SHETANI ALINIITA KUZIMU (4)
Zephiline F Ezekiel
6 min read
Mwandishi: Shiwawa Binasalaan Al Jabry
SEHEMU YA NNE
TULIPOISHIA...
TULIPOISHIA...
Kwa kuwa usiku huo nilikuwa na hamu sana ya kula nyama, sikuweza kupata usingizi kabisa, nikaamua kuiita ndege ya kichawi (ungo). Baada ya kufanya hivyo, hazikupita dakika nyingi nikasikia kitu kimetua sakafuni tii, nilipoangalia niliuona ungo.
KUNA MATANGAZO YANATOKEA YAGUSE ILI KUNIPA NGUVU YA KUENDELEA
KAMA UNASOMA SIMULIZI HII NJE YA CnZ Media APP INSTALL ILI USIPITWE NA MIENDELEZO
SASA TUENDELEE...
Usafiri huo ulikuwa na zana zote za kichawi yaani hirizi ya kinga, mafuta, tunguri na vitu vingine ambavyo wachawi huvitumia kufanya ulosi.
Nikiwa mtupu nilipanda kwenye ndege yangu na kunuiza inipeleke mochwari ya Hospitali ya Rufaa ya Bugando ya jijini Mwanza. Niliuambia ungo huo kwamba
nilihitaji sana kitoweo hivyo uondoke haraka kuelekea Bugando, ndipo ulitokea upepo mkali sana. Ingawa mle ndani tulikuwa watu wengi hakuna aliyesikia upepo
huo ukivuma isipokuwa mimi tu, upepo huo ulifunua paa kwenye kona ungo ukapaa. Kwa kuwa ndege ya kichawi inakwenda kwa kasi ya ajabu, kufumba na kufumbua ilitua nje ya mochwari ya Bugando.
Baada ya kuteremka niliingia ndani ambapo niliwakuta wachawi wenzangu waliofika pale kwa lengo kama langu, yaani kutafuta kitoweo. Kwa kuwa hatukufahamiana,
tulisalimiana kwa kugonganisha makalio yetu kisha niliwauliza walitokea wapi, mmoja wao akanijibu kwamba katika Kisiwa cha Ukerewe. Mchawi huyo
aliponifahamisha hivyo, nilishukuru ndipo kila mmoja wetu akaanza kuchagua ni maiti gani ilifaa kwa kitoweo.
Katika chumba hicho cha kuhifadhia maiti, kulikuwa na maiti za watu wazima, watoto na vikongwe, lakini binafsi nilihitaji maiti ya mwanamke mwenye mimba ambao nyama yao huwa tamu sana.
Tukiwa bize kutafuta maiti, wahudumu wa chumba hicho walifungua mlango wakaileta maiti ya mwanaume mmoja na kuilaza sakafuni. Wakati wakiilaza maiti hiyo,
hawakuweza kutuona na walipomaliza waliondoka bila kujua kama mle mochwari mlikuwa na wachawi. Baada ya kuondoka, wachawi wawili waliichukua ile maiti na
kuisogeza pembeni kabisa, wakaanza kucheka. Kufuatia kukosa maiti ya mwanamke mwenye mimba, niliamua kupiga darubini yangu wodini kujua kama kulikuwa na wagonjwa wenye ujauzito waliokuwa maututi.
Baada ya kuangalia wodi ya wazazi nikamuona dada mmoja aliyekuwa hoi, nikamfuata na kusimama mbele yake ambapo nilimtia roho ya mauti, hazikupita dakika tatu
akaaga dunia. Nilichokifanya niliichukua ile maiti kichawi na kuipeleka mochwari kwa wenzangu ambako nilikuta wameondoka na ile maiti ya yule jamaa mnene aliyekuwa ameletwa punde.
Kwa kuwa nilikuwa nimewasiliana na yule dogo kiongozi wetu ambaye wakati huo alikuwa kwenye kikao na wachawi wengine, alifurahi sana nilipomwambia nimepata
kitoweo akaniambia nikipeleke haraka sana. Baada ya kuniambia hivyo nilizipakiza maiti mbili kwenye ungo yaani ya yule mama mjamzito na ya kijana mmoja kisha
nilinuiza kwamba ungo upae, ukatii. Wachawi wenzangu waliponiona natua walifurahi sana, baada ya kutua niliibeba ile maiti ya mama mwenye mimba na kwenda kuiweka pembeni kidogo.
Wakati wachawi wenzangu wakiendelea kushangilia kwa kuwapelekea nyama, niliibeba maiti ya yule kijana na kuiweka kando. Kwa kuwa nilikuwa na roho ya kichawi
isiyo na huruma, nilichukua panga na kujongea ilipokuwa maiti ya mama mjauzito nikaichinja shingo yake kama kuku na kuilaza kwenye sufuria. Wachawi wenzangu
walipoona jinsi damu ilivyokuwa ikitiririka kama bomba walishangilia, ilipojaa nilibeba ile sufuria na kumpelekea yule dogo kiongozi wetu.
Kwa kuwa ilikuwa lazima aanze kunywa yeye, alipokea ile sufuria na kuipeleka mdomoni ambapo alikunywa kiasi na kunirudishia. Baada ya kunirudishia, nami
nilikunywa kisha nikawapatia wenzangu ambao nao walikunywa kwa zamu mpaka mchawi wa mwisho. Tulipomaliza kunywa ile damu ambayo ilikuwa tamu sana, tulianza kushirikiana kukata nyama za zile maiti huku wengine wakiongeza kuni kwenye moto tukaziinjika.
Wakati nyama zikiendelea kuiva, yule dogo kiongozi wetu wa uchawi akatuambia kwamba alihisi ile nyama isingetosha kulinganisha na uwingi wa wachawi
tuliokuwepo. “Jamani hii nyama itakuwa haitutoshi kwani leo tupo wengi sana,” yule dogo alituambia. Baada ya kusema hivyo aliagiza ikatafutwe nyingine haraka
sana, alipotoa kauli hiyo kutaka sifa nilimwambia nitaenda mimi. Wachawi wengine wakiwa wananishangilia, nilipanda kwenye ungo wangu nikanuiza unipeleke mochwari ya Bugando, kufumba na kufumbua ukapaa.
Sikuchukua muda mrefu nikatua nje ya mochwari hiyo ambapo niliingia ndani kichawi, nikabeba maiti mbili na kuzitoa nje. Baada ya kuzipakiza kwenye ndege
yangu, nikaondoka kurudi kwa wenzangu, kama ilivyokuwa awali, walipoona ungo unatua walishangilia sana. Baada ya kuzishusha zile maiti, dogo kiongozi wetu aliagiza zichomwe kama mishikaki kwa sababu zile za awali zilipikwa.
Alipotoa kauli hiyo alipaza sauti na kusema wote tumsikilize kwani kulikuwa na jambo muhimu alitaka kuongea nasi. Tukiwa tumetulia kimya aliniita na
kuniambia nisogee karibu yake, nikafanya hivyo. “Naomba mnisikilize kwa makini, mnamuona huyu kijana hapa!” Yule dogo mchawi aliwaonesha mimi akiwa kainua
mkono wangu wa kushoto juu. Kufuatia kuulizwa hivyo, wachawi wote walisema walijibu waliniona ndipo alisema kuanzia siku ile amenipandisha cheo nitakuwa msaidizi wake.
Aliendelea kusema ameamua kufanya hivyo kwa sababu nilikuwa najituma na nilikuwa nina busara ambazo zinatakiwa sehemu yoyote. Aliposema hivyo, wachawi
wenzangu walishangilia mno, mimi nikabaki ninatabasamu kwani sikutegemea kupewa madaraka makubwa kiasi kile. Baada ya kunitambulisha, kazi ya kuchoma nyama
na kupika iliendelea na zilipoiva mtu wa kwanza kupelekewa kitoweo hicho alikuwa yule kiongozi wetu.
Alipoonja alituruhusu tuendelee kupata kitoweo na kunywa damu iliyobakia na waliopenda kucheza ngoma wafanye hivyo. Tulipomaliza kula nyama, yule dogo
alituamuru tukusanyike pamoja kwani kuna mwenzetu mmoja alihitaji kuongea nasi. Tukiwa tumefanya hivyo, alimwita yule mwenzetu na kumwambia aeleze shida yake
ndipo alianza kwa kusema; “Ndugu zangu, mimi naishi na mjomba wangu ambaye ni mlokole, kwa kweli amekuwa akiharibu sana mambo yangu hasa usiku.
“Kutokana na ulokole wake, kila siku usiku anaamka na kuanza kuomba kitendo hicho kinaharibu nguvu zangu za kichawi hivyo naomba mnisaidie kupambana naye.”
Baada ya mwenzetu kutueleza hivyo, mkuu wetu alicheka sana na kutuambia kwamba ilikuwa kazi ndogo sana kupambana na huyo mjomba wake. “Mtu mmoja hawezi kukukosesha raha, usiku huu atakiona cha moto,”
yule dogo mkuu wetu alituambia na kuangua kicheko. Alipomaliza kucheka alimwambia yule mwenzetu aliyeomba asaidiwe kwamba awachague wachawi watano aliopenda
waongozane naye kwenda kumkabili huyo mjomba wake. Nataka mkifika mkamtie roho ya uchizi aanze kuongea maneno yasiyoeleweka na kufanya mambo ya ajabu ili
atambue kwamba sisi ndiyo wakuu wa ulimwengu wa giza.
Baada ya mwenzetu kuambiwa hivyo, mtu wa kwanza kumchagua nilikuwa mimi kisha aliwachagua wengine watatu pamoja na yeye tukawa watano. Yule dogo kiongozi
wetu alituambia niite ungo utakaotupeleka kwa yule mlokole, nikafanya hivyo ambapo hazikupita sekunde kumi ungo ukatua. Baada ya ungo kutua, tuliingia wote
kisha niliuamuru upae ndipo tukaanza safari ya kwenda nyumbani kwa mlokole.
Jambo la kushangaza tulipofika eneo ambalo nyumba ya yule mlokole ilikuwepo, nilipojaribu kuelekeza ungo utue haukutua badala yake ulielekea upande wa
kushoto. Kukufafanulia hapo ni kwamba, inapotokea wachawi wanakwenda sehemu kwa kutumia ndege ya kichawi (ungo) halafu kila wakitaka utue unagoma elewa hapo
si mahali salama. Kwa kuwa tulipania sana kumkomesha yule mlokole, licha ya ungo kugoma kutua tuliulazimisha na kuurejesha hadi juu ya anga ilipokuwepo nyumba ya mlokole.
Tukiwa hapo, tuliulazimisha utue ndipo uligeuka juu chini na kutumwaga kando ya nyumba hiyo na chombo hicho kuangukia upande mwingine. Kilichosababisha ndege
yetu ianguke ni maombi yaliyokuwa yakifanywa na mlokole huyo usiku ule kwani yalikuwa makali sana. Tukiwa tumeanguka, yule mlokole alifungua mlango na
kutoka, akatuona wachawi wanne kasoro yule ndugu yake aliyekuwa kaangukia upande mwingine.
Kama ilivyo kawaida ya walokole wanapoona hali ya hatari huamua kuomba, alianza kukemea huku akilitaja jina la Bwana Yesu. Kabla hajaanza maombi mimi na
wenzangu tulikuwa tumegandiana lakini kadiri alivyokuwa akiomba tulijinasua na kuwa huru na kuweza kusimama. Tukiwa tumesimama, yule mlokole aliendelea
kukemea kwa jina la Yesu ndipo tulipata nguvu tukafanikiwa kutoweka kila mmoja kwa njia yake. Mimi nilikwenda nyumbani na kufikia kitandani, nikajilaza na
kuanza kutafakari lile tukio, sikuchukua muda mrefu nilipitiwa na usingizi hadi nilipozinduka asubuhi.
Kutokana na uchovu wa safari ya kichawi na mkasa uliotukuta usiku, siku hiyo niliamua kukaa nyumbani bila kwenda kokote. Baada ya kunawa uso nilitoa kiti na
kwenda kukaa chini ya mti wenye kivuli uliokuwa kando ya nyumba yangu. Nikiwa hapo nilisikia kelele za watu wakilia kutoka nyumba jirani, nikawa najiuliza
kulikuwa na nini bila kupata majibu. Wakati kelele hizo zinaendelea, nilimuona yule dada mpangaji wangu ambaye hakuwa na mke akirejea kutoka zilikokuwa zikisikika kelele hizo.
Alipofika tulisalimiana na kumwuliza kwa nini hakwenda kazini, akaniambia aliamua kumpumzika kwani alichoka sana. Kwa kuwa dada huyo alitokea upande ambao
vilio vilisikika nilimwuliza vilikuwa vya nini akaniambia hakuelewa chochote kisha akaingia ndani. Nikiwa najiuliza kilichokuwa kikiwaliza watu hao, mara
nilimuona jamaa mmoja ambaye alikuwa mwanajeshi akija huku mkononi kashika fimbo nne kubwa.
Sikuwa na shaka naye kwani nilijua alikuwa akipita kuelekea mtaa wa nyuma lakini jambo la kushangaza aliponifikia alianza kunitandika mwilini. Nilipomwuliza
sababu za kunilamba bakora, akaniambia mimi na vijana wengine tulimwibia antena yake hivyo tutamtambua.
Licha ya kumwambia ilitakiwa afanye uchunguzi ambao ungemwezesha kumpata mwizi wa antena yake kisha kumpeleka polisi, hakunielewa. Mwanajeshi huyo aliyekuwa
na cheo kazini kwake alinijibu kwamba yeye mwenyewe alikuwa polisi, hivyo lazima tungerudisha antena yake. Kwa kweli kitendo hicho kilinikera sana ndipo nilimwambia atanitambua kwa sababu aliingia sehemu isiyoingilika lakini mwanajeshi huyo alinibeza na kuendelea kunitandika. “Eti nimeingia sehemu isiyoingilika, yaani kidudu mtu kama wewe unaweza kuniambia maneno hayo, lazima utasema antena yangu mmeiuza wapi!” yule mwanajeshi aliniambia huku akiendelea kunicharaza bakora.
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni