DHAMANA (19)
Zephiline F Ezekiel
6 min read
Mwandishi: Hassan O Mambosasa
SEHEMU YA KUMI NA TISA
TULIPOISHIA...
TULIPOISHIA...
"Hasbuk mzee mwenzangu shukran sana muache kijana apumzike mimi nitatumia sehewa hapo tu niende chapuchapu haina haja ya gari" Mzee Mahmud aliongea huku akitembea na Mzee Buruhan akawa anamsindikiza, walitoka hadi nje ya nyumba eneo linaloegeshwa baiskeli nyingi za kukodisha.
KUNA MATANGAZO YANATOKEA YAGUSE ILI KUNIPA NGUVU YA KUENDELEA
KAMA UNASOMA SIMULIZI HII NJE YA CnZ Media APP INSTALL ILI USIPITWE NA MIENDELEZO
SASA TUENDELEE...
Mzee Mahmud alikodi moja na dereva wake akamuaga Mzee Buruhan akaondoka.
****
Majira ya jioni kwa huku duniani upande mwingine wa himaya isiyokuwepo juu ya ardhi ya wanadami tayari kikao kilikuwa kimeshawekwa ndani ya chumba maalum cha mkutano, ilikuwa ni ndani ya himaya ya Majichungu katika ya bahari ambapo ndiyo makazi ya majini wasiyohusika na utumikishwaji katika nguvu za giza. Ndani ya chumba hiki cha mkutano walikutana viongozi mbalimbali wa himaya hiyo baada ya mkutano wa dharura kufanywa ghafla kutokana na hali inayokuja mwezi mmoja baadaye iliyoonwa na jicho la Salmin ambaye naye alikuwa ni mmoja kati ya waliohudhuria mkutano huo akiwa pamoja na baba yake mzazi.
Hali iliyokuwa inatarajia kuingia hapo mwezi mmoja baadaye ilikuwa ni hali ya kutishia usalama wa viumbe wote waliokuwa majini kwa asili zote kasoro wale wa mchanganyiko ndiyo pekee wangeweza kusalimika na mkasa huo na si vinginevyo, ilikuwa ni lazima hali hiyo idhibitiwe haraka iwezekanavyo lasi hivyo himaya hiyo itakumbwa na na balaa kubwa sana.
"Jamani hali ni tete katika himaya yetu na tusipofanyia ufumbuzi suala hili basi tujue himaya yetu itakubwa na balaa kubwa, hebu tumsikilize Salmin atuambie ni nini alichokiona katika maono yake ya kuona mambo yajayo" Zalabain alifungua mkutano huo kwa maelezo hayo.
"Asante sana kiongozi wetu na mfalme mtarajiwa wa himaya hii kwa kunipa nafasi hii, hali halisi inayokaribia kutufikia ni ujio wa wadudu kutoka himaya ya giza baada ya wao kubaini kuna ukosefu wa giza kwa muda mrefu katika himaya hii baada ya kufariki kwa mtukufu mfalme. Viongozi wa himaya ile ambao ni maadui wakubwa wa himaya hii wameona ndiyo njia pekee ya kuidunisha himaya yetu kwa kutuma wadudu watakaoachia vimelea ambavyo vikimpata jini yoyote ambaye hana damu ya binadamu yaani ambaye hajachanganyika au hajatokana na uzao wa binadamu na jini itakuwa ndiyo mwisho wa maisha baada ya vimelea hivyo kumtesa kwa muda mfupi tena kwa maumivu. Balaa hili namaanisha tutakaopona ni mimi na mfalme mtarajiwa tu ikiwa halitozuiwa ila kama likizuiwa ni himaya nzima itasalimika, hivyo mchango wenu ndiyo unahitajika katika kusaidia kulitatua hili janga" Salmin alitoa maelezo yake.
"wote tumemsikia Salmin mwenye nguvu kuliko sisi sote akitueleza juu ya kinachokuja kutokea ikiwa tu hatutalichukulia hatua hili suala. Sasa basi nimewaita hapa ili tujadiliane kwa pamoja kama ilivyo kawaida yakitokea matatizo kama haya huwa lazima viongozi wa himaya hii wahusishwe, nitasikiliza maoni yenu kila mmoja kuhusu hili suala" Zalabain aliongea, halafu akawatazama wote waliomo humo ndani mmoja baada ya mmoja na macho yake yalitua kwa mkuu wa majeshi wa himaya ambaye macho yake yaliwaka kama taa kuashiria ana jambo anataka kulisema.
"Ndiyo Jenerali" Zalabain alimuambia mkuu huyo wa majeshi wa himaya hiyo huku akimuashiria asimame, mkuu wa majeshi alisimama kisha akatoa heshima kwa Zalabain na wengine waliopo hapo ndani kisha akasema, "Kiongozi wetu mkuu na viongozi wengine napendekeza tuwawahi hao wanamajini wa himaya ya giza kabla hata hawajawaachia hao wadudu kuja huku, najua wadudu wote wanaotaka kuwaachia bado watakuwa wanawaunda kwani wangekuwa tayari wangeachiwa muda wowote. Hivyo mimi napendekeza tutume jeshi liende kwa siri likaharibu huo utengenezaji wa hao wadudu itakuwa tumeiokoa himaya nzima kuliko njia nyingine yoyote".
Mkuu wa majeshi alipomaliza kutoa kauli hiyo alikaa chini na viongozi kadhaa wakanyoosha mkono kuashiria wamekubaliana na hilo wazo la mkuu wa majeshi, upande wa mawaziri wa himaya hiyo mmojawapo macho yake yaliwaka kuashiria anataka kuongea.
"Ndiyo waziri tunakusikiliza" Zalabain alimuambia waziri huyo ambaye alisimama akatoa heshima zote halafu akasema, "Kiongozi wetu mtukufu nimekaa katika himaya hii kwa muda wa miaka 4000 hadi inatimu siku hii ya leo ninapopokea taarifa hii, katika miaka hiyo yote nimeshuhudia balaa kama hili liliwahi kutaka kutokea kwa kutengenezwa viumbe wenye sumu na himaya hiyo hiyo ya nguvu za giza lakini kwa masaada wa Dainun ya kale ambayo muda wake uliishia siku ile alipotawafu babu yako. Hivyo basi kinga mpya ya balaa hili ni kupatikana kwa dainun mpya ambayo ilikuwa ipo mikononi mwa hayati baba yako ndiyo itasaidia kuzuia haya mabalaa milele mpaka utakapoiacha dunia hii"
"Asante kwa maoni yako waziri, mzee Zultash ongea" Zalabain aliongea kisha akamruhusu baba yake Salmin aongee baada ya macho yake kuwaka. Mzee Zultash alisimama akatoa salamu kwa wote waliomo humo ndani pamoja na kuonesha heshima kwa viongozi wakubwa.
"Asante kiongozi wetu, mimi hapa naungana na wazo alilolitoa mkuu wa majeshi la kwenda kuharibu utengenezwaji wa hao wadudu kwani sote tunatambua kwamba Dainun mpya imeibiwa na mpaka ije kupatikana hatujui itatuchukua muda gani kwani hao viumbe wataingia ndani ya himaya hii mwezi ujao. Kumbukeni mwezi kwetu tunauona kama juma moja analoliona mwanadamu wa kawaida, sasa hamuoni hapo tutakuwa tumechelewa na maafa yatakuwa yameshatufikia jamani" Mzee Zultash aliongea na viongozi wote wakamuunga mkono hata yule waziri aliyetoa hoja ya kutafutwa Dainun naye alimuunga mkono.
"Kama ilivyo sheria yetu inavyosema, hoja ikiungwa mkono zaidi imepita. Basi jeshi la makomandoo litumwe kwenda kuharibu utengenezaji wa wadudu hao huku nikiwa naisaka Dainun kwani mwenye kuimiliki kashajulikana" Zalabain aliongea.
Kikao kilikwisha muda huo huo na maandalizi ya kikosi cha kuokoa himaya ya Majichungu yalianza mara moja, Kikosi kilichokuwa chini ya Salmin na mkuu wa majeshi ndicho kilichopewa jukumu zima la kuiokoa himaya hiyo. Vizuizi vya himaya hiyo vilifunguliwa na kikosi hicho kilitoka haraka sana na kisha vizuizi vikafungwa tena ili kuzuia himaya hiyo isivamiwe na maadui kwa ghafla, kikosi hicho kilitumia nguvu zao za ajabu za kijini kusafiri pasipo hata kutumia usafiri wa aina yoyote kama ilivyozoeleka kwa wanadamu wanapotaka kwenda mahali.
Majini haya yalikuwa yakielea katika anga la chini ya bahari kwa kasi sana yakielekea upande wa kusini wa himaya yao ambapo ni katika eneo lenye giza kubwa sana kiasi ambacho ingemlazimu mwanadamu wa kawaida kutumia mwanga wa aina yoyote kulivuka eneo hilo, lakini kwa hawa majini ilikuwa kawaida kwao kupita eneo kama hili bila kutumia nuru ya aina yoyote ile. Walipita eneo hilo lenye giza kwa mwendo wa kasi sana hadi walipokaribia eneo lenye miti mirefu ambayo ilienda juu pasipo kuonekana mwisho wake ilibidi wasimame baada ya kupokea amri kutoka kwa Salmin baada ya macho yake kuwaka kwa nguvu halafu yakazima.
"sasa tunaingia pori la giza linapakana na mapango ya Zabakut ambayo ndiyo hutumiwa na majini wataalam wa himaya ya giza kutengeneza viumbe mbalimbali kwa ajili ya kuangamiza himaya zingine, sasa basi katika pori hili kuna ulinzi mkali sana wa viumbe maalim waliotengenezwa mithilli ya miti ili kuwahadaa maadui wao wajue ni miti yote hii halafu wawaue kabla hata hawajalivuka hili pori.
Umakini wenu unahitajika kwani hakuna njia nyingine ya kufika kwenye mapango ya Zabakut zaidi ya hii kwani hii miti haina mwisho urefu wake hivyo hatuwezi kupita kwa juu, nadhani tumeelewana sasa tuingie tukiwa pamoja na si kugawanyika makundi" Salmin alihitimisha hapo akatoa ishara na kikosi chote kikaanza kuingia katika msitu huo kwa pamoja, walipoingia ndani ya pori hilo walipokelewa na giza nene zaidi hata ya lile walilolipita mwanzo na ukimya mkubwa sana ambao unatisha sana na laiti angehema mtu basi ungemsikia papo hapo. Walipita kwa umakini sana na kutembea kwao kulikuwa kwa umakini sana ili wasije wakaingia katika mikono ya maadui zao, walipofika katikati ya msitu mmoja wa wanajeshi wa kikosi chao aliyekuwa nyuma alitoa ukelele wa maumivu uliovuma pori zima na kuwafanya wenzake wageuke kwa haraka
****
Upande wa nyumbani kwa Shafii ilikuwa tayari usiku umeshaingia na Bi Farida alikuwa yupo sebuleni akiongea na Jamal, Shafii alikuwa yupo chumbani kapumzika muda huo kutokana na kunywa dawa kali sana ambazo zilimlazimu kulala usingizi mzito. Muda huo ndiyo ulikuwa muda ambao kidonda kingine kikubwa zaidi ya kile cha awali katika moyo wa Shafii kilijitokeza kwa namna isiyotarajiwa kabisa kama ingeweza kutokea, muda huo tayari watumishi wa nyumba hiyo walikuwa wamelala kutokana na kuwa ni usiku sana.
Mtumishi peke wa nyumba hiyo aliyekuwa macho ni mlinzi tu ambaye alikuwa bado alikuwa na kibarua cha kuilinda nyumba hiyo kwa muda wa usiku. Bi Farida akiwa anaendelea na mazungumzo na mpwa wake sauti ya maji yakimwagika katika matanki yaliyopo nje ya nyumba hiyo kwa upande wa uani ilisikika, Jamali aliponyanyuka kwenda kufunga maji hayo Bi Farida alimuambia aache akafunge yeye kisha akainuka akaelekea ulipo mlango wa uani.
Bi Farida alifungua mlango na akatoka nje akakutana na mazingira tofauti na ya nyumbani hapo, aliona nje ya nyumba yake kulikuwa kuna giza lakini alipotoka nje katika baraza la uani aliona wingu jekundu limetanda juu angani na kufanya eneo lote liwe jekundu kama vile muda wa machweo ya jua. Alipoangalia katika ngazi za kushuka chini aliona rundo la viumbe waliovalia mavazi ya maaskari wa zamani katika vita vya mapanga huko katika himaya roma wakiwa wamejipanga mstari na ngazi zilionekana na ndefu mno tofauti na zilivyo ngazi za baraza nyumbani kwake, hali hiyo ilimshtua sana na na akaamua ageuze ili arejee ndani alipotoka akiwa anapiga makelele ya uoga akimuita Jamali lakini alijikuta akikaa kimya baada ya kuona mazingira ya mlango huo ni tofauti na mazingira ya mlango wa nyumbani kwake.
Mlango huu ulikuwa wa dhshabu wenye mapambo mbalimbali ya kupendeza na mlangoni kulikuwana walinzi waliovaa makofia ya chuma wenye kimo kirefu tofauti na Binadamu wa kawaida, Bi Farida alijikuta anapiga kelele lakini mmoja wa walinzi alimnyooshea kidole na sauti yake ikakatika hapohapo ikawa haisikiki.
"Huyu mwanadamu anataka kutuzibua masikio sasa, yaani hajui kama sauti yake ni kubwa mno akiwa huku ndani ya himaya hii. Mchukueni nyinyi masikio yanatuuma sasa hivi" Mmoja wa walinzi aliongea kwa sauti nzito huku akiwa ameshika masikio kama ambavyo wenzake wote walivyokuwa wameshika masikio kutokana na kuumizwa na makelele ya Bi Farida, kauli ya yule mlinzi aliposema mchukueni hakuelewa anamaanisha nini na alikuja kuelewa baada ya kujikuta amezungukwa na wasichana watatu wenye urembo wa hali ya juu ambao haikujulikana walifika vipi hapo hadi muda huo.
USIKOSE SEHEMU INAYOFUATA
Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendeleza Simulizi
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni