DHAMANA (6)
Zephiline F Ezekiel
6 min read
Mwandishi: Hassan O Mambosasa
SEHEMU YA SITA
TULIPOISHIA...
TULIPOISHIA...
walivuka barabara wote kwa pamoja wakaupita uwanja wa mpira wakakuta umati wa watu ukiwa umezunguka nyumba hizo bado zilikuwa zinateketea na moto huo ulishindikana kuzimwa na kikosi cha zima moto kilichofika hapo kwani magari yao yalitumia maji hadi yakaisha lakini moto haukuzimika hata kidogo.
KUNA MATANGAZO YANATOKEA YAGUSE ILI KUNIPA NGUVU YA KUENDELEA
KAMA UNASOMA SIMULIZI HII NJE YA CnZ Media APP INSTALL ILI USIPITWE NA MIENDELEZO
SASA TUENDELEE...
Asp John pamoja na wale vijana waliwafuata wale askari wa jeshi la polisi kikosi cha zimamoto ambao walionekana kukata tamaa kabisa katika uzimaji moto, maaskari hao walitoa saluti kwake huku wakisema, "jambo afande".
"jamboo, nipeni taarifa mmefikia wapi katika kazi yenu kwani naona bado moto unawaka" Asp John aliwaambia.
"Afande tumefanya juhudi za kuuzima huu moto kwa kutumia kila njia ila imeshindikana hadi maji yanaisha hatukuweza kuuzima na ikatubidi tutumie gesi lakini bado tumeshindwa kuuzima na inasadikika Mkuu wa idara ya sheria makao makuu ya kampuni hizi yupo ndani ya nyumba ya tatu na hajatoka hadi muda huu na hata tulipofika tulikuwa tukisikia kelele za mtu akiomba msaada lakini sasa hazisikiki" Mmoja wa maaskari wa zimamoto aliongea kwa ufupi juu ya tukio hilo la kuungua kwa nyumba hizo, James aliposikia maelezo hayo alipiga kelele huku akiita, "Babaa!". Aliwapita askari wa kikosi cha zimamoto akakimbia kuelekea ulipo moto katika nyumba ya tatu ya kampuni, maaskari wote walianza kumkimbiza ili wamuwahi asiingie ndani ya moto huo kutokana na ukali wake.
Mbio za watu wote waliokuwa wakijaribu kumzuia James asiingie ndani ya nyumba hazikuzaa matunda yoyote katika kumzuia kwani James aliingia ndani ya nyumba hiyo kabla hawajamzuia, wenzake pamoja na maaskari wote walipojaribu kuikaribia mlango wa nyumba aliyoingia James walijikuta wakitupwa nyuma wote baada ya mlipuko mzito kutokea katika nyumba hiyo kisha nyumba nyingine zilizosalia nazo zikapata mlipuko wa aina hiyo hiyo.
Asp John, maaskari wa zimamoto pamoja na wenzake James wote walisikitika kwa kitendo cha James kuingia katika nyumba hiyo inayoungua ambayo tayari imeshatoa mlipuko mzito wa moto, bado walikuwa wamelala chini baada ya kutupwa na mlipuko mzito waliposogelea nyumba aliyoingia James ili wamuokoe. Ajabu ya mlipuko huo uliowatupa haukuwaunguza hata kidogo wala hata kunuka harufu ya moshi, walikuwa wameumia tu baadhi ya sehemu za miili yao baada ya kuanguka chini.
Wakiwa hawana hata akili ya kunyanyuka pale chini tayari jambo jingine la kustajaabisha lilianza kutokea ambalo liliwafanya wakimbie kuelekea ulipo uwanja wa mpira ili wakae mbali na ardhi ambayo imebeba nyumba hizo, lilikuwa ni tetemeko la ardhi lililoikumba ardhi iliyobeba nyumba hizo huku eneo la jirani na hapo likiwa limetulia bila kupatwa na tetemeko hilo. Matofali ya nyumba hizo ambazo bado zilikuwa zinawaka yaliporomoka katika mpangilio wake uliounda ukuta na yakajazana kama tanuli katika kila nyumba iliyokuwa imejengwa, tukio hilo lilishuhudiwa na halaiki ya watu ambayo tayari ilikuwa imeshajikusanya katika uwanja wa mpira kuangalia maajabu hayo. Waandishi wa habari kituo cha televisheni cha Tanga nao walikuwa wakilirusha tukio hewani, hata waandishi wa habari waliopo mkoa wa Tanga kuwakilisha vituo vyao wakikuwa wameshawasili pia walikuwa kazini.
Tetemeko hilo la ardhi la maajabu liliendelea kutikisa ardhi hiyo inayomilikiwa na kampuni ya Extoplus hadi hata matofali yalijijaza vifusi katika kila eneo lililokuwa limejengwa nyumba yakasagika yakawa mchanga mtupu, baada ya tetemeko kutulia ndipo askari wa zimamoto na uokoaji walipopata ujasiri wa kusogelea katika kifusi cha mchanga uliosagika ambao ulikuwa ni wa matofali wa nyumba ile waliyoingia James na Baba yake kwa nyakati tofauti. Walikifukua kifusi hicho kwa kutumia vifaa vyao na kukagua kila sehemu ili waweze kuitoa miili ya baba na mwana lakini hawakuambulia hata kiungo kimoja cha miili ya James na baba yake, askari walizidi kupigwa na mshangao watu tukio hilo kwani ilikuwa ni jambo la ajabu sana.
"mmh! Sijawahi kukutana na tukio kama hili tangu nianze kufanya kazi katika kikosi cha zimamoto na uokoaji katika jeshi la polisi" Kiongozi wa askari wa zimamoto na uokoaji alimuambia Asp John.
"hivi jambo kama hili linawezekanaje?" Asp John alijikuta akiuliza swali ambalo halina maana yoyote kwa mkuu wa kikosi cha zimamoto na uokoaji.
"hilo swali hata sijui nikujibu vipi unaona kabisa imezekana katika namna isiyokuwa rahisi, mtu aingie ndani ya nyumba halafu ilipuke tu kisha tetemeko liloikumba ardhi ya ukubwa wa ekari kumi na tano litokee liangushe matofali yasagike halafu moto uzime tusipate hata baki la mwili wa binadamu katika sehemu waliyoingia" Yule mkuu wa kikosi cha zimamoto aliongea.
"ama kweli hii ni dunia ina mambo ambayo usiyoweza kuyadhania" Asp John aliongea huku akisikitika.
"ndiyo hivyo afande" Mkuu wa kikosi cha zimamoto aliongea.
"hapa hamna la ziada ngoja nirudi nikaendelee na tukio la kule la Bwaga macho, vijana nina shida na nyinyi hebu nifuateni" Asp John aliongea huku akiondoka na wale marafiki zake James wakamfuata.
Hadi jioni inaingia tayari tukio lile la ajabu lilikuwa lishaenea jiji zima la Tanga na kwingineko ndani ya nchi ya Tanzania na hata Afrika ya mashariki, ilitokea kuwa habari iliyoteka vyombo vyote vya habari katika ukanda huu na hata katika kituo BBC idhaa ya Kiswahili ilitangazwa na kupelekea kuwa habari iliyosikika karibia dunia nzima kwa watu wanaongea kiswahili. Taarifa za vibweka vilivyotokea huko Duga zilimfikia mmiliki wa kampuni ya Extoplus Hamid akiwa yupo kitandani katika wodi ya zahanati ya kampuni yake tangu alipoanguka kwenye chumba cha mkutano, aliipata taarifa hiyo kupitia luninga iliyopo katika wodi aliyolazwa akawa amebaki na masikitiko tu kutokana na hasara aliyoipata kuungua kwa nyumba hizo ambazo zilimgharimu pesa nyingi hadi kukamilika kwake. Hadi saa nne usiku anaruhusiwa alikuwa na majonzi kutokana na jambo hilo, alirudi nyumbani kwake kwa msaada wa dereva wake.
Asubuhi ya siku iliyofuata alitoka mapema nyumbani akaenda ofisini akiwa na mawazo lukuki kichwani mwake, siku hiyo ilikuwa mbaya kwa Hamid kuliko siku zote za maisha yake kwani alipifika ofisini kwake tu akakumbana na kisanga kingine baada ya mwili wa kaimu mwenyekiti mtendaji wa kampuni yake Hisan kukutwa ukiwa chumba cha mkutano alichokuwemo siku iliyopita akiwa na wafanyakazi wake wakuu wakiongea.
Mwili wa Hisan ulikutwa na mfanya usafi wa kampuni hiyo ambaye alichanganyikiwa baada ya kuuona ukiwa hauna uhai upo sakafuni. Tukio hilo lilikuwa ni tukio jingine la aina yake ambalo ilionekana ni kama mkosi umeingia kwenye kampuni hiyo kutokana na kuzaliwa kwa jambo jingine lililozidi kumchanganya Hamid, baada ya polisi kuchukua vipimo vyote pamoja na kuondoka na mwili wa Hisan afisa ajira wa kampuni hiyo aliingia katika ofisi ya Hamid akiwa na faili kubwa aliloweka mezani kisha akaweka barua juu yake.
"Msuya ndiyo nini hii unaniletea" Hamid aliuliza.
"Bosi hiyo ni barua ya kuacha kazi katika kampuni hii ili niwe salama na maisha yangu" Msuya ambaye ni afisa ajira katika kampuni hiyo aliongea.
"unasema nini wewe?!" Hamid aliuliza kwa mshangao.
"ndiyo hivyo bosi kutokana na ndoto niliyoiota usiku wa leo iliyonipa onyo juu ya maisha nikiendelea kufanya kazi hapa sina budi kuacha kazi, uamuzi huu si wangu peke yangu bali ni wa mameneja wote pamoja na wakuu wa idara wote na barua zao zipo kwenye faili nililokuletea" Msuya aliongea maneno yaliyozidi kumchanganya Hamid.
"yaani Msuya pamoja na kuwa ni msomi mwenye elimu kubwa bado unaamini ndoto" Hamid aliongea kwa masikitiko.
"Sina budi kufanya hivyo kwani kila mtu aliyeandika barua hii ameota ndoto kama hii tena ameonywa kuhusu kifo kilichotokana na ubishi wa staff wa idara ya uhasibu waliokufa jana ikiwa atabisha. Nimeamua kuacha kazi mimi na wenzangu na kila mmoja hahitaji marupurupu yoyote tunaondoka kama tulivyokuja" Msuya aliongea kisha akatoka ndani ya ofisi hiyo akimuacha Hamid akiwa amechanganyika akiwa anakaribia hata kulia, alitulia ofisini kwake kwa muda mfupi kisha akaamua kutoka kupitia idara zote kuangalia kama kile alichoambiwa na Msuya ni kweli au ilikuwa ni utani. Huko ndipo aliposadikisha maneno ya Msuya baada ya kukuta ofisi zote zikiwa zipo tupu hakuna hata mfanyakazi, Hamid alijikuta akianza kulia mwenyewe na akaona hali aliyoikimbia kabla hajawa na familia sasa inaanza kumrudia. Yeye hakutaka hali hiyo imtokee tena na alikuwa yupo tayari kuizuia kwa namna yoyote ile na hapo ndipo alipopata ufumbuzi wa matatizo yake kwa mtaalamu wake maalum.
"Dokta Bundi atanisaidia niepukane na adha hii ngoja niwahi kwenda kwenda kwake Mwamboni" Hamid alijisemea mwenyewe kisha akaanza kutoka mbio kuelekea nje ya ofisi ambapo alipanda gari yake akaiondoa kwa mwendo wa kasi akiwa na haraka ya kuwahi safari yake. Aliendesha gari kwa mwendo wa kasi akiwa na ari ya kuwahi kufika Mwamboni kwa mganga wake ambaye huwa anamsaidia katika matatizo mbalimbali, akiwa yupo ndani ya gari akiwa anakatiza katika barabara ipitayo Chumbageni alisikia sauti ikimuambia "aisee nishushe hapohapo chumbageni police station nataka kuongea na jamaa yangu".
Hamid alishtuka sana akatizama nyuma kwa uoga na akijikuta anatamani hata apotee kimiujiza humo ndani ya gari, laiti kama moyo wake ungekuwa na nguvu kama ya vijiko vinavyojenga barabara ya kugusa ukuta tu na kuuangusha basi ungekuwa ushapasua kifua chake kwa jinsi ulivyokuwa unadunda kwa nguvu baada ya kumuona Hisan aliyekutwa akiwa amekufa katika chumba cha mkutano asubuhi ya siku hiyo.
"unashangaa nini Hamid hebu simamisha gari hapo Chumbageni polics station nikaangalie ripoti ya kifo changu kilichonipata jana kama polisi wamechunguza kiusahihi" Hisan aliongea huku akionekana yupo katika hali ya kawaida tu, Hamid alikuwa tayari ameshaachia mkojo ulimtoka bila hata kujijua.
"Ona sasa dume zima una miaka arobaini na nane unajikojolea kisa kumuona mtu aliyekufa akiwa anatembea, hebu simamisha gari nishuke wewe nishafika tayari nataka nikaangalie ripoti ya kifo changu nasikia anayo Inspekta Ismail Mdoe. Au hii sura inakuchanganya ngoja niibadilishe basi uoga ukupungue" Hisan aliongea kisha akabadilika kuanzia sura hadi mwili ukawa wa mtoto aliyemtokea Hisan kabla hajafa.
"Hapo vipi utaniogopa tena?" Aliuliza huku akimtazama Hamid ambaye alizidi kuogopa na akawa anahangaika kufungua mlango ili ajitupe nje kuikimbia sura aliyoiona sasa hivi ikiwa ina macho mekundu, milango ya gari ilikuwa haifunguki na hata alipotoa kifunga mlango bado haikufunguka hata kidogo.
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni