HAMUNAPTRA - MJI ULIOPOTEA (12)
Zephiline F Ezekiel
6 min read
Mtunzi: Richard Mwambe
SEHEMU YA KUMI NA MBILI
TULIPOISHIA...
TULIPOISHIA...
“Seidon na Amatagaimba, nilikuwa nikiwasubiri kwa hamu kubwa mfike hapa, niliwaona tangu mbali na nia yenu njema, nifuateni,” Yule mzee akawaambia, Amatagaimba na Seidon wakatazamana kisha wakapeana ishara ya kumfuata wakaenda pamoja naye.
TUENDELEE...
Mbele kidogo wakaingia kwenye piramidi moja dogo lakini lililoonekana kumegekamegeka vipande, lilionekana ni la kale kuliko yote. Wakaingia ndani, chumba kilikuwa na giza lakini mishumaa ilijitahidi kulishinda giza hilo, Seidon akiwa na mfuko wake barabara mkononi mwake na upanga wa Vernadi kiunoni mwake, alikuwa akifuata kwa makini kila apitapo mzee Yule, Amatagaimba naye vivyo hivyo, yeye alikuwa nyuma kabisa akiwaacha Seidon katikati na Yule mzee mbele yao.
Joto kali lilitawala katika piramidi lile, joto lililotokana na wingi wa mishumaa iliyojazwa katika vitu kama ngazi nyingi zilizozunguka katika piramidi hilo. Baada ya mwendo kidogo, Yule mzee akawanyooshea mkono kuwapa ishara ya kusimama, nao wakatii na kusimama. Hakuna kilichoendelea kati yao isipokuwa joto lililowafanya kulowa kama wamepita kwenye mvua.
“Joto kali, kwa nini msizime mishumaa hii?” Seidon akauliza. Yule mzee akatulia bila kujibu kisha akageuka kumtazama.
“Dunia yenu haiwezi kuwapa uhai ninyi bila mishumaa hii, endapo itazimika piramidi hili litajifunga nikimaanisha pande nne za piramidi hili ndizo pepo nne za dunia, hapa ndipo penye majira ya mwaka, panapogawa miezi, siku na miaka, ndipo panapofanya jua liwake, mvua inyeshe, hapa ndipo penye kila kitu, ukitaka kwenda mwaka 2000 unaweza, ukitaka kuona yatakayotokea kesho na miaka mia nne ijayo hapa ndio mahali pake, kwa kifupi niwaambie kuwa hapa ndipo katikati ya dunia, kitu chochote chenye madini ya chuma hakiwezi kuanguka chini wala kutoka mahali kilipo,”
Yule mzee akamjibu Seidon, kwa Seidon na Amatagaimbailikuwa kama simulizi ya kusadikika hakuna aliyeamini ukweli wa maneno hayo, wakatazamana kwa mara nyingine tena na kisha kila mmoja akacheka peke yake moyoni. Amatagaimba akaushika upanga wake na kujaribu kuuchomoa kutoka katika ala yake lakini upanga ule uling’ang’ania katika ala, haukutoka, Amatagaimba alijaribu tena na tena lakini hali ilikuwa ileile, akamwambia Seidon ajaribu naye kuutoa wa kwake lakini hakuna aliyeweza.
“Ina maana hamuniamini ninachowaambia?” Yule mzee aliuliza, “Sikieni ninyi wanadamu, katika dunia ya sasa huu sio mwaka mnaouishi, sasa mnaishi katika dunia ya kale, kama hamtakuwa na imani basi mjue safari yenu hamtofika kwa maana ili mfike Hamunaptra, mji wa wafu, mji uliopotea ambao upo chini kabisa ya ardhi lazima mvuke daraja la pepo, daraja ambalo lazima ufunge milango yako yote ya fahamu ndipo uweze kuvuka ukishindwa utatumbukia katika shimo kubwa ambalo kwenu duniani mnaliita kuzimu huku linaitwa bonde la uvuli wa mauti,” maneno hayo ya Yule mzee yaliwafanya Amatagaimba na Seidon kuingiwa na hofu kuu.
“Mbona hatuendelei mbele?” Amatagaimba akauliza.
“Ha ha ha ha haaaa!!!!” sauti ya kicheko cha kutisha kutoka kwa Yule mzee ikatawala mle ndani na kufanya mwangwi wa kutisha, “Hatuwezi kupita hapa sasa kwa sababu dunia hivi sasa inapishana na sayari ya Venus kwa upande huu wa Mashariki, hivyo kuna tetemeko kubwa la ardhi hatuwezi kuvuka,” Yule mzee aliwaeleza. Baada ya dakika chache waliona kitu kama vumbi kikipukutika kutoka katika kona za piramidi hilo, Amatagaimba akataka kufumba macho ili kuepuka vumbi hilo lakini alikatazwa na Yule mzee, akaambiwa kuwa ndani ya piramidi hilo hutakiwi kufumba macho hata mara moja. Ikabidi wote watulie hivyohivyo mpaka dhoruba ya tetemeko na vumbi ilipopita.
“Sasa tunaweza kwenda, kulikabili daraja la pepo, tukifika eneo linaloitwa milima mitano itabidi kufanya ibada ya kufunga milango ya fahamu ili kuvuka daraja hilo, hapo hapahitaji utani hata kidogo,” Yule mzee aliwaasa kisha wakaendelea na safari.
Giza lilikuwa nene, kati yao kulikuwa na wadudu wengi wa vimulimuli ambao walifanya nuru ya kupendeza, walitembea polepole wakimfuata Yule mzee aliyekuwa akiwaongoza njia. Mbele kidogo wakasikia sauti kama ya maji yanayopita mbali katika maporomoko makubwa. Amatagaimba akasimama na kugeuka huku na kule, ndani ya mlio huo wa maji alikuwa akisikia mlio wa farasi na mvumo kama upepo mkali. Yule mzee nae akasimama, akaonesha ishara tena ya mkono kisha wote wakasimama.
“Orion!” Yule mzee akasema kwa sauti ya taratibu, Amatagaimba akaushika upanga wake tayari kwa pambano lakini hali ilikuwa ni ileile, upanga haukutoka katika ala yake. Amatagaimba hakuwa na ujanja, Seidon naye alijaribu lakini haikuwezekana, “Tupo katikati ya usumaku wa dunia, hakuna kitu cha chuma kinachoweza kufanya lolote hapa,” Yule mzee aliwaambia. Kisha akawapa ishara ya kuondoka na kuongeza mwendo.
§§§§§
ORION alijua wazi kuwa hapo katika daraja la pepo ndipo pa kuweza kutimiza azma yake kwani alielewa wazi kuwa hakuna silaha ya chuma itakayotumika. Orion alipiga mbio na farasi wake kulikabili lile daraja.
“Ongeza mwendo Orion anatukaribia,” Yule mzee aliwahimiza akina Seidon ambao walikuwa wakitembea kwa tahadhari kwani giza lilikuwa nene mno. Amatagaimba akajipapasa na kujikuta akiwa na kamba kiunoni mwake, akafikiri jinsi ambavyo ataitumia kamba hiyo kuwa silaha dhidi ya Orion mwindaji mashuhuri wa enzi na enzi mwenye shabaha isiyokosa hata mara moja.
Seidon na Amatagaimba walikuwa wakionekana wazi kwa macho ya ajabu ya mwindaji huyo aliyepewa kazi maalum na wachawi wa Misri kuhakikisha analipata fuvu la Cleopas. Akainua uta wake mkubwa wenye nguvu alioamini kuwa kwa kasi ambayo mshale huo utachomoka katika uta wake lazima utapasua nguvu za usumaku na kumfikia Seidon ambaye alikuwa nyuma tu ya Yule mzee.
Akauvuta kwa nguvu zake zote huku misuli ya mikono yake mikakamavu ikiwa imedinda na kufanya nyama ya mikono hiyo kuwa ngumu ajabu.
Ilikuwa bado hatua chache sana Amatagaimba na Seidon kumaliza ule ukanda wa usumaku wa dunia, ila Yule mzee tayari alikuwa amepita eneo lile. Mshale wa Orion ukaja kwa kasi ya ajabu mvumo wake ukawastua wote, ulikuwa ni kama mruzi upigwao. Kutahamaki Yule mzee alipigwa kichwani na ule mshale wa Orion, mshale wa kichawi, ukamtawanya kichwa chote na kisha kiwiliwili chake kubaki kimesimama vilevile. Seidon aliuona mshale ule ukimjia usoni, akatamani kupiga kelele lakini akajikuta akishindwa, akashangaa mshale ule ukisimama sentimeta chache kutoka usoni kwake, ukaganda kama igandavyo barafu ndanin ya jokofu, Seidon akashusha pumzi ndefu na kujaribu kuushika ule mshale.
“Acha!,” Amatagaimba akamwambia Seidon, “Mshale huo umenasa katika nguvu za usumaku,” Seidon akaelewa kwa nini, akakumbuka Yule mzee alivyowaambia kuwa hakuna kitu cha chuma kinachoweza kufanya lolote katika eneo lile. Wakavuka na kufika eneo la pili eneo la milima mitano. Mbalamwezi ya kung’aa iling’aza eneo hilo lote na vilima vile vilionekana wazi umbali mfupi tu mbele yao, lakini hawakujua ni wapi watapita, Yule mzee tayari alikuwa hana kichwa na aliganda palepale kama nguzo. Mbele ya milima ile kulikuwa na giza linguine nene lisilo hata na vimulimuli, katikati ya giza hilo kulikuwa na kitu kama ujia mdogo uliokuwa uking’aa sana, daraja la pepo. Wawili hao wakatulia kwanza na kutafakari, wakiwa kimya kabisa, mara wakasikia mvuma mkali wa mbawa za ndege mkubwa.
“Pelargonis,” Amatagaimba akaongea taratibu.
“Umesemaje?” Seidon akauliza, kabla Amatagaiba hajajibu alijikuta kapigwa na ubawa mkubwa wenye nguvu wa ndege huyo na kuanguka mbali, Yule ndege akataka kunyakuwa ule mfuko wa Seidon, lakini Seidon naye hakukubali, mara hii alipoufuta upanga wake ukatoka ndani ya ala, akaushika kwa mikono yake miwili na kuanza kupambana na ndege huyo mkubwa.
Amatagaimba alijaribu kuinuka, na alipofanikiwa tayari idadi ya ndege wale iliongezeka na kumfanya Seidon kuelemea nao. Amatagaimba akautoa uta wake mgongoni na kuchukua mshale katika podo lake, shabaha yake haikuwa haba, kila mshale mmoja ulikuwa ukiangusha ndege mmoja. Yule ndege aliyeonekana kama ndio mama yao akaona wenzake wanavyopukutika, akamuacha Seidon akipambana na wengine yeye akamjia Amatagaimba, shabaha yam shale wa Amatagaima ilikielekea kichwa cha ndege Yule, lakini hakuamini kilichotokea, Yule ndege akaudaka mshale ule kwa midomo yake mirefu na kuuvunja. Amatagaimba akatoa kamba iliyokuwa kiunoni mwake na kuanza kumkabili ndege huyo wa kutisha. Aliizungusha ile kamba kwa ustadi mkubwa na alipoiachia Yule ndege alishuka chini zaidi na ile kamba ikapita juu, Amatagaimba alijirusha upande mwingine na shambulizi la ndege huyo likakosa lengo.
Seidon kwa kutumia upanga wake aliweza kukata ndege wengi sana lakini alikuwa amechoka sana nab ado pambano lilikuwa likiendelea. Amatagaimba akiwa chini alikuwa hana ujanja mwingine Yule ndege alikuwa akija tena huku kapanua domo lake tayari kumdonyoa, akili ilikuja mara moja, kulikuwa na jiwe pembeni akaliinua na kulirusha, likatua sawia ndani ya domo la ndege huyo, likamkwama kooni, akaanguka na kujirusharusha huku nakule, Amatagaimba akachukua nafasi hiyo akauchomoa upanga wake na kumkata kichwa. Alipohakikisha kiumbe huyo amekwisha, ndipo alipomtazama Seidoni aliyekuwa bado akipambana na ndege hao. Kwa kutumia upinde na mshale wake aliweza kuwapiga ndege wote na kumkamata mmoja kwa kutumia ile kamba. Walimfunga barabara, alikuwa ndege mkubwa sana na wa kutisha ambaye hakuwahi kuishi wakati wetu huu, wote wawili walitweta wakiwa na kiu cha ajabu lakini hawakuwa na hata tone la maji.
“Amatagaimba, tutavukaje daraja la pepo ilhali aliyekuwa akituongoza amekufa?” Seidon akauliza.
“Swali gumu Seidon, tazama daraja lilivyo refu, na halina ukingo katika pande zake,” Amatagaimba alionesha mashaka katika hilo.
“Na hapa si salama kwetu, itakuwaje kama Orion atatukuta hapa?” Seidon akauliza. Amatagaimba hakujibu neno, akainua mkono wake na na kuigonga kwa kwenzi mara tatu ile pete yake. Mara mbele yake pakatokea moshi mikubwa mno, Amatagaimba akatulia akiutazama na katikati yake alionekana Bagoza, bibi jinni wa Solondo, akiwa kazungukwa na upepo mkali uliochanganyika na ndimi za moto.
“Nimeiona shida yako, nimesikia kilio chako lakini jambo moja ninaloweza kukwambia ni kwamba, nguvu zetu na nguvu za huku ni kinzani sana, nikikuahidi kukuvusha katika daraja la pepo nitakuwa mkaidi mbele ya watu wangu, kwa kukusaidia ewe shujaa wetu, nitakuonesha njia ya kuzunguka ambayo itakufikisha katika lango la Hamunaptra,
Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi
USIKOSE SEHEMU IJAYO
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni