KITABU CHA SHETANI (3)

0
Mtunzi: Aziz Hashim

SEHEMU YA TATU
TULIPOISHIA...
“Ok hakuna shida dada’angu,” alijibu Edmund kisha simu ikakatwa, tabasamu pana likachanua kwenye uso wake kwani licha ya ukweli kwamba msichana huyo alikuwa amemfanyia kitendo cha kumdhalilisha sana asubuhi ya siku hiyo,

IKIWA UNASOMA SIMULIZI NJE YA APP YA CnZ Media IPAKUE ILI USIPITWE NA SIMULIZI

TUENDELEE...
alijikuta akimsamehe kirahisi na kutamani kumjua zaidi, akaona hiyo ndiyo nafasi yake.

“Ebwana mbona mudi yako imebadilika ghafla? Tabasamu pana muda wote utafikiri umeokota pochi ya Mzungu?” Walungasa, mfanyakazi mwingine waliyekuwa akifanya kazi na Edmund alimuuliza baada ya kumuona muda wote akiwa na tabasamu pana, akaishia kucheka tu bila kueleza chanzo cha furaha yake.

Saa zilizidi kuyoyoma, hatimaye muda wa chakula cha mchana uliwadia, Edmund akawa anaitazama simu yake kwa shauku kubwa akisubiri Samantha ampigie kwani walikubaliana kwenda kula chakula cha mchana pamoja.

Hata hivyo, muda mfupi baadaye, ujumbe mfupi uliingia kwenye simu yake, harakaharaka akaufungua na kuusoma.

“Sorry! Nimeshindwa kuja kuna kazi zimenibana. Naomba nikupitie jioni baada ya muda wa kazi tukakae sehemu tubadilishane mawazo,” ulisomeka ujumbe huo kutoka kwa Samantha, Edmund akashusha pumzi ndefu na kumjibu kwamba asijali.

Akaendelea kufanya kazi huku mawazo yake yakiendelea kumuwaza msichana huyo. Hatimaye muda wa kutoka kazini ukawadia, Edmund akiwa ameshakamilisha karibu kazi zote alizopaswa kuzifanya kwa siku hiyo. Akazima kompyuta yake na kuwaaga wenzake kisha taratibu akatoka mpaka mapokezi.

Kabla hajatoka kwenye geti kubwa, alisikia simu yake ikiita, harakaharaka akaitoa mfukoni na kutazama namba ya mpigaji, hakuwa mwingine bali Samantha, akaipokea huku tabasamu likiwa limeupamba uso wake.

“Umeshatoka kazini?”

“Ndiyo najiandaa kutoka.”

“Ok basi nisubiri hapohapo, nipo jirani nakuja,” alisema Samantha kisha akakata simu, Edmund akashusha pumzi ndefu na kurudi kwenye chumba cha mazungumzo, akawa anajitazama kwenye vioo vya chumba hicho na kujiweka vizuri.

Baadaye alitoka mpaka nje lakini kabla hajakaa kwenye benchi lililopo nje ya ofisi yao, alisikia simu yake ikiita mfululizo, alipotoa aligundua kuwa ni Samantha.

“Napaki gari hapa nje ya ofisi yenu, uko wapi?” alisema msichana huyo, harakaharaka Edmund akasimama na kuanza kuangalia gari lililokuwa linapaki, akaliona Jeep Grand Cherokee (New Model) la msichana huyo likiingia eneo la maegesho, akatembea kulifuata huku akipunga mkono.

“Mambo!” Samantha alisema kwa sauti nyororo huku akishusha kioo cha gari lake.

“Poa! Vipi za kazi,” Edmund alijikakamua na kuuvaa uchangamfu wa kulazimisha. Alishindwa kujielewa kwa nini kila alipokuwa akimuona msichana huyo alikuwa akiishiwa nguvu kabisa.

“Nzuri! Zunguka upande wa pili uingie kwenye gari,” alisema msichana huyo, tabasamu pana likiwa limechanua kwenye uso wake. Edmund akazunguka mpaka upande wa pili na kufungua mlango, akapokelewa na harufu ya manukato mazuri yaliyokuwa yamepuliziwa ndani ya gari hilo.

Akaingia na kukaa pembeni ya Samantha, kipupwe kilichokuwa kinapuliza ndani ya gari hilo, ukichanganya na muziki laini uliokuwa unapiga kwa sauti ya chini, vilimfanya Edmund ajihisi kama yupo kwenye ulimwengu mwingine wa tofauti kabisa.

“Vipi za tangu asubuhi,” alisema Samantha huku akimtazama Edmund, tabasamu likiwa limeujaza uso wake.

“Poa kabisa, sijui wewe.”

“Niko poa kabisa, sasa naomba twende Kunduchi, kule kuna hoteli nzuri huwa naipenda sana,” alisema msichana huyo, Edmund akatingisha kichwa kuonesha kukubaliana naye, akawasha gari na kuingiza gia, akalitoa eneo la maegesho na kuingia barabarani, akaongeza kidogo sauti ya muziki na kuelekea kwenye barabara ya lami.

“Ooh! Samahani naomba ufunge mkanda,” alisema Samantha baada ya kugundua kuwa kumbe Edmund hakuwa amefunga mkanda. Kijana huyo akiwa anahangaika kufunga mkanda, Samantha alisimamisha gari na kumsaidia, hali iliyowafanya wawili hao wasogeleane miili yao. Mapigo ya moyo wa Edmund yakaongezeka kasi ghafla.

Baada ya kumaliza kumsaidia kufunga mkanda, safari iliendelea huku Samantha akimuonesha Edmund uchangamfu ambao hakuutegemea. Dakika kadhaa baadaye, tayari walikuwa wamewasili Kunduchi, msichana huyo akaenda kupaki gari sehemu ya maegesho kisha wakateremka na kutafuta sehemu nzuri ya kukaa.

“Nimefurahi sana kufahamiana na wewe japokuwa tumekutana kwenye mazingira ya ajabu,” Samantha alivunja ukimya baada ya kuwa ameshamuagiza vinywaji, Edmund akatabasamu bila kusema neno lolote.

“Naomba uniambie kama umenisamehe.”

“Nimekusamehe wala usiwe na wasiwasi Samantha,” alisema Edmund huku akijitahidi kupambana na hofu ndani ya moyo wake. Kila kitu kilikuwa kigeni kwake, japokuwa alikuwa akiishi Dar es Salaam hakuwahi kuingia kwenye hoteli hiyo hata mara moja, akawa anaona kila kitu kilichokuwa kinatokea kama muujiza kwake.

“Kwani we unaishi wapi?” Samantha alimuuliza Edmund ambaye alimuelekeza mpaka mtaa anaoishi.

“Unaishi na nani?”

“Peke yangu.”

“Kwa nini unaishi peke yako? Kwani huna mke?” Samantha alimuuliza Edmund kimasihara huku akivuta juisi taratibu kwa kutumia mrija, akacheka sana na kumjibu kwamba hakuwa ameoa bado.

“Ila una mchumba?”

“Hapana, bado sijabahatika, najipanga kimaisha kwanza,” alisema Edmund na kuanza kumuuliza msichana huyo kuhusu maisha yake.

“Mimi naishi na wazazi wangu Upanga, nafanya kazi ya kusimamia kampuni kadhaa za baba kwani mimi ni mtoto wake wa pekee,” alisema Samantha huku akiendelea kunywa juisi taratibu.

Wakaendelea kuzungumza mambo mbalimbali ambapo msichana huyo alimueleza Edmund vitu vingi kuhusu maisha yake. Ungeweza kudhani wawili hao wamefahamiana siku nyingi zilizopita kutokana na jinsi walivyokuwa wakipiga stori.

Baadaye, walikula chakula cha usiku pamoja kisha wakaondoka hotelini hapo baada ya kuwa msichana huyo amelipia gharama zote.

“Nataka niende kupaona nyumbani kwako,” alisema Samantha huku safari ikiendelea, Edmund akamgeukia na kumtazama, macho yao yakagongana.

“Hakuna tatizo Samantha,” alijibu Edmund, wote wakatabasamu. Safari iliendelea na baadaye Edmund akaanza kumuelekeza msichana huyo mtaa waliokuwa wanaishi. Edmund alitegemea kwamba baada ya kufika na kuiona nyumba anayoishi, msichana huyo ataaga na kuondoka kutokana na ukweli kwamba nyumba aliyokuwa anaishi ilikuwa na hadhi ya chini ukilinganisha na maisha ya msichana huyo.

Cha ajabu, walipofika, Samantha naye alitaka kushuka ili akakione chumba alichokuwa anaishi Edmund, kijasho chembamba kikaanza kumtoka kijana huyo akihofia msichana huyo atamdharau baada ya kuona maisha aliyokuwa anaishi.

Samantha hakujali kitu, wakaingia kwenye nyumba aliyokuwa amepanga kijana huyo na hatimaye wakaingia mpaka ndani, ikiwa tayari imeshatimia saa tatu za usiku.

“Ka..karibu sa..na,” Edmund alimkaribisha Samantha kwa kubabaika, msichana huyo akaachia tabasamu pana kwani alishagundua hofu iliyokuwa ndani ya moyo wa Edmund.

“Unaishi na nani?” Samantha alirudia kuuliza swali ambalo tayari alishajibiwa huku akiwa anazunguka huku na kule ndani ya chumba hicho.

“Naishi mwenyewe,” alijibu Edmund huku akiendelea kujisikia aibu kubwa ndani ya moyo wake. Kwa hadhi aliyokuwa nayo Samantha, alijikuta akishindwa kabisa kujiamini kwani maisha yake yalikuwa ya kawaida sana ukilinganisha na ya Samantha, japo bado hakuwa amefika nyumbani kwao lakini mwonekano wake tu ulitosha kutoa picha kamili.

“Huku ndiyo chumbani kwako?” Samantha aliuliza huku akisukuma mlango wa kuingilia chumbani, kabla hata Edmund hajajibu kitu, tayari msichana huyo alikuwa ameshafungua mlango.

“Unawashia wapi taa,” aliuliza kwa sauti ya chini, Edmund akamfuata kwa nyuma na kuwasha taa ukutani huku akiendelea kujisikia aibu kwani asubuhi ya siku hiyo alikurupuka kuwahi kazini na hakukumbuka hata kutandika kitanda wala kupanga vitu vyake vizuri.

“Ahahaaa!” Samantha alicheka sana baada ya kuona chumba cha Edmund kilivyokuwa kimekosa mpangilio mzuri.

“Inabidi uoe mke atakayekuwa anakusaidia hata kutandika kitanda na kupanga nguo vizuri kabatini,” alisema msichana huyo huku akikaa kwenye kitanda cha Edmund, macho yake yakawa yanaendelea kuangaza huku na kule, tabasamu pana likiwa limechanua kwenye uso wake.

Edmund naye alianza kuhangaika kupangapanga vitu vizuri, akaanza kwa kuokota nguo zilizokuwa zimezagaa sakafuni na kuziweka kwenye kapu la nguo chafu kisha akatoa shuka safi kabatini na kuanza kutandika, ikabidi Samantha amsaidie kwani alimuona alivyokuwa anahangaika.

“Mh! Mbona humu ndani kwako kuna joto sana? Huna feni?” aliuliza Samantha wakati akimalizia kutandika kitanda, Edmund akaanza kubabaika tena kwani ukweli ni kwamba feni yake ilikuwa imeharibika na aliipeleka kwa fundi siku mbili zilizopita lakini akakosa muda wa kwenda kuichukua.

“Sasa nitakaaje? Mwenzio nasikia joto sana?” alisema Samantha huku akianza kufungua vifungo vya shati jeupe alilokuwa amevaa, akabaki na sidiria nyeupe na kufanya kifua chake kilichojaa vizuri kianze kuonekana na kusababisha Edmund azidi kukosa uvumilivu.

Japokuwa hakuwa akiishi na mwanamke na hakuwa na mpenzi kwa kipindi kirefu baada ya kuumizwa na aliyekuwa mpenzi wake wa kwanza, takribani miezi kumi iliyopita, Edmund alikuwa mwanaume aliyekamilika kila idara.

Ukichanganya na ukweli kwamba alikuwa akivutiwa sana na msichana huyo licha ya alichomfanyia asubuhi ya siku hiyo, Edmund alijikuta akizidi kuwa kwenye wakati mgumu mno kihisia.

“Basi ngoja nifungue dirisha,” alisema Edmund huku akijitahidi kuyakwepesha macho yake yasitue kwenye mwili wa Samantha ambaye alikuwa akijigeuzageuza kimitego pale kitandani huku akiendelea kulalamika kwamba anasikia joto kali.

“Hapana! Usifungue nitavumilia tu, ila naomba kama hutajali nivue shati labda nitajisikia vizuri,” alisema msichana huyo, Edmund akakosa cha kujibu. Msichana huyo akasimama na kumuomba Edmund amsaidie kumfungua vifungo vya shati vilivyobakia, akatii bila shuruti.

Wakati akiendelea kumfungua vifungo vya shati, Samantha alikuwa akimtazama Edmund kwa macho yaliyobeba ujumbe mzito, akamsaidia kulivua na kulitundika ukutani.

“Edmund! Naomba sogea nikwambie kitu,” alisema msichana huyo kwa sauti iliyokuwa inatokea puani, Edmund akatii alichoambiwa ambapo katika hali ambayo hakuitegemea, msichana huyo mrembo kupindukia alimkumbatia kwa nguvu kifuani huku akipumua kwa fujo mithili ya mtu aliyetoka kukimbia mbio za marathon, ngozi yake laini iliyokuwa na joto la huba vikazidi kumchanganya Edmund.

Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA

JIUNGE KWA UPDATE NA BURUDANI ZAIDI
WhatsApp Channel=> CnZ Media(Follow)
Telegram Channel=> CnZ Media(Join)

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)