Vita vya Mapenzi (13)
Zephiline F Ezekiel
6 min read
Mtunzi: Maundu Mwingizi
SEHEMU YA KUMI NA TATU
TULIPOISHIA...
TULIPOISHIA...
“Suhail mwanangu nisikilize kwa makini sana.. umekuja Tabora leo umetukuta wazazi wako wote, Una Baba hapa na Mama pale lakini hofu yangu usije ukaondoka ukiwa na Mama tu badala ya wote wawili, kitu ambacho ni hatari sana katika maisha yako yote yaliyosalia..”
KAMA UNASOMA SIMULIZI HII NJE YA APPLICATION YA CnZ Media INSTALL ILI USIPITWE NA MIENDELEZO
SASA TUENDELEE...
“Kwanini unasema hivyo baba, kufa ni mipango ya Mungu tu naweza kuwanza hata mimi ninyi mkabaki”
“Sina maana hiyo mwanagu..” Alijibu kwa utulivu Mzee Kusekwa kisha akamuangalia mkewe na punde akayarejesha macho yake kwa Suhail na kuendelea “Kukosa kwako baba si mpaka afe tu hata atakapokuwambia kuwa hana motto wa aina yako, usingekuja leo nisingebadili kiapo changu nilichokuwapia kwenye simu kuwa sitakuwa baba yako tena.. Nashukuru Mungu umekuja na sasa nakupa kiapo kingine mwanangu unisikilize kwa makini sana..” Kabla hajamalizia kuongea akakatishwa tena na mkewe
“Lakini mume wangu mbona unaendekeza sana tabia ya viapo kwa watoto? Si vizuri ujue”
“Umemaliza?!” alihoji Mzee Kusekwa huku akimtumbulia macho mkewe kana kwamba ameongea pumba, alipoona hajajibiwa akaendelea “..Nitaendelea kuwa baba yako endapo utaondoka hapa Tabora na kurejea Dar ukiwa ni mume wa Sharifa, kinyume na hapo mimi sitakuwa baba yako” Maneno yale yaliwafanya familia nzima iliyokuwa imejumuika pale Sebuleni ibutwaike,
“Lakini baba kwanini imekuwa ghafla hivyo? Hili suala linahitaji muda na pesa pia”
“Muda wa nini tena? Tangu ulipokuwa shuleni sisi kama familia na wewe ukiwemo tulikubaliana kuwa tutasubiri umalizapo tu masomo utarejea kufunga ndoa, Je muda wote huo unaona hautoshi? Kama haukutosha muda huo basi hakuna muda utakaotosha kamwe, pili hilo la kuhusu Pesa usilirejee tena mbele yangu maana mimi ni mtu mzima sipendi kufanywa Juha.. Pesa gani unazohitaji tena zaidi ya hizi ulizozitaja mwnyewe hapa!..”
Kimya kikatanda huku mawazo sasa yakikishambulia kichwa cha Suhail, hakuwa na hamu hata chembe ya kuchokoza vita na Shekhia wala baba yake Mzee Sufian Bin Shamhurish kwa hicho anachotaka kukifanya Mzee Kusekwa, kila mmoja sebuleni pale alizama katika tafakuri kivyake “..Sijui kama unakumbuka kipindi kile unasoma Sekondari ya Isevya jinsi ilivyotaka kuwa songombingo hapa baada ya Mzee Fungameza kuwambiwa na wale waalimu wenu kuwa unajihusisha kimapenzi na binti yake, lakini tulikaa na bwana Yule tukayaongea na kuyamaliza kiutu uzima, usidhani amesahau na hata ulipopatwa na ajali tulishirikiana nae kwa karibu kama mwanafamilia..
Mlipohitimu shule na kuwa watu wazima wenyewe mkaridhia kuwa wachumba na kuwahidiana kufunga ndoa mbele yetu sasa leo unataka kusuasua wakati kila sababu ya kulitekeleza hilo ipo! Narudia tena kuwa mimi kama Baba yako nasema hivi Tabora utaondoka na mke” Alihitimisha Mzee Yule mwenye msimamo wa aina yake, kimya kikatanda tena huku upepo ukipiga kwa mbali kupitia madirishani, Ikawa ni zamu tena ya Mama Suhail kuvunja ukimya “Ila katika hilo hata mimi sina kipingamizi, Suala la ndoa halikwepeki kwa sasa japo hua sipendi hiyo tabia yako bwana wewe ya kuwapizaapiza watoto..” Aliongea kwa ustadi na utulivu Mama Suhail na kumfanya sasa Suhail ahisi kuwa hana mtetezi katika hilo, alijaribu kadri ya uwezo wake kujitetea bila mafaniko mpaka mjadala ukafungwa
“Leo jioni nitaenda kuongea na Bwana Fungameza juu ya utekelezaji wa hili jambo lakini kabla sijaonana nae nahitaji wewe uonane nae, tena ikiwezekana sasa hivi uende nyumbani kwake.. hakuna kazi ngumu utakayoenda kuifanya huko zaidi ya kuonesha heshma na kumjali kwa kwenda kumsabahi kabla yeye hajazisikia habari mjini huko kuwa umekuja”
Hilo likapita bila kupingwa, mazungumzo mapya yakachukuwa nafasi japo akilini mwa Suhail hakuwepo kabisa pale alimfikiria Shekhia, akamuwazia Sharifa kila mmoja kwa vitimbi vyake kasha akajisemea kimoyomoyo
‘Amaa kweli hivi ndivyo vita vya mapenzi alivyoniasa mzee Atrash’
Akatoka nyumbani kwao akiwaacha mama na ndugu zake wakimuandalia chakula japo hakuwa tena na hamu ya chakula chao, alipofika nje ikambidi sasa aingie nyumba kadhaa kwa majirani wao wa karibu kwa ajili ya kuwasabahi, na kutokana na mkasa wa ajali uliovuma kila kona akajikuta anapoteza muda mrefu wa mazungumzo katika kila nyumba aliyoingia, hata kufikia saa sita akawa ndio tena amerejea barabarani akielekea mjini akachuke usafiri wa kumfikisha Chemchem kwa Mzee Fungameza
Baba yake na Sharifa japo hakuwa amemtaarifa hata Sharifa kuwa amewasili, alitembea kwa miguu katika mtaa wa rufita mpaka alipofika mwanzoni kabisa mwa mtaa ule ambapo unakutana na Barabara kubwa inayokatisha mbele ya Soko Kuu la Tabora, sasa kabla hajafika huko mbele ikambidi asimame kidogo nje ya hotel ya Berenja kwa pembeni kidogo kuna Mkungu mkubwa ambapo kila siku iendayo kwa Mungu hukusanyika watu wa rika zote kwa ajili ya kupiga soga huku wakinogeshwa na michezo mbalimbali ikiwemo Bao, Draft, Rudo, Dhunna, Keram, na Pool table, kila mchezo ulijizolea washabiki wengi sana kutoka karibu kila pembe ya mkoa wa Tabora
Eneo hilo la mkunguni pia lilibarikiwa mvuto wa kibiashara bila shaka kutokana na idadi ile ya watu hivyo huduma kama Chakula, vinyaji, kahawa, Studio za muziki, Vinyozi, matunda nk vilishamiri sana. Sasa kutokana na umaarufu wa Suhail pamoja na baba yake basi ajali ile iliyopata kumkuta Suhail ilijadiliwa vilivyo kila mmoja akiwa ni gwiji wa kusimulia, basi alipowasili pale kijana Yule akapokelewa kwa Shangwe ya aina yake huku kila mmoja akitaka kumsikia Suhail mwenyewe, ikamchukuwa karibu nusu saa nzima kuiongelea ajali ile huku akijibu maswali kadhaa kutoka kwa wazee na vijana wenzie, akajitahidi kuyafupisha mazungumzo ili sasa awahi kwa Mzee Fungameza
Nyumba ya Mzee Fungameza ilikua katika hali yake ya ukimya, hapakua na bughdha ndani ya nyumba ile bila shaka ni kutokana na ukweli kwamba hakuna watoto wadogo wala idadi kubwa ya watu wazima zaidi ya Mzee Fungameza, Mama Sharifa, Sharifa mwenyewe na mdogo wake Sharifa ambae mara nyingi hua shuleni huko. Suhail akapitiliza mpaka ndani, alipofungua mlango tu akakutana ana kwa ana na Sharifa ambae hakika uzalendo ulimshinda akavibwaga vyombo alivyokua akipatia chakula akatimua mbio kumkimbia mchumba wake akamrukia na kumkumbatia huku akicheka na kubwabwaja maneno mengi na matamu yasiyomithilika, Suhail nae akajikuta katika hali ya furaha kiasi cha kumsahau kwa muda Shekhia,
“Yaani hata siamini Suhail, halafu kwanini umekuja bila taarifa we mwanaume?”
“Nilitaka kuku Surprise mpenzi wangu,” Alijibu Suhail huku akifuatishia tabasamu lake pana, kisha kabla Sharifa hajaongeza jambo lolote Suhail akamtoa maungoni mwake alipokua amemganda kama Ruba
“Mbona unanitoa?”
“Baba yupo?”
“Ndio yumo kule ndani kabisa”
“Sasa akitokea ghafla hapa?”
“Hee jamani kwani hajui kama mwane nimeshapenda?” wakaangua kicheko cha pamoja kabla ya Suhail kuongezea
“Tena umekufa umeoza.. Sasa potezea kwanza, acha nikamsalimie” Wakaachana na Suhail akaingia ndani moja kwa moja mpaka ‘Seating room’ huku akimuacha Sharifa akiwa hana tena hata haja ya kula
“Owhoo, we bwana leo nd’o umeibuka kama nyota ya Jaa,’ Alitania Mzee Fungameza baada kumuona Suhail akiingia ndani, akaacha haraka kitabu pale juu sofa lake akasimama na kumsogelea Suhail, akampokea kwa furaha huku akimkumbatia na kumkaribisha baada ya kusalimiana
“Karibu uketi.”
“Ahsante sana, habarini za hapa tu”
“Ah nzuri tu pole na misukosuko”
“Tumeshapoa midhali nimerejea salama nashukuru Mungu” Baada ya Salamu michapo ikaendelea kwa muda mrefu mpaka na mama Sharifa aliekua amelala nae akaamka na kujumuika nao pale katika makochi. Baada ya maongezi ya muda mrefu Suhail akaaga ili aondoke japo alikumbana na vipingamizi vya hapa na pale akilazimishwa akae kwa ajili ya kupata chakula cha mchana alipambana nao mpaka wakamuelewa na kumuacha akiondoka, wakamtoa mpaka barabarani hivyo kumnyima fursa Sharifa kuongea lolote tena na Mchumba wake,
Lakini hakikuharibika kitu, Simu zilitenda kazi!
*****
Suhail alirejea nyumbani kwao kwa ajili ya kupata chakula cha mchana, ilikua ni mahanjumati kwelikweli, Pilau lililokolea zabibu na Abdalasini, Mchuzi wa kuku uliungwa shatashata kwa nyanya za kuchuna.. Unaweza kujiuma ulimi aisee, Familia nzima ilijumuika pamoja kupata wasa’a mzuri wa chakula wakiwa pamoja. safari hii hapakua na mazungumzo mengi zaidi ya kuwapa salamu kutoka kwa Mzee Fungameza, wakati akiwa nyumbani kwao alikua akiwasiliana na mchumba wake Sharifa na wakakubaliana kua ifikapo saa kumi alaasiri wakutane katika hotel ya Saratoga iliyopo maeneo ya Bachu ambapo watachukua chumba ili wapate faragha tulivu ya kupiga stori zao huku Suhail akidhamiria kupasua ‘jipu’
*****
Mashariki mwa chumba Kochi moja aina ya sofa lenye uwezo wa kukaliwa na watu wawili liliegeshwa ukutani chini ya dirisha kubwa lililofunikwa upande mmoja kwa pazia pana. Laiti kama kochi hilo lingekua limekaliwa na mtu basi macho ya mtu huyo yangekua yakitazamana moja kwa moja na Kioo kikubwa cha Luninga aina ya Hitach iliyokua ikionesha tamthiliya ya kihindi kiasi cha kufanya nyimbo za malalamiko ya mahaba kutawala Chumba kile kilichopo Ghorofa ya tatu katika hotel ya Saratoga.
Pembezoni mwa Luninga ile palikua na mlango mdogo unaoingia moja kwa moja mpaka maliwatoni, na kukiacha Kitanda kikubwa cha sita kwa sita kikiwa sentimeta kadhaa kutoka katika mlango huo, Juu ya Kitanda hicho walikua wamejilaza vijana wawili wapendanao huku kila mmoja akiwa na lake kichwani. Suhail kusekwa akiwa amevalia jinzi yake safi pamoja na fulana yake mchinjo alikua amejilaza chali kitandani hapo huku akitafakari namna bora ya kuanza kumaliza ‘Mzozo’ uliokua ukimsukasuka moyoni Wakati Msichana aliekua amemlalia kwa juu usawa wa kifuani huku amevalia Suruali yake laini na fulana nzito alikua akiiwazia ndoa tu aliyokua akiisubiri kwa hamu kitambo kirefu.. Hakika moyoni kwa mtu mbali, hakuna aliejua mwenzie anafikiria nini muda ule!
“Leo nilipanga nikawasalimie jamaa zangu pale kijiweni kwao,” Suhail alivunja ukimya uliokua umetawala baada ya kua wameshasalimiana na kuoongea mambo mawili matatu tangu walipoachana mara ya mwisho na habari za ajali iliyomsibu mpaka aliporejea Dar na kuanza kazi
“Hivi kumbe haujaenda tu?”
“Huo muda ningeupata saa ngapi sasa? Yaani kila napopita inanibidi nikae karibu nusu saa kuongea..Kuanzia nilipotoa mguu wangu nyumbani kwa Mzee Kusekwa nikaanza kukutana na watu tunaofahamiana, Rufita nzima nilikua nikisimama simama, na pale Mkunguni ndio nilikaa sana, mara Kwa Mzee Fungameza..”
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni