Vita vya Mapenzi (15)
Zephiline F Ezekiel
6 min read
Mtunzi: Maundu Mwingizi
SEHEMU YA KUMI NA TANO
TULIPOISHIA...
TULIPOISHIA...
Kabla hajafanya lolote akiwa anatweta huku akimuangalia Mchumba wake kwa hasira na hofu ghafla akasikia mlango ukigongwa kwa nguvu sana, akauangalia mlango kwa mashaka makubwa akijua sasa mambo yameshaharibika, akataka kwenda kuufungua lakini akahofia kumuacha Sharifa peke yake pale chini akihofia kua asije akapata tena upenyo wa kujirusha kwa mara ya pili, akaamua kumnyanyua na kusogea nae mpaka mlangoni..
KAMA UNASOMA SIMULIZI HII NJE YA APPLICATION YA CnZ Media INSTALL ILI USIPITWE NA MIENDELEZO
SASA TUENDELEE...
Akaufungua na kumruhusu aliegonga aingie, akaingia mwanaume mmoja akiwa ametaharuki vibaya, bila shaka alilishuhudia tukio lile
“Vipi?,” Suhail alimsaili jamaa yule alieingia ndani
“Vipi Kuhusu nini?” Jamaa yule alijibu kwa hasira zilizochanganywa na dharau kubwa, Suhail akajikuta ameishiwa cha kuongea kabla Yule jamaa hajaanza tena kuongea kwa kasi ya ajabu
“We ni mpumbavu sana pamoja na huyu mwenzio, hivi unataka kuniletea dhahama hapa, kama mna matatizo yenu kwanini msiende kuuania huko maporini?”
“Tafadhali bwana mkubwa usiniite mpumbavu, We unajua kilichotokea humu ndani mpaka unaanza kulalama tu? Acha dharau,” Suhail alibwata kwa ghadhabu
“We unanijua vizuri mimi?, mimi ndie Meneja wa Hotel hii sasa ulitaka nije kukupongeza kwa upuuzi mlioufanya humu ndani?..” Jamaa Yule akasita kidogo, akamgeukia Sharifa pale chini akiwa analia na kutoka damu eneo la kichwani, Akaenda mpaka pale Kitandani akachukua shati la Suhail akalichanaa kipande kisha akamwambia Suhail asogee haraka wasaidizane kumfunga kichwani ili kuzuia damu isizidi kutoka, Wakamfunga na kumuinua pale Sakafuni akiwa bado analia tu, Kisha Mwanaume Yule akamtupia swali
“Hivi wewe Sharifa una akili kweli wewe,” Aliuliza jamaa Yule aliejitambulisha kama meneja wa hotel, akamfanya Sharifa aache kulia kwa mshtuko wa kutajwa jina lake na mtu asiemfahamu “Hivi kwa nini unataka kujiua kwa upumbavu we mtoto? Nd’o kupenda sana ama nini? Baba yako ninasali nae kanisa moja, na ni Mzee wa kanisa anaehishimika sana sasa unataka kumtia aibu kubwa kiasi hiki, sasa mimi nampigia simu sasa hivi aje hapa” Kusikia vile Moyo wa Suihail ukapiga chogo chemba, akahamanika haswa, akajua sasa kua siri zote zitakua hadharani, akamsogelea jamaa Yule aliekua ameshatoa simu yake ya kiganjani kisha akamzuia
“Tafadhali kaka usifanye hivyo, nipo chini ya miguu yako kaka, naomba tu tusaidiane”
“Usaidiane na nani? Mimi sihitaji msaada wako wowote”
“Sawa kaka, naomba unisaidie mimi, tuyaongee tu usipige simu tafadhali”
“No, hivi we unadhani hili tukio ni dogo eeh? Mmeharibu mali pia mmejeruhiana humu ndani, je akifa huyu binti hapa?”
“Kaka usijali kuhusu kila kilichoharibika nitakulipa gharama zote kisha kitokeo cha hapa nampeleka hospitali..” Baada ya maelezo yale Suhail akamsogelea jamaa Yule kasha akamnong’oneza neno akijaribu kumshawishi kua atampoza pesa kidogo mbali ya hizo za matengenezo ya dirisha ili tu asitoe habari ile, Jamaa akalainika kusikia pesa akamsogelea Sharifa, akamshika mkono ili sasa watoke waanze safari ya kwenda hospitali
Ila akampa tahadhari Suhail kwamba akae na Sharifa wamalize tofauti zao ili Sharifa asije akafanya tena huo mchezo aliotaka kuufanya pale halafu ikaja kugundulika kua alishawahi kufanya hivyo pale Hotelini kitu ambacho kitamletea matatizo yeye kwa kulikali kimya jambo hilo zito, akaahidi angemueleza kila kitu Mzee Fungameza kawa wasingeyamaliza mambo hayo. Ikawa ni kitanzi kingine kwa Suhail, Baada ya majibizano ya muda kidogo Wakakubalina. Suhail akatoa pesa za kumuachia jamaa Yule kisha wakashuka ghorofani, wakaita Teksi na Safari ya kuelekea Hospitali ikaanza
*****
Majira ya saa mbili kasorobo usiku walikua kwakiendelea kupatiwa huduma nzuri tu pale Hospitali, hawakwenda katika Hospitali ya Kitete kwa kuhofia kuzalisha maswali na mwishowe huenda taratibu za kipolisi kuingia kati hivyo walikwenda mpaka Mtaa wa Ujiji katika Hospitali ya Dokta mkubwa sana anaekubalika pale mkoani, na kwakua pesa iliongea hivyo huduma ikaenda kwa kiwango kizuri, Suhail alipoona mambo si mabaya sana akamwambia Sharifa ampigie simu mama yake kumjuza kua amepatwa na matatizo, ikabidi amfundishe uongo wa harakaharaka kua aseme amekatwa na vioo vilivyodondoka kutoka katika gari moja kubwa lililopita karibu yake lakini hali yake si mbaya sana, Akafanya hivyo!
Muda mfupi baade Mama Sharifa alifika Hospitalini hapo na kujumuika na wanawe, Baada ya huduma kukamilika Wakaondoka huku wakitakiwa tena kesho yake kwenda kupata sindano, Sharifa na mama yake wakaenda kwao Chemchem na kumuacha Suhail nae akirejea kwa Rufita akiwa na mawazo na mchoko usiosemekana, Hakika alijutia!
*****
SUHAIL aliporejea nyumbani kwao akawapa habari ya kilichomkuta Sharifa lakini hakuwaeleza kama tukio lilivyokua, Alidanganya na kulifanya tukio lile kuonekana ni dogo na la kawaida tu kuliko uhalisia wake ulivyo. Na kutokana na Msongamano wa mawazo kichwani mwake hakutaka kabisa kupoteza muda wa kuendelea kukaa pale sebuleni japo familia ilionekana kua na hamu nae sana. akawaaga ili aende zake chumbani kulala, hiyo ilikua ni baada ya kupata chakula cha usiku. Lakini baba yake hakumpa nafasi hiyo akamzuia kwa ajili ya kuanzisha majadiliano kuhusu Suala la Ndoa yake, safari hii majadiliano hayakua makubwa sana kwakua ilikua ni kama marejeo tu kwani mada walikwisha ijadili, Wakamalizana japo si kwa muafaka wa asilimia miamoja. Wakaingia kulala.
SAA tisa usiku, hali ya ukimya ikiwa imetawala karibu maeneo mengi sana huku walio wengi wakiwa wanavuta shuka tu vitandani mwao, Suhail yeye alikua njiani akielekea Mbezi, Dar es Salaam. hakua na usafiri wowote zaidi ya Pete yake iliyomtoa pale Tabora kwa kasi ya ajabu baada ya kuiamrisha tu kufanya hivyo, Moja ya faida ya Pete ile ilianza kuonekana! Ndani ya dakika tano tu akawa amewasili Mbezi, Dar es Salaam huku wazazi wake wakijua yuko chumbani amelala
*****
“Shekhia mke wangu najua una uwezo wa kuona mbali, bila shaka umeona kila kilichojiri huko Tabora.. Hali ni mbaya Baba anataka kunitolea radhi kama sitaoa, Sharifa nae anataka kujiua...,” Suhail aliongea kwa hofu na kwa harakaharaka kama anaetaka kuwahi kuondoka
“Kwa hiyo mimi nifanyaje?” Shekhia aliekua ameegama katika kabati kubwa alijibu katika mtindo wa Swali huku akitikisa mguu wake kwa dharau, inaonekana ni kweli aliona kila kilichojiri kule Tabora
“Shekhia nakupenda mke wangu, ila ili mambo yaende sawa inabidi tu Nimuoe Sharifa”
“Nini wewe? Nyang’au wewe” Shekhia alijibu kwa hasira kisha akamnyooshea mkono wake wa kushoto uliokua umevikwa pete katika kidole chake cha kushoto, ilikua ni Pete yenye nguvu za kijini japo haina uwezo mkubwa kama ile aliyonayo Suhail, alipomuelekezea tu ile Pete ikatoa miale mikali ya moto, yenye uwezo wa kuangamiza na hata kuua, hakika alipatwa na hasira kiasi cha kudhamiria kumdhuru Suhail, lakini kutokana na nguvu alizonazo Suhail kupitia katika Pete yake kubwa ya ‘Khatam Budha’ ikashindikana kudhurika
“Unataka kufanya nini Shekhia? Yaani unataka kunidhuru mimi? We una akili kweli?” Suhail nae alimjia juu Shekhia kwa kitendo kile, ikawa sasa hakuna maelewano ndani kila mmoja alijiona anaweza kufanya lolote, ila kwakua Shekhia alitenda kosa kutaka kumdhuru mume wake ikabidi awe mpole kiasi na hapohapo Suhail akautumia mwanya huo kumshinikiza Shekhia kukubali Suala la yeye kumuoa Sharifa lakini hapo pakawa pachungu haswa, ikawachukua muda mrefu sana kulijadili suala hilo huku Suhail akitumia maneno aliyotolewa na baba yake kua kama fimbo wakati Shekhia nae akimkumbusha Suhail kua makubaliano yao siku walipofunga ndoa ni kwamba yeye atakua ndie Mke pekee wa Suhail. Patamu hapo!
“Sasa mimi siwezi kukosa radhi ya mzazi wangu kwa ajili yako, sawa nakupenda ila na wazazi wangu nawaheshimu sana, siwezi kukhalif amri zao, nitakosa Baraka na radhi zao.. Maisha yangu yote yataharibika hapa duniani na kesho Mbinguni”
“Hayo yote haukuona umuhimu wake tangu mwanzo ulipokubali kuoa kwa masharti mbele ya Mzee Sufiani? Na kwa taarifa yako nikimueleza Baba huu ujinga wako atakuangamiza hata kabla jua halijachomoza”
“Najua hilo mke wangu nd’o maana nataka tuyaongee mimi na wewe kwakua tunapendana, sasa Baba yako akiniangamiza mimi hata wewe utakua umepoteza mume, si ndio?”
“Yeah Kuliko kuchangia mwanaume ni bora tu nikupoteze” Majadiliano yalikua makubwa sana mpaka hatimae wakaanza kufikia maamuzi, Shekhia akakubali Suhail aoe lakini kwa sharti moja tu kwamba asikutane kimwili kamwe na Sharifa, hiyo nayo ikawa na mada mpya
“Sasa itawezekanaje hiyo? Hakuna Ndoa bila Tendo, hauoni kua ni kujiletea matatizo makubwa zaidi,” alimaka Suhail
“Itawezekana tu kwakua tayari ameshajua kua wewe ni Mbovu hivyo hatokua tena na sababu ya kukusumbua, zaidi ya hapo sitokua na muafaka na wewe kwa jambo lolote tena, na ukae ukijua kua kama una mpango wa kufanya tofauti hakika jihesabu wewe ni Mfu mtarajiwa” Alhitimisha Shekhia kwa mkwara mzito. Suhail akabaki njia panda ila akawa hana budi kuafikiana na Shekhia akiamini japo kwa hatua hiyo ya awali, aliamini kwamba huo ni mwanzo mzuri na Mengine yatajipa ndani kwa ndani!
Kwa kasi ileile Suhail akarejea Tabora, Usiku uleule
*****
Mpaka saa tatu asubuhi familia nzima ya Mzee Kusekwa walikwishaamka isipokua Suhail tu aliekua akikoroma kitandani kwake. Shughuli za usafi na maandalizi ya kifungua kinywa ilikua ikiendelea, na hata ilipokamilika waliendelea kumsubiria Suhail aamke ndipo waweze kupata kifungua kinywa hicho kwa pamoj, Hakika Suhail Alichoka sana na Pilika za mchana na usiku kucha, hakuamka mpaka alipoamshwa!
Alipoamka kitu cha kwanza alichokifanya ni kumpigia simu Sharifa lakini simu haikupatikana, akatoka chumbani na kwenda bafuni kujiswafi mwili kisha akarejea kujumuika na familia kupata kifungua kinywa huku wakipiga stori za hapa na pale,
“Jamani mimi nataka nitoke kidogo,” Suhail aliwaaga wazazi wake
“Unaenda wapi?,” Mzee Kusekwa nae alisaili haraka
“Naenda mara moja kwa jamaa zangu kule Minazi Mikinda, sijaonana nao tangu nimekuja” majibu ya Suhail yalikua ni ‘Funika kombe, mwanaharamu apite’ lakini lengo lake lilikua ni kwenda Hospitali kumuwahi Sharifa kwakua alijua kua angekwenda pale kwa ajili ya kupata sindano
“Ooh, ngoja basi tufuatane tutakwenda kuachania mbele maana name naenda kwa Bwana Fungameza” Baada ya maelezo hayo Mzee Kusekwa aliinuka na kuingia chumbani kwake kujiandaa ili waweze kutoka
*****
Mkabala na Hospital kubwa ya Dr Nyango Bango kubwa lililosomeka ‘KWA MZEE ANDOGA’, Lilikua likiunadi mgahawa mkubwa wa kupatia chakula pamoja na vinywaji, watu wengi hujumuika maeneo yale kupata chakula safi.
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni