HAMUNAPTRA - MJI ULIOPOTEA (2)
Zephiline F Ezekiel
6 min read
Mtunzi: Richard Mwambe
SEHEMU YA PILI
TULIPOISHIA...
TULIPOISHIA...
Kelele nyingi zilimfuatia nyuma yake kana kwamba kuna watu walikuwa wakimfukuza. Aliongeza mwendo kukimbia, hamad! Alijikwaa na kuanguka chini, alipojigeuza kutazama juu kwa mtindo wa ‘chali’,radi kali ilimpiga usoni hata kuhisi kuwa amepoteza nuru ya kuona.
TUENDELEE...
Kaupepo katamu kalimpitia Vernad, alijaribu kuamka pale alipokuwa lakini ilikuwa ni vigumu kwake. Alilala tena kwa utaratibu katika vumbi lile, kwa haraka haraka hakujuwa ni wapi alipo, jangwa kubwa lilimzunguka na jua kali lilimchoma uso, alichokiona sehemu hiyo ni misafara ya ngamia kutoka eneo moja kwenda lingine. Alifanikiwa kunyanyuka baada ya kukusanya nguvu nyingi sana, aliinuka na kujipukuta vumbi lilioujaza mwili wake na kumfanya awe kama kinyago. Aliyaficha macho yake kwa viganja vya mikono yake ili kupambana na nuru kali ya jua iliyomlenga moja kwa moja machoni kwake.
Kutoka mbali aliona farasi aliyekuwa akielekea pale alipo kwa kasi sana, Vernad alitulia kuona kitachoendelea. Punde si punde farasi yule alisimama mbele yake na mtu aliyekuwa kapanda juu yake aliteremka na kuuvuta mkoba wake toka mgongoni, akatoa kibuyu cha maji na kumpa Vernad aliyekuwa amekaushwa kwa jua kali lenye hasira.
“Asante bwana! Bila shaka wewe ni mtu wa Mungu” Vernad alimshukuru yule mtu.
“Ha ha ha ha ha !!!” yule mtu alitoa cheko lililomfanya Vernad akumbuke yaliyompata usiku ule.
“Umejuaje niko hapana nahitaji maji?”
“Nimekuona tangu mbali sana, na lengo lako la kusaidia watu wako, Warelvesh. Vernad! Naitwa Ismokum, mimi ni mtu kutoka kuzimu, nilishakufa miaka mingi nyuma na sasa naishi katika hii dunia ya chini, mji wa Hamunaptra.” Alikohoa kidogo, huku akishuka kutoka katika farasi wake na kusimama chini katika ardhi yenye mchanga mwingi. Alimsaidia Vernad kunyanyuka na pamoja wakasogea pembani palipokuwa na jabali kubwa wakakaa hapo.
“Sijaelewa! Umesema wewe ni mtu uliekwishakufa?”
“Ndiyo, bila shaka, mimi nilishakufa miaka mingi ambayo hata babu yako alikuwa hajazaliwa.”
“Hamunaptra ni kitu gani?” Vernad aliendelea kwa maswali.
“Huo ni mji wanaokaa watu waliokufa zamani, mji wa wafu, mji uliopotea. Mji ambao sasa upo chini ya ardhi, mji usio na shida wenye kila kitu utakacho isipokuwa mapenzi.” Yule mtu alimjibu Vernad.
Vernad alimkazia macho mtu yule mwenye manywele na mandevu marefu sana, midomo myekundu kama aliyekula nyama mbichi, macho yake ambayo yalikuwa yameangalia kilamoja upande wake, hakika alikuwa marehemu jinsi alivyoonekana.
“Na hapa nimefikaje?”
“Jana usiku ulikuwa ukinifatilia mimi, na nilijua unachotaka kwangu, sasa usihofu, umepata. Fuvu la Cleopas! Kulipata si kazi ndogo, kwanza Cleopas mwenyewe analitafuta pepo zote nne za dunia” Vernad, alistuka kidogo ‘analitafuta?’
“Ndiyo, analitafuta!” yule mtu alimwambia Vernad, ambaye alistuka kwa mara ya pili, ‘kajuaje kama nimejiuliza analitafuta?’. Vernad alijua kuwa, haswa kujiingiza katika kutafuta kitu usichokijua ni hatari lakini afanye nini? Kwa ajili ya watu wake. Yule mtu alivuta hatua chache mbele na kumpita kwa karibu Vernad, alipompita aligeuka kumwangalia, hakuwa mtu yule, sura yake ilionekana kama iliyooza ikibubujika mabonge ya damu, meusi, mdomoni, puani na machoni. Vernad alitetemeka kwa woga, hakujua kama akimbie au abakie pale pale.
“Ukilipata fuvu hilo ulirudishe kwenye mji wa Hamunaptra na ulipachike kwenye shingo ya Cleopas na hapo Clakos atakupa utakacho. Ukikaidi litakuteketeza wewe na jamaa yako yote”. Upepo wa ghafla ulipita kati yao na vumbi la jangwa likawatenganisha, lilipotulia Vernad hakuona mtu wala kitu mbele yake. Sauti zilifikia masikioni, sauti za ajabu zikijirudiarudi ndani yake zikitamka jina Hamunaptra, Hamunaptra, Vernad aligeuka huku na huku, akisumbuliwa na sauti zile lakini hakuona aliyeongea wala hakujua zimetoka wapi, aliziba masikio lakini bado aliendelea kuzisikia kwa nguvu sana.
1850
Sehemu Fulani huko India
Jua liliwaka kwelikweli, vibarua walifanya kazi ngumu ya kuvunja mawe na kusogeza hapa na pale, kukusanya vyuma ili kutandika reli mpya kwa manufaa ya koloni la Uingereza. Askari wa Kiingereza walisimama kando wakipuliza moshi wa kiko na cigar, huku mijeledi ikiwa viunoni mwao, hutakiwi kusema umechoka wala unaumwa, utafanya kazi mpaka pumzi yako iishe.
Haikuwa rahisi hata kidogo, mataruma mazito yalivutiwa hapo na kazi ya kuunganisha njia ya reli iliendelea chini ya engineer wa kiingereza aliyejawa na dharau na nyodo kupita kiasi.
Ili kupata mawe yanayotakiwa hasa katika kazi hiyo iliwabidi kupasua majabali makubwa na miamba ya kutisha, vibarua wengi walipoteza maisha kwa kupigwa na mawe hayo yaliyoruka huku na huko. Baada ya kupasua mawe hayo an kuyamaliza sasa walianza kuchimba kuelekea chini. Hakukuwa na mashine kama hizi tulizo nazo wao walichimba kwa dhana duni lakini zilikuwa bora kwa wakati huo.
Prakesh Minto, kibarua aliyeipenda kazi yake aliinua juu sururu yake na kuitelemsha ili kupiga jiwe lililoonekana kujitokeza katika shimo hilo, kabla sururu ile haijatua alijikuta ikimtoka mikononi na kuruka pembeni, kisha alisikia sauti zikiongea maneno yasiyoeleweka. Prakesh alichanganyikiwa na kuanza kukimbia hovyo. Waingereza wale waliokuwa hapo katika kusimamaia shughuli ile walimuona Prakesh kama aliyeruykwa na akili, walimpiga risasi na kumuua.
Kisha wakasogea eneo lile, kijana mwingine alikuwa akichimba lufuata kitu kama ukuta. Walipoona ukuta ule hauna dalili ya kufika mwisho ndipo walipoomba wataalamu kutoka Uingereza kuja kutoa msaada katika hili.
Baada ya Miezi kadhaa ya kuchimba na kusafisha eneo lile walijikuta mbele ya mji mkubwa, mji wa kale ambao kwa wakati huo ulikuwa umesha zama ardhini kwa karne na karne, hata waenyeji walikuwa wakiishi hapo miaka hiyo hawakulijua hilo. Kuta zenye nguvu, nguzo kubwa, milango iliyotengenezwa kwa mbao ngumu ambazo zilidumu hapo bila kuliwa na nondo.
Paul Smith, aliivua kofia yake aina ya pama na mkono mmoja alikuwa kajishika kiuno. Mtaalam huyo wa mambo ya kale, alijivunia sana ugunduzi wake, aliendelea kupiga mluzi akiimba moja ya nyimbo za kwao. Baada ya kuhakikisha kuwa eneo lote liko safi, waliadhimia sasa kuingia ndani ya mji huu kujionea kilichopo, mioyoni mwao waliamini kuwa sasa utajiri upo jirani. Walijaribu kuvunja mlango lakini hata hawajathubutu mlango ulifunguka wenyewe na kiza kinene kiliwa karibisha.
888
Vernad aliitoa mikono yake masikioni, nyuma yake alikuwa amesimama mtu mmoja wa makamo aliyeva kanzu la hariri, kichwani kajiviriga kilemba cha rangi ya hudhurungi. Vernad alimtazama mtu huyu kwa woga hakujua kama ni yule aliyeondoka kwanza au huyu ni mwingine, aliendelea kumtazama huku kasimama kidete mono wake wa kulia ukiwa tayari umeshika mpini wa jambia lake.
“Ha! ha! ha! ha! ha! Vernad, karibu sana Hamunaptra. Huku hatutumii silaha kwa kuwa wote tunaoishi hapa ni wafu, huu ni mji wa wafu, wafu siku zote hawafi tena” yule mtu alimaliza kauli yake na kuelekea upande wa maghalibi wa jangwa lile, naye Vernad alimfuata uko huko.
“Wewe ni nani?” Vernad alimuuliza mtu yule huku akimfuata nyuma kwa kukimbia maana mwendo aliyekuwa akitembea haukuwa wa kawaida.
“Mimi ni Maghalibi” alimjibu Vernad ambaye sasa alikuwa amesimama akimtazama mtu yule akitokomea vumbini na kadiri alivyokuwa akienda aligeuka kuwa vumbi. Vernad alisikia sauti za watu wakimpita huku na huko lakini hakuweza kuona mtu yoyote, alihisi kama yuko sokoni lakini bado hakuona chochote zaidi ya mchanga mwingi uliyojaa katika eneo laote hilo. Kwa namna moja au nyingine Vernand alikuwa anahangaika hakujua yuko wapi, anakwenda wapi na anatoka wapi.
Miezi michache nyuma…
“Seidon!” sauti ya kizee iliita
“Naam!” Seidon aliitikia huku akikurupuka kutoka alipolala na kumuwahi babu yake ambaye alikuwa mzee sana na katika uzee huo daima alipenda kukaa na mjukuu wake, Seidon.
“Seidon!” yule babu aliita tena, sekunde chache za ukimya zikapita kati yao, “Umeshakuwa kijana sasa! Watu wetu wanaishi kwa shida sana, hatuna maji, hatuna mvua, ardhi imepoteza rutuba kabisa, hii ni laana kwetu. Inabidi ukatafute fuvu la Cleopas”, Seidon alistuka kidogo aliposikia hilo, babu yake akampigapiga mgongoni kwa upole “Usiogope, siri ya fuvu la Cleopas na baraka za Klakos, ziko na sisi watu wa Relvelsh, chukua farasi wangu, piga mbio kuelekea Maghalibi mapaka Hamputra, pita kijia kidogo cha kuelekea katika mpaka wa Pakistan na India, ingia kwenye mapango ya Dosh na utatokea Mesopotamia, funga safari mpaka kwenye mapiramid ya Misri kwa njia ya chini, nenda kalete fuvu la Cleopas”.
Seidon aliangalia chini, hofu kuu ilimjaa moyoni akijaribu kupima ugumu wa safari hiyo na umbali wa njia lakini hofu ilimuondoka mara tu alipokumbuka kuwa farasi wa babu yake alikuwa na mbio za ajabu.
“Sogea hapa Seidon,” babu yake alimwita Seidon na kuichukua mikono yake na kuipachika mapajani kama ishara ya kula kiapo.
“lazima uwe muaminifu, babu wa babu zako Vernad alifanikiwa kulipata fuvu hilo kutoka katika mikono ya Wamisri baada ya kupambana kiume na shujaa Orion, na sasa lipo katika mikono ya Waajemi baada ya kuja na kutunyang’anya apa hapa kwetu, ukiwa njiani usitamani mwanamke wala kulala nae, la, utapata nuksi ambayo kazi niliyokupa itakushinda” Babu yake alimaliza wosia na seidon akatoka na kuketi chini.
“Babu nitahakikisha nafanikisha hilo kwa uaminifu.” Alijibu kwa utii.
“Chukua upanga wa Vernad hapo juu, na roho yake ikuangazie katika mapito yako.”
Jioni hiyo Seidon alichukua farasi wa babu yake, farasi mweupe, na kujifutika upanga wa Vernad kiunoni, kisha kutokomea kuelekea jua linapozama. Safari ilikuwa nyepesi sana mwanzoni, farasi alipiga mbiyo za kutosha zilizofanya Seidon kuifurahia safari hiyo, alipita miji mbalimbali, majangwa na mapori akiutafuta mji wa Hamputra.
Usiku mnene sana alifika Hamputra, mji mtulivu kila mtu alikuwa amejifungia ndani na kuota ndoto zake. Ni kiumbe mmoja tu, Seidon alikuwa nje akipita taratibu katika barabara ya mawe iliyopita katikati ya mji huo, mwendo mfupi mbele akasimama, akatoa kibegi chake na kufungua kishapo akaketi chini ya mti na kula chakula chake taratibu akishushia na maji.
Kwa mbali aliona mtu akielekea upande ule alioketi yeye, alimwangalia kwa makini sana, hakuamini macho yake, akayafikicha, maana aliona labda kasinzia. Msichana mrembo wa sura, mwenye rangi mororo ya kuvutia alikaribia eneo lile aliloketi Seidon, mwendo wake wa kunesa ulianza kuusumbua moyo wa Seidon, shujaa wa Relvesh ‘njiani usitamani mwanamke wala kulala nae’, kauli hii ya babu yake ilimkosesha raha kila alipoikumbuka.
Naomba Bonyeza Matangazo Kila Unapoyaona ili Kunipa Nguvu ya Kuendelea Kuwaletea Simulizi
USIKOSE SEHEMU IJAYO
Chapisha Maoni
Chapisha Maoni