HAMUNAPTRA - MJI ULIOPOTEA (7)
Zephiline F Ezekiel
6 min read
Mtunzi: Richard Mwambe
SEHEMU YA SABA
TULIPOISHIA...
TULIPOISHIA...
“Amata, nakualika katika hili, ufuatane nami tukakamilishe kazi hii, tuondoe laana katika jamii na baraka za Klakos zitumwagikie kama umande wa asubuhi” Seidon alimtupia ombi Amata kwa lugha ya kushawishi.
TUENDELEE...
“Hamna shaka, ombi lako limefika panapostahili, bega kwa bega tutakamilisha hilo, mimi nitakusindikiza kwa jua na mvua, kwa baridi na joto, kwa shida na raha,” walipeana mikono ya ushindi, kisha Amata akamuacha Seidon aendelee kupumzika.
Baada ya majua 14
Mazoezi makali yalikuwa yakiendelea kati ya Amata na Seidon katika misitu ya Progos, mazoezi ya kutumia panga, mishale yote yalichukua nafasi ili kumuweka fiti Seidon.
Walipokuwa wameketi wakiota moto, Amata akamwambia,
“Naona sasa tupo vizuri, twaweza kwenda” Amata alimwambia Seidon
“Yah! Kumbuka tunaanzia kwa Wahamsud ambao ndiyo sasa wanalo fuvu hilo” Seidon alimkumbusha Amata.
“Nakumbuka, Wahamsud tunawavamia usiku wa manane kupitia milima ya Ararat, tukiteremka ule mlima kwa chini utaona kijiji chao pale wewe utaenda kuliichukua hilo fuvu na mimi nitakulinda, inabidi tuhakikishe usiku uohuo tuwe tumeikamilisha kazi hiyo, maana wakitukamata tutakuwa nyama ya mbwa” Amata alimueleza Seidon huku wakiwa njiani kurudi kijijini.
Mchana walijiweka sawa na jioni yake kuondoka kijijini kwao kwa dhumuni la kukikabili kijiji cha Wahamsud. Amata aliufutika upanga wake vizuri, aliiweka sawa pete yake ya ajabu aliyoipata kwa bibi kizee wa Msitu wa Solondo, kwa ujumla Amata alikamilika. Seidon, mpiga mbio, alikuwa tayari juu ya farasi wake, akiwa na upanga wa Vernad kiunoni na sasa alidhamilia kuupata upanga wa Orion iwe isiwe.
Safari ikaanza wawili hawa wakaingia safarini, safari ilikuwa ngumu sana, kwa maana ilikuwa ni kupanda na kushuka milima yenye mchanga mwingi, mara kwa mara walikutana na dhoruba za jangwani zilizowapa taabu lakini walivumilia, safari yote hiyo hakuna hata aliyeongea na mwenzake kila mmoja alikuwa akiitafakari safari hiyo ngumu.
Jua lilipokuwa maghalibi waliukabiri mlima mkubwa uliojaa mawe na miiba, kwa tabu walipanda mlima huo wakiwa juu ya farasi wao na baada ya muda tu walifanikiwa kufika kwenye tambarare iliyojazwa na uoto wa mkakati na mimea mingine yenye kustahimili shida, kando ya jiwe kubwa kulikuwa na mti wa mtende uliomea vizuri.
“Seidon, tuketi hapa, tusubiri muda ufike ili tuweze kuwashukia Wahamsud,” Amata alimwambia Seidon.
“Kwani haiwezekani kuwavamia sasa?” aliuliza
“Hapana, Wahamsud wanategemea nguvu ya nyota inayoitwa LEO, inabidi tusubiri hapa kwa masaa kama mawili, nyota ile ikifika maghalibi tayari hawana nguvu, tutafanya kazi yetu kwa urahisi ambao hautautegemea, na tukishalipata fuvu ni safari ya moja kwa moja Hamunaptra kupitia upande wa kusini kandokando ya bahari nyekundu mapaka kaskazini mwa Kushi, tusipite kwa yule mchawi Sherhazad atatusumbua sana kwa kuwa bado ana chuki na wewe.”
Waliketi chini ya mtende huku Amata ga Imba akiendele kuburudika na kibuyu chake cha pombe.
“Amata, huoni kwamba pombe unayokunywa inaweza kuharibu mipango yetu?” Seidon aliuliza baada ya kuchoka kuvumilia kwa kuwa wao kwao pombe ni mwiko kabisa kwani wamelelewa na falsafa inayosema pombe hulowesha roho.
“Hapana, hii inasaidia sana kwa kuwa kuna baadhi ya nguvu za kishetani ambao hazitaki pombe, sasa mimi na wewe hatujui tukienda huko tunaenda kukutana na nini,” lilikuwa jibu la Amata ga Imba.
Ilipotimu usiku wa manane, sauti ya Mbweha wa jangwani ikasikika, Amatagaimba aliinuka kutoka pale chini ya mtende, mbala mwezi ilikuwa iking’aa sana, Amata alisimama na kuangaza macho yake huku na kule, akamwamsha Seidon.
“Kijana, amka, saa imefika inapaswa tutende lile tulilolikusudia,” Amatagaimba alimuamsha Seidon. Seidon alisimama na kujinyoosha, akachukua gudulia lake la maji na kugugumia mafunda kadhaa, kisha akalitua na kulirudisha kiunoni.
“Na hii mbalamwezi huoni kama itatuharibia?” Seidon aliuliza.
“Usiwe na shaka, Seidon, nitaifunika kwa nguvu za ajabu, na wingu litasimama juu yake mpaka tutakapomaliza kazi yetu,” Amatagaimba, alimtazama farasi wake na kumshikashika kichwani, “Seidon, tunaingia katika mji bila farasi, kwa mwendo wa miguu yetu,” Amata alizungumza huku akiweka podo lake mgongoni na kuukamata vyema uta wake, kwa mwendo wa taratibu walianza kuushuka mlima ule huku Seidon akishuhudia wingu zito likianza kuifunika ile mbalamwezi taratibu na kutengeneza kivuli kizito. Haikuwachukua muda walifika katika kilima kingine kidogo tu, walipokwea mpaka juu waliweza kuona mji wa Wahamsud ukiwa kimya ni mioto tu ya hapa na pale iliyokuwa ikiendelea kuwaka. Amata ga Imba alitulia akiangalia kwenye zile nyumba za Wahamsud, Seidon hakuthubutu kumuuliza anaangalia nini bali aliendelea kumtazama.
“Seidon, hapa kazi ni ndogo tu, unaiona nyumba ileeeeeeee,” Amata alimuonesha Seidon nyumba iliyopo katikati ya zingine, iliyokuwa ikiwaka taa hafifu, “Pale ndipo penye fuvu la Cleopas, ulinzi uliopo pale ni mkali sana usione pametulia, sasa jiweke tayari tunaenda na lolote linaweza kutokea, mimi nitalinda nje wakati wewe utaingia ndani kulichukua hilo fuvu,” Amata alitoa maelekezo na kisha akauchukiua uta wake na kuuweka sawa, akachomoa mshale na kuutunga vyema kisha akauvuta kwa nguvu sote, “Seidon, washa moto hapo mbele, nataka niwapelekee kizaizai,” Seidon akawasha moto kwenye ncha yam shale wa Amatagaimba iliyokuwa imefungwa kwa kitambaa kizito chenye mafuta mazito ya mimea, kiliposhika moto sawia, Amata aliutazma mshale wake ulikuwa tayari kwa shambulizi, “Nakuagiza, katika jina la Amatagaimba, shujaa wa msitu wa Solondo, alieukonga moyo wa Baghoza na kuushusha utawala wa Kerume kwa mshale huu, mshale wa urithi wa mzee Nkhunulaindo, uende ukaanzishe kile tunachokikusudia,” akaunuia mshale wake aliokuwa amekwishauvuta kwa nguvu zote, akauachia nao ukaondoka kwa kasi ya ajabu, mvumo wake ulitikisa miti michache iliyo jirani na mle ulimopita, wakasimama juu ya kilima kile wakiuangali ukienda ulikotumwa.
Juu ya paa la nyumba ya mtawala wa Hamsud, mshale wa ule ulitua na kuwasha moto paa lile lililojengwa kwa aina Fulani ya mimea iliyoshika moto ule kwa kasi.
“Twende sasa!” Amatagaimba akamwambia Seidon kisha wote wawili wakashuka wakikimbia upande ule kuliko na ile nyumba lilikohifadhiwa lile fuvu, Seidon, mpiga mbio alikuwa mbele na upanga wake mkononi, upanga wa Vernad mwana wa Velvesh. Watu walitoka kwenye nyumba zao na kujilinda huku wengine wakienda kusaidia kwa mfalme.
“Tumevamiwa!!!” sauti ilitoka kwa mtu mmoja mwenye tambo kubwa aliyekuwa juu ya paa la nyumba mojawapo lililoonekana lilijengwa kama ngome ya kuweza kuwaona adui wanapokuja kutokea pande za milima Ararat.
“Tumevamiwaaaaaa!” Yule mtu aliendelea kutoa hamasa kwa wengine, milio ya panga zilizofutwa kutoka katika ala zake ilisikika kila upande, Yule mtu kule juu alichukua baragumu na kupuliza, ikiwa ni ishara ya kuruhusu mapigano ya damu, kabla hajatua lile baragumu lake, mshale mmoja wa Amatagaimba ulipenya kifuani na kumdondosha kutoka juu mpaka chini, Amatagaimba alitua ardhini kutoka juu ya nyumba moja wapo na kuufuta upanga wake, hakujali ni wangapi wamemzunguka na silaha gani lakini ustadi wake wa kuuzungusha ule upanga uliweza kuwapunguza nguvu adui kwa kuwakata vibaya, ijapokuwa walionekana ni wengi lakini walionekana kana kwamba hawana nguvu za kufanya mapigano hayo ya kushtukiza.
Seidon, alipambana na upinzani mkali kuweza kulifikia lango la ile nyumba, huku nje tayari akiwa ameshaua askari kadhaa, aliupiga teke mlango na ukafunguka bila kipingamizi, aliingia ndani na kutazama huku na huku, mara akasikia sauti ya kicheko nyumma yake, alipogeuka aligongana macho na mfalme wa Hamsud aliyevalia guo lake jeusi, mkononi akiwa na upanga wa makali kuwili, Seidon alisimama kimapigano na upanga wake mkononi.
“Umekuja mwenyewe sio, sasa kama siku ile nilikuacha hai leo lazima nikikate kichwa chako kwa upanga huu, upanga wa Hamsud, wenye mapigo ya ajabu,” Yule mfalme aliongea kwa jazba huku akimfuata Seidon kwa kasi.
“Hakika, nimekuja kuitaka roho yako na kulichukua fuvu la Cleopas ambalo si mali yako, amin nakuambia upanga huo mkononi mwako leo hii utakuwa mikononi mwangu,” kabla Seidon ahajamaliza kusema, ilisikika kelele ya panga mbili zilizogongana na kutoa cheche, ilikuwa ni pigo la kifo lililotoka katika mikoni ya Yule mfalme, lilikuwa likikielekea kichwa cha Seidon ambaye tayari nay eye Alisha inua upanga wake na kuuzuia ule wa Yule mfalme, kisha wote wawili wakashusha mikono yao chini na zile panga bado zikawa zimesigana katakati yao, wakisukumana na kutazamana kwa gadhabu. Seidon alijisogeza pembeni kwa ghafla na kumpiga pigo la kiwiko Yule mfalme, lakini kabla hajafanya lolote, upanga wa mfalme ulipita katika tumbo la Seidon na kuchana upande wa vazi lake, Seidona akaruka sarakasia kutua upande wa pili alijishika tumbo kwa maumivu, lakini bado alikuwa katika mapambano, mapigo kadhaa ya mapanga yaliifunikiza nyumba ile huku Seidon akionekana kuzidiwa maarifa na Yule mfalme, hakuna mtu aliyeingia katika pambano hilo.
Amata ga Imba alikuwa nje akiimarisha ulinzi kwa kupambana na askari wale ambao walijiziuka naye wakisahau kuwa ndani ya hekalu lao kuna mwingine anayepambana na mfalme wao. Amata ga Imba aliangusha wengi awezavyo huku akiwakwepa kwa ustadi wa hali ya juu, akijaribu kuvuta muda ili Seidoni afanikishe lile alilotumwa.
Amata ga Imba alipoona Seidon hana dalili za kutoka alifanya kila hila za kimapigano na kukimbilia upande, mwingine ambao alikuwa jirani kabisa na lile hekalu la Wahamsud, mara akajikuta amezingirwa na askari wenye uchu wa kuitoa roho yake, aliishika pete yake na kuifanya anachojua yeye, mwanga mkali ukatoka kwenye pete ile na kuwaumiza mcho wale askari hata wasiweze kuona tena. Amata aliukaribia mlango wa hekalu na kuona jinsi pambano lile lilivyokuwa likiendelea lakini Seidon hakuonekana na upanga mkononi, “Seidoooooonnnnn!” Amata aliita na kumrushia upanga wake, Seidon alijrusha kwa ustadi na kuudaka ule upanga, alijiviringisha kwa ufundi kumuelekea Yule mfalme ambaye alishidwa kujua amshambulie nani.
Mfalme wa Wahamsud akiwa katika kutahamaki Seido alikuwa ameshafika miguuni pake na kumshindilia upanga wa tumbo uliompelekea kutokwa na uhai. Seidon akampisha adondokee pembeni kisha akanyanyuka kwa haraka na kumkata kichwa, aliurudisha upanga wa Amata kwa kuurusha na kisha akauokota ule wa kwake, akaurudisha alani na kuingia kwenye kijichumba kimojawapo, mara giza likatawala ndani ya hekelu lile. Amata ga Imba alipoona giza hilo akajua kumekucha, akapiga mbinja kali na muda mfupi tu, farasi wale wawili walikuwa tayari wamefika, Seidon akarukia juu ya mmoja wapo na Amata vilevile kisha wakapiga mbio kuelekea upande wa kusini. Nyuma yao jeshi lilikuwa likija kwa kasi na farasi.
Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi
USIKOSE SEHEMU IJAYO
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni