DHAMANA (4)
Zephiline F Ezekiel
6 min read
Mwandishi: Hassan O Mambosasa
SEHEMU YA NNE
TULIPOISHIA...
TULIPOISHIA...
Waliyaona magari mawili yaliyoungua yakiwa yapo jirani na dimbwi kubwa la damu lililokuwa limeanza kukauka tayari. Dimbwi hilo pamoja na magari yaliyoungua yalikuwa yamezungushiwa utepe ili kuzuia watu wasiingie.
KUNA MATANGAZO YANATOKEA YAGUSE ILI KUNIPA NGUVU YA KUENDELEA
KAMA UNASOMA SIMULIZI HII NJE YA CnZ Media APP INSTALL ILI USIPITWE NA MIENDELEZO
SASA TUENDELEE...
Vijana hawa walijikuta wakitaka kuingia katika eneo liloozungushiwa utepe lakini askari hao waliwazuia na kuwaelewesha wapo kazini lakini vijana hawa hawakutaka kabisa tena mmoja wao ndiyo alionekana kutaka kufanya fujo na mwisho wake wote wakawekwa chini ya ulinzi. Walipelekwa hadi upande wenye askari wengi wakawekwa chini ya uangalizi wa askari na mmoja kati ya wale vijana alikuwa muda wote alikuwa akilia huku akiiangalia gari ya abiria ambayo ilikuwa imebeba wale wafanyakazi kutoka idara moja ya makao makuu ya kampuni ya Extoplus.
"Hebu nyamaza mtoto wa kiume wewe unalialia nini" Mmoja wa maaskari ambao alikuwa akiwangalia hawa vijana wa kampuni ya Extoplus alimwambia yule kijana aliyekuwa analia.
"mama yangu yupo ndani ya gari lililoungua sasa wewe ulitaka nicheke" Kijana alimjia juu yule askari aliyekuwa anamwambia hivyo.
"kijana una uhakika gani kama gari lile ndiyo mama yako alikuwemo?" Yule askari aliuliza.
"uhakika ninao kibao cha namba za gari hiki hapa tumekiokota kule kwenye majani" Aliongea yule kijana kisha akampatia askari kibao chenye namba za usajili wa gari.
"tena askari gari yenyewe ni hii hapa niliwahi kupiga nayo picha" Kijana yule aliyeiweka picha ya gari la wafanyakazi kwenye simu yake akiwa amepiga nalo picha naye aliongea huku akimuonesha askari picha aliyoipiga na ile gari yenye namba sawa na namba zilizokuwa kibao cha namba za usajili walichokiota. Yule askari aliziangalia kwa umakini kisha akaangalia muundo wa mabaki ya gari la abiria lililoungua halafu akawaambia, "hebu nifuateni mara moja"
Yule askari aliondoka mara moja akaelekea mahali pengine kwenye kundi kubwa la maaskari waliovaa kiraia na waliovaa sare za polisi, alimfuata askari mmoja aliyevaa kiraia akatoa heshima kisha akamuuma sikio huku akiwaonesha kidole wale vijana. Yule askari aliyevaa kiraia aliwasogelea wale vijana akiwa na yule askari aliyewaleta kisha akawaashiria wamfuate, alielekea kwenye gari ya polisi aina ya toyota land cruiser yenye viti katika sehemu ya kuwekea mizigo kisha akapanda akawamuru nao wapande.
"naitwa ASP John Faustin natokea kito cha polisi Mkwakwani, wenzangu mnaitwa nani majina yenu" Asp John alijitambulisha kwa wale vijana huku akionesha kitambulisho chake cha kazi kisha akawauliza majina yao, wale vijana walitaja majina yao wote.
"ok James naomba naomba uache kulia unieleze kila kitu" Asp John alimuambia yule kijana aliyekuwa analia baada ya kuona gari lile lililoungua.
"afande sisi wote ni wafanyakazi wa kampuni ya Extoplus na tulikuwa tupo Duga kwenye sherehe za uzinduzi wa nyumba mpya za kupangishwa za kampuni yetu, tulikuwa tukitarajia ujio wa staff wa idara ya uhasibu kuiwakilisha ofisi ya makao makuu tangu asubuhi lakini hadi inafika saa sita hawakuwa wamefika. Sisi tulitumwa kuwafuatilia na tulifuatilia ndipo tulipokuta hali hii tena tulianza kuanza kuona kibao cha namba za usajili za gari ya kampuni, na tuliifananisha na picha ya gari la kampuni tukaona linafanana kila kitu" James aliongea huku akiwa na uchungu.
Asp John aliyanakili maelezo ya James kisha akajiandaa kuuliza swali jingine lakini king'ora cha gari la zima moto kilimkatisha na akajikuta akiangalia lilipo gari la zima moto. Wale vijana nao waliliona lile gari la zimamoto likipita pembezoni mwa eneo la tukio kwa tabu kisha likaingia barabarani kisha likaingia barabarani likawa linaelekea Duga Maforoni kwa mwendo wa kasi sana huku milio ya ving'ora vyake ikiwa imetawala njia nzima. Asp John alipoona hali hiyo alihisi kuna jambo na akawa anataka kujua kuna nini kilichotokea, alinyanyua simu ya upepo akaongea kwa muda kisha akatulia akasikiliza upande wa pili na akajikuta amegwaya.
"nyumba za kampuni yenu zilizokuwa zinazinduliwa zote zimeungua kwa moto wa hitilafu ya umeme" Asp John aliwaambia wale vijana.
"eti nini?" James alisema kwa mshangao.
****
"Ndiyo maana yake hizo nyumba mlizotakiwa kuzizindua leo zote zinateketea kwa moto" Asp John alimuambia James ambaye alionekana kutoamini kwa alichomuambia, vijana wote wa kampuni ya Extoplus walichoka kuliko walivyochoka baada ya kusikia mali ya kampuni ikiwa inaungua. Taarifa hizo zilikuwa ni kama kupigilia msumari wa moto kwenye kidonda ambacho hakijapona kwa James, kilio chake kilichoanza kunyauka usoni mwake mithili ya mche usiopata matunzo kilianza kuchipua tena kwa taratibu mithili ya mti wa muhogo unavyoota majani baada ya kuwa umechimbiwa chini kwa muda wa siku kadhaa.
Kilio hicho kilikolea baada muda wa dakika mbili tu mithili ya garimoshi la makaa ya mawe lililosaza mabeleshi kadhaa ya makaa ya mawe, Asp John ilimbidi asitishe kufanya mahojiana na akawa ana kazi ya kumbembeleza James akishirikiana na wenzake ili waendelee na mahojiano. Ilikuwa ni kazi ngumu sana kumtuliza James ambaye alionekana kuna jambo jingine linamuuma ambalo halikujulikana kwa wenzake wala kwa Asp John.
"nina mkosi gani mimi?" James aliongea akiwa yupo katikati ya kilio chake.
"ya nini useme hivyo wakati huna dalili ya kuonekana na mkosi katika maisha yako" Asp John alimfariji.
"we afande hujui hulisemalo na mimi ninajua nilisemalo" James aliongea huku akipangusa michirizi ya machozi iliyokuwa inatiririka mashavuni mwake.
"James unaongea nini mbona hatukuelewi?" Kijana mmojawapo aliyefika na James aliyefika eneo hilo alimuuliza akionekana kutatizwa sana na kauli zake.
"Gasper yaani ungejua nilichokutana nacho juzi" James alisema huku akimtazama yule kijana aliyesema hawamwelewi.
"hebu wengine nyamazeni kwanza, James hebu eleza vizuri nikuelewe" Asp John aliongea akiwa amemahika bega James.
"Afande juzi nikiwa natoka kazini niliamua kuelekea Makorora jirani na kituo kikubwa cha mabasi yaendayo mikoani, niliamua kwenda kwa mguu kutokana na eneo lenyewe kutokuwa mbali na ofisi yetu. Wakati navuka reli zilizopo njiani kuelekea kwenye kituo cha basi nilikutana na mwanamke wa kiarabu ambaye alinichangamkia kwa kunisalimia ingawa hatufahamiani. Yule msichana aliniambia kuwa anafikiri kuwa mimi nimepotea njia na alitaka anielekeze njia iliyosahihi kuifuata, nilimwambia mbona sikuelewi na yeye akaniambia hivi punde utanielewa wala usijali.
Aliniambia nyenzo yangu kuu ya maisha imegharamiwa kwa kitu kilicholetwa baada ya kuondoka maisha ya mwingine, mzazi wako wa kiume anatambua hili ingawa analificha ndiyo maana ana maslahi mazuri kutokana na kusitiri kisichostahiki kusitiriwa. Sasa basi tambua na wewe unafuata njia ambayo baba yako ndiyo maana nikakuambia umepotea njia sasa basi unatakiwa ubadili muelekeo uende njia nyingine la si hivyo utakuja kuzama shimo moja ukiteketea ambalo wazazi wako watazama wakitekea siku ya sherehe ya nje ya mji.
Kusema kweli nilimuona yule msichana ni kachangayikiwa na nilibaki nikiwa nashindwa hata kumuuliza swali, msichana yule nilimuona akivuka barabara kisha akawa anafuata uelekeo wa reli zinazopita pembeni ya shule ya sekondari ya Usagara . Nilibaki namtazama hadi pale lilipopita basi kubwa la abiria ambalo llinikinga nisimuone na basi hilo lilipopita sikumuona tena yule msichana na sikuelewa ameondoka vipi. Nilibaki nilishangaa kwa muda wa dakika kadhaa hadi pale nilipohisi kushikwa bega na nilipogeuka nilimuona mwanamke ambaye kiumri anafaa kunizaa akiniuliza nina tatizo gani, nilipomjibu sina akaniuliza kwanini nilikuwa naongea mwenyewe kwa muda mrefu.
Nikamwambia nilikuwa naongea na mtu ambaye tayari ameshavuka barabara ameelekea njia iliyopo relini inayoelekea katika shule ya Usagara, nilpomuambia maneno hayo aliniambia nina matatizo maana yeye alikuwa akinitazama kwa muda mrefu na ameniona nikiongea peke yangu. Niliona huyo mwanamke ananichanganya tu kama alivyonichanganya yule msichana kwa kauli zake" James alieleza akiwa amepunguza kulia kwa muda na alipomaliza aliendelea kulia, maelezo yake yaliwashangaza sana wwnzake hadi ingawa hayakuwa wazi kwao kuelewa kinamchomliza James. Imaniza kishirikina pamoja na uchawi ndiyo uliyotawala maelezo ya James, wenzake wote walimshangaa sana.
"James unajua maelezo yako hayana tija yoyote katika ushahidi wa kiserikali kwani hakuna kipengele chochote cha sheria za serikali inayosema uchawi unahusika katika ushahidi pia katika maelezo yako hayajaonsha kiini cha wewe kulia uliposikia kuhusu kuungua kwa hizo nyumba" Asp John aliongea kwa upole huku akimtazama James usoni.
"Afande nimeambiwa wazazi wataketea katika shimo moja siku ya sherehe ya nje ya mji, huoni kama siku ya sherehe yenyewe ndiyo leo na mzazi wangu mmoja ameshateketea kwenye huu mlipuko wa basi la kampuni. Unafikiri moto wa pili atakuwa salama huko hebu jaribu kufikiri, tena ngoja niende hukohuko" James aliongea akionekana amechanganyikiwa kabisa kwa matukio yaliyomtokea hadi muda huo, aliamua kunyanyuka ili aondoke lakini Asp John akamzuia na kupelekea aanze kizazaa kutokana na fujo alizozianzisha James. Wenzake nao walijaribu kumtuliza lakini ilishindikana kabisa na hata walipomzuia alipiga makelele kama kichaa akiwasihi wamuachie.
"James hebu tulia kwanza huna uhakika wa kifo cha baba yako sasa fujo za nini?" Asp John alimuambia
"unasemaje wewe? Hivi ingekuwa ndiyo wewe unakutana na mtu anakupa habari za namna hii na siku himi uliyoambiwa unakutana na mabalaa kama hili utakuwa katika hali gani? Hebu fikiri ingekuwa ndiyo mzazi wako na si kufikiri imemtokea mwenzako" James aliendelea kulalamika huku akizidi kuleta utata kwa Asp John na wenzake waliombana ili asiondoke.
"subiri basi nimalize kukuhoji ndiyo uende James" Asp John alimsihi.
"hapa hahojiwi mtu ikiwa sijaenda Duga kumuona kama baba yangu yupo hai au la, ukitaka mahojiano nami basi uniache niende na nikitoka huko ndiyo unihoji" James alizidi kuwela utata.
"ok haina shida ngoja twende wote huko kwa gari....Kostebo ondoa gari usawa wa Duga Maforoni" Asp John alimuambia James kisha akapaza sauti kumuambia askari aliyekuwa amekaa kwenye usukani.
"afande" Aliitikia yule askari kidha akawasha gari na akaweka gia akaanza kulipitisha gari pembeni ya barabara kuvuka eneo lenye utepe halafu akaongeza mwendo kuelekea Duga maforoni.
****
Muda ambao ajali ya pili ya moto inatokea kwa upande mwingine mkoa wa Tanga katika sehemu ya jiji kulikuwa kuna kikao kizito cha viongozi waiuu wa kampuni ya Extoplus wakiongozwa na mwenyekiti mtendaji na mmiliki wa kampuni hiyo bwana Hamid Buruhan, kikao hicho kilikuwa kinajadili mambo mbalimbali kwa ajili ya kukuza kampuni hiyo.
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni