Vita vya Mapenzi (14)
Zephiline F Ezekiel
6 min read
Mtunzi: Maundu Mwingizi
SEHEMU YA KUMI NA NNE
TULIPOISHIA...
TULIPOISHIA...
“Huo muda ningeupata saa ngapi sasa? Yaani kila napopita inanibidi nikae karibu nusu saa kuongea..Kuanzia nilipotoa mguu wangu nyumbani kwa Mzee Kusekwa nikaanza kukutana na watu tunaofahamiana, Rufita nzima nilikua nikisimama simama, na pale Mkunguni ndio nilikaa sana, mara Kwa Mzee Fungameza..”
KAMA UNASOMA SIMULIZI HII NJE YA APPLICATION YA CnZ Media INSTALL ILI USIPITWE NA MIENDELEZO
SASA TUENDELEE...
“Wee Sio Mzee Fungameza, sema Baba Mkwe’” Sharifa alimkatisha mchumba wake kwa utani, kikafuata kicheko kidogo kabla ya Sharifa kuendelea “Unadhani hata utapakumbuka hapo kijiweni kwenu?”
“Kumekuwaje kwani?”
“Wamepaboresha hadi raha, ukifika tu barabara ya ujiji pale kwenye Kona inayoungana na mtaa wa Heri, nyumba kama ya tatu tu hivi Utaona Bango Kubwa likinadi MIKINDA PROJECTS CAMP(MPC) na anuani zao pamoja na huduma zitolewazo ofisini hapo..”
“Aisee wamekua na ofisi kabisa inayotoa na huduma? Safi sana”
“Ndani kuna huduma za kifedha, huduma za Steshenari, malipo ya umeme nk, huku kwa nje kuna vijana wa bodaboda wameegesha pikipiki zao na biashara ndogondogo zikiendelea, Camp ile imekua sana yaani nd’o kioo cha vikundi vyote vya hapa mjini kwa sasa”
“Safi sana, sasa wamejichanga wenyewe ama nani amewafadhili?”
“Wao wenyewe tu lakini pia si unajua tena wanasiasa wakishaona kipindi cha uchaguzi kinaanza nao nd’o wanajifanya kuwajali na kuwawezesha vijana, sasa nasikia kuna Mheshimiwa mmoja anautaka ubunge nd’o kawawezesha lakini wengine wanasema kua ni wao wenyewe wamejichanga, nafikiri ukienda kwakua wewe ni jamaa zako watakupa ukweli wa mambo” Alijibu Sharifa kisha mazungumzo mengine yakashika kasi, Iliwachukua muda mrefu kuongea huku wakiliwazana kwa maneno matamu ambayo kwa kiasi kikubwa yalikua yakitoka kwa Sharifa huku Suhail akijikuta akiwa na mchombezaji tu mpaka giza la Magharibi likaanza kuingia..
“Sharifa mpenzi wangu kuna jambo moja kubwa sana na la muhimu nahitaki kuongea na wewe leo.. nahitaji umakini wako na Subra kubwa katika hili..” Suhail alianzisha sasa mjadala alioukusudia na kumfanya Sharifa ajitengeneze vizuri katika kifua cha kijana Yule, kisha bila ya kujibu chochote akaendelea kusikiliza “Mimi na wewe tuna historia ndefu sana tangu tuliingia katika mahusiano yetu, tukapambana na vikwazo vingi kuanzia kwa baadhi ya wanafunzi wenzetu pale shule, kwa walimu, na hatimae kwa wazazi wetu..
Tukaishinda vita ile huku tukikubaliana kua yatupasa tuishinde vita ya pili ambayo ni kutokukutana kimwili mpaka siku ya ndoa yetu, hakika vita ile tuliishinda ingawaje ni sahihi zaidi endapo nitasema kwamba wewe ndie ulieishinda zaidi.. Sasa kuna vita ya mwisho yatupasa tuishinde pia..” Kufikia hapo Suhail akatulia kidogo ili kuruhusu maneno yale yapenye kichwani mwa Sharifa,
“Una maana gani Suhail, usiniambie kua ulinisaliti huko Dar?” alibwata Sharifa kwa sauti ya juu huku akijiinua kutoka kifuani kwa Suhail ambae alimzuia na kumrejesha katika himaya yake kisha akaendelea
“..Nasema wewe ndie ulieishinda ile vita kwasababu uliyatekeleza makubaliano yetu kwa lengo lilelile makhsusi ukiamini siku ya ndoa yetu tutafurahia kwa pamoja.. Tofauti na mimi nilieishinda vita hiyo kwa kushinikizwa zaidi na matakwa ya mwili wangu” Suhail akavuta pumzi huku akitafuta maneno mazuri ya kuyatumia kwa ushawishi alioupanga “…Mimi pia nimejizuia kama wewe japo mimi ni zaidi ya wewe.. Wakati wewe ukijua kua uvumilivu huo una mwisho wake ambao ni siku ya Ndoa yetu lakini kwangu mimi hali iko tofauti kwani nitaendelea kua katika hali hii ya kutokukutana na wewe na hata mwanamke mwingine kiasi cha maisha yangu yote yaliyobaki hapa duniani..”
“We Suhail mbona sikuelewi wewe?” Sharifa alimkatisha Suhail kuendelea kuongea huku akijitoa kwa nguvu toka pale kifuani alipokua amejilaza, hali ya hatari ilishabisha hodi moyoni mwake
“Sikukueleza hili tangu tulipokua shuleni pamoja, Mimi mwenzio ni Mbovu… siwezi kua Mume kwa mwanamke yoyote katika dunia hii, sipaswi kufunga ndoa kisheria..”
“Whaaat?!” Alimaka mwanadada yule kwa sauti kali huku akiendelea kuongea kwa ghadhabu “Siamini kabisa.. siamini Suhail, yaani umeona mimi ni bwege kiasi hiki? Umeamua kuniacha kwa kwa ‘Style’ hii!!! Haiwezekani” Sharifa aliendelea kulalamika kwa sauti ya uchungu kiasi cha kuanza kutiririsha machozi usoni mwake, Suhail aliekua kimya muda wote wakati Sharifa akilalama alijiinua kitandani ili ambembeleze mchumba wake lakini aliambulia patupu, Sharifa alimsukumia kwa nguvu kitandani kisha akaendelea kulia kwa sauti “Suhail kwanini unataka kunifanyia hivi lakini? Nimekukosea nini we mwanaume? Kumbuka yote niliyoyafanya kwa ajili yako, kumbuka Isevya Sec tulipotokea, yaani leo umeamua kuniacha kwa sababu ya hivyo vijisenti vyako, nakwambia sikubali Suhail.. Sikubali”
“Hebu tulia kwanza Sharifa tuongee mpenzi wangu, kumbuka mwanzo nilikuomba uwe na Subra na makini katika jambo hili, kumbuka hili ni suala zito kuliko hivi tunavyoliongelea, linahitaji uelewa, umakini, subra, na usiri mkubwa.. Sijawahi kumueleza yoyote hapa duniani zaidi yako kwakua nakupenda na kukuamini hivyo kunielewa kwako ni faraja kwangu..”
“Hakuna cha Subra wala nini hapa.. tangu mwanzo nilishaanza kukushitukia kua unataka kunigeuka, Kama wewe ni Mbovu si kuna dawa kemkem zinatolewa kwanini ukimbilie tu kua eti hauwezi kuoa? Hila zako nimezibaini Suhail,” Sharifa aliendelea kujibu huku akilia kwa sauti na kumfanya Suhail ajisikie vibaya sana, hakika alihisi dhambi kubwa sana kwa kitendo kile alichodhamiria kukifanya lakini hakua na jinsi
“..Sharifa mpaka hapa unapoona nimeamua kukueleza jambo hili usifikiri sijapita kwa wataalamu, nimepita kila kona lakini majibu nayopewa naambiwa kua sitaweza kupona ugonjwa huu, usifikiri mimi napenda fedheha hii, naomba unielewe mpenzi wangu.. na ninakuahidi kwamba katika mali hizi ninazozimiliki kwa sasa kuna sehemu kubwa ya mali hiyo nitakupatia wewe ili upate pa kuanzia katika maisha yako mapya na mtu utakaekua nae..
Nakupenda sana Sharifa lakini sijiwezi katika hili” Maongezi yalikua marefu sana lakini Sharifa hakukubaliana hata kidogo zaidi ya kuendelea kuongea kwa jazba na uchungu huku mara kadhaa akimsogelea Suhail pale kitandani na kumkwida kwa nguvu mpaka ile fulana yake ikawa kama iliyotafunwa na Ng’ombe
“Oky, Ok Suhail, nimekuelewa, tena vizuri sana,” Sharifa alianza kuongea tena upya huku akijizuia kulia “Sina tena Mume aitwae Suhail, sina tena furaha na amani moyoni, sina tena thamani duniani, hivyo nitakuacha na pesa zako na wanawake zako uendelee nao kwa uhuru.. Mimi bora tu sasa Nife nikapumzike, siwezi kuendelea kuishi katika hali hii..” Maneno hayo ya Sharifa yalimshtua sana Suhail aliekua amejilaza kitandani, akainuka haraka ili ajue nini maana ya maneno yale.
Loo salale!
Hakika Sharifa alikua akimaanisha akisemacho, Suhail aliishia kumshuhudia Sharifa akiwa ameshaparamia juu ya Dirisha kubwa la chumba kile kilichopo Ghorofa ya tatu katika hotel ya Saratoga iliyopo kata ya Gongoni kiasi cha kuvunja vioo vya dirisha hilo, Vioo hivyo vikamchana sehemu ya kichwa chake akawa ananing’inia tu juu huku anavuja damu kichwani
“NOOO, Sharifa pleeeese usifanye hivyo’,” Suhail alihamanika na kuanza kupayuka hovyo
“No Suhail, I can’t.. Lazima nife tu”
“Usifanye hivyo Sharifa mpenzi wangu, Hebu fikiria hayo maamuzi unayotaka kuyachukua, wafikirie wazazi wako na unifikirie na mimi.. nakuomba tukae tuzungumze”
“Hakuna mazungumzo Suhail, nitaiweka wapi Sura yangu mimi jamani, yaani kukupenda kote kule umeamua kunidhalilisha namna hii! siwezi nakuambia ni bora nife” Kila Suhail alipotaka kumsogelea ndivyo alivyojisogeza mpaka kwenye ncha ya dirisha hilo ikiwa na sehemu kidogo tu iliyobakia ili akijiachia tu atabadilika jina na kuitwa Marehemu.
Wakati hayo yanaendelea Meneja wa Hotel hiyo akiwa katika ofisi yake iliyopo ndani ya hotel hiyo alishtushwa sana na tukio hilo aliloliona kupitia katika Kompyuta yake iliyounganishwa na Kamera nyingi zilizotegeshwa kila kona kwa nje ya hotel hiyo, na kwakua sasa Sharifa alikua ameshatokeza nje ya dirisha hivyo aliweza kuonekana kwenye kompyuta kupitia kamera zilizokua nje ya chumba hicho. haraka Meneja akamtumia taarifa mlinzi wake ambae akatokezea kwa chini ya chumba kile akawa anampigia kelele Sharifa arejee ndani, Hakika lilikua ni tukio la fedheha na kuogofya.
Sasa wakati Sharifa amemgeukia yule mlinzi aliekua akipiga kelele akaona imeshakua dhahma hivyo akaona liwalo na liwe Bora ajirushe tu.. ndipo haraka Suhail akautumia mwanya huo akaruka kwa kasi ya ghafla kutokea pale alipokua amesimama kuelekea kule Dirishani alipokua anataka kujirusha Sharifa., Sharifa nae alikua kaishagundua kua anarukiwa basi hakua tena na sababu ya kujichelewesha, Akarijusha kwa nguvu ili aangukie nje aitoe roho yake mwenyewe. Mlinzi aliekua chini aliishia kupiga kelele kali za uwoga huku Suhail nae alipiga kelele za hamaniko na woga mkubwa..
*****
“Kwanini umeamua iwe haraka hivyo?,” Mzee Fungameza alimsaili Mzee Kusekwa aliekua amewasili nyumbani kwake kwa ajili ya mjadala wa Ndoa ya vijana wao Suhail na Sharifa
“Sikuhitaji iwe haraka lakini kwa hali ya mazingira naona kama itakua ni busara tukifanya hivyo maana hawa ni vijana bila kuhimizwa basi lolote laweza kutukia.. na nimeona Suhail ameshapata kazi inayomfanya awe busy kiasi cha kua haeleweki hata alipo sasa hii chelewachelewa unaweza kukuta mwana si wako”
“Ok sawa, sidhani kama ni vibaya ukizingatia kwamba ndoa za kiislam hua hazina haja ya kuchukua muda mrefu lakini itakua ni busara zaidi tukisema na walengwa wewnyewe ili nao tusikie wanataka hili suala liende kwa mtindo gani..”
“Sawa, hakuna shida mimi leo nitaongea na Suhail japo nimeshafanya hivyo, sasa Kesho nitakuja kuongea nawe kujua umefikia wapi” Wakati wazee wanaendelea na mipango ya Ndoa ya vijana wao hawakua wakijua kua mambo yanaharibika huko Saratoga Hotel, Laiti wangelijua pengine wasingelikua pale muda huo wakijadili kitu chenye utata mkubwa sana..
Bahati nzuri wakati sharifa anajirusha Suhail alikua ameshakamata sehemu ya kiunoni katika suruali aliyoivaa, hakumuachia.. akamng’ang’ania japo kutokana na uzito wa Sharifa aliekua akining’inia kule juu Dirishani Suhail nae akajikuta akizidiwa na kuvutwa yeye nje badala ya yeye kumvuta Sharifa, ikawa kititim sasa. Akaendelea kumzuia na kujizuia yeye ili wasianguke wote mpaka hatimae akafanikiwa kumvuta ndani kwa nguvu kupitia palepale dirishani,
Kabla hajafanya lolote akiwa anatweta huku akimuangalia Mchumba wake kwa hasira na hofu ghafla akasikia mlango ukigongwa kwa nguvu sana, akauangalia mlango kwa mashaka makubwa akijua sasa mambo yameshaharibika, akataka kwenda kuufungua lakini akahofia kumuacha Sharifa peke yake pale chini akihofia kua asije akapata tena upenyo wa kujirusha kwa mara ya pili, akaamua kumnyanyua na kusogea nae mpaka mlangoni..
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni