DHAMANA (18)
Zephiline F Ezekiel
6 min read
Mwandishi: Hassan O Mambosasa
SEHEMU YA KUMI NA NANE
TULIPOISHIA...
TULIPOISHIA...
Ilipotimia majira manne ya mwaka katika kijiji hicho walihamia familia ya wasafiri kutoka mbali ambao walipenda sana kuweka makazi katika kijiji hicho na walipewa ukaribisho mkubwa kutoka kwa kiongozi wa kijiji hicho, familia hiyo nayo ilikuwa gumzo kijiji hapo kutokana na kuwa na kijana aliyekuwa na mvuto wa ajabu na usafi uliopitiliza kuliko hata vijana wengine wa kijiji hicho.
KUNA MATANGAZO YANATOKEA YAGUSE ILI KUNIPA NGUVU YA KUENDELEA
KAMA UNASOMA SIMULIZI HII NJE YA CnZ Media APP INSTALL ILI USIPITWE NA MIENDELEZO
SASA TUENDELEE...
Kijana huyo alijulikana kama Mufedi ambaye alikuwa na asili mchanganyiko iliyomfanya awe na nywele za kipekee sana ambazo hata angeishi bila chanuo basi zingeonekana ni nzuri sana na zipo kama zimechanwa. Mufedi alikuwa ni mtu wa kukaa na vijana wenzie wa rika lake hadi wakamzoea kutokana na ucheshi wake alionao ambao uliwafanya vijana wenzake wafurahi kila kukicha, ndani ya muda mfupu tu katika kijiji hicho tayari Mufedi alikuwa yupo midomoni mwa mabinti wa kijiji hicho kama ilivyo kwa Giguna alivyokuwa yupo katika midomo ya wavulana wa kijiji hicho.
Ilifika kipindi hata wasichana wa kijiji hicho wakawa wanakuja nyumbani kwao Mufedi na kumsaidia mama yake Mufedi kazi mbalimbali wakiwa na lengo tu la kuiona sura ya Mufedi jinsi ilivyokuwa ni nzuri na yenye kuvutia, baadhi ya wasichana waliokuja hapo nyumbani kwao Mufedi na kumuona akiwa sehemu kubwa ya kifuani mwake haijastiriwa walikiri kwamba alikuwa ni mvulana mwenye uzuri wa ajabu. Maneno ya chini kwa chini juu ya uzuri wa ajabu alionao kijana huyo yalienea hapo kijijini kama ilivyokuwa akisemwa Giguna na wavulana wa kijiji hicho, muda wote huo si Giguna wala Mufedi aliyewahi kumuona mwenzake kwa macho na kila mmoja alisikia sifa za mwenzake kupitia marafiki zake.
Siku moja ambayo ndiyo ilikuwa chanzo cha kuanzishwa kitu ambacho hakikutarajiwa kuanzishwa ndiyo siku ambayo wawili hawa kwa mara ya kwanza walionana, siku hiyo Mufedi alikuwa akiongea na marafiki zake vipenzi walioitwa Nikeze na Nunele. Giguna siku hiyo aliagizwa kupeleka mzigo nyumbani kwao Mufedi baada ya wazazi wake na mufedi kufanya biashara ya kubadilisha mali kwa mali kwani kipindi hicho bado fedha zilikuwa hazijaanza kutumika.
Ilikuwa ni muda mrefu Giguna alikuwa hajaonekana kutokana na kuwasaidia sana wazazi wake na bibi yake kazi za hapo nyumbani kwao, eneo alilopita ndiyo walikuwa wamekaa Mufedi, Nikeze na Nunele wakipiga soga na kuchia vicheko. Giguna alipokaribia Nikeze alimuita lakini hakuitikiwa ndipo Nunele alipomuita akasimama kutokana na heshima aliyokuwa nayo, Nunele na Giguna walikuwa ni ndugu wa damu na Nunele ndiyo mkubwa kwa Giguna. Hivyo Giguna alijongea hadi walipo akiwa amejitwisha furushi kichwani lililokuwa na mzigo aliotumwa kuupeleka, hapo ndipo kwa mara ya kwanza Giguna alimuona Mufedi na Mufedi alimuona Giguna na wakaongea kwa lugha ya macho na nyoyo pasipo wengine kutambua wanachozungumza.
"Giguna u waitwa wanyamaza si vizuri hivyo" Nunele alimuambia Giguna baada ya kunyamazia salamu ya Nikeze.
"Kaka nataka wahi nilipotumwa niweze wahi rejea" Giguna aliongea kwa sauti nyororo huku akimtazama Mufedi kwa jicho la kuibia.
"hapana dada sifanye hivyo muache wslau akusindikize kidogo tu hutachelewa kurudi" Nunele alimuambia kisha akampa ishara Nukeze amfuate Giguna, Nukeze hakufanya ajizi alimfuata Giguna na taratibu akaanza kwenda huku akiongea kwa maneno ambayo hayakusikiwa na yoyote zaidi yao wenyewe. Huo ndiyo mwanzo uliozua safari nyingine kabisa isiyosafiriwa kwa umbali mrefu, ilikuwa kama ukurasa ila haukuwa na karatasi. Siku na siku zilisogea na hatimaye dalili za dhahiri kabisa zikachipuka na kuonesha kila mmoja alikuwa akimuhitaji mwenzake, katika msogezo huo wa siku ndipo ikafika siku ambayo haitasahaulika kwenye ukurasa mpya wa upendo ulioanza kuchipuka katika mioyo yao" Mzee Mahmud aliweka kituo hapo katika kusimulia na kumuangalia Mzee Buruhan ambaye alionekana kuwa na hamu ya kuendelea kuisikiliza hicho kisa anachosimuliwa.
"Aaaah! Mzee mwenzangu wakatisha pasipo stahiki kukatishwa" Mzee Buruhan alimlaumu mzee Mahmud kwa kukatishiwa uhondo mwanana uliokuwa unapita kwenye masikio yake na kujenga taswira kwenye ubongo wake kama vile alikuwa anaangalia sinema ya kile anachosimuliwa na kusikiliza simulizi tu.
"Weka mafuta kwanza tuendelee na safari huoni kikombe kitupu hicho na birika lina mafuta tele ya kunifanya niendelee kutoa burudani" Mzee Mahmud alimuambia mzee Buruhan huku akimpa kikombe chake cha kahawa ili aongezewe kahawa aweze kuendelea kusimulia.
"simulia walau kidogo basi mzee mwenzangu huku nakuongezea kahawa" Mzee Buruhan alimuambia Mzee Mahmud akiwa amenyanyua birika la kahawa ili amuongezee kahawa.
"Basi bwana siku hiyo si wakaombana namba za simu ili waweze kuongea vizuri maana ya vijana unayajua" Mzee Mahmud aliamua kusimulia kitu kingine kabisa tofauti kabisa na kufanya Mzee Buruhan amtazame kwa mshangao.
"Ushaanza visa vyako tayari mzee mwenzangu, sasa umesema zamani na hizo namba za simu zimeingia vipi" Mzee Buruhan alimuambia Mzee Mahmud huku akianza kucheka.
"Sasa si wewe unalazimisha gari kwenda wakati mafuta yamekwisha, umeona wapi likatembea huku likisubiri mafuta" Mzee Mahmud aliongea huku akicheka kidogo na kusababisha Mzee Buruhan acheke kwa nguvu kutokana na vituko vya mzee mwenzake.
"Yaani mzee mwenzangu hubadiliki kabisa tangu upo kijana tabia ni zile zile tu" Mzee Buruhan aliongea huku akimtilia kahawa mwenzake.
"ewaaa! Mambo si hayo sasa twende kazi" Mzee Mahmud aliongea huku kisha akinywa kahawa kidogo.
"sasa endelea mzee mwenzangu usikatishe habari" Mzee Buruhan alimuambia.
"Siku hiyo ilikuwa ni majira ya jioni baads ya jua kuzama, Giguna alicheleewa kuchota maji mtoni na ikambidi akimbie mara moja mtoni ili walau apate maji ya kuoga kwa usiku wa siku hiyo kwani ilikuwa ni kawaida kulala akiwa nadhifu usiku. Alipofika mtoni ndipo akakutana na Mufedi akiwa na kabeba vazi lake la juu lilionekana kuloa na alibakiwa na shuka kubwa aliyojifunga kiunoni iliyofika juu ya kitovu, kitendo cha wao kuonana tu walibaki wakitazamana tu kwa muda mrefu bila hata kusema chochote.
Walikuwa wapo kwenye njia nyembamba iliyochongwa baada ya miguu ya watu kukanyaga nyasi hizo kwa muda mrefu hatimaye baadhi zikakauka na kufanya njia, ilikuwa lazima mmoja ampishe mwenzake kwenye hiyo njia ili apite kwani haikuwa inatosha kupishana. Kwa ufinyu wa njia hiyo hakuna aliyefanya hivyo wote walisimama tu wakizamana tu hatimaye Mufedi akajikaza akamshika Giguna bega, walisogeleana karibu zaidi na muda huo hakuna yoyote aliyetambua nini wanafanya kwani walijikuta wamefikwa na hisia za ajabu kila mmoja kutokana upendo walionao kwa mwenzake.
Ule usemi aliousema nabii wa Mungu kwamba kwenye watu wawili wa jinsia tofauti basi watatu wao atakuwa ni ibilisi ndiyo ulijidhihirisha hapo na wakajikuta wameingia sehemu isiyotakiwa kuingilika, tangu siku hiyo ndiyo ukurasa haswa wa mapenzi ya dhati baina yao ukafunguliwa na mapenzi ya siri baina yao yakawa yanaendelea. Katika kipindi hicho ndipo Mufedi alipokuja kubaini kwamba Nukeze alikuwa akimtaka Giguna kwa muda mrefu lakini hakukubaliwa kabisa ndiyo maana hata siku ile alipomuita hakuitika kutokana na kuchoka usumbufu wake, mapenzi baina yao yaliendeshwa kwa usiri mkubwa na hawakumueleza yoyote hadi pale siku moja mmoja wa watu hapo kijijini alipokuja kubaini uhusiano huo.
Ginota rafiki kipenzi wa Giguna ndiye mtu aliyekuja kufahamu uhusiano huo baada ya kuwakuta wakitoka kuvuja ile amri sijui ya ngapi ya imani ya wenzetu hao, siku hiyo ilibidi Giguna amuambie ukweli juu ya uhusiano wao na akamuapiza kumtunzia hiyo siri pasipo kujua anamuaminisha nyoka. Giguna jambo ambalo hakuwa analijua ni kwamba Ginota ni mmoja kati ya wasichana waliokuwa wamezama kabisa katika kumpenda Mufesi lakini hakuwahi kumuambia Giguna kwasababu ana mahusiano na Nunele na laiti angemwambia ungekuwa ugomvi kati yao kwani Giguna asingekuwa tayari kuona kaka yake Nunele anasalitiwa.
Pia katika jambo ambalo Giguna hakulitambua ni kwamba Nukeze alikuwa akimtumia sana Ginota katika kumshawishi Giguna amkubali lakini jitihada hizo ziligonga mwamba kwani macho ya Giguna hayukutamani hivyo moyo wake haukuhitaji, kumbuka macho yasipotamani moyo hauwezi kuhitaji. Ginota hakuweza kustahimili kuona rafiki yake kampata mwanaume aliyekuwa anagombewa hapo kijijini na wasichana wote kama vile ni lulu yenye thamani, Ginota aliifikisha habari hiyo kwa mpenzi wake Nunele na kupelekea taarifa hiyo ifike kwa Nukeze.
Hapo ndipo vita mpya ya mapenzi ilipoanza chini kwa chini, Nunele na Nukele walikuwa wanacheka na Mufedi kwa jino pembe tu lakini walikuwa wakipanga kumuua Mufedi kila muda lakini ilishindikana na kila walipoenda kwa waganga ili wamuue kazi yao ilikataliwa na mwisho wake wakafanya kitu ambacho kilimuumiza sana Mufedi na ikawa ndiyo mwisho wa mapenzi ya Giguna na Mufedi. Waliamua kwenda kwa mganga wakafanya dawa ili ambayo walimtilia Giguna kwenye maji ambayo alikuwa anakunywa na alipoyanywa ndiyo ikawa mwanzo wa Giguna kumpenda Nukeze na Mufedi kukosa penzi lake baada ya kukataliwa wazi na kutolewa maneno yasiyofaa na Giguna.
Mufedi alidhani utani lakini alikuja kujua ni kweli baada ya kutaka penzi mtoni wakati Giguna alipoenda kuchota maji, Giguna alipiga kelele ya kuwa anavakwa na kusababisha watu wajae na Mufedi aliambulia kipigo nusura afe. Tangu siku hiyo Mufedi hakumgusa tena Giguna na alipopona tu aliondoka kijijini hapo akiiacha familia yake baada ya wanakijiji kutomuhitaji, huo ndiyo mwisho wa kwanza wa simulizi hii na muendelezo utaujua mzee mwenzangu tuombeane uzima tu" Mzee Maud aliishia hapo kuelezea simulizi hiyo.
"Mzee mwenzangu unajua ninamuonea huruma sana huyo kijana yaani naona kama nimefanyiwa mimi hivyo" Mzee Buruhan aliongea baada ya kuisikiliza hiyo simulizi kwa umakini.
"Fahari yetu waswahili kujaliwa sanaa inayokuteka akili zako ukaona kama tukio ni la kweli" Mzee Mahmud aliongea huku akimalizia kikombe cha kahawa.
"Yaani hata bao nimesahau kulicheza" Mzee Buruhan aliongea huku akitabasamu.
"Mzee mwenzangu huku leo silali naondoka maana narudi Mkinga leo leo nimekuja kukupa pole tu ujue sijakutupa rafiki yako wa toka utotoni" Mzee Mahmud alisema huku akinyanyuka kivivu.
"Haya mzee mwenzangu ngoja nikuitie kijana akutoe na usafiri hadi Makorora ukapate gari ya kurudi nyumbani" Mzee Buruhan alimuambia mzee Mahmud.
"Hasbuk mzee mwenzangu shukran sana muache kijana apumzike mimi nitatumia sehewa hapo tu niende chapuchapu haina haja ya gari" Mzee Mahmud aliongea huku akitembea na Mzee Buruhan akawa anamsindikiza, walitoka hadi nje ya nyumba eneo linaloegeshwa baiskeli nyingi za kukodisha.
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni