi ulimpata alfajiri. Alikurupuka na kumkuta Unono yuko juu yake!
Kulipopambazuka alitayarishiwa maji ya moto ambayo aliyaoga haraka haraka. Alipotoka bafuni alikuta Unono kaandaa chai nzito. Baada ya kuinywa aliambiwa, “Sasa hujambo. Tafadhali tulale kidogo kabla hujanikimbia kama wenzako wote.”
“Kukimbia?” Joram alihoji, akijitia kushangaa. Bado nauhitaji sana msaada wako.” Akaitoa pochi yake. Ninahitaji sana msaada wako,” aliongeza. “Pesa hizi ni nauli yako. Na hii hapa ni picha ya mtu ambaye nitakuomba uipeleke kwa msichana mmoja. Anwani yake ni hii…” akamweleza. “Utanisaidia mpenzi.”
Unono hakuwa amemsikiliza kwa makini. Lakini “Mpenzi” lilimfanya ayakumbuke yote aliyoelezwa kwa uhakika kabisa. Kuitwa “Mpenzi” na kijana mzuri kama huyu, aliyekuwa amemnyima usingizi usiku kucha. Hakumbuki kama kuna binadamu yeyote wa kiume aliyewahi kumuita hivyo. “Nitakusaidia kwa lolote,” alimjibu.
“Ahsante,” Joram alijibu. “Jambo jingine nitakalokuomba ni la siri. Tafadhali sana usimfahamishe mtu yeyote kuwa unaishi na mtu hapa. Wala usimfahamishe mtu yeyote kuwa mtu huyu alinusurika ajali ya bomu. Tafadhali iweke vyema siri hiyo. Ningependa kuishi hapa kwa wiki nzima bila mtu yeyote kufahamu.”
Wiki! Unono hakuyaamini masikio yake. Alizidiwa na furaha. Hakuahidi tu bali aliapa kuwa asingeitoa siri hiyo hata kwa ncha ya kisu. Baada ya kujiandaa, aliaga na kutoka nje ambako alipanda basi kama alivyoelekezwa na Joram. Ndipo alipomwendea Neema na kumpa ile picha, ingawa kwa ajili ya wivu, hakueleza kikamilifu yote ambayo Joram alikuwa amemwelekeza. Wivu ambao ulimharakishia Neema Idd kifo chake.
Baada ya Unono kuondoka, Joram pia alifuata. Aliingia mitaani ambako alinunua mavazi fulani fulani na miwani myeusi, akajibadilisha.Mtu asingeweza kumfahamu kwa urahisi, hasa mtu ambaye alikuwa na uhakika kuwa Joram Kiango alikwisha fariki. Ktoka hapo, alienda kwa Neema. Alishuku kuwa binti huyo alikuwa anachunguzwa. Aliingia katika nyumba hiyo kwa siri mno bila ya jirani yeyote kumwona. Alishangaa kutomkuta Neema ndani ingawa picha aliyoihitaji ilikuwa mezani ikiwa na maelezo yote nyuma yake. Baada ya kusubiri kwa muda, aliondoka tena kwa siri kama alivyoingia. Alirejea kwa Unono ambaye Joram alimkuta tayari kanuna na kukata tamaa. Hivyo alipomuona Joram alimrukia na kumkumbata. Lakini Joram alijitoa mikononi mwake kwa kumuomba aende kwa Neema kupata majibu. Alimpa pia maelezo mengine.
Unono aliondoka, lakini hakurudi.
Subira ya Joram haikuzaa matunda yoyote. Kiza kilipoingia, aliondoka hadi kwa Neema. Mbele ya nyumba hiyo alisikia maongezi ya watu juu ya ajali ya “Mwanamke kichaa, mfupi…” Ndani kwa Neema, alimkuta kalala kitandani, Kapoa kitambo.
Kifo cha Neema kilimshtua Joram zaidi ya kitu chochote kilichowahi kutokea. Hakutegemea. Alitaka kulia ingawa hakujua kwa nini machozi hayakujitokeza machoni mwake. Neema kafa! Msichana pekee ambaye waliondokea kupendana zaidi ya dada na kaka au mtu na mkewe. Msichana ambaye daima alikuwa tayari kuhatarisha maisha yake kwa ajili yake. Binti ambaye mara nyingi ameyaokoa maisha yake. Asingeweza kusahau mchango wake katika kisa cha Najisikia Kuua Tena. Wala asingekosa kumkumbuka kila alipofikiria tukio la Dimbwi La Damu. Neema! Mtoto Mpole, msikivu, mwenye hekima. Mtoto mzuri kwa sura na umbo. Kapotea bure kwa uzuri ule katika mikono ya mtu mwenye roho ya kinyama na fikira za shetani…
Hatimaye machozi yakamtoka.
Joram hakuwa na haja ya kuambiwa kuwa kifo hiki ni matokeo ya kazi ndogo Aliyompa Neema kupeleleza juu ya mtu au watu hawa waliokusudia kumwua. Akaaapa kuwa asingestarehe hadi amtie mikononi mtu huyu! Mikononi? Alijiuliza kwa hasira. Ndiyo, Joram hajawahi kuua. Wala leseni yake haimruhusu kuua isipokuwa katika kujitetea tu. Lakini huyu lazima amwue kwa mkono wake. Aliapa. Damu ya Neema na wote wasio na hatia waliouawa na mtu huyu lazima ilipwe. Deni la damu hulipwa kwa damu.
“Wazimu wa hali ya juu… Wazimu wa hatari…” Kombora aliendelea kufoka kimya kimya, masaa kadhaa baada ya kuhudhuria kile kikao ambacho kiliendeshwa na Joram. Karatasi zile zilikuwa kando mbele yake, zikimtisha na kumtamanisha. “Mtu kadhamiria kuua kinyama umati mzima wa viongozi, kwa njia za kipekee ambazo si rahisi kubainika! Mtu huyu yu hai na huru mahali fulani katika Jamhuri hii! Wazimu ulioje? Hana haki ya kuendelea kuishi. Lazima afe haraka iwezekanavyo”.
Hayo Kombora alikuwa ameyasema mara nyingi usiku huu. Tangu Joram alipomwacha, alitoa amri ya kuwahifadhi ‘Waheshimiwa’ wote na kisha kuanza jukumu la kumsaka Proper. Kati ya karatasi alizoacha Joram, zilikuwa pia zile ambazo zilifichua makazi yake yote na majina yake mbalimbali. Hivyo makachero walitumwa sehemu mbalimbali kumsaka. Mengi ya kutisha yalibainika, lakini mtu waliyemhitaji hakupatikana. Alikuwa ametoweka kama moshi unavyopotelea hewani. Ndipo Kombora alipoelekeza juhudi zake kumtafuta Joram kwa matumaini ya kwamba angeweza kuwa na fununu ambayo ingerahisha kupatikana kwa mtu huyo. Lakini alishangaa alipoona kuwa juhudi za makachero za usiku kucha hazikufanikiwa. Sasa kulikuwa kukipambazuka bila dalili zozote za Joram kupatikana. Yeye pia alikuwa ametoweka!
Ulikuwa usiku wa manane. Lakini Kombora hakusinzia hata kidogo. Wala hakudani kama angeweza kupitiwa na lepe la usingizi usiku wowote hadi wakati mtu huyo hatari atakapokuwa ameuawa au kutiwa mbaroni. Zilikuwa zimesalia siku chache sana kabla ya mkutano huu maalumu wa viongozi wa nchi ziliko mstari wa mbele ufanyike mjini Arusha Tanzania. Ilisemekana pia kuwa viongozi wa nchi nyingine huru za Afrika wangehudhuria mkutano huo. Na mtu huyu – lanakum – anayekusudia kuwaangamiza viongozi hawa kinyama, yuko mahali fulani katika nchi hii! Vipi Kombora angeweza kustarehe?.
Alikuwa na wajibu. Wajibu muhimu na wa haraka kuliko wowote mwingine uliowahi kumhusu kama kiongozi wa kikosi hiki maalumu: kumpata muuaji huyu mapema iwezekanavyo. Ni hili lililomfanya aendelee kuwa ofisini hadi muda huo, akipokea simu na taarifa mbalimbali za makachero waliosambazwa kote Jijini kufanya kazi moja tu, kumpata Proper akiwa hai ama maiti.
Hakupatikana. Saa tisa… saa kumi… na moja! bado hakukuwa na taarifa yoyote ya uhakika, jambo ambalo lilizidisha hasira na mashaka katika kichwa chake. Akaelekeza imani yake kwa makachero wa uwanja wa ndege waliodai kuwa mtu wa aina hiyo alikuwa amepanda ndege iliyoelekea mkoani Mwanza. Hata hivyo, Kombora hangeweza kukubali taarifa hiyo mara moja, hakuona kama Proper alikuwa mtu wa kukubali kushindwa hata kukimbilia Mwanza. Kombora aliamini kuwa mahali ambapo mtu mwehu kama huyo angekimbilia ni Arusha ambako angesubiri ili kujaribu kuukamilisha uendawazimu wake kwa vitendo. Hivyo akatoa amri kwa makachero kuendelea na upelelezi hadi mtu huyo apatikane.
Mapambazuko yalifika kabla Proper hajapatikana. Baada ya kunywa vikombe viwili vya kahawa, ili kupunguza uchovu, Inspekta Kombora alijikuta akiinua simu na kuzungusha namba za nyumbani kwa Katibu Mkuu wa Wizara.
Usiku mzima alikuwa amepingana na wazo hilo. Hakuwa mtu mwenye tabia ya kuyatupa matatizo yake kwa wakubwa. Lakini hili aliliona kuwa la hatari zaidi.
Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
JIUNGE KWA UPDATE NA BURUDANI ZAIDI
WhatsApp Channel=> CnZ Media(Follow)
Telegram Channel=> CnZ Media(Join)